|
Mashairi
Kheri tisini na nane
Bismillahi naanza, kwa jina lako Raufu,
Naanza kuzungumza, na washairi sanifu,
Leo kwenu nachomoza, nipokee maradufu,
Kheri tisini na nane, karibu tisa tisini.
Tumekaa kwa amani, tena kwa uaminifu,
Tukimwabudu Dayyani, kusujudu safu safu,
Kamwe hatukujihini, Juma, Haruna na Sefu,
Kheri tisini na nane, karibu tisa tisini.
Mohammed H. Machella,
Masjid Answaar - Makonga,
Newala. Na. 182.
Si ngomayo usicheze (jibu)
Bismillahi la awali, kutaja ndio kanuni,
Kwake ninatawakali, Mola mpaji yakini,
Aniwezeshe na hili, nasaha za gazetini,
Si ngomayo usicheze, mwaka hatujamaliza.
Salamu nakutumia, Machella ulo kusini,
Zikukute metulia, AN-NUUR mkononi,
Ukisha macho fungua, uzisome kwa makini,
Si ngomayo usicheze, mwaka hatujamaliza.
Mwaka sisi haujesha, hatujafika mwishoni,
Ramadhani ikiisha, ndio wa kumi mwanzoni,
Ulikosea kukesha, kuiga ya kwao dini,
Si ngomayo usicheze, mwaka hatujamaliza.
Dini imetilimilia, hatuchanganyi imani,
Ya watu kuparamia, na kujipa tumaini,
Hilo nakkatalia, amana umeikhini,
Si ngomayo usicheze, mwaka hatujamaliza.
Sisi si wa msalaba, “kafara” hatuamini,
Na Mola wetu si “Baba”, si jinale kitabuni,
Mafunzo yetu si haba, twahangaika kwa nini!
Si ngomayo usicheze, mwaka hatujamaliza.
Ulomalizika mwaka, huo ni Anno Domini,
A.D. huandika, rudi mwao vitabuni,
Kuwaiga si mwafaka, sisi siyo wapagani,
Si ngomayo usicheze, mwaka hatujamliza.
Wenzio hujiimbia, na maombi Kanisani,
Na salamu za Maria, hukesha nazo nyimboni,
Huku wakifurahia, sisi walivyotuhini,
Si ngomayo usicheze, mwaka hatujamaliza.
Twauongoja Muharramu, akituweka Manani,
Kwa huo tunayo hamu, sote tuwe shereheni,
Tuyapange ya muhimu, ya nyuma tutathmini,
Si ngomayo usicheze, mwaka hatujamaliza.
Hapa mwisho wa salamu, witiri sikuikhini,
Si kama nakulaumu, bali ninakuauni,
Nasaha ni jambo tamu, nisikuase kwa nini?
Si ngomayo usicheze, mwaka hatujamaliza.
Jihad R. Saballa,
Box 347, Shinyanga.
Misukosuko ikoje! (jibu)
Mwaka umeusifia, umekuwa wa amani,
Vyema umeabudia, bila ya khofu moyoni,
Hongera nakutumia, kwa huo wako uoni,
Kiwa hii ndo amani, misukosuko ikoje!
Nduguzo wamevamiwa, wakiwa Msikitini,
Baadhi wakauliwa, wengine kutiwa ndani,
Dada zako kuvuliwa, na mateso gerezani,
Kiwa hii ndo amani, misukosuko ikoje!
Luambano katiiwa, sisi kutiwa tabuni,
Wakubwa wakapagawa, na kutangaza ilani,
Mara ikawa twalengwa, “piga, ongeza” haini,
Kiwa hii ndo amani, misukosuko ikoje!
Chuki alivyolemewa, hukusoma gazetini?
Kalala hakutibiwa, na pingu za kitandani,
Wewe ulivyoelewa, yuko katika amani!
Kiwa hii ndo amani, misukosuko ikoje!
Lile la Tume kuundwa, limetoswa kikapuni,
Baraka tunayopewa, kukejeli yetu dini,
Na mengi kusingiziwa, ugaidi na uhuni,
Kiwa hii ndo amani, misukosuko ikoje!
Balozi kulipuliwa, za mbabe Clintoni,
Wenzetu wakauliwa, wapitao mitaani,
Uongo ukazuliwa, wahusika ni Sudani,
Kiwa hii ndo amani, misukosuko ikoje!
Ya Nzasa hukuambiwa, ndo mana huna huzuni,
Wenzetu wameonewa, sio watu utadhani,
Makazi wamechomewa, sasa waishi mitini,
Kiwa hii ndo amani, misukosuko ikoje!
Na maisha hivi kuwa, shilingi hatuioni,
Mno tumeelemewa, dhiki tunayo shingoni,
Ukihoji waambiwa, tunayakidhi madeni,
Kiwa hii ndo amani, misukosuko ikoje!
Idhini imetolewa, bastola madukani,
Iwe rahisi kuwindwa, tuuwawe kama nyani,
Waona yote muruwa, eti tunayo amani,
Kiwa hii ndo amani, misukosuko ikoje!
Na fedha zinakusanywa, zitumike elfeni,
Tupate kughilibiwa, kwa uchaguzi kukhini,
Wanatwambia “wakubwa”, vyema mikanda fungeni,
Kiwa hii ndo amani, misukosuko ikoje!
Inatosha kuelewa, ulosema si yakini,
Najua ulipitiwa, au hukuyabaini,
Witiri haiwi shufwa, wala shari si amani,
Kiwa hii ndo amani, misukosuko ikoje!
Jihad R. Saballa,
Box 347, Shinyanga.
|
YALIYOMO
Tahariri
Fundisho toka Mtambani
Waislamu wataka serikali iwajibike
Serikali yakiri kupokea malalamiko
ya Waislamu: Mkapa awataka Watanzania waepuke kubaguana
Mtambani wasema kamwe hawakubali pumbao
la kisiasa
Maoni: Kweli ikisimama uongo hujitenga
MARADHI YA KISAIKOLOJIA: TRANSVESTISM
Mjue Usama bin Ladin
Risala ya Waislamu katika Baraza la
Idd kwa Mgeni Rasmi Rais Benjamin Mkapa
Wafanyakazi TANESCO waingiwa hofu
ya wingu la udini
Hotuba ya Rais Mkapa kwenye Baraza
la Idd Diamond Jubilee Jan. 19, 1999
Makala: Hotuba ya Mkapa, Magazeti
ya Ruzuku na Waislamu
Na J. Hussein
Kutoka magazeti ya zamani: Washitakiwa
walipelelezwa
Hivi siku ya ibada ni ipi?: Ijumaa,
Jumamosi au Jumapili?
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu
'Msitarajie kupambana na adui
kwa upanga wa Hamza'
Sasa ni kulishwa nguruwe kwa
nguvu
Sayansi na Teknolojia
[KUPELEKA FAX NCHI ZA NG'AMBO BURE!]
Masomo ya Dini ya Kiislamu
Barua za Wasomaji
Mashairi
Chakula na lishe
[Faida na hasara za kupika chakula]
|