NASAHA
Na. 052 Jumatano Juni 14 - 20, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Makala maalum ya Maulid 
Kumpenda Mtume Muhammad (s.a.w.) 

(Imetayarishwa na Africa Muslims Agency) 

SIFA njema anazistahiki Mwenyezi Mungu; tunamsifu, tunamuomba msaada na tunamuomba msamaha. Tunaomba hifadhi kwa Mwenyezi Mungu atulinde na uovu wa nafsi zetu na matendo yetu mabaya. 

Yeyote ambaye Mwenyezi Mungu amemuongoza hakuna wa kumpotosha na yeyote ambaye Mwenyezi Mungu amempotosha hakuna wa kumuongoza. Ninakiri moyoni na kutamka kinywani kuwa hakuna mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu tu na kwamba Muhammad ni mja wake na ni Mtume wake ambaye Mola wake amemtuma kwa uongofu na dini ya kweli ili dini hiyo izishinde dini zote, wajapochukia makafiri (1) 

Ndugu yangu mpenzi, Mwenyezi Mungu akimpa mja wake imani na matendo mema ni alama ya wema wa mja huyo katika maisha ya ulimwenguni na akhera. Miongoni mwa imani ni kumpenda Mtume Muhammad, Mwenyezi Mungu amfikishie rehema na amani, kipenzi cha Mwenyezi Mungu na kiumbe bora zaidi katika viumbe vya Mwenyezi Mungu ikiwa ni pamoja na binadamu, bali hata majini. Vipi isiwe hivyo na ilhali kumpenda yeye Mtume ni katika masharti ya imani? 

Anasimulia Abuhurairah, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, akinukuu kutoka kwa Mtume ambaye amesema kwamba: "Nina'apa kwa [Mwenyezi Mungu] ambaye nafsi yangu iko mkononi mwake kwamba hawi muumini mmoja wenu mpaka [mimi] niwe napendwa zaidi kwake kuliko mzazi wake na mtoto wake" (2) 

Aidha, haitoshi kuwa unampenda tu bali utangulize kumpenda yeye juu ya kumpenda mzazi na mtoto wako. Hii pia haitoshi bali hakuna budi utangulize kumpenda yeye juu ya kumpenda mke wako, mali yako na watu wote kwa jumla. Anasema Anas kuwa amesema Mtume kwamba: "Hawi muumini mmoja wenu mpaka [mimi] niwe napendwa zaidi kwake kuliko mke wake, mali yake na watu wote" (3) Aidha hii pia haitoshi, bali ni wajibu kutanguliza kumpenda Mtume juu ya kuipenda nafsi yako iliyopo kati ya mbavu zako. Ni kwa sababu hii, ndio maana wakati Omar bin Al-Khattaab aliposema kumwambia Mtume :"Nina'apa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wewe nakupenda zaidi kuliko kila kitu isipokuwa nafsi yangu. Mtume alisema: Hapana [imani yako haiwi kamili] ewe Omar mpaka mimi niwe napendwa zaidi kwako kuliko nafsi yako. Baada ya Mtume kusema hivyo, Omar alisema: Nina'apa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wewe nakupenda zaidi kuliko kila kitu hata nafsi yangu. Hapo Mtume alisema: Sasa [imani yako imekamilika] ewe Omar" (4) 

Ndugu yangu mtukufu, chukua habari hii njema: Je, unapenda uwe pamoja na Mtume huko akhera? Bila shaka jawabu ni: Ndio, ndio, ndio. Lakini pengine inawezekana kuwa huwezi kufanya mengi, hivyo basi chukua Hadithi hii: "Mtu mmoja alimuuliza Mtume kuhusu Qiyama. Mtume naye akamuuliza: Umekiandalia nini? Akajibu yule mtu: Sikukiandalia chochote isipokuwa tu kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Mtume akasema: Wewe ( siku hiyo)utakuwa pamoja na unayempenda" (5)

Endapo unataka uwe pamoja na Mtume ni wajibu wako umpende mapenzi ya kweli yatokayo moyoni, na kuyathibitisha mapenzi hayo katika maneno na vitendo 

Lakini pamoja na hayo, kuna jambo muhimu ambalo Waislamu wengi hulikosea. Jambo hilo ni kwamba Je, kumpenda Mtume kunapatikana moyoni tu au ni kwa nyimbo zinazoimbwa huku na huko katika baadhi ya shughuli? Au kumpenda Mtume kunapatikana kwa kumsifu kwa mashairi katika siku za sherehe za Maulidi na nyenginezo? 

Mapenzi ya kweli, ewe ndugu yangu, yana dalili na vielelezo vinavyoyathibitisha. Kamatana na dalili na vielelezo hivyo. Iwapo unataka kujua ukweli wa mapenzi yako kwa Mtume yapime mambo haya katika nafsi yako:- 

1.KUMFUATA MTUME 

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba: "Hakika, kimepatikana kwenu kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kiigizo chema kwa anayemtaraji [anayemwamini] Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho" (6) Pia amesema Mwenyezi Mungu kuwa: "Na mfuateni [Mtume] ili mpate kuongoka" (7) 

Na amesema Mtume katika Hadithi sahihi kwamba: "Hawi muumini mmoja wenu mpaka mapenzi yake yawe yanafuata mambo niliyo kuja nayo" (8)

Kumfuata Mtume kunatakiwa kuwe katika kila jambo; katika ibada, mahusiano ya kijamii [muaamalaat], tabia na mambo mengine yasiyokuwa hayo.Ni kwa sababu hii ndio maana sharti la kumfuata na kumuiga Mtume limefanywa kuwa ni mojawapo ya masharti mawili ya kukubaliwa amali [Ibada]. Amesema Mwenyezi Mungu: "Basi yeyote anayetaraji [anayeamini] kukutana na Mola wake atende amali njema na asimshirikishe yeyote katika kumwabudu Mola wake" (9) 

Amali njema ni kumfuata na kumuafiki Mtume. Ni kwa sababu hii ndio maana Mtume katika kuielezea sala amesema: "Salini kama mlivyoniona [mimi] nikisali" (10) Na katika kuielezea Hija amesema: "Chukueni kutoka kwangu [namna ya kutenda] matendo yenu [ya Hija]"(11) 

Iwapo litatokea jambo unalotaka kulifanya jiulize: Je, Mtume amelifanya jambo hilo? Jawabu likiwa ni "Ndio", lifanye jambo hilo na jawabu ikiwa ni kinyume cha hivyo basi acha. 

2.KUMTII MTUME NA KUTOMUASI

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa: "Na mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na jihadharini [ na kumpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake] na iwapo mtakataa, basi jueni kuwa hakuna vingine isipokuwa kwamba lililo wajibu kwa Mtume wetu ni kufikisha ujumbe ulio wazi"(12) Na amesema Mwenyezi Mungu: "Na alilokuleteeni Mtume lichukueni na alilowakatazeni liacheni" (13) Na amesema Mwenyezi Mungu: "Na yeyote anayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume bila shaka amefaulu kufaulu kukubwa" (15) Aidha imepokewa kutoka kwa Abuhurairah, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, akisema kuwa: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu kuwa: "Watu wote wataingia peponi isipokuwa yule atakayekataa. Sahaba wakauliza: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, na ni vipi mtu akatae [kuingia peponi]? Mtume akajibu: Yeyote atakayenitii ataingia peponi na yeyote atakayeniasi basi amekataa [kuingia peponi]" (15) 

3. KUMHESHIMU NA KUMUENZI MTUME 

Amesema Mwenyezi Mungu kwamba: ".. ili mumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na mumuenzi Mtume na mumheshimu" (16) Na amesema Mwenyezi Mungu kuwa: "Msifanye kumwita Mtume kati yenu kama mnavyoitana baadhi yenu kwa baadhi yenu" (17) Hii ina maana kwamba msimwite Mtume kwa jina lake kwa kusema: Ewe Muhammad, na badala yake mumuite kwa kusema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu.

4.KUWA NA MSIMAMO WA WASTANI KATIKA KUMPENDA

Kutokana na umuhimu wa kipengele hiki na kutokana na makosa mengi yanayotokea katika kipengele hiki, tutakisisitiza kwa kusema haya yafuatayo:- 

a] Mtume Muhammad, Mwenyezi Mungu amfikishie rehema na amani, ni binadamu. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa: "Sema: Hakuna vingine isipokuwa kwamba mimi ni mwanadamu tu kama nyinyi, ninaletewa wahyi [ufunuo]" (18) Mwenyezi Mungu katika aya hii ameweka wazi kuwa Mtume ni mwanadamu isipokuwa tu amehusika na wahyi [ufunuo]. Pia amesema Mwenyezi Mungu kupitia katika ulimi wa Mtume wake kwamba: "Ametakasika Mola wangu. Sikuwa mimi isipokuwa tu ni mwanadamu niliyepewa Utume"(19) 

b] Wakati Mtume aliposahau katika sala na Sahaba wasimkumbushe kwa kudhani kuwa sala imepunguzwa, Mtume alisema kwamba: "Hakuna vingine isipokuwa kwamba mimi ni mwanadamu tu kama nyinyi, ninasahau kama mnavyosahau. Hivyo, wakati nikisahau nikumbusheni"(20) 

c] Mtume hajui ghaibu [mambo yaliyofichika] isipokuwa tu anasimulia yale mambo aliyofahamishwa na kupewa Wahyi na Mwenyezi Mungu. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa: "Sema: Siwaambii kuwa nina hazina za Mwenyezi Mungu na wala sijui ghaibu na wala siwaambii kuwa mimi ni Malaika.Mimi sifuati isipokuwa tu yale ninayoletewa Wahyi" (21) 

Aidha Mtume aliyakanusha maneno ya vijakazi wawili waliokuwepo kwa Rabia bint Muaawidh waliposema: "Na kwetu yupo Mtume anayejua mambo ya kesho" (22) Aidha Bibi Aisha, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, amesema kuwa: "Yeyote atakaye kuhadithia kuwa [Mtume] Muhammad anajua [mambo takayotokea] kesho, basi usimsadiki" (23) 

e] Mtume hamiliki kujidhuru au kujinufaisha yeye mwenyewe achilia mbali kumdhuru au kumnufaisha mtu mwengine. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa: "Sema: Similiki kwa nafsi yangu manufaa wala madhara isipokuwa tu yale anayoyataka Mwenyezi Mungu" (24) Pia amesema Mwenyezi Mungu kuwa: "Sema: Similiki kwenu madhara wala uongofu" (25) Hiyo ni kwa sababu tu ufalme ni wa Mwenyezi Mungu pekee. Yeye ndiye ambaye kuko mkononi mwake kudhuru, kunufaisha, kutoa na kuzuia, na yeye ndiye mwenye kumiliki ufalme; mwenye kuzuia amri yake. 

Imethibiti katika Hadithi sahihi kwamba Mtume aliwaonya jamaa na ndugu zake na kuwaambia kwamba: "Ziokoeni nafsi zenu na moto. Mimi siwatoshelezeni kwa Mwenyezi Mungu kitu chochote". 

Bali Mtume, Mwenyezi Mungu amfikishie rehema na amani, katika vita vya Uhud alichanwa na kuvunjwa jino lake na wala hakuweza kujizuia asipatwe na hayo. 

f] Kutochupa mipaka katika kumsifu Mtume. Imethibiti katika Sahihi Bukhariy na Sahihi Muslim ikinukuliwa kutoka kwa Omar bin Al-Khattaab, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, kwamba Mtume amesema: "Msichupe mipaka katika kunisifu kama walivyochupa mipaka Wakristo katika kumsifu [Issa] Mwana wa Maryam. Hakuna vingine isipokuwa kwamba mimi ni mja tu, hivyo semeni: Mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake".

Aidha imepokewa kutoka kwa Anas, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, kwamba kuna watu walisema [katika kumsifu Mtume na kumwambia] kuwa: " Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Ewe Mbora wetu na mtoto wa mbora wetu". Mtume akasema: "Enyi watu, semeni maneno yenu na asiwapotoshe Shetani. Mimi ni Muhammad Mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Sipendi mnitukuze zaidi ya daraja aliyonipa Mwenyezi Mungu".

Je, umefahamu hivi sasa, ewe ndugu yangu, maana ya kumpenda Mtume wako na vipi tuyathibitishe mapenzi hayo katika maisha yetu?

Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuweze kumpenda na kumfuata Mtume wetu, na rehema na amani zimfikie yeye, Jamaa na Sahaba wake wote. 

REJEA:

(1) Sura As-Saff 61, aya 9. 
(2) Ameipokea Hadithi hii Imam Bukhariy. 
(3) Ameipokea Hadithi hii Imam Muslim. 
(4) Ameipokea Hadithi hii Imam Muslim na Bukhariy. 
(5) Ameipokea Hadithi hii Imam Bukhariy. 
(6) Sura Al-Ahzaab 33, aya 2. 
(7) Sura Al-Aaraaf 7, aya 158. 
(8) An-Nawawiy. 
(9) Sura Al-Maaida 5, aya 92. 
(10) Ameipokea Hadithi hii Imam Bukhariy. 
(11) Ameipokea Hadithi hii Imam Muslim. 
(12) Sura Al-Maaida 5, aya 92. 
(13) Sura Al-Hashr 59, aya 7. 
(14) Sura Al-Ahzaab 33, aya 71. 
(15) Ameipokea Hadithi hii Imam Bukhariy. 
(16) Sura Al-Fat'h 48, aya 9. 
(17) Sura An-Nuur 24, aya 63. 
(18) Sura Al-Kahf 18, aya 110. 
(19) Sura Al-Israa' 17, aya 93. 
(20) Ameipokea Hadithi hii Imam Muslim na Bukhariy. 
(21) Sura Al-Aaraaf 7, aya 188. 
(22) Ameipokea Hadithi Imam Tirmidhiy. 
(23) Ameipokea Hadithi Imam Bukhariy. 
(24) Sura A-Aaraaf 7, aya 188. 
(25) Sura Al-Jinn 72, aya 21. 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
NASAHA yatimiza mwaka mwaka mmoja

Mkapa, Karume wapewa tiketi za CCM kugombea urais

CCM walilia kiti cha CUF

Kufuatia kukamatwa kwa Sheikh Mbukuzi na Ricco:
Viongozi wa Serikali  watakiwa kuacha udini dhidi ya Waislamu

HABARI
Mauaji ya Mwembechai: Hatimae inquest yafunguliwa

DC aishukuru Finland

Amiri Mbukuzi ahojiwa na polisi

Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi watajwa

USHAURI NASAHA
Mapambano dhidi ya dhuluma ni ya kudumu

MAKALA
Dini na siasa haviwezi kutenganishwa

MAKALA
Mchango wa taasisi ya Dhiynurayn

MAKALA
Sayyidat Fatma:Jumuia iliyosimama dhidi ya dhulma 

MAKALA
Kupiga vita udini zisiwe kauli za kuendeleza udini dhidi ya Waislam

HOJA BINAFSI
Kwa Rafiki yangu Mpendakula

Makala maalum ya Maulid
Kumpenda Mtume Muhammad (s.a.w.)

MAKALA
CCM  na sera za maendeleo

Habari za Kimataifaza Kimataifa

Lishe 
Vyakula vitupatiavyo vitamini C

BARUA

MASHAIRI

RIWAYA
Mapinduzi ya fikra - 4 

MICHEZO
Ongara, Salvatory, Nteze, Mwansasu waenda Ulaya
Mokake aikosoa Yanga


   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita