AN-NUUR
Na.185 Shawwal 1419, Januari 22 - 28, 1998
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
‘Msitarajie kupambana na adui kwa upanga wa Hamza’

Wito umetolewa kwa Waislamu nchini kujiimarisha kiuchumi kupitia "NGOs" zao na kwa mtu mmoja mmoja. 

Agizo hilo lilitolewa kwenye Baraza la Idd, lililoandaliwa na taasisi ya Jamaatul Kheir katika ukumbi wa Hoteli ya Kola Prieto mnamo Idd mosi. 

Mzungumzaji mkuu katika baraza hilo alikuwa Sheikh Mohamed Harir wa Maawal-Islam ya mjini hapa. 

Alisema, matatizo ya Waislamu mijini na vijijini ni makubwa na utatuzi wake ni mzito. Aliongeza kwa kusema hilo linachangiwa zaidi kwa kutokuwepo na waliyul Amr. 

Aliongeza kusema kuwa na kweli tumehimizwa kufanya Dawa, lakini kwa hali ilivyo kazi hiyo haiwezi kufanyika kwa vizuri na juhudi za mtu mmoja mmoja Sheikh Mohamed alihimiza Waislamu kuanzisha NGO’s zao katika nyanja mbali mbali ili ziwe nuru ya kujiletea maendeleo. 

"Waislamu tukiwa na nguvu za kichumi ndipo tutakapoingia vyema karne ijayo ya Sayansi na teknolojia," alisema. Na kwamba Waislamu kwa sasa wasitarajie kupambana na adui zao vita itakapozuka kwa kutumia panga za Sayyidna Hamza. 

Misaada kutoka kwa wahisani kuna hatari ya kutokupatikana siku zijazo kutokana na mienendo mibaya ya kiuchumi duniani ndiyo maana Ulaya kwa hofu hizo imejiundia umojwa EURO. 

Aliendelea kwa kuwataka Waislamu walenge vile vile katika kutatua matatizo mbali mbali ya vijana wetu. Kwani wakati kuna vikundi vinavyoanzishwa kwenye miji yetu vyenye malengo na "programu" zisizokubalika na dini yetu, bado Waislamu hawaonekani kulitafakari jambo hilo. Alitoa methali isemayo "Mtoto ukimnyang’anya kisu ni lazima umpe banzi", yenye maana vijana wa Kiislamu wakikatazwa kwenda huko ni lazima waonyeshwe pengine ya kwenda. 

Hata hivyo Sauala la kuanzishwa NGO’s lilipata upokezi tofauti miongoni mwa masheikh walipata fursa ya kuchangia. Mmoja alitaka utatuzi wa matatizo yetu ufuate utaratibu uliokwishakupangwa na Mwenyezi Mungu; wa Zaka. 

Mchangiaji mwingine alikumbusha kwamba taasisi zilizopo hivi sasa tayari ni NGO’s mfano TAMTA, ZAHRAU, MAAWAL n.k., linalotakiwa muhimu ni kubadili mielekeo tu; kuondokana na sura ya kuziendesha kifamilia familia. 

Sheikh Hussein Abdalla, kwa upande wake, alisema suluhisho la matatizo yote litapatikana kwa kuongeza Da’awa. "Si rahisi kufikia hatua za maendeleo ya kisayansi kama ya Marekani kwa kuanza mwanzo. Muhimu ni kuwalingania wao na kuwafanya Waislamu, baada ya hapo na tangu hapo kila kitu kitakuwa chetu" alisema Sheikh Hussein. 

Hivyo alitoa wito kwa Jamatul Kheir kuendeleza mialiko ya namna ya baraza, kwa wafanya biashara, wasomi, wakulima na wengineo ili kuwapa ulinganio kufuatana na fani zao.



Sasa ni kulishwa nguruwe kwa nguvu


WAKAZI na waumini wa dini ya Kiislamu waishio Mbezi Luis wamewashitaki wafanyabiashara wawili kwa serikali ya Mitaa ya eneo lao kutokana na wafanyabiashara hao kufanya shughuli za uuzaji wa nyama ya nguruwe katika mazingira yanayoweza kuwalisha wakazi na waumini hao. 

Wafanyabiashara waliolalamikiwa kwa uongozi wa serikali ya Mtaa ya Mbezi Luis nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ni Bw. Silvester Kimario anayeendesha biashara ya mishikaki na supu ya nyama ya nguruwe kando ya shule ya msingi ya Mbezi na karibu na kituo cha basi cha Mbezi Luis ambapo inahisiwa wageni na wanafunzi wa Kiislamu wasomao katika shule hiyo hulishwa nguruwe bila kujua. 

Mwingine ni mfanyabiashara aliyejulikana kwa jina moja tu la Bw. Kanga ambaye anafuga ng’ombe na nguruwe na anaendesha utengenezaji wa mikate ndani ya maeneo yatumiwayo kwa ufugaji wa wanyama hao na inadaiwa kuwa watumishi wachungao na kuhudumia nguruwe ndio wenye kutengeneza na kuandaa mikate, hali inayotishia wakazi na waumini wa dini ya Kiislamu kulishwa nguruwe bila kufahamu walapo mikate hiyo. 

Wakazi hao waliyatoa malalamiko yao kwa uongozi wa serikali ya mtaa kwa kuwaandkia barua mapema Desemba 4 mwaka jana, lakini uongozi wa serikali hiyo ilipowaita wafanyabiashara hao, walipuuza na kuendelea kama kawaida. 

Katika barua hiyo ambayo Mwandishi wa habari hizi anayo nakala yake, iliandikwa na kamati ya Msikiti wa Ijumaa wa Mbezi Luis kata ya Kibamba, waumini wamewalalamikia wafanyabiashara hao licha ya kujua kuwa eneo hilo linakaliwa na watu wenye imani tofauti za kidini, lakini wamekuwa wakifanya kusudi kuuza nguruwe eneo la wazi shuleni bila kuweka tahadhari kwa watu wageni au wanafunzi watakaokuwa na hamu ya kula mishikaki au kunywa supu, ambayo ni ya nyama ya nguruwe. 

Pia walisema kuwa Bw. Kanga anayemiliki Bakery ambayo iko ndani ya nyumba yake na ambapo watumishi watayarishaji wa mikate ndio watumishi wa mabanda ya nguruwe, na kuna uwezekano wanunuao mikate hiyo hulishwa kutokana na hali halisi ilivyo na kwamba wameamua kutoa malalamiko hayo kwa uongozi wa serikali kabla ya kuchukua hatua nyingine zaidi. 

Mmoja wa wajumbe wa serikali ya mtaa wa eneo hilo, akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni, alisema ni kweli malalamiko hayo yamefikishwa kwao, lakini wafanyabiashara hao licha ya kuandikiwa barua ya kuitwa wamekuwa wakipuuza. 

Mjumbe huyo Bw. Juma Hamis alisema kuwa wafanyabiashara hao waliitwa kwenye kikao Desemba 18, mwaka jana, lakini hawakutokea na kwamba waliletewa watumishi tu badala ya wahusika. 

Aliongeza kuwa malalamiko hayo ni kweli kutokana na kwamba Bw. Kimaro anayemiliki pia baa bubu, aliyemuweka muuzaji anayejulikana kwa jina la Chale, amekuwa akiuza supu na mishikaki kando ya shule na kuwezesha wanafunzi kuila wanapokuwa wanahitaji bila kujua kutokana na kutowekwa tahadhari yoyote kutahadharisha kuwa nyama ile ni ya nguruwe. 

Pia juu ya Bw. Kanga, aliyehamia maeneo hayo siku nyingi, anatengeneza mikate ambayo huliwa na watu mbalimbali, wakiwemo Waislamu na wasiokuwa Waislamu, lakini katika mazingira ya kulishana nguruwe. 

Uchunguzi wa mwandishi wa habari hizi uliweza kufika hadi sehemu ya kuuziwa supu hiyo na kukuta hakuna kibao chochote zaidi ya kimoja kilichoandikwa barabarani, kando ya baa yenye jina la Quench Garden kwa maandishi ya "Kiti Moto" na kuweza kung’amua kuwa nyumba itumiwayo kwa biashara ya baa na uuzwaji wa supu hiyo ni ya Dk. Endrew. 

Mkazi mmoja wa maeneo hayo na mkazi wa nyumba hiyo ya Dk. Andrew aliyejitambulisha kwa moja moja la Kiraka, alisema kuwa watu wengi walio wageni maeneo hayo huuziwa na kula supu au mishikaki ya nguruwe na pia wao wenyewe wanashindwa kujua kama uongozi wa kata hiyo umeshindwa kuwadhibiti wafanyabiashara hao. 

Mwenyekiti wa Mtaa, Bw. Sultani Shomari hakuweza kupatikana kuelezea juu ya tatizo hilo, lakini mjumbe mmoja Juma Hamisi alisema kuwa hali hiyo ya kiburi cha wafanyabiashara hao katika kuitikia wito inaweza kujenga uhasama kati wa wakazi na waumini dhidi ya wafanyabiashara hao kutokana na kuonekana kuingilia imani za kidini na kufanyiana hila zinazoweza kuleta ugomvi au kuhatarisha amani. 

Mjumbe huyo alieleza kuwa iwapo watashindwa kufika wafanyabiashara hao ofisini hapo, basi wao watawapa kibali waumini wa Kiislamu na kamati ya Msikiti wa Ijumaa chini ya Imamu wao Rajabu Kondo kulifikisha tatizo hilo mbele zaidi ili kulipatia ufumbuzi wa kudumu.
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Fundisho toka Mtambani

Waislamu wataka serikali iwajibike

Serikali yakiri kupokea malalamiko ya Waislamu: Mkapa awataka Watanzania waepuke kubaguana

Mtambani wasema kamwe hawakubali pumbao la kisiasa

Maoni: Kweli ikisimama uongo hujitenga

MARADHI YA KISAIKOLOJIA:  TRANSVESTISM

Mjue Usama bin Ladin

Risala ya Waislamu katika Baraza la Idd  kwa Mgeni Rasmi Rais  Benjamin Mkapa

Wafanyakazi TANESCO waingiwa hofu ya wingu la udini

Hotuba ya Rais Mkapa kwenye Baraza la Idd Diamond Jubilee Jan. 19, 1999

Makala: Hotuba ya Mkapa, Magazeti ya Ruzuku na Waislamu
Na J. Hussein

Kutoka magazeti ya zamani: Washitakiwa walipelelezwa

Hivi siku ya ibada ni ipi?: Ijumaa, Jumamosi au Jumapili?
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu

'Msitarajie kupambana na adui kwa upanga wa Hamza'

Sasa ni kulishwa nguruwe kwa nguvu

Sayansi na Teknolojia
[KUPELEKA  FAX NCHI ZA NG'AMBO BURE!]

Masomo ya Dini ya Kiislamu

Barua za Wasomaji

Mashairi

Chakula na lishe
[Faida na  hasara za kupika chakula]
  


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org

 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita