|
Na.185 Shawwal 1419, Januari 22 - 28, 1998 |
|
Kweli ikisimama uongo hujitenga
Rasmi; madai ya Waislamu yapo mezani Daima Muislamu atasimama katika ukweli hata kama wengine wote wataukataa. Katika wajibu wake wa kidini imemwajibikia kukemea na kuondoa uovu wowote katika jamii. Katika hatua ya awali ni lazima autambue na auchukie uovu, hatua ya pili aukemee kwa ukali wake na ikiwa hapana budi atumie mikono yake (nguvu) kuondoa. Na hatua hiyo ndio kipimo cha imani na kufuzu kwake. Kuwepo uovu wowote katika jamii ikiwa ni pamoja na dhulma, uonevu na ubaguzi miongoni mwa watu katika jamii, lakini ikawa shwari; hakuna juhudi yoyote ya kuondoa uovu huo, ni ishara tosha kwamba jamii hiyo haina Waislamu. Kwa bahati mbaya ,Tanzania yetu imekuwa na historia mbaya ya kuwepo uovu unaotafsiriwa kwa sera (rasmi au zisizo rasmi) za kibaguzi, ukandamizaji, unyonyaji na upendeleo. Wakati wa ukoloni, sera hizi zilikuwa rasmi na Waislamu kama wajibu wao wa kidini wakapiga vita uovu huo hadi ukoloni ukang’oka. Dhulma ya mkoloni iliwagusa wananchi wote ndio maanaWatanzania wote walishiriki katika mapambano. Waislamu kama wajibu wao wa Kidini walishiriki kikamilifu katika vita hiyo wakitaraji usawa haki kwa wote baada ya uhuru kupatikana. Imekuwa bahati mbaya kwamba matarajio ya Waislamu hayakutimia Ubaguzi, uonevu na upendeleo ule ule ukajitokeza kwa sura na mbinu nyingine dhidi yao. Kwa wajibu ule ule wa kidini Waislamu wamekuwa wakiupiga vita uovu huo kwa kuuchukia, kuulalamikia na kuukemea, hatua ambayo bado inaonyesha kasoro katika imani zao kwani hawajafikia kilele cha kuonyesha chuki yao dhidi ya uovu. Kama bishara njema ya mustakbali mwema, Mh.Rais Benjamin William Mkapa ameungana na Waislamu katika kuisafisha jamii yetu. Kwanza, ameyapokea malalamiko na matatizo ya Waislamu na pili ameahidi kuyashughulikia. Hatuna budi tumshukuru Mh. Rais kwa hatua yake hiyo ya ujasiri. Katika historia ya nchi yetu, marais waliomtangulia walikuwa wakichukulia malalamiko ya Waislamu kama ni masuala nyeti yasiyofaa kuzungumzwa hadharani kama alivyofanya mheshimiwa Rais katika baraza la Idd, lililofanyika Januari 19, 1999 katika ukumbi wa Diamond Jubilee,Dar es Salaam. Na wakati mwingine, hata yalipozungumzwa yaligeuzwa mdahalo wa viziwi. Waislamu katika mabaraza yao wanailalamikia Serikali yao. Wao Serikalini wakisimama huwashutumu Waislamu wala hawagusi kabisa yale wanayodai Waislamu. Lakini kila mmoja (Waislamu na Serikali) anataka mwenzake amuelewe. Tuna imani kwamba huu ni mwanzo mzuri, ingawa baadhi ya wapinzani wanadai ni kumpeni za uchaguzi 2000. Hata kama ni kampeni basi tungewategemea wao walizungumze zaidi. Suala la Mwembechai lilipotokea, lilipokewa kwa jazba na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaamu, Polisi wakahamaki na kutumia nguvu za kuua, Waziri Mkuu naye akapongeza vitendo vya polisi kwa hamasa kubwa na hatimaye na CCM yenyewe ikapongeza. Tungetegemea wapinzani wachukue fursa hiyo kuonyesha dhulma hii ya Serikali dhidi ya wananchi. Lakini wapi kimya. Na ilipokuwa wapinzani hawakuifanya dhulma hiyo agenda Mh. Rais asingekuwa na sababu ya kuidaka kama jukwaa la kuingilia 2000. Ni kweli Waislamu wameuliwa katika kipindi chake na nchi inaserereka kuelekea kubaya. Na yeye kama kiongozi ana dhima kubwa. Hatuna budi kuamini kauli yake japokuwa imani hii itapata nguvu tu baada ya utekelezaji wa dhati na wa haraka. Kutokana na kushangazwa kwake na yale yaliyoelezwa katika risala aliyosomewa na kukabidhiwa inaelekea kuwa kwa muda mrefu Rais amekuwa hafikishiwi malalamiko mbalimbali ya Waislamu kuhusu madhila wanayotendewa katika nchi! Mheshimiwa Rais alifurahishwa kwamba kwa mara ya kwanza aliweza kupokea malalamiko ya Waislamu ambayo mengi kati ya hayo inaelekea hakuwa amefikishiwa kabla ingawa hotuba yake iliashiria kujibu baadhi ya malalamiko hayo. Inashangaza Kuwa kwa muda mrefu Waislamu wamekuwa wakitoa malalamiko yao na kuyafikisha serikalini lakini imeonekana kuna watendaji ambao hawakuwa wakiyafikisha kwa Rais. miongoni mwa malalamiko yaliyowahi kutolewa na Waislamu ni pamoja na upendeleo katika elimu, ajira na uwiano katika nafasi za madaraka. Aidha kumekuwa na unyanyasaji juu ya Waislamu katika masuala ya vazi la hijabu, swala ya Ijumaa, ufugaji ovyo wa nguruwe mashuleni na mitaani. Na hata katika uendeshaji na uamuzi wa kesi mahakamani. Mfano wa hivi karibuni ni kuhusu kesi za Mwembechai ambapo Waislamu wamekuwa wakicheleweshewa au kunyimwa dhamana, wakati ambapo Wakristo, akina Simbaulanga walipewa dhamana mara moja na hata kesi zao hazijulikani zilipoishia. Malalamiko haya yamewahi kutolewa na watu na jumuia mbalimbali kama vile Mufti Hassan bin Amir katika waraka wake wa mwaka1963, Warsha ya waandishi wa Kiislamu mwaka 1981, dokezo la Malima akiwa Waziri wa Elimu mwaka 1987, Waraka wa Baraza Kuu wa mwaka 1992, Barua ya Masheikh wa Dar es Salaam ya mwaka 1993 kuhusu mabucha ya nguruwe, kitabu cha Alhaji Aboud Jumbe aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa kwanza wa Rais cha mwaka 1994, Waraka wa Ponda wa mwaka 1998 na Waraka wa AbuAzizi (1998) kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao aliunakili ofisi ya Rais. Ni jambo la faraja kwamba hivi sasa hakutakuwa tena na urasimu wa vikwazo vya watendaji Serikalini kwani mheshimiwa Rais ameahidi kuacha milango wazi ya mawasiliano na kamati iliyowasilisha malalamiko katika baraza la Idd. Mheshimiwa Rais ameahidi pia kuyapeleka malalamiko hayo ya Waislamu kwenye baraza lake la Mawaziri kwa mashauriano na uchambuzi. Na ametoa changamoto kwa kamati yaWaislamu, nayo vile vile ifanye uchambuzi wa kina wa malalamiko yote ya Waislamu. Katika hilo kamati hii ina jukumu muhimu sana kwani inawezekana uchambuzi utakaofanywa na mabaraza la mawaziri usiwakilishe kikamilifu hisia za Waislamu, japo katika baraza hilo wapo Waislamu. Hii ni kwa sababu Waislamu walio katika baraza la mawaziri hawakuchaguliwa kuwakilisha Waislamu. Ni muhimu kamati hii kuzingatia kuwa kukubalika kwake na mheshimiwa Rais isijione kuwa ni taasisi pekee inayowakilisha fikra za Waislamu wote nchini. Ikifanya hivyo haitakuwa tofauti na Bakwata. Kama vile Bakwata iliundwa na Serikali (1968) bila ridhaa ya Waislamu, isije ikadhaniwa na hii nayo ni kamati ya Rais. ikifanya hivyo itakosa ridhaa ya Waislamu nchini. Mfano wa karibu ni kushindwa kamati hii kuwashawishi Waislamu wote na kuwepo kwa mabaraza matatu ya Iddi. Hali ya Waislamu waliokodisha magari kutoka mikoa mbalimbali ili kuhudhuria baraza la Idd Mtambani, na maelfu ya Waislamu wa Dar es Salaam waliohudhuria baraza hilo, ni dalili tosha kwamba kamati hii inahitaji ridhaa yaWaislamu wote nchini. Kilichofanya maelfu ya Waislamu kumiminika Mtambani ni matarajio yao ya kupata fursa ya kujadili na kuyatafutia ufumbuzi madhila wanayofanyiwa Waislamu hapa nchini ambayo kilele chake ni mauaji ya Mwembechai. Kwa kuwa kamati iliwasilisha kwa mheshimiwa Rais malalamiko ya baadhi ya madhila hayo ipo tamaa ya kamati hiyo kusikilizwa endapo itajitahidi kupata ridhaa ya Waislamu wote nchini, kama ilivyoridhiwa kamati ya Ponda. |
YALIYOMO
Tahariri
Waislamu wataka serikali iwajibike Serikali yakiri kupokea malalamiko ya Waislamu: Mkapa awataka Watanzania waepuke kubaguana Mtambani wasema kamwe hawakubali pumbao la kisiasa Maoni: Kweli ikisimama uongo hujitenga MARADHI YA KISAIKOLOJIA: TRANSVESTISM Risala ya Waislamu katika Baraza la Idd kwa Mgeni Rasmi Rais Benjamin Mkapa Wafanyakazi TANESCO waingiwa hofu ya wingu la udini Hotuba ya Rais Mkapa kwenye Baraza la Idd Diamond Jubilee Jan. 19, 1999 Makala: Hotuba ya Mkapa, Magazeti
ya Ruzuku na Waislamu
Kutoka magazeti ya zamani: Washitakiwa walipelelezwa Hivi siku ya ibada ni ipi?: Ijumaa,
Jumamosi au Jumapili?
'Msitarajie kupambana na adui kwa upanga wa Hamza' Sasa ni kulishwa nguruwe kwa nguvu Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|