|
Na.185 Shawwal 1419, Januari 22 - 28, 1998 |
|
KUPELEKA FAX NCHI ZA NG’AMBO BURE! Labda umevutiwa na kichwa cha makala hii, na mara moja ikakujia fikra, "Hao tena waandishi wa magazeti wamezidi kutuongopea ili tusome magazeti yao! Itawezekanaje kupeleka fax nchi za ng’ambo bure!!?". Tafadhali endelea kusoma makala hii uone ukweli au uongo wa suala hilo zima. Kama nilivyoahidi kwenye makala yangu iliyopita, nitaendelea kuelezea huduma mbali mbali ambazo zinapatikana kwenye Internet. Kwenye makala yetu ya leo nitapenda kuelezea kwa undani kidogo ile huduma niliyoitaja kwa ufupi tu, ya kuweza kupeleka fax mahali popote pale duniani kwa kutumia njia ya e-mail; yaani "email-to-fax service"! Nimeamua kuanza kuelezea huduma hii ya email-to-fax kwa sababu mbili kuu. Sababu ya kwanza ni kuwa si kila mtu duniani ana uwezo wa kupokea au kupeleka ujumbe kwa njia ya e-mail. Watu wengi, hasa kwenye nchi zinazoendelea kama Tanzania, hawana anuani za e-mail, lakini kwa bahati nzuri, wengi wanao uwezo wa kupokea au kupeleka ujumbe kwa njia ya fax. Japo kuwa si kila mtu anamiliki mashine ya fax, watu wengi wanaweza kutumia fax za ofisini kwao, za marafiki zao, na hata za kulipia kwenye maduka mbali mbali yanayotoa huduma za fax. Huduma ya email-to-fax inawapa fursa wale wenye uwezo wa kutumia njia ya rahisi ya e-mail, (ambao pengine hawana mashine ya fax), kuweza kuwapelekea fax wale ambao wanapendelea kupelekewa ujumbe kwa njia hiyo. Sababu ya pili ni kuwa gharama za kutuma fax kwenda nchi za ng’ambo kwa njia za kawaida ni kubwa sana. Kwa mfano, kupeleka ukurasa mmoja wa fax kutoka Tanzania kwenda Marekani, Canada au Uingereza, gharama zake hazipungui dola 3 za kimarekani (US$3.00) ukibahatika. Kama mtu ana kawaida ya kutuma fax nyingi nchi za ng’ambo, gharama za mawasiliano ya fax zinaweza kuwa kubwa sana. Kwa mfano, kampuni inayofanya biashara za nje au ofisi ya serikali inayotuma fax zaidi ya 100 ng’ambo kila mwezi, ni rahisi sana kugharimika maelfu ya dola za kimarekani (mamilioni ya shilingi za Tanzania) kila mwezi kwa mawasiliano hayo ya fax. Kama mtu nyumbani kwake au ofisini kwake, ana uwezo wa kutuma e-mail,basi anaweza kukata gharama za kutuma fax kwa kiwango kikubwa sana akitumia huduma ya email-to-fax kama itakavyoendelea kuelezwa kwenye makala hii. Kwa bahati nzuri, hivi sasa Tanzania, watu binafsi, na wafanyakazi wa ofisi za kibinafsi na za serikali, wanazidi kuwa na uwezo wa kuweza kupeleka ujumbe kwa njia ya e-mail. Na kwa hivyo, wanaweza sana kufaidika na huduma hii ya email-to-fax. Huduma za email-to-fax zipo za aina mbili. Zipo ambazo ni za "bure" na zipo ambazo ni za kulipia. Huduma za bure huwa za bure kweli kweli kama hulipi chochote unapotuma e-mail. Lakini la uhakika ni kuwa kwa huduma hiyo ya bure, fax itapelekwa unakotaka bila ya kuhitaji kulipa chochote zaidi ya unacholipa kuweza kutuma e-mail. Lakini tatizo la huduma ya bure ya email-to-fax, ni kuwa kwa njia hii huwezi kupeleka fax popote tu unapotaka. Kuna miji maalum ambayo unaweza kupeleka fax bure kwa njia ya e-mail. Endelea kusoma makala hii uone ni miji gani unayoweza kupeleka fax bure kwa njia ya e-mail. Makampuni yanayotoa huduma ya email-to-fax ya kulipia yapo mengi sana duniani na mengi yao yapo Marekani. Ili kuweza kupata huduma za makampuni hayo inakupasa kuwapelekea pesa kwanza kwa njia ya hundi (money order), yaani unalipa kwanza kabla ya kupata huduma. Ukishalipa, kila unapopeleka fax kwa kutumia mitambo yao (email-to-fax gateways), wanakata malipo kutoka kwenye pesa ulizozilipa na wanakujuilisha kwa njia ya e-mail ni kiasi gani cha fedha zako zilizobaki. Unaweza pia kutumia credit card kama Visa na Master Card. Uzuri wa makampuni yanayotoa huduma za kulipia za email-to-fax ni kuwa yanaweza kupeleka fax yako nchi yoyote ile duniani na gharama zake si kubwa hata kidogo ukilinganisha na gharama za kutuma fax moja kwa moja kutoka Tanzania. Kwa mfano, kutuma ukurasa mmoja wa fax kwenda Marekani, unaweza kukugharimu US$0.20 (yaani senti ishirini tu za Marekani), ambayo ni kama TSh. 140! Linganisha gharama hiyo na zaidi ya US$3.00 (TSh. 2,000) utakayolipa kwa kutuma fax Marekani kwa njia ya kawaida kutoka Tanzania! Katika makala hii, tutaelezea kwa urefu huduma ya bure ya kutuma fax kwa njia ya e-mail. Inshaallah, huduma ya kulipia tutaielezea kwenye makala zijazo. Kuna mashirika, jumuiya, na watu binafsi wengi wanaotoa huduma za bure za email-to-fax. Iliyo maarufu zaidi na yenye ufanisi mkubwa sana ni ile inayoitwa The Phone Company’s Remote Printing Service au kwa kifupi TPC. Makala hii itakita kuelezea namna ya kupata huduma ya email-to-fax kutoka TPC. Unaweza kuangalia maelezo ya huduma hiyo kutoka kwenye ukurasa wake wa web wenye anuani: http://www.tpc.int/TPC.INT, kama inavyopendelewa kuitwa, inakupa njia mbili za kuweza kutuma fax kwa kupitia Internet. Njia ya kwanza ni kwa kutumia web. Ukiingia kwenye ukurasa uliotajwa hapo juu unaweza kuchagua "mirror site" ya TPC.INT (yaani ukurasa wa web ulio mahali tafauti lakini wenye mambo sawa kabisa na ukurasa wa TPC.INT) iliyo karibu nawe. Ukishaingia kwenye hiyo mirror site, chagua sehemu ya kutuma fax yaani kwa kubonyeza picha yenye maandishi "Send A Fax" ambayo mara nyingi huwa juu kabisa ya ukurasa huo. Kwa mfano, kwa kutumia mirror site iliyo kwenye chuo kikuu chaToronto (University of Toronto), kilicho Toronto, Canada, fomu ya kutuma fax inapatikana kwenye anuani ya web (URL) ifuatayo: http://madhaus.cns.utoronto.ca/tpc/sendfax.html Sehemu muhimu za kujaza kwenye fomu hiyo ni jina la unayempelekea fax ambalo unaliandika kwenye kisanduku chenye maandishi "To (Recipient Name)", nambari ya fax ambayo unaiandika kwenye kisanduku chenye maandishi "The FAX Number", na anuani yako ya e-mail ambayo unaiandika kwenye kisanduku chenye maandishi "Your Email address". Nambari ya fax unatakiwa kuiandika katika mfumo ufuatao: +CountryCode-AreaCode-FaxNumber. Kwa mfano kupeleka fax kwendaToronto, Canada, kwa mtu mwenye fax yenye nambari 123-4567, nambari yake utaiandika: +1-416-123-4567 ambayo inaonyesha "1" ni Country Code ya North America (Marekani na Canada), "416" ni "Area Code" ya Toronto, na nambari ya fax yenyewe ni 123-4567. Kwenye sanduku lililo chini ya maandishi "The body of the fax, as you wish it to appear:", utaandika ujumbe unaotaka kupelekwa kwa fax. Ukishamaliza kuandika, bonyeza kifungo chenye maandishi "Fax it!" kilicho chini ya fomu hiyo. Ukibonyeza tu, fax yako itapelekwa ulikosema ipelekwe. Kwa majaribio niliyoyafanya, hata dakika moja haifiki kabla ya fax kupelekwa kwenye mashine ya fax ya mtu uliyempelekea. Taarifa ya e-mail inatumwa kwako kujuilishwa kama fax yako imepelekwa bila ya matatizo yoyote au kama imeshindikana kupelekwa kwa sababu zozote zile, pia utajuilishwa. Njia ya pili, na maarufu zaidi ya kutuma fax kupitia kwenye mitambo ya TPC.INT ni kwa kutumia e-mail. Kwa mfano, ukitaka kumpelekea fax rafiki yako Akili Mali aliye London, Uingereza (Country Code "44"), kwenye eneo lenye Area Code "181", na mwenyewe nambari yake ya fax ni 123-4567, utatumia programu yako ya kawaida ya kupelekea e-mail, kwa mfano Eudora, Netscape Mail, Microsoft Outlook, n.k, kupeleka ujumbe wako kwenda kwenye anuani ya e-mail ifuatayo: remote-printer.Akili_Mali@441811234567.iddd.tpc.int Ujumbe wako ukipokelewa tu na TPC.INT fax itapelekwa London dakika hiyo hiyo! Ukitaka kutuma fax kwenda sehemu nyengine, sehemu inayobadilika kwenye anuani iliyotolewa mfano hapo juu ni "Akili_Mali@441811234567". Kwa mfano, ukipeleka ujumbe kwenda: remote-printer@14161234567.iddd.tpc.int fax itapelekwa Toronto sawa kabisa na mfano tuliouleza hapo juu wa kutuma fax kwa kutumia njia ya web. Kwa mfano huu, jina la anayetumiwa fax halikuandikwa kabisa - na hiyo ni sawa kabisa. Jina la mtumiwa fax unaweza pia kuliandika kwa mfano, Pandu_Kiboko/Room_347 ambalo litaandikwa kwenye "fax cover" (yaani ukurasa wa kwanza wa fax yako) kama ifuatavyo: Pandu Kiboko Room 347. Utaona hapo kila alama "_" (yaani "underscore") hutafsiriwa kuwa nafasi tupu (space), na kila alama "/" hutafsiriwa kuwa maandishi yaendelee kwenye mstari mpya (new line). Kama nilivyosema kabla, TPC.INT inakuruhusu kupeleka fax bure kwenye baadhi ya sehemu tu ingawa ni nyingi sana. Orodha ya sehemu unazoweza kupeleka fax bure kwa kupitia mitambo ya TPC.INT inapatikana kwenye anuani ya web ifuatayo: http://madhaus.cns.utoronto.ca/tpc/fax_cover_auto.html Kati ya hizo, kwa bahati mbaya Tanzania haimo, lakini miji maarufu iliyo kwenye orodha hiyo ni pamoja na: +1-202 Washington D.C., USA +1-212 Manhattan, USA +1-281 Houston, USA +1-312 Chicago, USA +1-403 Calgary, Canada +1-416 Toronto, Canada +1-613 Ottawa, Canada +1-630 Chicago, USA +1-646 Manhattan +1-800 Toll Free (USA & Canada) +1-888 Toll Free (USA & Canada) +1-902 Nova Scotia, Canada +1-917 New York Cityi, USA +267 Botswana (nchi nzima) +27-31 Durban, South Africa +30-1 Athens, Greece +31 The Netherlands (nchi nzima) +39-50 Pisa, Italy +44 United Kingdom (nchi nzima) +46 Sweden (nchi nzima) +49-2 Germany +49-7 Germany +61-293 Sydney, Australia +62-31 Surabaya, Sidoarjo, Gresik (yote) +65 Singapore (nchi nzima) +852 Hong Kong (nchi nzima) +86-10 Beijing, China +886-2 Taipei, Taiwan +90-212 Istanbul, Turkey +91-11 Delhi, India +91-22 Mumbai (Bombay), India (fax inapelekwa usiku) +91-44 Madras, India +94 Sri Lanka (nchi nzima) +961 Lebanon (nchi nzima) Kila baada ya muda, orodha hiyo inapungua baadhi ya miji na kuongezeka miji mengine zaidi. Ni vyema kuiangalia kabla hujahangaika kutuma fax. Huduma za TPC.INT zinapatikana kwa ushirikiano wa vikundi na watu mbali mbali. Kuna baadhi ya wanaotoa huduma za bure za email-to-fax ambao hawajajumuika bado na TPC.INT. Ukitafuta kwenye web maneno "email-to-fax" bila shaka utapata taarifa nyingi kuhusiana na huduma hiyo muhimu. Nilifanya utafiti kidogo na nikaona kuwa unaweza kutuma fax Kuwait (ambayo haimo kwenye orodha iliyotolewa hapo juu) bila malipo kwa njia ya e-mail kama utapeleka ujumbe wa e-mail kwenda kwenye anuani: fax@kuwait.net na kichwa (Subject) cha ujumbe wako kiwe na nambari ya fax yenyewe tu bila ya kuweka Country Code, Area Code, nafasi (spaces) au herufi nyengine zozote. Maelezo tuliyoyaeleza hapo juu yatakuwezesha kutuma fax
kwa njia ya e-mail lakini ujumbe wako wa e-mail uwe na matini (text) tu,
yaani hutaweza kutuma picha. Kwenye makala ijayo, inshaallah tutazungumzia
namna ya kutuma fax yenye picha kupitia mitambo hiyo hiyo ya TPC.INT.
|
YALIYOMO
Tahariri
Waislamu wataka serikali iwajibike Serikali yakiri kupokea malalamiko ya Waislamu: Mkapa awataka Watanzania waepuke kubaguana Mtambani wasema kamwe hawakubali pumbao la kisiasa Maoni: Kweli ikisimama uongo hujitenga MARADHI YA KISAIKOLOJIA: TRANSVESTISM Risala ya Waislamu katika Baraza la Idd kwa Mgeni Rasmi Rais Benjamin Mkapa Wafanyakazi TANESCO waingiwa hofu ya wingu la udini Hotuba ya Rais Mkapa kwenye Baraza la Idd Diamond Jubilee Jan. 19, 1999 Makala: Hotuba ya Mkapa, Magazeti
ya Ruzuku na Waislamu
Kutoka magazeti ya zamani: Washitakiwa walipelelezwa Hivi siku ya ibada ni ipi?: Ijumaa,
Jumamosi au Jumapili?
'Msitarajie kupambana na adui kwa upanga wa Hamza' Sasa ni kulishwa nguruwe kwa nguvu Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|