|
Na.185 Shawwal 1419, Januari 22 - 28, 1998 |
Wafanyakazi
TANESCO waingiwa hofu ya wingu la udini
Hofu hiyo inafuatia hatua ya shirika hilo kongwe nchini kutokutoa fungu la pesa sawa kwa Waislamu kusherehekea Sikukuu ya Idd mwaka huu kama lilivyotolewa kwa wafanyakazi wenzao Wakristo walipokwenda kusherehekea Sikukuu ya Christmas wiki tatu zilizopita. Mwezi Desemba mwaka jana shirika hilo lilitoa mikopo ya Shilingi laki moja kwa kila mfanyakazi kuwawezesha wao na familia zao kushereheka Krismas kwa ‘wasaa’. Ingawa wafanyakazi wote, bila kujali dini zao, walinufaika na mikopo hiyo, wafanyakzai Waislamu walionyesha dukuduku lao kutaka kujua iwapo mikopo kama hiyo ingetolewa pia wakati wa Sikukuu ya Idd, katikati ya mwezi Januari mwa huu. Imedaiwa kuwa baada ya minong’ono hiyo ya Waislamu kuufikia uongozi wa shirika hilo, uongozi huo ulisema kuwa mkopo uliokwisha tolewa ulikusudiwa kwa sikukuu zote mbili, ingawa katika karatasi zao za mishahara ulitajwa kama mkopo wa Krismas (Christmas Loan). Jibu hilo, kwa mujibu wa wafanyakazi waliozungumza na gazeti hili, halikuwa baya na kwamba lilikuwa limetoa matumaini mapya. Lakini uongozi wa shirika hilo uliwashangaza wafanyakazi Waislamu pale ulipoamuru makato ya mkopo huo yaanze kabla hiyo sikukuu ya Idd ambayo kwayo mikopo hiyo ilikusudiwa haijasherehekewa. Wafanyakazi wote wa TANESCO wameanza kukatwa robo ya kwanza ya mikopo hiyo kutoka mishahara yao ya mwezi Januari, 1999, ambayo ilitolewa katikati ya mwezi huu ili kuwahi sikukuu ya Idd el Fitr. Akiongea na mwandishi wa habari hizi katika jengo la Makao Makuu ya TANESCO, Barabara ya Samora, jijini Dar es Salaam, mfanyakazi mmoja wa shirika hilo alisema wenzao (Wakristu) walikwenda kula Krismas na fungu zima (la mkopo) lakini wao (Waislamu) wamekula Idd na fungu pungufu. Mfanyakazi huyo hakutaka jina lake litajwe gazetini ingawa alikubali kumuonyesha mwandishi kitambulisho chake cha kazi (TANESCO). Dada mmoja ambaye naye ni mfanyakazi wa shirika hilo makao makuu, akiongea kwa unyonge, alisema, "walituambia eti mikopo hiyo nia Krismasi na Idd kumbe waongo watupu...waliitoa kwa ajili ya sikukuu yao [Krismasi] tu". "Mambo mengi wanatubagua hawa,"aliongeza dada huyo bila kufafanua ni mambo gani mengine wanabaguliwa na kumalizia, " lakini Mungu anawaona, na alhamdulillah tumesherehekea kiasi chetu". Nje ya jengo la makao makuu hayo katika uzio unaotenganisha jengo hilo na lile la British Council, mwandishi wetu aliwakuta wafanyakazi watatu wakiwa katika sare zao za kazi. Mmoja wao aliyejitambulisha kama dereva wa siku nyingi (lakini kama waliotangulia hakukubali jina lake litajwe gazetini) alisema kuwa kweli walikuwa wanabaguliwa kwa vile makato yameanza kabla ya hiyo Idd iliyokusudiwa. Aliongeza kuwa mikopo ile hasa ilikuwa ni ya Krismas ila tu walishidwa namna ya kuwanyima wao [waislamu]. Kwa hamaki dereva yule alitoa karatasi mbili za mshahara wa mwezi Desemba 1998 na Januari, 1999 na kukabidhi mwandishi, "Ona mwenyewe bwana, hii ‘slip’ ya Desemba imeandikwa CHRISTMAS LOAN, hakuna Idd hapo, sawa ?...lakini baadaye wakaona wamefanya kosa kuandika hivi, sasa katika ‘slip’ hii ya Januari kwa ajili ya makato wameandika SPECIAL ALLOWANCES ili kuficha ile Krismas". Dereva huyo wa siku nyingi alipohojiwa zaidi kuwa ni kwa nini asishukuru kwa hicho alichobaki nacho hadi siku ya Idd kwa vile wapo Waislamu kadhaa ambao hawakuwa na kitu kabisa siku ya Idd, bwana huyo alifoka, "Usitufanye sisi wajinga, unasikia bwana...tunacholalamikia sio kiasi cha fedha tulichobaki nacho, sawa... bali ni hii tabia ya kutubagua. Walishindwa nini kusubiri Februari ili nasi tule Idd tukiwa na fungu zima la mkopo kama wao walivyokula Krismas. Na hii sikukuu yetu ndiyo ya kweli siyo ya uzushi". Dereva huyo aliendela kutoa malalamiko yake kuwa kila mwaka TANESCO inaingia gaharama kubwa kupamba majego yake nchi nzima kwa ajili ya Krismas kana kwamba shirika hilo linamilkiwa na Wakristu, wafanyakzi wake wote ni Wakristu na wateja wake wote ni Wakristu au lipo katika nchi ya Kikristu. "Unasikia bwana mwandishi, hata Director wetu hutoa salamu za Krismas tu. Yote haya hatuyaoni kwenye Idd. Nenda pale kwenye ubao wa matangazo kajisomee mwenyewe salamu zake", alimaliza dereva huyo akasimama na kuwaacha wenzie wakiwa wameduwaa. Mwandishi hakuweza kujua madereva wawili hao walikuwa ni dini gani. Katika ubao wa matangazo mwandisi aliukuta waraka huo wa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO wenye salamu za Krismas na Mwaka Mpya 1999 kwa wafanyakazi wote wa shirika hilo. Waraka huo ambao pamoja na salamu hizo ulizungumzia hali ya maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme na kuwakumbusha wafanyakzi umuhimu wa kumfanya mteja kuwa ni mfalme, ulianza hivi: Kutoka: Mkurugenzi Mtendaji Kwenda: Wafanyakazi wote kumb. Na.: MD/C/2 Tarehe: 2 Desemba 1998 SALAMU ZA KRISMAS NA KHERI YA MWAKA MPYA 1999 "Ndugu wafayakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mwaka unakaribia kwisha na napenda nichukue nafasi hii kuwatakia wafanyakazi wote pamoja na familia zenu Kheri na baraka tele wakati wa sikukuu ya CHRISTMAS na MWAKA MPYA 1999". Aidha mwandishi alifanikiwa kuona masalia ya mapambo ya Krismas kama ilivyodaiwa na dereva yule wa siku nyingi. Katika ofisi za TANESCO zilizoko Mikocheni mwandishi aliweza kuongea na dada mmoja tu ambaye alijtambulisha kuwa ni Massawe na si Muislamu. Alipoulizwa angejisikiaje kama angekuwa ni Muislamu alisema, "of course nisingejisikia vizuri", na kuongeza kuwa hata sasa hajisikii vizuri kwa vile makato hayo yamekuja mapema mno hali ya kuwa wafanyakazi wengi wanakabiliwa na mzigo wa kulipa ada za shule za watoto wao. Alishauri kuwa ni bora shirika lingetoa nafuu angalau japo mpaka mwezi wa Aprili ndipo hayo makato ya robo robo yaanze. Katika ofisi za TANESCO Ilala, Dar es Salaam mama mmoja wa makamo ambaye alijitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa shirika hilo kwa miaka mingi na alionesha kitambulisho chake aliulaumu vikali uongozi wa shirika hilo kwa kutawaliwa na hisi za kidini katika maamuzi yao. Alisema kuwa hali hiyo ni ya hatari sana na kuongeza, "hivi unafikiri hali itakuwaje wakati wa redundancy (zoezi la kupunguza wafanyakazi), hii ni dalili kuwa waislamu tutaondoka kwa wingi". "Nakwambia hatabaki mtu (muislamu) hapa kwa vile katika viongozi wanaoingia katika vikao vya juu Waislamu ni wa kutafuta", alimalizi mama huyo. Shirika hilo la umeme nchini linatarajia kupunguza wafanyakazi wake mwanzoni mwa mwaka huu kama iliyotangazwa katika taarifa ya Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Bw. Aboud Maalim, katika kikao cha mwaka cha Baraza la Wafanyakazi (Workers Council) kilichofanyika Morogoro mwishoni mwaka jana. Kupunguza wafanyakazi ni hatua ya awali ya kulibinafsisha shirika hilo. Mwaka 1996 katika moja ya matoleo yake gazeti hili liliwahi kufanya uchambuzi wa watu walioshika nafasi mbalimbali za uongozi katika shirika hili kongwe nchini kwa mujibu wa dini zao. Uchambuzi huo ulibaini kuwa zaidi ya asilimia 80 ya nafasi hizo zinashikiliwa na wakristu. Si serikali wala menejimenti ya TANESCO iliyojaribu kufafanua uwiano huo mbaya wa madaraka. Ni katika mantiki hizi ndipo wafanyakzi waislamu katika TANESCO wameingiwa na hofu juu ya hali yao ya baadaye. Juhudi za gazeti hili kumpata msemaji wa TANESCO kuzungumzia madai hayo
ya ubaguzi hazikufanikiwa na mpaka tunakwenda mitamboni hatukuwa na salamu
zozote toka kwa Mkurugenzi Mtendaji au japo manaibu wake za kuwatakia wafanyakazi
na familia zao KHERI YA IDD kama ilivyokuwa wakati wa Krismas ya Bwana.
|
YALIYOMO
Tahariri
Waislamu wataka serikali iwajibike Serikali yakiri kupokea malalamiko ya Waislamu: Mkapa awataka Watanzania waepuke kubaguana Mtambani wasema kamwe hawakubali pumbao la kisiasa Maoni: Kweli ikisimama uongo hujitenga MARADHI YA KISAIKOLOJIA: TRANSVESTISM Risala ya Waislamu katika Baraza la Idd kwa Mgeni Rasmi Rais Benjamin Mkapa Wafanyakazi TANESCO waingiwa hofu ya wingu la udini Hotuba ya Rais Mkapa kwenye Baraza la Idd Diamond Jubilee Jan. 19, 1999 Makala: Hotuba ya Mkapa, Magazeti
ya Ruzuku na Waislamu
Kutoka magazeti ya zamani: Washitakiwa walipelelezwa Hivi siku ya ibada ni ipi?: Ijumaa,
Jumamosi au Jumapili?
'Msitarajie kupambana na adui kwa upanga wa Hamza' Sasa ni kulishwa nguruwe kwa nguvu Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|