|
Na.185 Shawwal 1419, Januari 22 - 28, 1998 |
|
Hotuba ya Mkapa, Magazeti ya Ruzuku na Waislamu Na J. Hussein
Juzi Januari 19,1999 siku ya Jumanne Mufti Mkuu wa Bakwata Sheikh Hemed Bin Jumaa Bin Hemed wakati akimkaribisha Rais kuhutubia baraza la Idd alionyesha kufurahishwa kwake kwa kile alichokiona kuwa baraza hilo ni la kihistoria. Mufti huyo aliliona kuwa baraza hili ni la kihistoria kwa sababu kwa mara ya kwanza katika orodha ndefu ya mabaraza ya Idd ambayo yameshafanyika nchini, Bakwata ilikuwa imefanikiwa kushirikiana na baadhi ya taasisi zingine za Kiislamu na Waislamu wa madhehebu mbalimbali nchini kufanikisha baraza hilo. Furaha ya Mufti, nahuenda ya viongozi wengine wa Bakwata kwa ujumla inaeleweka. Inaeleweka kwa sababu kwa muda mrefu taasisi nyingine za Kiislamu hapa nchini pamoja na Waislamu walio wengi ndani ya madhehebu zao mbalimbali wamekuwa wakiichukulia Bakwata kama chombo kilichoundwa makusudi na Serikali kudumaza maendeleo ya Uislamu na Waislamu nchini. Kwa kifupi ni kwamba Bakwata ilikuwa imetengwa, na kwa bahati mbaya sana kwake mabadiliko ya kisiasa ambayo yamekuwa yakiendelea nchini tangu Serikali ya awamu ya pili ilipoingia madarakani katikati ya miaka ya themanini kuliipunguzia Serikali uwezo wake wa kulisimika baraza hilo juu ya Waislamu wote. Napenda kuungana na Sheikh Hemed Bin Jumaa kuwa ni kweli kabisa baraka la Idd lililofanyika juzi lilikuwa la kihistoria. Ni la kihistoria si kwa sababu tu Bakwata imefanikiwa kuungana na taasisi na jumuiya nyingine za Kiislamu nchini kuandaa hafla ya pamoja, bali pia kwa sababu kwa mara ya kwanza Waislamu wale ambao siku zote wameepuka adha ya kubandikwa majina "Imani Kali", "Siasa Kali", "Wakorofi Wachache", n.k., kutokana na kukosa ujasiri wa kuutetea Uislamu wao barabara, Alhamdulillah wamekuwa majasiri kiasi cha kutosha kuweza kusimama hadharani, tena mbele Rais na kutamka wazi kwamba naam, kuna dhulma dhidi ya Waislamu hapa nchini. Mbali ya haya uhistoria wa baraza hili umetokana pia na ukweli kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hili madai haya ya Waislamu yamepata fursa ya kusikika katika maeneo mbali mbali nchini kwa wakati ule ule kupitia radio ya taifa. Mwisho kabisa uhistoria wa baraza hili umeletwa na ukweli kwamba Serikali kwa mara ya kwanza katika historia kupitia hotoba ya Rais Mkapa imeahidi kuyafanyia kazi madai hayo ya Waislamu. Mojawapo ya sifa kubwa za tukio lolote la Kihistoria ni ule uwezo wake wa kuleta mabadiliko ya kimsingi kabisa katika jamii. Ni kutokana na hali hii ndio sababu taasisi yoyote iliyopevuka inakuwa mstari wa mbele kulipa tukio linalohusika uzito unaostahili kama njia ya kujiandaa kutoa mchango wa kuyapa mwelekeo mabadiliko yanayotarajiwa. Taasisi na vyombo vya habari, hususan magazeti kwa jumla zinaamini kuwa mstari wa mbele katika suala hili. Ni ukweli usiopingika kuwa magazeti ya Tanzania, huenda kwa kiwango cha asilimia tisini na tisa nukta tisa hayana upenzi wowote juu ya Uislamu. Magazeti haya yamekuwa mstari wa mbele kutoa kipaumbele kwa habari zenye lengo la kuwakera Waislamu, kuwachonganisha kuwa dhalilisha na hata kuwazulia uwongo. Ni rahisi kwa mtu kuilewa hali hii iwapo atazingatia kuwa kila gazeti lina sera yake na iwapo watunzi wa sera hizi ni maadui wa Uislamu, basi sehemu ya sera hizi ni kuupiga vita Uislamu. Pamoja na hali hii mtu angetarajia kuwa viongozi wa vyombo hivi angalao wengekuwa na uwezo wa kutambua hatari ya kuvuka mipaka iliyowekwa na sheria za kiasili za kiuchumi au zinazolazimisha umuhimu wa kuzingatia kwa uzito unaostahili matukio ya kihistoria. Zaidi ya asilimia hamsini na tano ya Watanzania wote ni Waislamu na hivyo basi tunatarajia zaidi ya asilimia hamsini na tano ya wasomaji wote wa magazeti nchini wawe ni Waislamu. Haiingii akilini hata kidogo kwa mtu yeyote anayeifahamu A,B,C, ya kuuza na kununua awe anaitukana, tena kwa makusudi asilimia hamsini na tano ya wateja wake, bila kuwa na kitu anachokitegemea. Mara nyingi mtu wa namna hii atakuwa anategemea ruzuku inayomfanya asichunge nidhamu yake mbele ya soko analotarajia kuuzia bidhaa zake. Utafiti usio wa kina unatosha kuthibitisha mtu yeyote mwenye nia ya kujua kuwa magazeti mengi ya Tanzania yameaanzishwa kwa ruzuku na yanajiendesha kila siku kwa ruzuku. Hata hivyo kwa kuwa ni kinyume na maumbile kuwepo na kisima kisicho na mwisho kilichojaa ruzuku ya kujichotea tu kila ile iliyotangulia inapoisha, mengi kati ya haya yameshatoweka na mengi katika yale ambayo bado yapo imeanza kusikia minong’ono kuwa mambo si shwari kuhusiana na kulipana mishahara n.k. Katika mazingira kama haya mtu angetarajia kuwa marekebisho ya msingi yangefanywa hasa kwa nia ya kurudisha uhusiano mwema na Soko. Lakini inaelekea wahusika hawajagundua hali yao halisi au agenda waliyokabidhiwa dhidi ya Waislamu imewapofusha. Kama si hivyo ni vipi basi unaweza ukakielezea kitendo kilichofanywa na magazeti haya kujaribu kufikisha kwa makusudi tukio kubwa na la kihistoria tuliloshuhudia hivi majuzi? Baadhi ya haya magazeti yaliona ajali ya kuvunjia kwa ukuta katika msikiti wa Idrisa inastahili hadhi kubwa kimaandishi kuliko historia iliyofanyika pale Diamond Jubilee wakati wa baraza la Eid. Mengine yalidiriki hata kukiuka taratibu za kiitifaki kwa kutoa hadhi zaidi kimaandishi kwa ujumbe wa Makamu wa rais alioutoa asubuhi wakati wa sala ya Eid kuliko yale aliyoyazungumza rais mwenyewe jioni ya siku hiyo hiyo wakati wa baraza la Eid pale Diamond Jubilee. Ukiondoa ruzuku za chee na kulishwa kasumba, huenda sababu nyingine
inayofanya magazeti humu nchini yakose mwelekeo ni kukosa ushindani wa
dhati. Ni bora yakakaa chonjo kwani wahusika wangepevuka kiasi cha kuweza
kusoma dalili wangegundua kuwa iwapo wale ambao hawakutarajiwa hatimaye
wamepata ujasiri kiasi cha kuvunja ‘mwiko’ hadharani, tena mbele ya mheshimiwa
rais, huenda siku haiko mbali wakaamua kuwa wamle ng’ombe mzima. Jee, wana
magazeti ushindani ukizuka toka kwa wale wanaotoa fedha yao mfukoni - na
alhamduli laah, baadhi yao wanazo - mtaweza kuhimili?
|
YALIYOMO
Tahariri
Waislamu wataka serikali iwajibike Serikali yakiri kupokea malalamiko ya Waislamu: Mkapa awataka Watanzania waepuke kubaguana Mtambani wasema kamwe hawakubali pumbao la kisiasa Maoni: Kweli ikisimama uongo hujitenga MARADHI YA KISAIKOLOJIA: TRANSVESTISM Risala ya Waislamu katika Baraza la Idd kwa Mgeni Rasmi Rais Benjamin Mkapa Wafanyakazi TANESCO waingiwa hofu ya wingu la udini Hotuba ya Rais Mkapa kwenye Baraza la Idd Diamond Jubilee Jan. 19, 1999 Makala: Hotuba ya Mkapa, Magazeti
ya Ruzuku na Waislamu
Kutoka magazeti ya zamani: Washitakiwa walipelelezwa Hivi siku ya ibada ni ipi?: Ijumaa,
Jumamosi au Jumapili?
'Msitarajie kupambana na adui kwa upanga wa Hamza' Sasa ni kulishwa nguruwe kwa nguvu Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|