|
Na. 052 Jumatano Juni 14 - 20, 2000 |
|
|
|
|
|
Rais Mkapa ulidanganywa na Mkuu wa Wilaya Ndugu Mhariri, NAPENDA kuunga mkono barua ya ndugu Juma Mkuru wa Lugoba Bagamoyo. Yenye kichwa cha habari Bagamoyo haipo hivyo. Kusema kweli ukiacha mambo mengi aliosema huyo bwana kuna moja alosema la mkuu wa Wilaya kumuongopea Rais, kuhusu maendeleo yetu. Mimi nilikuwepo kijijini Matimbwa tarehe 26 Mei 2000 nilimshuhudia mkuu wa wilaya huyo akija pale kijijini baada ya muda mrefu wa kutokufanya hivyo, na kuitisha kikao cha watendaji wa kijiji na wazee wachache wa hapa kijijini na kuwatisha wawadhibiti vijana wao pale kijijini, baada ya kupata tetesi kuwa vijana hao waliazimia kutumia ziara ya Rais wilayani kwao kuwasilisha kilio chao cha muda mrefu cha kuporwa ardhi yao na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia jeshi la magereza (Kigongoni), kilio ambacho kimeshindwa kufanyiwa kazi na ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa muda mrefu tokea (1988-2000). Kwa muda mrefu vijana hao wanaoishi kwa kutegemea kilimo wamejitahidi bila ya mafanikio kupeleka kilio chao hicho kwa viongozi wao wakuu wilayani humu, ili warudishiwe ardhi yao hiyo inayokaliwa na magereza (Kigongoni). Baada ya kutiwa hasara ya mazao na kuvunjiwa vibanda vyao na kufukuzwa huku wakielekezewa mtutu wa bunduki na wababe hao cha kusikitisha pamoja na kiongozi huyo mkuu wa wilaya ofisi yake ilipelekewa barua nyingi hata siku moja hajakaa na pande hizi mbili ili walau tu asikilize matatizo yao na kueleza ukweli halisi kwa wanakijiji wa Matimbwa.Hadi tukadhani barua zetu zilikuwa hazimfikii. Lakini kwa mshangao wa wengi hapa kijijini ni kumuona kiongozi huyo wa wilaya akija kwa vitisho kuzuia kupitia kwa watendaji na baadhi ya wazee, vijana wasitoe kilio chao cha muda mrefu kwa Rais cha kudhulumiwa ardhi yao. Ndugu Rais, na Mkuu wa Wilaya Bagamoyo kwa taarifa kamili mpango huo wa kutoa kilio chao ulikuwepo na utaendelea kuwepo ,na kama mkuu wa wilaya alidhibiti wanakijiji kutoa kilio chao basi tunatumia nafasi hii kukutaarifu Rais kuhusiana na mtendaji wako kutuzuia kutoa kilio chetu kwako.Wananchi wa Matimbwa tunajua tatizo letu haliwezi kumalizwa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Rais kwa heshima upatapo habari za barua hii tutumie mwakilishi wako. Bila kupitia wilayani, maana tushapoteza imani na msimamo wa kiutendaji wa mkuu wa wilaya huyu aje kutusikiliza kilio chetu na haki itendeke. Ardhi hii tulipatiwa na Bwana Paul Sozigwa 1988 nasi vijana tukafyeka msitu na kupanda mazao na kujenga vibanda vyetu. Hatua ya mkuu wa wilaya kutangulia kijijini Matimbwa kabla ya msafara wa rais kututisha ni Ishara tosha, CCM inatawala badala ya kuongoza kama inavyodaiwa na wapinzani. Na hivyo itatufanya tuamini wapinzani ni wenzetu na kutupa tamaa kuwa huenda tukiwachagua watatusikiliza na kutuondolea matatizo yetu. Shabani M. Kiate,
Haki sawa kwa wote 1961, 1964 lakini fursa sawa kwa wote bado? Ndugu Mhariri, Jamani mnaopata nafasi za kuongea majukwaani tuoneeni huruma wasikilizaji. Na wale wanaopambana kisiasa watuonee huruma wananchi wasitufanye nyasi za kusagwasagwa. Iweje tuambiwe "Haki sawa kwa wote iliishapatikana mwaka 1961 na 1964 lakini watu hao hao watueleze kuwa "fursa sawa kwa wote bado haijapatikana?" Waswahili wanamsemo wao:"Mjinga wakati wa kwenda,wakati wa kurudi hapotei njia." Nyie semeni tu.Siye njia ya kwenda tunaijua. Tutaonana mbele ya safari. Shabani Juma,
Kigoma tuko nyuma ya Profesa Ndugu Mhariri, NAANDIKA barua hii kwa uchungu mkubwa nikiwasilisha hisia za watu wa Kigoma. Siyo muda mrefu sana tangu tupitiwe na ndugu yetu Profesa Ibrahim Lipumba hapa Kigoma na kuzungumza wazi mengi juu ya matatizo yetu na akatuahidi kurudi tena. Sisi watu wa Kigoma tumedumazwa sana na kuumizwa sana na sera za CCM kwa miaka yote tangu washike hatamu. Kigoma ni mkoa wenye neema nyingi mfano tunalo ziwa Tanganyika, tuna ardhi nzuri na kubwa yenye rutuba na pia hali ya hewa nzuri.Hata hivyo tumefanywa kuwa maskini wa kutupwa kutokana na sera mbovu za CCM na juhudi za makusudi kuturudisha nyuma kimaendeleo. Kwa kweli tumeshachoka na tulikuwa tukisubiri fursa tu ya kuleta mabadiliko. Katika harakati zetu tulishaanza kwa kujichagulia mbunge wetu Dr. Walid Kabouru. Tangu Profesa aondoke sisi tumeingia katika utekelezaji wa yale aliyotueleza. Hata asiporejea tena sisi hapa tayari kura zetu tunafahamu pa kuziweka hapo Oktoba 29, 2000. Haji M. Maalim,
CCM inaomba kura za nini? Ndugu Mhariri, NI maoni yangu kuwa kila mwenye moyo wa upendo na huruma hawezi kuipa CCM kura yake. Tazama chama hiki, licha ya kuwepo madarakani kwa muda mrefu kilichofanikiwa ni kuzorotesha uchumi wetu kwa kiasi kikubwa mno. Pili kimesababisha matatizo makubwa ya kielimu, kiafya na kijamii kwa kushindwa kuweka sera bora na kuzisimamia. Mimi nashangaa tena kwa kiasi kikubwa kuwa hawa walioifilisi nchi hapa tulipo hawana hata chembe ya haya na bado wanaomba kura zetu. Ndiyo sababu najiuliza wanaomba kura zetu za nini? Tanzania si nchi ya kuwa maskini kiasi hiki. Haya ni matokeo ya ukosefu wa watawala walio wabunifu. Popote ulipo mwananchi jitokeze wakati ukifika ukapige kura kuing'oa CCM na mizizi yake. Usisikilize uzushi wa CCM eti Amani, Amani,! Amani hii imekutwa hata na TANU yenyewe. Machafuko yataletwa na ung'ang'anizi wa CCM kulazimisha kubaki madarakani na siyo upinzani. Kilangagi H. Kilangagi,
Hongera Prof. Lipumba kwa kutufungua
masikio
Ndugu Mhariri, NAOMBA nafasi japo kidogo katika gazeti lako, ili nami nitoe yangu machache. Ni hivi karibuni tu mgombea Urais kwa tiketi ya chama cha wananchi (CUF) Prof. Ibrahim Lipumba aliwaambia ukweli wananchi kupitia kwa waandishi wa habari kwamba CCM hakikufanya lolote la maana kwa wananchi katika kipindi ilichokuwa madarakani. Hayo maneno ni ya kweli kabisa na tunamshukuru Prof.Ibrahimu Lipumba kwa kutufungua masikio Watanzania na kutueleza ukweli wa mambo. Nae katibu mkuu wa CCM Bw.Philip Mangula anadai eti, CCM imeleta maendeleo. Tunataka atueleze ni maendeleo gani ya kiuchumi ya maana ambayo CCM imeyaleta ukilinganisha na miaka na miaka iliyokaa madarakani? huku siyo kutubabaisha tu?. Eti BW. Philip anadai idadi ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba imeongezeka ukilinganisha na wakati tulipopata uhuru. Hivi Bw. Philip anajivunia idadi kubwa ya wanafunzi bila kuangalia ubora wa elimu yenyewe? Hivi sasa watoto wanakwenda kuanza elimu ya msingi ili wakue tu na sio kupata elimu husika. Ndio maana hivi sasa sio ajabu kumkuta mtoto kamaliza darasa la saba lakini hajui kusoma na kuandika. Darasa moja hivi sasa katika shule nyingi za msingi lina wanafunzi zaidi ya 100.Elimu hiyo hiyo ya msingi inakabiliwa na matatizo chungu nzima kubwa kabisa likiwa ukosefu mkubwa wa waalimu. Na sio kwamba walimu hakuna bali eti pesa za kuajiri walimu hakuna, wakati msafara mmoja tu wa Rais Mkapa unafungasha magari chungu nzima tena ya kifahari. Je, utasema hapa serikali haina pesa? Bw.Philip anadai eti Prof. Ibrahim Lipumba amemshauri Rais Museveni wa Uganda kwenda kupigana vita Jamhuri ya Congo. Maelezo haya yanaonesha Bw. Philip ni muongo na hajui kabisa ukweli wa mambo, nia yake ni kuwachanganya wananchi. Prof. Ibrahim Lipumba alikwenda Uganda kama mshauri wa Rais katika mambo ya uchumi tu. Na angalia uchumi wa Uganda ulivyo juu ukilinganisha na kipindi ambacho kabla Prof. Ibrahim Lipumba hakuwa mshauri wa Rais katika mambo ya uchumi wa nchi hiyo. Mwisho kabisa tunakuomba kwa heshima na taadhima Prof. Ibrahim Lipumba uendelee na moyo huo huo wa kuweka mambo wazi, kadri inavyotakiwa. Umewabana CCM vilivyo na usiache bali ongeza "dose" mpaka wakubali ukweli. Dk. K.K.Rashid,
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Mkapa, Karume wapewa tiketi za CCM kugombea urais Kufuatia
kukamatwa kwa Sheikh Mbukuzi na Ricco:
HABARI
Amiri Mbukuzi ahojiwa na polisi Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi watajwa USHAURI NASAHA
MAKALA
MAKALA
MAKALA
MAKALA
HOJA BINAFSI
Makala maalum ya Maulid
MAKALA
Habari za Kimataifaza Kimataifa Lishe
RIWAYA
MICHEZO
|
|
|
|
|