AN-NUUR
Na.185 Shawwal 1419, Januari 22 - 28, 1998
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
Hotuba ya Rais Mkapa kwenye Baraza la Idd Diamond Jubilee Jan. 19, 1999


MHESHIMIWA Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania Sheikh Hemed bin Jumaa bin Hemed, Mheshimiwa Makamu wa Rais Dk. Omar Ali Juma, Waheshimiwa Masheikh Wakuu wa madhehebu mbalimbali, Mzee wetu Mkutufu Mzee Kawawa, Waheshimiwa Mawaziri, Waheshimiwa Mabalozi, ndugu Waislamu, Ndugu wananchi, mabibi na mabwana Assalam aleykum na Idd Mubaraka.

Mheshimiwa Mufti nilipokubali mwaliko wenu nilijua ninakuja kwenye shughuli ya furaha, sikujiandaa kupokea na kujibu masikitiko mazito kama haya niliyoyasikia. Hivyo mtanielewa kama sitajibu kila mojawapo ya masikitiko yaliyoorodheshwa, mengi yanahitaji uchambuzi na utafiti wa kina na kisayansi kabla ya kujibiwa, aidha kanuni za uongozi bora zinanitaka nishauriane kwanza na wenzangu serikalini. Lakini ninashukuru sana kwa vile mmekuwa wazi kwangu. 

Kama nimeyasikia vizuri masikitiko yenu makubwa ni haya yafuatayo: 

Kwanza, kwamba upo udini na upendeleo dhidi ya Waislamu katika baadhi ya vyombo vya dola na kwamba kuna watendaji serikalini ambao wanakwamisha mambo ya Kiislamu, hawajali hisia za Waislamu na wanawafanya Waislamu kama wageni au watu wa tabaka la pili. 

Pili, kwamba suala la Mwembechai bado halijatatuliwa. Tatu, suala la mahakama za Makadhi bado linazingatiwa. Nne, kwamba idadi ya Waislamu katika vyuo vikuu na maofisi ya serikali ni ndogo. Tano, kwamba idadi ya Waislamu ni kubwa katika jela na miongoni mwa wahalifu na wazururaji. 

Na sita, kwamba Tanzania inachelea kuboresha uhusiano wake na nchi za Kiislamu, hususan hatujajiunga na OIC na hivyo tunakosa misaada ya maendeleo kutoka katika taasisi zake kama vile Islamic Development Bank. 

Hayo mmesema ni baadhi tu ya masikitiko yenu, kama nilivyosema ni mazito, nimeipokea risala yenu na nitashauriana na wenzangu katika baraza la mawaziri hatimaye tutawasiliana nanyi tena. 

Lakini kwa leo napenda nisema mambo matatu tu: 

Kwanza, nimefurahi na nawapongeza sana kwa kuunda umoja wenu huu ambao natumaini sasa utakuwa ndiyo sauti ya kweli na ya pamoja ya Waislamu nchini. Ikiwa hivyo ndivyo itarahisisha sana mawasiliano na mazungumzo kati ya serikali na umma wa Waislamu nchini, ikiwemo kuhusu masikitiko yenu haya. 

Pili, serikali itayapa uzito unaostahili masikitiko yenu, hakuna hata moja litakalopuuzwa. Kila moja litafanyiwa utafiti na uchambuzi wa kina na ningependa nanyi vile vile katika umoja wenu myafanyie utafiti na uchambuzi wa kina zaidi ili tutakapokutana mazungumzo yetu yasiwe ya jazba bali ya kisayansi na uhakika yatakayotufikisha mahali pa kufanya maamuzi sahihi yanayozingatia ukweli, haki za msingi za Waislamu na wananchi wote kwa maslahi ya taifa, historia ya nchi yetu na uwezo wa serikali. 

Tatu, serikali yangu haipendi raia yeyote binafsi au kundi lolote la wananchi yakiwemo makundi ya dini na madhehebu ya dini wajihisi wanyonge au raia wa daraja la pili. Hiyo ni kinyume kabisa na itikadi, maadili na historia ya chama cha mapinduzi na serikali yake. Ndiyo mana nimeshukuru kuwa mmetoa dukuduku lenu katika siku hii ya furaha, huu ni mwanzo mzuri na hivi tutajiandaa vizuri kwa mazungumzo ya kina ili kupata chanzo halisi cha malalamiko yenu, ili kuondoa hisia zisizo na sababu na kushughulikia matatizo ya kweli pale ambapo yapo. 

Baada ya kusema hayo niruhusuni sasa nisema yale niliyokusudia na kujiandaa kuyasema siku ya leo. Leo ni siku ya furaha kubwa kwangu, kwa mara ya kwanza tangu nipewe heshima ya kuongoza taifa letu nimepata fursa ya kushiriki nanyi, furaha ya kumaliza salama mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Mmenipa pia heshima kubwa ya kuzungumza na jumuiya za Waislamu na wananchi wote kwa ujumla kupitia baraza hili la Idd. Nawashukuru sana kwa dhati kabisa kwa kunialika na kwa upendo mlionionyesha. Nimejisikia kuwa mimi na nyie kweli ni watu wana ndugu tukiunganishwa na upendo wa kweli na mashikamano ya Watanzania wote, umoja wa taifa letu na heshima uhuru na haki za kila raia, akhsanteni sana. 

Mheshimiwa Mufti, fursa hii hutokea mara moja kwa mwaka baada ya Waislamu wa ulimwengu mzima kutekeleza kwa unyenyekevu ibada ya saumu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ambayo ni nguzo ya nne ya Uislamu. Hivyo nawapongezeni sana Waislamu wote kwa kuiheshimu na kuitii amri hii ya Mwenyezi Mungu iliyoagizwa katika sura ya pili aya ya 183 hadi 185 ya Qur’an tukufu. 

Lakini amri ya kufunga saumu ipo katika dini zote kubwa duniani. Kilichotofautiana ni utaratibu tu wa kufunga. Kwenye dini zote lengo la saumu ni kuwafikisha waumini kwenye ucha Mungu; kuwaepusha na maasi na kuwaleta karibu zaidi na Mwenyezi Mungu. Ndiyo maana wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani Misikiti hujaa waumini wakiabudu na kuomba toba, wakivitiisha na kuviabudisha viungo vya miili yao, wakiwakumbuka walio na dhiki na kuwasaidia na kwa ujumla wakiwa raia wema. 

Maratajio yangu ni kuwa usafi wa nia, moyo na upendo uliojidhihirisha ndani ya jamii ya Waislamu wakati wa saumu utaendelezwa na utaigwa na waumni wa dini nyingine. Hiyo itasaidia kukuza umoja wa taifa, kukuza uchumi na kuboresha huduma za jamii nchini. Uadilifu huo pia ni silaha madhubuti katika mapambano yetu dhidi ya maovu na uhalifu na vile vile ni kichocheo cha maendeleo na udumishaji wa haki, umoja, usawa, amani na utulivu. 

Mheshimiwa Mufti, kipindi cha mwezi mkutufu wa Ramadhani mwaka huu kimeangukia wakati ambapo waumini wa dini ya Kikristo nao walikuwa katika sherehe za sikukuu ya Krismasi. Siku chache zilizopita nilikuwa ninasoma gazeti moja lililokuwa linaelezea matokeo ya hali hii kule Beirut Lebanon ambapo kama sisi hapa Tanzania wapo wananchi wengi Waislamu na wengi Wakristo. Mwandishi wa habari ile alisema kuwa tarehe 24 Desemba 1998 aliambiwa na Muislamu mmoja kuwa aliandaa kile mwenyewe alichokiita futari ya X-Mas. Habari hiyo ilinikumbusha hali ilivyo katika nchi yetu hali ambayo ilijengwa kwa makusudi na waasisi wa taifa hili bara na visiwani. 

Hali ya wananchi wote kuishi pamoja kwa upendo, kwa amani, kwa kushirikiana bila kujali au hata kuulizana dini zao au madhehebu ya dini zao. Watanzania wote wa dini na madhehebu ya dini zote lazima tuishi kwa amani na waumini wa dini nyingine na madhehebu mengine ya dini. Tuepuke pia shari zinazoletwa na mfarakano kati ya taasisi na makundi ndani ya dini moja au dhehebu la dini moja. Jukumu hilo si la dini moja au dhehebu moja pake yake, kila dini na kila dhehebu la dini lina wajibu sawasawa wa kuimarisha amani, utulivu na upendo nchini mwetu. 

Mazungumzo na majadiliano ndani ya dini au baina ya dini na ndani ya kundi la waumini au baina ya makundi ya dini na madhehebu ya dini lazima yafanyike kwa hekima na busara bila ya kubughudhi au kuwadhuru wengine. Mazungumzo na majadiliano hayo pia yaheshimu sheria za nchi yetu, pale yanapotokea matatizo ya waumini kuendesha dini zao zipo njia na taratibu zilizo wazi za kutatua matatizo yao kwa amani, kwa mfano sioni kwanini waumini wacha Mungu wavamie Makanisa, Misikiti au kuumizana. Mifano niliyoitoa ya bodi ya misamaha ya wahalifu (Parole Board) na mitihani ya kidato cha nne nadhani ni ishara ya kutosha ya nia njema ya serikali. 

Mheshimiwa Mufti, Tanzania ya leo na ya kesho ni ile ile waliyoasisi Mwalimu Nyerere na Mzee Abeid Karume. Ni wajibu wangu mzito wa kizazi hiki na uongozi wake wote wa serikali na wa dini kuhakikisha sifa nzuri za nchi hii zinahifadhiwa na kuendelezwa daima. Ninaamini hayo ndiyo matakwa ya wananchi walio wengi na hayo ndiyo mambo mema kwa nchi yetu, kwa wananchi wetu na kwa maendeleo yao. Mwenye imani, itikadi au vitendo vinavyokwenda kinyume na upendo, ushirikiano na umoja wa aina hiyo haitakii mema nchi hii iliyozoea amani na umoja wa kitaifa unaopigiwa mfano katika bara zima la Afrika. 

Tunaona fahari kuwa Watanzania, na ni wajibu wa kila mmoja wetu kuwa mzalendo wa kweli, na kuwa macho wakati wote dhidi ya mtu binafsi au taasisi ambayo dhahiri lengo lake kupanda mbegu ya chuki na kutokuaminiana au wa kupunguza upendo na mshikamano baina ya Watanzania kwa sababu yeyote ile. Maana athari za ugomvi kwa msingi wa dini ni mbaya zaidi kuliko athari za ugomvi wa ukabila ulioua malaki ya watu nchini Rwanda mwaka 1994. 

Kwa kila tufanyalo lenye uwezo wa kutukuza udini au kukuza tofauti na chuki za kidini tujiulize hatima yake kwa hisia za wenzetu wa dini nyingine na taifa letu. Maana madhara yake yatatuumiza sote wa dini zote waliokuewepo na wasiokuwepo. Ipo methali isemayo kisu kinachodhani kinaharibu ala ya zamani kinaharibu nyumba yake chenyewe. 

Tusije kwa hamaki tuharibu nyumba nzuri iliyojaa amani na upendo waliyotuachia wazee wetu. Tujenge umoja na heshima kati yetu kwenye macho ya dini na tujenge pia umoja na heshima kwa Watanzania wenzetu katika mambo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 

Akija kijana kumchumbia binti yako inaeleweka ukitaka kujua dini yake au anakotokea, lakini kwa mambo mengine hakuna haja yeye ni mtu anastahili heshima kwa utu wake yeye ni Mtanzania anastahili haki zote kamili kama Mtanznaia mwingine. 

Nchi yetu inaongozwa kwa misingi ya Katiba, sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kwa taratibu za demokrasia, haki na usawa vinatumika na ni lazima viendele kutumika bila upendeleo au ubaguzi katika kutekeleza matakwa ya Katiba, sheria, kanuni na taratibu. Huo ni msingi wa utawala bora na kudumisha amani katika nchi. Sisi katika serikali tutafanya kila tutakaloweza kuhakikisha utawala bora wa aina hiyo unakuwepo katika nchi yetu. Sheria mama ya nchi yetu yaani katiba, napenda kukumbusha tu inasema kuhusu haki za wananchi kwenye mambo ya kidini kifungu cha 19; kinasema ifuatavyo: " Kila mtu anastahiki kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake na bila kuathiri sheria zinazohusika za Jamhuri ya Muungano kazi ya kutangaza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje za shughuli za mamlaka ya nchi". Mwisho wa kunukuu. 

Tusema nini tena zaidi ya hapo. Maana mimi ninaongoza serikali ya chama cha Mapinduzi ambacho si tu wanachama wake wanaapa kwa kusema: Binadamu wote ni ndugu zangu bila kujali dini, jinsia n.k. Pia ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 iliyoniweka mimi katika uongozi katika kifungu cha 27 inanielekeza hivi: CCM itahakikisha kuwa tunakuwa na utawala bora kwa misingi ifuatayo: (i) "Kuona kwamba serikali wakati wote inaendeshwa kwa kuheshimu na kuzingatia utawala wa sheria yaani katiba ya nchi, sheria, kanuni na taratibu zetu zilizopo na ambazo zinaweza kutungwa ili kukidhi haja ya wakati uliopo". Mwisho wa kunukuu. 

Kwa sababu hiyo basi, sisi ni serikali inayoheshimu kwa dhati kabisa dini zote na madhehebu yote ya dini. Nafanya hivyo kama Rais na nafanya hivyo kama mtu binafsi. Tena ninao jamaa na marafiki wengi tu ambao ni Waislamu haijawahi hata siku moja tofauti zetu za dini zikawa sababu ya chuki wala chanzo cha ugomvi au mfarakano kati yetu, na siyo mimi tu, Watanzania wengi wanatoka katika familia kama hizo. Jambo hili ninaloliamini na kulifanya kama mtu binafsi nitahakikisha linafanyika pia katika ngazi ya taifa na ndani ya serikali. 

Katika kulinda amani na usalama wa raia na mali zao ili visihatarishwe, vyombo vya dola vitatumia tu kiasi cha nguvu kinacholingana na hatari iliyopo kwa amani na usalama. Maana tunataka tuongozwe kwa kuheshimu haki za msingi za binadamu, wala sitaki serikali yetu ipate ile sifa aliyoitaja zamani Jaji wa mahakama nchini Misri. Jaji huyo aitwaye Abu Yusufu aliyeishi karne ya tisa katika kitabu chake kiitwacho "Kitabul Akhlaq" alisema, na ninanukuu, "Watawala ni balaa ambalo kupitia kwao Mungu huwaadhibu wale anaotaka kuwaadhibu kwa hiyo mnapokutana na balaa hilo msiwe wenye hamaki wala hasira bali kwa utiii na uvumilivu". Mwisho wa kunukuu.

Serikali ya Tanzania haitaki kuonekana kama vile ni balaa bali kama chombo ambacho kinahakikisha haki inatendeka, usawa unadumishwa, heshima inajengwa, kila raia anaamini na kuabudu atakavyo, sheria za nchi zinafuatwa na amani inatunzwa kati ya makundi yote ya wananchi waliopo.

Miezi michache iliyopita nilialikwa kwenye shughuli mojawapo ya Wakristo wa madhehebu fulani, katika hadhara ile nilisema maneno ambayo ningependa niyarejee mbele yenu. Nilisema hivi, na ingawa siyo vizuri kujinukuu, hapa lazima nijinukuu. Nilisema hivi "Tumo katika kujenga taifa la demokrasia ya vyama vingi, lenye watu wa makabila mengi, dini na madhehebu ya dini mbalimbali. Tofauti zetu hizi ni utajiri wa aina yake, na zikitumiwa vizuri zinaweza kuwa chanzo cha nguvu ya umoja wetu. Lakini zikitumiwa vibaya tofauti hizo zinaweza kuleta mganwanyiko katika jamii, kudhoofisha nguvu na umoja wa Watanzania na kuhatarisha amani na utulivu wetu". Mwisho wa kunukuu.

Napenda kusisitiza jambo hili maana kama sote tunavyojua ni vigumu sana kujenga upendo, utaifa na mshikamano, ni mambo yaliyojengwa kwa makusudi na kwa miaka mingi, lakini vinaweza kubomolewa mara moja tukifumbia macho uchochezi wa aina yoyote ile. Mimi binafsi ninaamini kwamba Mwenyezi Mungu ni mmoja kwa sababu hiyo ninaamini sote tumeumbwa naye na anatujua kuliko tunavyomjua sisi wenyewe. Hivyo aliyemuumba mwanaume ndiye aliyemuumba mwanamke, aliyemuumba Msukuma ndiye aliyemuumba Mmakonde, na aliyemuumba Muislamu ndiye aliyemuumba Mkristo. Kwanini basi tutake kuhukumiana, kusutana au kujenga chuki. Kwanini tukiwa na akili zetu timamu tutafute shari isiyo na thawabu wala faida.

Mheshimiwa Mufti, Uislamu ni mojawapo ya dini kubwa sana na muhimu duniani, tangu enzi za Mtume imefanya mengi ya kumkomboa binadamu katika mambo ya imani, uonevu, ukandamizwaji na ubaguzi. Ninavyoelewa mimi neno Islamu lina maana ya kutii mapenzi ya Mwenyezi Mungu, kama hivyo ndivyo haitegemewi Muislamu akafanya yaliyo kinyume na mapenzi ya Mungu. Pia haitazamiwi kwa waumini wa kweli wa dini nyingine kufanya kinyume cha mapenzi ya Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu ni wa haki na usawa, wamwabuduo lazima wapende na kutenda haki na usawa. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa upendo, huruma na rehema, wamchao hawana budi kuongozwa na upendo, huruma na rehema. Mwenyezi Mungu ni mstahimilivu wa kupindukia na mwenye kusamehe. Sisi tunaomwamini lazima tuvumiliane na kusameheana.

Mheshimiwa Muft, serikali ya awamu ya tatu inawaheshimu sana, inawaamini na inawachukulia viongozi wote wa dini kuwa sehemu na nguzo muhimu ya safu za uongozi nchini na chimbuko la uadilifu katika jamii. Kauli na vitendo vyao kwa namna moja au nyingine vinagusa moja kwa moja fikra na mtazamo wa jamii yetu katika rika zote. Kwa hiyo ni wajibu usioepukika wa viongozi wa dini zote kushirikiana na serikali katika kulea jamii, katika kukemea na kusitisha maovu na uhalifu wote ndani ya jamii, ikiwemo rushwa, wizi, ubadhilifu n.k. 

Aidha, viongozi hao lazima waamrishe na kuhimiza yale yote yaliyo mema kama vile malezi bora kwa watoto na vijana wetu, amani, mshikamano na uadilifu katika ndoa na maisha, ukweli na uwazi. Viongozi wote tushirikiane basi pia katika kupiga vita mtindo wa maisha na mavazi ambayo yanakinzana na utamaduni wetu. Tuvane kwa stara na tuishi kwa adabu. Lazima pia tupigane na uvivu na uzembe mambo ambayo yanarejesha nyuma maendeleo yetu binafsi na ya taifa letu. Vijana kwa wazee lazima tupende na tufanye kazi ili kuboresha maisha yetu binafsi, ya familia zetu na yale ya jamii yetu.

Tuwahimize na kuwasaidia vijana wetu kuthamini mafunzo na kazi za mikono kwa kuzingatia sayansi na teknolojia stahiki, uvivu na uzururaji ni adui wa maendeleo na yote hayo yanapigwa vita na dini zetu zote. Viongozi wa dini wanayo nafasi ya pekee katika kupanua, kuimarisha na kuboresha elimu itolewayo katika shule na vyuo vyote hapa nchini. Nasema hivyo kwa sababu kwa mfano Waislamu wameamriwa kusoma na kujifundisha hata kama elimu hiyo inapatikana Uchina ambapo zama hizo haukuwepo Uislamu.

Amri hiyo inaashiria jinsi dini inavyothamini elimu katika kukidhi mahitaji ya duniani na ya akhera. Mwanafalsafa mmoja aliyeishi zamani sana aliwahi kusema kila mtu anahitaji vioo vitatu ili ajione alivyo kwa njia tatu tofauti. Kioo cha kwanza kitamwonyesha anavyojiona yeye mwenyewe, cha pili, kitamwonyesha jirani zake wanavyomuona. Na cha tatu kitamwonyesha anavyoweza kuwa akipenda na akiamua kubadilika.

Ningependa zaidi mngejiona kwa kioo cha tatu ili kubaini kile mnachoweza kuwa. Nchi yetu ni nchi ya haki sawa kwa wote, elimu kwa wote sawa, nafasi za uongozi kwa wote sawa bila ubaguzi wa rangi, dini, jinsia n.k. Kinachotakiwa ni maandalizi mazuri na hakuna maandalizi bora kuliko elimu.

Mheshimiwa Mufti Uslamu na Waislamu walifanya mengi kuikomboa nchi kutoka kwa makucha ya wakoloni na kujenga taifa huru la Tanzania. Nafasi hiyo ya kuendelea kujenga taifa hilo huru bado ipo na lazima ichukuliwe na Waislamu sambamba na wananchi wa imani nyingine. Kazi ya serikali ni kuchochea, kuhamasisha na kusaidia jitihada hizo, iwe katika kuelimisha vijana wa Kiislamu, katika kujenga na kutoa huduma za elimu na afya katika kushiriki sawa na wengine kuongoza nchi katika biashara na katika kujenga taifa kwa ujumla kwa faida ya Watanzania wote.

Vijana wa Kiislamu wana uwezo na haki sawa na wengine wa kwenda shule, wa kufanya vizuri kwenye masomo na kuandaliwa vizuri kuwa raia wema na viongozi wa taifa letu. Tuwaandae kwa kuwapa elimu nzuri na ya kutosha ili hatimaye waweze kuwa wanavyotaka kuwa na kujiendeleza kwa kadri ya uwezo wao. Mimi na serikali yangu tuko tayari kutoa kila msaada unaowezekana kutimiza lengo hili kama ambavyo nitakuwa tayari kumsaidia yeyote anayetaka kuchangia maendeleo ya elimu katika jumuiya mbalimbali.

Tajiri mmoja aliyekuwa karibu na kufa aliwaita vijana wake watatu akawaambia: Ningependa mali yangu isigawanywe bali yote irithiwe na mmoja wenu, hivyo nitawapeni kazi kuwapima nani kati yenu ana uwezo zaidi wa kusimamia kazi hii.

Kwenye ghala langu kuna vyumba vitatu vyote vikiwa na ukubwa sawa. Chukueni kila mmoja mfuko wa fedha. Nendeni kila mmoja akanunue anachoweza ili kujaza chumba chake. Kijana wa kwanza akatumia fedha zote kununua mchanga uliotosha kujaza theluthi moja ya chumba chake. Kijana wa pili akatumia fedha zake zote kununua udongo, akapata udongo uliojaza nusu ya chumba chake. Kijana wa tatu baada ya kutafakari kwa kina alitumia fedha kidogo sana kati ya fedha alizopewa na baba yake akanunua mishumaa na kiberiti akajaza chumba chake mwanga na hivyo kutimiza masharti yaliyomwezesha kurithishwa mali yote ya baba yake.

Ndugu Waislamu elimu ni mwanga na mwanga hufukuza kiga na kuangaza njia nyingi za kuboresha maisha ya aliyesoma na kumuwezesha kustahiki madaraka na uongozi. Na kama nilivyosema mimi na serikali yangu niko tayari kuhamasisha na kusaidia jitihada hizo nafurahi kusema kuwa katika miaka 25 iliyopita taasisi nyingi za Kiislamu zimejenga shule kadhaa za sekondari ili kuchangia maendeleo ya elimu kitaifa, nazipongeza juhudi hizo ingawa bado kuna haja ya kuongeza shule nyingine na vyuo zaidi pamoja na kuziboresha taasisi zilizokamilika.

Tusaidiane maana serikali peke yake haina uwezo wa kueneza huduma za jamii kama vile elimu, afya na maji kila pembe ya nchi hii kubwa, lakini inapotokea taasisi za Kiislamu kuweka mikakati ya kueneza huduma hizo bila shaka serikali itaunga mkono juhudi hizo na kuchangia ufanisi wake. Wafadhili wanaotusaidia kujenga Misikiti tuwaombe pia watusaidie kujenga shule, nguvu zao zikichanganywa na zetu. Ninawapeni changamoto ili msaidie kwa kiwango cha juu zaidi maendeleo ya nchi yetu na watu wake.

Mheshimiwa Mufti, katika nchi yetu Waislamu ni wafanyabiashara wazuri na hodari, nawaombeni basi mmoja mmoja au kupitia katika vyama, jumuiya na taasisi mchangie zaidi kukuza uchumi wa nchi kwa haraka zaidi, kwa mfano katika sekta za kilimo, uvuvi, madini na utalii. Wekeni mkazo unaostahili kwa sekta hizi.

Aidha, mkazo zaidi unahitajika katika kuboresha hali ya maisha ya wananchi walo masikini, naomba tuchangie jitihada za kuwapa nyenzo na uwezo wanaotaka kujiendeleza kwa jasho lao. Nawaomba mchukue hatua zipasazo na nawaahidi ushirikiano na msaada wa serikali.

Ningependa pia kuwakumbusha viongozi wetu wa dini zote na waumini wa dini zote, kwamba maradhi mabaya ya ukimwi yanamaliza watu wetu ambo jamii inawahitaji sana. Ipo haja na umuhimu wa kuwaelimisha waumini wetu wajiepushe na janga hili ambalo halina chanjo wala tiba.

Isaidieni serikali yenu kuwaokoa wale wananchi ambao hawaogopi maradhi haya msituachie serikali tukemee peke yetu, vita hivi si vya mtu mmoja au taasisi moja, tukishirikiana vizuri katika kampeni ya ukimwi bila shaka tutafanikiwa kuokoa maisha ya vijana na watu wengi. 

Kama nilivyoeleza katika risala yangu ya mwaka mpya nchi yetu hivi sasa imekumbwa na uhaba mkubwa wa chakula na katika mikoa mingine hali hiyo ni mbaya sana. Serikali imechukua hatua za dharura na pia imeomba msaada na ushirikiano wa jumuiya ya kimataifa, sekta binafsi na jumuiya za dini ndani ya nchi. 

Tutafanya lile lililo ndani ya uwezo wetu, lakini mengine ni ya Mwenyezi Mungu mwenyewe. Ni vyema basi sote tudumu katika kumwomba Mwenyezi Mungu atuepushe na baa la aina hii, atupe mvua za kiasi na kubariki kazi ya mikono yetu. Wakati serikali itajitahidi kukahikisha hakuna mwananchi atakaye kufa kwa njaa kwa kuwapatia wananchi chakula cha msaada, chakula kwa kazi na chakula kwa kununua. 

Kulingana na hali halisi ya eneo husika nawaomba viongozi wote wa dini wawaelimishe watu wetu jinsi ya kukabiliana na hali hiyo. Aidha naomba mashirika ya dini yenye mtandao wa kimataifa nayo yaombe msaada kimataifa utakaochangia kutunusuru na baa hili la njaa na hatimaye sote tushirikiane na kuhakikisha kuwa baada ya janga hili kila familia inajiwekea akiba ya chakula cha kutosha, hivyo kila kijiji, kata hadi taifa. 

Napenda kurejea tena pongezi zangu kwa kukamilisha kwa amani na salama saumu yenu, na mimi nipo nanyi katika kuisherehekea siku ya leo. Nataka kurudia tena niliyoyasema kwamba serikali yangu haipendi raia yeyote binafsi au kundi lolote la wananchi ikiwemo makundi ya dini na madhehebu ya dini wajihisi wanyonge au raia wa daraja la pili. Hivyo ni kinyume kabisa na itikadi, siasa, maadili na historia ya CCM na serikali yake. Narudia tena ndiyo maana nimeshukuru kuwa mmetoa dukuduku lenu katika siku hii ya furaha. Huu ni mwanzo mzuri na ninaahidi tutajiandaa vizuri katika mazungumzo ya kina ili kupata chanzo halisi cha malalamiko yenu ili kuondoa hisia zisizo na sababu kama zipo na kushughulikia matatizo ya kweli pale ambapo yapo. 

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza, Mungu ibariki Tanzania. Idd Mubaraka.
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Fundisho toka Mtambani

Waislamu wataka serikali iwajibike

Serikali yakiri kupokea malalamiko ya Waislamu: Mkapa awataka Watanzania waepuke kubaguana

Mtambani wasema kamwe hawakubali pumbao la kisiasa

Maoni: Kweli ikisimama uongo hujitenga

MARADHI YA KISAIKOLOJIA:  TRANSVESTISM

Mjue Usama bin Ladin

Risala ya Waislamu katika Baraza la Idd  kwa Mgeni Rasmi Rais  Benjamin Mkapa

Wafanyakazi TANESCO waingiwa hofu ya wingu la udini

Hotuba ya Rais Mkapa kwenye Baraza la Idd Diamond Jubilee Jan. 19, 1999

Makala: Hotuba ya Mkapa, Magazeti ya Ruzuku na Waislamu
Na J. Hussein

Kutoka magazeti ya zamani: Washitakiwa walipelelezwa

Hivi siku ya ibada ni ipi?: Ijumaa, Jumamosi au Jumapili?
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu

'Msitarajie kupambana na adui kwa upanga wa Hamza'

Sasa ni kulishwa nguruwe kwa nguvu

Sayansi na Teknolojia
[KUPELEKA  FAX NCHI ZA NG'AMBO BURE!]

Masomo ya Dini ya Kiislamu

Barua za Wasomaji

Mashairi

Chakula na lishe
[Faida na  hasara za kupika chakula]
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org

 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita