|
Na.185 Shawwal 1419, Januari 22 - 28, 1998 |
| Serikali
yakiri kupokea malalamiko ya Waislamu:
Mkapa awataka Watanzania waepuke kubaguana Rais Benjamini Mkapa amewataka Watanzania kuondokana na tabia ya kubaguana kwa misingi ya dini na kwamba kama raia wa nchi waishi kwa kuzingatia katiba na sheria za nchi ili kuleta maelewano na mahusiano mema miongoni mwao. Rais aliyasema hayo wakati akijibu risala ya malalamiko ya Waislamu dhidi ya utendaji wa Serikali iliyowasilishwa kwake katika Baraza la Idd lililofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubelee jumanne wiki hii. Rais mkapa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, alikiri kupokea malalamiko hayo na kuahidi kuchukua hatua baada ya kuyafanyia uchunguzi na kushauriana na Baraza lake la Mawaziri. Katika risala hiyo iliyosomwa mbele yake na Alhaji Madabida kwa niaba ya kamati ya maandalizi ya hafla hiyo, yameorodheshwa mambo kadhaa ambayo yamedaiwa kukwaza Uislamu na Waislamu hapa nchini. Mambo hayo ni pamoja na udini na upendeleo dhidi ya Waislamu katika baadhi ya vyombo vya dola na watendaji Serikalini, suala la Mwembechai, mahakama ya kadhi, uwiano wa kidini katika vyuo na maofisi ya Serikali, idadi ya vijana Waislamu magerezani na kusita kwa Tanzania kujiunga na OIC. Katika hotuba yake, Rais akiri mchango mkubwa uliotolewa na Waislamu katika harakati za kudai uhuru wa nchi hii na akasema kwamba mchango kama huo unahitajika katika kujenga na kuleta maendeleo ya Tanzania huru. Rais Mkapa aliwaasa Watanzania kutatua migogoro na kuyapatia ufumbuzi matatizo mbalimbali yanayowakabili kwa njia ya busara badala ya kutumia jazba. Hata hivyo, kauli hii ya Rais imekuja huku baadhi ya watendaji katika serikali yake wameripotiwa kutoa kauli za jazba kuhusiana na suala la Mwembechai, kauli hizo ni pamoja na zile zilizotolewa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Luteni Yusufu Makamba kufuatia kilio cha Padri Lwambano, Waziri wa mambo ya ndani bwana Ali Ameir kuzihusisha baadhi ya balozi na kadhia ya Mwembechai pasina ushahidi na ile iliyotolewa na Waziri Mkuu bwana Frederick Sumaye Februari 13 wakati akifunga kikao cha Bunge. Mheshimiwa Rais vile vile alivitaka vyombo vya dola kuzingatia hisia za wananchi katika utekelezaji wa majukumu yake na kwamba nguvu itumike kulingana na uzito wa matatizo. Huku akinukuu katiba ya nchi ibara ya 19 kif. 1 na 2 Rais Mkapa alisema, Wananchi wana uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa dini zao bila ya kuingiliwa na Serikali. Hata hivyo, katika suala hili upo utata ambapo mihadhara ya dini ya Kiislamu imekuwa ikipigwa marufuku na viongozi wakuu wa serikali. Mheshimiwa Mkapa alikemea tabia ya kuhoji dini ya mtu katika utoaji wa huduma au fursa mbali mbali za kijamii kwa kusema kwamba mtu aulizwe dini yake anapokwenda kuposa nyumba ya mtu. Aliwataka Watanzania wote wajione ni raia walio na haki sawa katika nchi yao na aliwaomba waondokane na hisia za kujidunisha kwamba kuna raia daraja la kwanza na raia daraja la pili katika nchi moja. Kuhusu mavazi, Rais Mkapa aliwataka Watanzania waache kuiga mitindo isiyozingatia hadhi na heshima ya Mtanzania. Wakati huo huo, hotuba ya Rais Mkapa imepokelewa kwa hisia tofauti miongoni mwa wananchi na viongozi wa vyama vya upinzani. Wananchi kadhaa wamedai kuwa Rais kukiri hadharani malalamiko ya raia ni ishara nzuri. Hata hivyo, wengine wamepokea kwa tahadhari kubwa hotuba hiyo. Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wameitafsiri hotuba ya Rais kama ni kampeni ya kisiasa inayofanywa na CCM kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka ujao (2000). Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa chama cha NRA ambaye pia ni Katibu Jumuiya ya Wazazi wa Kiislamu nchini bwana Shaaban Kakinga amedai kwamba Rais Mkapa anajaribu kuteka hisia zaWaislamu ili kujijenga kisiasa kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2000. Bwana Kakinga amedai hakuna jipya katika hotuba hiyo zaidi ya kuwa ni kampeni za CCM kujiosha kwa wananchi kutokana na inayowafanyia. Naye katibu mkuu wa CHADEMA bwana John Guninita aliliambia AN-NUUR kufuatia hotuba hiyo kuwa ameshangazwa na kauli Rais kuwa ndiyo kwanza anayajua matatizo ya Waislamu pale. Bwana Guninita alisema kauli hiyo inaonyesha Rais hayuko karibu na wananchi wake kiasi cha kutojua matatizo yao ya muda mrefu. "Hii inaonyesha Rais hajui matatizo ya makundi mbali mbali ya wananchi ikiwa ni pamoja na Waislamu", alisema bwana Guninita wakati akiongea na gazeti hili kwa njia ya simu. Aidha, alisema huo huenda ukawa ni ujanja wa CCM wa kujijenga kwa wananchi
kila inapokaribia uchaguzi.
Alipohojiwa ni kwa nini wapinzani hawakutoa kauli ya kulaani mauaji
ya Mwembechai na kwamba je hadhani ukimya huo wa wapinzani huenda ukatafsiriwa
na wananchi hususani Waislamu kwa wapinzani na CCM kuwa lao moja, bwana
Guininita alijibu kifupi kuwa wao (Chadema) walishalizungumza suala hilo.
|
YALIYOMO
Tahariri
Waislamu wataka serikali iwajibike Serikali yakiri kupokea malalamiko ya Waislamu: Mkapa awataka Watanzania waepuke kubaguana Mtambani wasema kamwe hawakubali pumbao la kisiasa Maoni: Kweli ikisimama uongo hujitenga MARADHI YA KISAIKOLOJIA: TRANSVESTISM Risala ya Waislamu katika Baraza la Idd kwa Mgeni Rasmi Rais Benjamin Mkapa Wafanyakazi TANESCO waingiwa hofu ya wingu la udini Hotuba ya Rais Mkapa kwenye Baraza la Idd Diamond Jubilee Jan. 19, 1999 Makala: Hotuba ya Mkapa, Magazeti
ya Ruzuku na Waislamu
Kutoka magazeti ya zamani: Washitakiwa walipelelezwa Hivi siku ya ibada ni ipi?: Ijumaa,
Jumamosi au Jumapili?
'Msitarajie kupambana na adui kwa upanga wa Hamza' Sasa ni kulishwa nguruwe kwa nguvu Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|