|
Na.185 Shawwal 1419, Januari 22 - 28, 1998 |
|
Ijumaa, Jumamosi au Jumapili?
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu
MIONGONI mwa maswali yanayoleta utata mkubwa kwa maelfu ya watu duniani ni hili. Hata limegawa watu katika makundi makubwa matatu ya ibada. Wanaofanya ibada zao rasmi siku ya Ijumaa, wanaofanya ibada siku ya Jumamosi na wale wanaofanya hivyo siku ya Jumapili, hivi kweli Mungu hakutufunulia wazi jambo hili? Kwa makala hii fuatana nami ili kupata hatima ya swali hili. BIBLIA katika kitabu cha Waefeso 4:5-6 inasema: "Bwana mmoja, Imani moja, ubatizo mmoja, Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na ndani ya yote". Kama maandiko yanavyosema kwamba Mungu ni mmoja, imani ni moja, ubatizo ni mmoja, lazima siku ya ibada iwe ni moja. Hivyo, yatupasa tuelewe wazi kwamba kuna mahali tumefanya makosa, maana haiwezekani Mungu huyu mmoja atuwekee siku mbalimbali za ibada kiasi hiki, na kutufanya tuchanganyikiwe na kujiuliza ipi ni ipi. Ukweli ni kwamba Mungu tunamsingizia bure, maana Yeye ameweka wazi kila jambo linalohusu wokovu wa maisha yetu, wenye shida ni sisi wenyewe. Na ili tuweze kujua siku halisi ya ibada hatuna budi kujua mpango wa Mungu wa uumbaji na kwamba Mungu aliumba mbingu na nchi na vyote vilivyomo kwa muda wa siku sita ya saba akapumzika, akaacha kufanya kazi zake zote alizoumba na kufanya. Mwanzo 2:1-4. Tunaweza kuona jedwali la uumbaji kwa kifupi kama ifuatavyo:
Mungu alifanya kazi ya uumbaji kwa siku sita, na siku ya saba Mungu aliacha kufanya kazi yake akastarehe, akaibariki na kuitaka kwa ajili ya ibada. Huo ndio mpango wa Mungu. Swali la kujiuliza, ikiwa Mungu alitenga siku moja tu katika juma kwa ajili ya ibada. Mbona sisi binadamu leo tunazo siku tatu za ibada kwa juma, tumepata wapi? Hosea 4:6: " Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa, kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi, kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako. Mimi nami nitawasahau watoto wako". Mungu analia juu ya watu wake kwamba, wanaangamia kwa sababu ya kukosa maarifa, na si kwamba maarifa hayapo, bali wameyakataa na hii ndiyo hatari kubwa kuliko zote. Biblia iko wazi na kila jambo limewekwa wazi. Ili uelewe siku ya ibada ni ipi unahitajika pia ufahamu kwamba kwenye Biblia kuna siku tatu zimetajwa kwa majina, nazo ni siku ya maandalio, siku ya Sabato, na siku ya kwanza ya juma na hayo yameandikwa katika Luka 23:54 na Luka 24:1-6. Maelezo mengine ya siku hizi ni haya, siku ya maandalio ni siku ya Ijumaa. Siku ya Sabato ni siku ya Jumamosi, na siku ya kwanza ya juma ni siku ya Jumapili. Ufafanuzi huu pia unaweza kuupata katika Luka 23:53-56 na Luka 24:1-6 Agano Jipya Kiswahili cha kisasa. Siku ya kwanza ya juma ni siku ya Jumapili na ndiyo siku Mungu alianza kazi ya uumbaji Nuru na Giza, na akamaliza kazi yake siku ya Maandalio yaani siku ya Ijumaa siku aliyoumba binadamu. Na siku ya Sabato ambayo ni Jumamosi Mungu alistarehe akaibariki na kuitakasa kwa matumizi ya ibada. Hivyo, siku ya ibada ni siku ya Sabato ambayo ndiyo Jumamosi. Ndiyo maana Mungu amesisitiza sana siku hii katika amri yake ya nne Kutoka 20:8-11 kwa maneno haya: " Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku ya sitafanya kazi, utende mambo yako yote, lakini siku ya saba ni sabato ya Bwana Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliyendani ya malango yako. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba, kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya sabato akaitakasa". Hivyo ndivyo amri inayowaelekeza wanadamu wote katika siku ya ibada waikumbuke wasije wakaisahau maana iliwekwa mara tu baada ya uumbaji. Maelezo mengine ya siku ya ibada yamefafanuliwa na kifo cha Yesu pale msalabani. Kwamba Yesu alikufa kuzikwa siku ya Maandalio yaani Ijumaa. Na siku ya Sabato alistarehe kama ilivyoamriwa Luka 23:56 na siku ya kwanza ya juma yaani Jumapili Yesu alifufuka. Pia tumeambiwa tufanye ukumbusho wa kufa na kufufuka kwa Yesu katika ibada ya Pasaka (meza ya Bwana) 1Kor 11:24-26 na Luka 22:19-20. Hatuna andiko lolote ndani ya Biblia linalotuagiza tufanye ibada zetu siku ya Jumapili, hakuna, na haliwezi kuwepo maana Mungu wetu si kigeugeu. Kama wewe msomaji umeliona mahali tuambie hiki ni kipindi cha ukweli na uwazi, cha kufichana fichana maandiko kimepitwa na wakati. Hivyo, kufanya ibada kando au nje ya siku hiyo ni kuihujumu siku ya Bwana. Wapo watu wengine wanasema siku ni siku tu, haina ubaya wowote. Hayo ni maneno ya kujifariji tu ili kukwepa ukweli. Hebu nitoe mfano mdogo tu wa kidunia: Tarehe 9/12/1961 Taifa la Watanganyika lilijipatia uhuru wake, na kila mwaka tarehe ya mwezi Desemba tunasherehekea kukumbuka siku tuliyopata uhuru. Sasa atokee mtu fulani au kiongozi fulani mwenye uwezo wa kutangaza na atutangazie kwamba, sasa sherehe ya uhuru wa Tanganyika itakuwa tarehe 8/12 au tarehe 10/12 kila mwaka. Hatutamwelewa mtu huyo, sana sana anaweza akawa mgeni wa gereza la Keko ama Ukonga kama hakupelekwa Segerea! Maana anahujumu siku ya Uhuru wetu. Hata wenyewe wanaosherehekea siku ya kuzaliwa kwao hawachukui siku tu ili mradi siku, lazima siku yenyewe ifike. Sembuse siku ya Bwana! Hebu tumwangalie Yesu na Mitume wake walionyesha kielelezo gani juu ya siku ya ibada, Mathayo 5:17: "Msidhani ya kuwa nimekuja kuitangua Torati au Manabii, la, sikuja kutangua bali kutimiliza". Yesu anawaeleza wazi kwamba hakuja kubadili amri, na siku ya ibada ni amri ya nne ya Mungu, Kutoka 20:8-11 Yeye mwenyewe alikuwa anafanya ibada zake siku ya Sabato, Luka 4:16. Mitume nao walifanya ibada zao siku za/ya sabato, Matendo 17:2, Matendo 18:4. Yapo maandiko kadhaa yanayotumiwa vibaya na baadhi ya watu, mojawapo ni Marko 2:23-28 hata Yohana 5:8 Yesu na wanafunzi wake walikuwa wanapita njiani siku ya Sabato, wanafunzi wake wakavunja masuke. Mafarisayo wakamletea mashitaka Yesu kwamba, mbona wanafunzi wako wanafanya yasiyo halali siku ya Sabato? Kumbuka kwamba, hawa Mafarisayo, Masadukayo na Waandishi ndio waliokuwa wapinzani wakubwa wa Yesu. Hawa ni watu waliozijua sheria za Mungu ikiwemo ya Sabato, lakini kosa lao walikuwa wameingiza mila na desturi zao kwa mambo ya Mungu. Na juu ya Sabato waliiongezea "vikolombwezo" vingi wakaitia miiba, ikawa mzigo kwa watu kinyume na mapenzi ya Mungu. Yesu alipokuja aliliona hili na akachukua hatua mahususi za kuwasaidia. Kwanza alianza kwa kuwafundisha kwamba Sabato imeletwa kwa ajili ya wanadamu, si wanadamu ndiyo walioleta Sabato hapana, na yeye mwenyewe ndiye Bwana wa Sabato, ama kwa lugha nyingine Yesu ndiye Msabato namba moja, kumbuka pia kwamba wapinzani wa Yesu walikuwa wanamwinda Yesu wamkamate kwa makosa makubwa mawili, moja ni kwamba alikuwa anavunja amri za Mungu ikiwemo na Sabato, na pili alimwita Mungu Baba, yaani mwana wa Mungu akajilinganisha sawa na Mungu. Shutuma hizo ndizo zilizowafanya wakaendelea kumwinda na kumkosoa kwa kila alilotenda. Katika kuwasaidia aliwapa mifano wa swali hili, Je, ng’ombe wenu akitumbukia topeni ama shimoni siku ya Sabato mtafanyaje? Wote wakagwaya. Kawaambia ni heri kutenda mema (kuponya) siku ya Sabato kuliko kuua. Mafundisho yote hayo yalikuwa ya kuwasaidia watoe mila na desturi zao katika mambo ya Mungu. Pengine tuangalie kuhusu wenzetu wanaofanya ibada zao rasmi siku ya Ijumaa, Qur’an inasema nini juu ya Ijumaa (Qur’an 62:9-10) inasema: "Enyi mlioamini! Kukiadhiniwa kwa ajili ya swala ya Ijumaa, nendeni upesi kumtaja Mwenyezi Mungu na acheni biashara. Kufanya hivi ni bora kwenu, ikiwa mnajua (hivi basi fanyeni). Na itakapokwisha sala, tawanyikeni katika ardhi mkatafute fadhila za Mwenyezi Mungu, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi ( ili msipate kufanya mabaya), ili mpate kufaulu". Qur’an haikatazi mtu asifanye kazi siku ya Ijumaa, maana ni siku ya kazi. Na ndiyo siku Mungu alimaliza kazi yake ya Uumbaji kwa kumuumba mwanadamu. Na kuhusiana na siku ya sabato yaani Jumamosi (Qur’an 2:65-66) inasema hivi: "Na kwa yakini mmekwisha kujua (khabari za) wale walioasi miongoni mwenu katika (amri ya kuihishimu) Jumamosi. Basi tukawaambia kuweni manyani wadhalilifu. Kwa hiyo tukaifanya (adhabu hiyo) kuwa onyo kwa wale waliokuwa katika zama zao na waliokuja nyuma yao, na (tukaifanya ni) mauidha kwa wamchao Mwenyezi Mungu". Qur’an yaeleza kwamba wapo watu walipigwa laana kwa sababu ya kutoiheshimu siku ya Ibada - Jumamosi, na tena imefanywa mauidha kwa wamchao Mwenyezi Mungu. Binafsi sielewi ni kwa nini mambo mengi yamewekwa wazi kiasi hiki na watu wakaendelea kutenda kinyume cha maandiko. Bila shaka hii ni kazi ya sheitwani kupofusha watu wasione japo wanatazama. Mungu anatuhimiza na kusisitiza tuiheshimu siku ya Sabato kwa sababu kubwa zifuatazo: Sabato ni mali ya Mungu, aliianzisha Yeye mwenyewe mara tu baada ya uumbaji, hivyo haifungamani na mila ama desturi ya mtu au taifa lolote. Mungu Mwenyewe alistarehe, akaibariki na kuitakasa kisha kutuachia kielelezo. Kwa sababu imebarikiwa na kutakaswa, hivyo imewekwa Wakfu kwa matumizi ya ibada kumwabudu aliye mtakatifu na muumbaji. Hiyo ni amri yake ya nne Kutoka 20:8-11 inayomtofautisha Mungu na miungu ambayo haikuumba chochote. Hivyo tufanyapo ibada siku hiyo tunakumbuka uumbaji wa Mungu, na kwamba sisi pia ni viumbe tulioumbwa. Hiyo ni ishara ya Mungu na watu wake, Ezekieli 20:12, 20 "Tena naliwapa Sabato zangu ziwe ishara ya Mimi na wao, wapate kujua ya kuwa Mimi Bwana ndiye niwatakasaye. Zitakaseni Sabato zangu, nazo zitakuwa ishara kati ya Mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa Mimi ndimi Bwana Mungu wenu". Hilo ndilo jibu halisi la swali letu lenye utata mkubwa kwa maelfu ya watu duniani. Mpendwa msomaji, ninakukaribisha sana tumwabudu Mungu Muumba wa mbingu na nchi katika siku yake aliyoitenga baada ya uumbaji ili tusiwe ni miongoni mwa wenye hasara siku ya KIAMA. MJADALA uwazi juu ya dhana ya Mungu kufanya kazi akachoka akahitaji kupumzika. • Mhariri.
|
YALIYOMO
Tahariri
Waislamu wataka serikali iwajibike Serikali yakiri kupokea malalamiko ya Waislamu: Mkapa awataka Watanzania waepuke kubaguana Mtambani wasema kamwe hawakubali pumbao la kisiasa Maoni: Kweli ikisimama uongo hujitenga MARADHI YA KISAIKOLOJIA: TRANSVESTISM Risala ya Waislamu katika Baraza la Idd kwa Mgeni Rasmi Rais Benjamin Mkapa Wafanyakazi TANESCO waingiwa hofu ya wingu la udini Hotuba ya Rais Mkapa kwenye Baraza la Idd Diamond Jubilee Jan. 19, 1999 Makala: Hotuba ya Mkapa, Magazeti
ya Ruzuku na Waislamu
Kutoka magazeti ya zamani: Washitakiwa walipelelezwa Hivi siku ya ibada ni ipi?: Ijumaa,
Jumamosi au Jumapili?
'Msitarajie kupambana na adui kwa upanga wa Hamza' Sasa ni kulishwa nguruwe kwa nguvu Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|