NASAHA
Na. 052 Jumatano Juni 14 - 20, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA 

CCM na sera za maendeleo: 
Kudumisha ujinga na umaskini ili waendelee kutawala 

Na Rajab Kanyama 

INAFAHAMIKA na kila mtu mwenye akili timamu, kwamba, elimu ndio ufunguo wa maisha, na ndiyo msingi mkuu unaowawezesha wananchi katika nchi yoyote ile kuwa na mafanikio katika shughuli zao za kilimo, ufugaji na biashara.

Ni kweli pia kwamba watu wenye elimu ya kutosha au angalau ile ya kuwawezesha kufikiri huwa wagumu kutawaliwa kienyeji. 

Huwa wagumu kudanganywa na watawala na mara zote hutumia vigezo sahihi katika kufikia maamuzi. 

Watawala, hasa madhalimu huwa hawapendi kuwa na wananchi wenye upeo mzuri wa kufikiri,na ndio sababu tangu utawala wa awamu ya kwanza, elimu ilipewa sifa ya kinadharia tu, katika utendaji hakuna hatua zozote zilizochukuliwa KUBORESHA HALI YA ELIMU NCHINI. 

Na pale elimu nzuri ilipotolewa ilikuwa ni kwa kundi la watu maalumu ambao waliaminika kwamba watakuwa tayari kuendeleza mfumo ule ule wa kudumaza fikra za wananchi kwa propaganda kinyume na hali halisi ilivyo. 

Hii ndio sababu ya kuwepo kwa semi kama "mtapewaje madaraka na huku hamkusoma" na kauli nyingine kama hizo, walionyimwa au waliofanyiwa mazingira ya kupata elimu kuwa magumu ndio wale watambuzi, wasiopenda dhuluma, ambao ni tishio kubwa kabisa la madhalimu tena si Tanzania tu, bali duniani kote. 

Hawa,hawaruhusiwi kukaa pamoja na kuzungumza chochote juu ya mustakbali wa nchi, na wala uhuru wa maoni wao hauwahusu. 

Makala hii, imeshawishiwa na taarifa nilizosoma katika gazeti moja, wiki iliyopita kwamba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa zawadi ya shilingi laki tano, kwa mkazi mmoja wa kijijini, huko Kisarawe, kama pongezi ya hekima zake, pale alipoandika ukuta wa nyumba yake kwa maandishi makubwa kwamba"mtaji wa maskini ni nguvu zake." 

Taarifa hiyo ilieleza kwamba, Mheshimiwa alifurahishwa sana na maneno hayo. 

Mimi nilishangazwa sana na hatua hiyo, maana katika karne hii ya sayansi na teknolojia,masuala ya nguvu kuwa mtaji yamepitwa na wakati. 

Katika karne hii "elimu ndio mtaji wa maskini" lakini kwa vile Mheshimiwa nae ni lazima aendeleze propaganda za kiongozi wa utawala wa Awamu ya Kwanza, anatoa shilingi laki tano kwa mtu binafsi, badala ya kikundi cha maendeleo kilichopo katika eneo hilo, ambako tunaamini zingekuwa na manufaa zaidi, badala ya mtu mmoja ambaye sana atajengewa chuki na wanakijiji wenzake kwa vile wataona kuwa ameukata, maana ugumu wa maisha, hasa vijijini unajulikana. 

Ulaghai wa aina hii ndio umetufikisha Watanzania hapa tulipo, maana kwa sasa walio wengi wanaishi chini ya mstari wa umaskini. 

Asilimia kubwa ya wananchi wa Tanzania, wanaishi kwa kutegemea jembe la mkono, kipato wanachopata kutoka katika kilimo cha aina hiyo, sote tunatambua kwamba hakiwasaidii kukidhi, mahitaji yao muhimu ya kila siku. 

Kama nguvu ndio ingekuwa mtaji, wananchi wengi wa Tanzania wangekuwa matajiri. 

Alichokifanya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuipa nguvu hoja ya wapinzani kwamba serikali ya Awamu ya Tatu imeshindwa kufahamu matatizo halisi ya wananchi na kuchukua hatua za kuyaondoa. 

Wapo watoto wengi tu, wa wananchi wasio na uwezo, wenye vipaji maalum, lakini wameshindwa kuendelea na masomo kwa sabahu ya wazazi wao kukosa uwezo wa kulipa ada na mahitaji mengine chungu nzima. 

Matatizo ya kiuchumi yanayowakabili wazazi wengi, hasa wa vijijini ndio kikwazo kikubwa cha maendeleo ya elimu nchini, jambo linalochangia kuendelea kuwepo kwa umaskini. 

Hakuna maendeleo yoyote ya maana yanayoweza kupatikana katika nchi yoyote bila ya wananchi kushrikishwa. 

Hatua ya kwanza ya kuwashirikisha wananchi ni kuwaelimisha kuhusu mambo yanayowahusu na kuendelea kuwapa watoto elimu bora itakayowawezesha kupanua uwezo wao wa fikra. 

Mtindo wa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na serikali yake kuendelea kudumaza fikra za wananchi utatufikisha pabaya. 

Mwezi Mei mwaka 1999, Mheshimiwa Dk. Omari Ally Juma, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alifanya ziara huko Yombo Vituka na kukutana na wananchi. 

Wakati akiwahutubia, aliwaeleza kwamba, wapinzani wanataka kuvuruga amani ya nchi, kwa kusema kwamba serikali ya Rais Mkapa inapanda mbegu ya kuvuruga amani, kwa vile pengo kati ya matajiri wachache na maskini walio wengi linazidi kupanuka. Bila shaka haya ni maneno yaliyokusudiwa watu wasio na elimu. 

Hawa, ndio viongozi wa Chama Cha Mapinduzi; hawataki kabisa kukosolewa na kupewa tahadhari ya kwamba, matendo yao ya leo, ni hasara kwa taifa siku za mbele. 

Ni jukumu letu wananchi kutumia kura zetu mwezi wa Oktoba 2000 ili tujiletee ukombozi wa kweli. 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
NASAHA yatimiza mwaka mwaka mmoja

Mkapa, Karume wapewa tiketi za CCM kugombea urais

CCM walilia kiti cha CUF

Kufuatia kukamatwa kwa Sheikh Mbukuzi na Ricco:
Viongozi wa Serikali  watakiwa kuacha udini dhidi ya Waislamu

HABARI
Mauaji ya Mwembechai: Hatimae inquest yafunguliwa

DC aishukuru Finland

Amiri Mbukuzi ahojiwa na polisi

Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi watajwa

USHAURI NASAHA
Mapambano dhidi ya dhuluma ni ya kudumu

MAKALA
Dini na siasa haviwezi kutenganishwa

MAKALA
Mchango wa taasisi ya Dhiynurayn

MAKALA
Sayyidat Fatma:Jumuia iliyosimama dhidi ya dhulma 

MAKALA
Kupiga vita udini zisiwe kauli za kuendeleza udini dhidi ya Waislam

HOJA BINAFSI
Kwa Rafiki yangu Mpendakula

Makala maalum ya Maulid
Kumpenda Mtume Muhammad (s.a.w.)

MAKALA
CCM  na sera za maendeleo

Habari za Kimataifaza Kimataifa

Lishe 
Vyakula vitupatiavyo vitamini C

BARUA

MASHAIRI

RIWAYA
Mapinduzi ya fikra - 4 

MICHEZO
Ongara, Salvatory, Nteze, Mwansasu waenda Ulaya
Mokake aikosoa Yanga


   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita