AN-NUUR
Na.185 Shawwal 1419, Januari 22 - 28, 1998
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
Risala ya Waislamu katika Baraza la Idd kwa Mgeni Rasmi Rais Benjamin Mkapa


Assalaam Alaykum na Idd Mubaraka. Kwa niaba ya kamati ya maandalizi ya baraza la Idd napenda kuwakaribisha wote waheshimiwa mliohudhuria hapa na wageni wetu katika hafla hii kwanza ya kujipongeza kwa kumaliza mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na pia kusherehekea sikukuu hii ya Idd-el-Fitri.

Kwa mara ya kwanza baraza hili la Idd limeandaliwa kwa pamoja kwa ushirikiano wa madhehebu na jumuiya mbalimbali za Kiislamu zikiwemo Bakwata, Bohora, Sunni,Ibadhi, Ismailia, Shia Ithnasheria, Dar es Salaam Islamic Club na Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi. Hii ni hatua moja kubwa ya kijumuia kwa Waislamu kwa kuonyesha ushirikiano na mshikamano wa pamoja na Inshaallah Mungu audumishe umoja huu.

Mgeni rasmi na viongozi wa dini mliokuwepo hapa napenda kuwatambulisha kwamba mbele yenu ni wawakilishi wa madhehebu na jumuiya mbalimbali za Kiislamu. Pia wamo wawakilishi wa misikiti na vyuo vya Kiislamu toka katika wilaya za mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

Tunawashukuru wote kwa kuhudhuria baraza hii leo. Kabla sijamkabidhi mwenzangu Alhaj Sheikh Suleiman Gorogosi kuendelea na ratiba ningependa kuwajulisha tu kwamba wakati sisi leo tunasherehekea hapa kuna bahati mbaya maafa kidogo yametokea katika msikiti wa Idrisa. Habari tulizozipokea ni kwamba kuna ukuta wa msikiti wa upande wa akina mama umeanguka na kwamba kuna akina mama karibu saba walioumia kuna mmoja amefariki kwa hiyo tumwombee dua huyo aliyefariki Mwenyezi Mungu ampeleke Peponi Amin. Na hao ambao wameumia waweze kupana haraka.

Kwa hiyo mpaka hapo hii niliyo soma siyo ndiyo spichi maalum hii ni utangulizi kuweza kuwajulisha wageni rasmi na kuwatambua viongozi waliokuwa hapa mbele yenu.

Audhubillah Minasheitwan Rajim. Bismillahir Rahmanir Rahiim. Alhamdulillah Rabil Alaminn Waswalatu Wasalaam Alaan Ashraful Mursaliim Waalaa Ahli Wasahbih Ajumayn.

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bwana Benjamin William Mkapa, Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaj Dk. Omar Ali Juma, Mheshimiwa Mzee wetu Alhaj Rashid Mfaume Kawawa,waheshimiwa Masheikh wetu wakuu, Maimamu, wazee wetu na viongozi mbalimbali, waheshimiwa Mawaziri na Wabunge, waheshimiwa Mabalozi, waheshimiwa wageni waalikwa, mabibi na mabwana Assalaam Aleykum Warahmatullah Wabarakatuh.

Siku ya Idd kwetu sisi Waislamu ni siku tukufu sana, Waislamu duniani kote wanaosherehekea kumalizika kwa funga ya Ramadhani, nachukua fursa hii kwa niaba ya Waislamu wote kuwapongeza Waislamu na kumuomba Mwenyezi Mungu (s.w.) akubali funga yetu Amin.

Pamoja na Idd Waislamu tuna mengine mengi ya kusherehekea wakati huu, kwanza tunasherehekea kuimarika kwa umoja wetu, viongozi wa Bakwata, Jumuiya za Bohora, Ibadhi, Ismailia, Shia Ithinashiri na Sunni wamekubali kuungana na kushirikiana kwa yale wanayokubaliana. Wamekubaliana kuwa na kamati ambayo ina mwakilishi kutoka kila madhehebu. Kamati hiyo sasa ndiyo itakayowakilisha Waislamu wa madhehebu tofauti. Ni nia yetu kuuendeleza umoja huu kwa ajili ya kuyakabili masuala mbalimbali yanayowaathiri Waislamu.

Kutokana na mshikamano huu, tarehe 8 Ramadhani waumini wa madhehebu mbalimbali tuliweza kukutana tukafuturu pamoja, pamoja na hata kuswali nyuma ya Imamu mmoja. Aidha Baraza la Idd mwaka huu limeandaliwa na kuhudhuriwa na waumini wa madhehebu zote. Imewezekana pia waheshimiwa, mimi kuteuliwa leo hii na kusimama hapa mbele yenu na kuyasema haya ninayoyasema kwa niaba ya Waislamu hao.

Mheshimiwa Rais; Waislamu pia tunasherehekea kuwa nawe katika hafla hii. Hii ni fursa ambayo hatuipati mara kwa mara. Na kama vile leo tumeipata ni vyema tuitumie kikamilifu kukueleza siyo tu ya furaha bali pia ya masikitiko. Matarajio yetu kwa Wakristo wema ni makubwa, kwao tunatarajia upendo kama Qur’an inavyosema katika sura ya tano (5) aya ya 82 kuwa walio karibu zaidi ya Waislamu kwa upendo ni Wakristo. 

Aidha, kwa uongozi mwema wa Kikristo tunatarajia uadilifu hata walipozidi kuteswa na washirikina wa Makkah Waislamu wa awali waliamrishwa na Bwana Mtume (s.a.w.) wakimbilie Abisinya ambako mtawala alikuwa Mkristo muadilifu.

Mheshimiwa Rais sisi tunaamini kwamba wewe ni Mkristo muadilifu, tunaziona na tunazitambua juhudi zako katika kuyasikiliza matatizo ya Waislamu na kuyafanyia kazi. Kwa mfano ulizivunja bodi za Parole pale ilipodhihiri kuwa hazikuwa na uwiano ulitoa picha sahihi ya jamii yetu. Tarehe za mitihani ya kidato cha nne zilibadilishwa ili zisiangukie siku ya Idd ingawa bado mitihani hiyo iliendelea kufanyika katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, lakini sisi tunaamini kwamba umeanza kuyatekeleza yale uliyoazimia kuyafanya na kwetu sisi tunaamini pia kwamba safari ya maili elfu moja siku zote huanza na hatua ya kwanza. Kwa hayo yote tunapenda kukushukuru na kukuombea kwa Mwenyezi Mungu (s.w.) azidi kukupa moyo wa ujasiri wa kuyakabili matatizo ya jamii yetu katika misingi ya usawa na haki.

Mheshimiwa Rais tunasema masuala haya umeyasikia na umeanza kuyatatua, huku tukikushukuru wewe kwa hayo bado kuna masuala ya msingi inabidi tujiulize na yapatiwe majibu. Bado kuna mengine mengi yenye sura hii hii ya upendeleo dhidi ya Waislamu ambayo bado hujayapatia uvumbuzi.

Kuna suala la Mwembechai ambalo liko mahakamani limechukua muda mrefu na bado halijatatuliwa. Waislamu bado wanaomba uchunguzi huru ufanyike na ukweli ujulikane na haki itendeke. Kadhia ya Mwembechai imechukuliwa nisuala la fujo za Waislamu wenye udini na siasa kali wanaotaka kuvuruga amani. Imedhihirika kwamba waliokamatwa katika kadhia ile hawakuwa Waislamu peke yao. 

Vile vile waliohujumiwa hawakuwa Wakristo kwani pale Mwembechai sote tunafahamu kuna Makanisa mawili ambayo hata moja halikuathiriwa wakati wa kadhia ile, hakuna hata jiwe moja lililotupwa katika Makanisa hayo, kwa hiyo hili siyo suala la udini wa Waislamu, lakini bado vyombo vya dola viliwalenga Waislamu na kuwaona ndiyo walioleta uchochezi kwa lengo la kuleta vurugu (ee samahani) wanaoleta uchochezi kwa lengo la kuvuruga amani.

Hatuelewi hii ni kwanini. Hii imepelekea kuwa na hisia katika jamii kwamba hiki ni kielelezo cha hitilafu iliyopo katika jamii katika kutafsiri sheria za msingi za nchi. Ili kuondoa hisia hizo hapana budi uchunguzi huru ufanywe, ukweli ujulikane, haki itendeke na pia ionekane kwamba inatendeka.

Aidha, Mheshimiwa Rais kuna suala la mahakama za Makadhi nalo bado linalaumiwa. Nchi jirani zenye Waislamu wachache kuliko Tanzania zina mahakama hizo. Tanzania Visiwani pia ziko. Hapa bara zilikuwepo zikaondolewa. Mpaka leo Waislamu hawajapewa sababu wala mantiki ya kuondolewa mahakama za makadhi. Tunataka ieleweke kwamba suala la mahakama za Makadhi ni sehemu isiyomegeka na masuala ya sheria za Kiislamu. Sheria za Kiislamu ni mwongozo, maamrisho na makatazo ambayo yanagusa maisha ya kila siku ya muumini wa Kiislamu kama yalivyo katika Qur’an na Sunnah za Bwana Mtume (s.a.w.). 

Zinatawala masuala ya kuratibu mwenendo, desturi, ndoa, mirathi, mavazi, utendaji kazi, uhusiano baina ya mtu na mtu, mahusiano ya kibiashara, majukumu kwa wazazi, viongozi na watawaliwa, mke, mume, watoto pamoja na jamii n.k. Kwa maneno mengine mfumo wa sheria za Kiislamu ni mfumo kamili wa maisha ya Waislamu. Kwa haya Muislamu hana hiyari. Tunaomba sheria za nchi zisipingane na maamrisho na makatazo ya sheria za Kiislamu kama zilivyo katika Qur’an na Sunnah za Mtume (s.a.w.).

Kuwepo mahakama za Makadhi pamoja na Makadhi waadilifu kutaisadia serikali kupata tafsiri sahihi ya masuala ya Waislamu. 

Mheshimiwa Rais kuna suala la idadi ya Waislamu katika mashule ya sekondari ya umma, pamoja na vyuo vikuu na maofisi mbalimbali za serikali kuwa ndogo na idadi yao katika majela na miongoni mwa wazururaji kuwa kubwa. 

Ni ukweli usiofichika kwamba vijana wetu wa Kiislamu hupata nafasi finyu katika kujiendeleza kielimu. Hatudhani kwamba vijana wa Kiislamu si waadilifu. Ni dhahiri kwamba mfumo wa kutahini, kuchuja na kuchagua wanafunzi kuendelea na elimu una kasoro za msingi na hivyo hauna budi kurekebishwa. Mtu anapokosa elimu uwezo wake kimaendeleo pia huwa mdogo. Uwezo wa kupata ajira unatoweka, na uwezekano wa kujiingiza katika wizi, uzururaji, ujambazi na uhalifu kwa ujumla huwa dhahiri. Wakulaumiwa katika hali kama hii siyo vijana au wahalifu hao ingawa wengine wana makosa, bali ni jamii.

Aidha, kutokana na sababu za kihistoria, nchi yetu imekuwa na uhusiano wa karibu zaidi na nchi ambazo si za Kiislamu. Hivyo basi wawekezaji wengi hutoka nchi hizo hasa taasisi za kidini wamepata uhuru na fursa za kuwekeza katika elimu na huduma nyingine za jamii bila ya bughudha wala kero. Walengwa wamekuwa waumini wa dini zao. 

Kwa upande mwingine wawekezaji wa kutoka nchi za Kiislamu wanapotaka kuwekeza katika huduma za jamii na hasa elimu, Waislamu wakiwa kama walengwa hukutana na vikwazo vingi, bughudha na kero, aghalabu wao huonekana kama ni wachochezi na wenye kutaka kuvunja amani. Tunachotaka Waislamu ni uhuru wa Waislamu wenzetu pamoja na sisi wenyewe wanaotaka kuwekeza katika fani hizo wapewe fursa hiyo bila bughudha wala vikwazo visivyo kuwa vya msingi.

Isitoshe, Mheshimiwa Rais nchi yetu bado inachelea kuboresha uhusiano wake na nchi za Kiislamu. Nchi jirani kama vile Kenya, Uganda, Msumbiji zenye Waislamu wachache ukilinganisha na Tanzania zimejiunga na Organization of Islamic Conference (OIC) Tanzania yenye Waislamu wengi bado haijajiunga bila ya kuwapo kwa sababu za msingi. Ni dhahiri kwamba ingejiunga ingestahili misaada mingi mbalimbali kutoka kwenye umoja huo na taasisi zake kama vile Islamic Development Bank. 

Mheshimiwa Rais kwa kuwa vile leo ni siku ya Idd si vyema kuendelea kulalamika na kusikitika. Malalamiko yetu ni mengi za hatuwezi kuyamaliza katika hafla hii. Leo ni siku ya furaha na ni siku ya kutembeleana na kupeana sikukuu. Sikukuu yetu kwako ni huu umoja wetu ambao lengo lake ni kuchangia katika harakati za kudumisha amani na kuleta maendeleo. 

Kutoka kwako tunaomba sikukuu yetu kwanza tunaiomba serikali itambue umoja huu na ishirikiane nao. Kuwe na mawasiliano ya karibu na ya kudumu juu ya masuala yanayohusu maendeleo ya nchi yetu na ya jamii. Kisha tunaiomba serikali ilete usawa na uadilifu kwa wananchi wa dini zote.

Mheshimiwa Rais tunakushuru sana kwa kuja kwako kuhudhuria Baraza hili la Idd tukiamini utayazingatia haya tuliyokueleza. Tunataka kukuhakikishia kwamba jamii ya Kiislamu itaendelea kuwa raia wema ili kuleta maendeleo na amani kwa Watanzania wote. Wazee wangu, ndugu zangu katika Uislamu; Assalaam Aleykum Warahamatullah Wabarakatuh.
 
 

Juu
 

YALIYOMO
  

Tahariri
Fundisho toka Mtambani

Waislamu wataka serikali iwajibike

Serikali yakiri kupokea malalamiko ya Waislamu: Mkapa awataka Watanzania waepuke kubaguana

Mtambani wasema kamwe hawakubali pumbao la kisiasa

Maoni: Kweli ikisimama uongo hujitenga

MARADHI YA KISAIKOLOJIA:  TRANSVESTISM

Mjue Usama bin Ladin

Risala ya Waislamu katika Baraza la Idd  kwa Mgeni Rasmi Rais  Benjamin Mkapa

Wafanyakazi TANESCO waingiwa hofu ya wingu la udini

Hotuba ya Rais Mkapa kwenye Baraza la Idd Diamond Jubilee Jan. 19, 1999

Makala: Hotuba ya Mkapa, Magazeti ya Ruzuku na Waislamu
Na J. Hussein

Kutoka magazeti ya zamani: Washitakiwa walipelelezwa

Hivi siku ya ibada ni ipi?: Ijumaa, Jumamosi au Jumapili?
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu

'Msitarajie kupambana na adui kwa upanga wa Hamza'

Sasa ni kulishwa nguruwe kwa nguvu

Sayansi na Teknolojia
[KUPELEKA  FAX NCHI ZA NG'AMBO BURE!]

Masomo ya Dini ya Kiislamu

Barua za Wasomaji

Mashairi

Chakula na lishe
[Faida na  hasara za kupika chakula]
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org

 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita