AN-NUUR
Na.185 Shawwal 1419, Januari 22 - 28, 1998
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
Waislamu wataka serikali iwajibike
 
  • Ali Ameir, Makamba, Gewe wavuliwe madaraka
  • Wasema Mwembechai ni kilele cha ukandamizaji cha ukandamizaji
  • Kamanda wa polisi ataka kuongea na Imamu wa Mtambani, aambiwa amekufa
Waislamu wameendelea kusisitiza kuwa haki itendeke kwa tume huru kuundwa, walioua wafikishwe kwenye vyombo vya Sheria na baadhi ya viongozi wa Serikali na vyombo vyake wawajibishwe kutokana na utendaji wao kuwa wa jazba ambao haukuzingatia katiba wala sheria za nchi kuhusiana na kadhia ya mwembechai.

Msisitizo huo ulitolewa katika Baraza la Idd lililofanyika jumanne wiki hii katika Msikiti wa Mtambani uliopo wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam. 

Akitoa ripoti ya kamati ya kutetea haki za Waislamu nchini mbele ya maelfu ya Waislamu kutoka maeneo mbali mbali Jijini na mikoa ya jirani, bwana Musa Mtaki kwa niaba ya kaimu katibu wa kamati hiyo, alisema tukio la Mwembechai ni kilele cha madhila ya muda mrefu wanayofanyiwa Waislamu hapa nchini. 

Alikumbusha Historia ya harakati za kudai uhuru wa nchi hii na kusema kwamba ni Waislamu waliosimama kupinga udhalimu wa wakoloni wakati Kanisa likisimama upande mmoja na utawala huo. 

Aidha alikitaja kitabu cha bwana Mohammed Said kama ni mojawapo ya rejea zinazouweka bayana ukweli huo. 

Akizungumzia tukio la Mwembechai bwana Musa alisema kumekuwa na jitihada za makusudi za kupotosha ukweli juu ya chanzo cha kadhia ya Mwembechai. 

Alisema Waislamu wakiongozwa na kamati ya kutetea haki zao, wanafahamu vyema kuwa chanzo cha tukio la Mwembechai ni hotuba za baadhi ya viongozi wa Serikali dhidi ya mihadhara ya Waislamu ambazo zilipokelewa na viongozi wa Kanisa kwa kishindo ambapo Padri Lwambano wa Kanisa Katoliki Mburahati aliishinikiza Serikali ichukue hatua dhidi ya kile alichokiita kashfa za kidini zilizokuwa zikitolewa katika mihadhara iliyokuwa ikifanyika katika Misikiti ya Kibo, Mtambani na Mwembechai. 

Bwana Musa alieleza kwa uchungu hatua za jazba za viongozi wa Serikali na vyombo vyake zilizofuata baada ya kilio cha Padri Lwambano. 

Alisema mnamo februari 9 mwaka jana Waislamu walianza kukamatwa ovyo katika misikiti ya kibo, mtambani na Mwembechai. 

Aliwataja waliokamatwa katika Misikiti hiyo ni pamoja na mzee Katambo ambaye hivi sasa amechanganyikiwa baada ya mateso ya miezi kadhaa gerezani, Marehemu Mzee Chata Imamu wa Msikiti wa Mtambani ambaye alifariki dunia mara tu baada ya kutoka gerezani na Waislamu wengine kadhaa kutoka Misikiti hiyo. 

Akiendelea kutoa ripoti hiyo, bwana Musa alisema ilipofika tarehe 12 ya mwezi huo polisi walivamia msikiti wa Mwembechai na kumkamata bwana magezi Shaaban. 

Alisema ‘walimpora’ Magezi na kuondoka nae kisha wakarejea tena kuuvamia msikiti na kulipua idadi kubwa ya mabomu ya machozi ambayo yaliwaathiri akina mama waliokuwemo Msikitini humo. 

Aidha alisema askari hao walivunja milango ya msikiti huo na kuingia ndani ambamo walifanya kila aina ya unyama na udhalilishaji. 

Wakati taarifa hiyo ikiendelea kutolewa, pale yalipokuwa yakitajwa majina ya baadhi ya viongozi walioamuru uvamizi huo, kauli za "laanatullah" zilisikika kutoka kwa maelfu ya waumini waliokuwa wasikiliza kwa makini. 

Mwishoni mwa taarifa hiyo kamati kwa niaba ya Waislamu imeitaka Serikali iunde tume huru ya kuchunguza kadhia hiyo, iwafikishe mahakamani wauaji na iwawajibishe Waziri wa Mambo ya Ndani Bwana Ali Ameir, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bwana Yusufu Makamba na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam Bwana Alfred Gewe. 

Baraza la Id la mtambani limefanyika katika mazingira ya vitisho kutoka vyombo vya Dola na baadhi ya viongozi wa Serikali ngazi ya mkoa. 

Imedaiwa kuwa mapema kabla ya baraza hilo kuanza kamanda wa polisi bwana Alfred Gewe alifika msikitini hapo kutaka kuongea na Imam wa msikiti huo. Hata hivyo waumini waliokuwepo walimjibu kamanda huyo kuwa Imamu wao ni Marehemu Sasa. 

"Imamu wetu Mzee Chata ameuliwa," wamesikika wakisema waumini hao bila kufafanua kauliwa vipi na nani. 

Baadhi ya wapita njia walioshuhudia Umati mkubwa wa watu uliojazana mtambani walisema kuwa waliitaka serikali kutumia njia za kidiplomasia zaidi badala ya vitisho na mabavu. 

"Hawa watu hawawezekani, kila kukicha wanaongezeka hawaogopi vitisho wala hawamsikilizi kiongozi yoyote yule wasiyemkubali, bora Serikali itumie busara vinginevyo ipo hatari kubwa baadae, amedai mfanyabishara mmoja wa Soko lililo jirani na Msikiti huo.
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Fundisho toka Mtambani

Waislamu wataka serikali iwajibike

Serikali yakiri kupokea malalamiko ya Waislamu: Mkapa awataka Watanzania waepuke kubaguana

Mtambani wasema kamwe hawakubali pumbao la kisiasa

Maoni: Kweli ikisimama uongo hujitenga

MARADHI YA KISAIKOLOJIA:  TRANSVESTISM

Mjue Usama bin Ladin

Risala ya Waislamu katika Baraza la Idd  kwa Mgeni Rasmi Rais  Benjamin Mkapa

Wafanyakazi TANESCO waingiwa hofu ya wingu la udini

Hotuba ya Rais Mkapa kwenye Baraza la Idd Diamond Jubilee Jan. 19, 1999

Makala: Hotuba ya Mkapa, Magazeti ya Ruzuku na Waislamu
Na J. Hussein

Kutoka magazeti ya zamani: Washitakiwa walipelelezwa

Hivi siku ya ibada ni ipi?: Ijumaa, Jumamosi au Jumapili?
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu

'Msitarajie kupambana na adui kwa upanga wa Hamza'

Sasa ni kulishwa nguruwe kwa nguvu

Sayansi na Teknolojia
[KUPELEKA  FAX NCHI ZA NG'AMBO BURE!]

Masomo ya Dini ya Kiislamu

Barua za Wasomaji

Mashairi

Chakula na lishe
[Faida na  hasara za kupika chakula]
  


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org

 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita