|
Na. 052 Jumatano Juni 14 - 20, 2000 |
|
|
|
|
|
Sayyidat Fatma:Jumuia iliyosimama dhidi ya dhulma
JUMUIA ya wanawake wa Kiislamu ya Sayyidat Fatma iliyopo mjini Moshi, mkoani Kilimajaro, ni moja ya jumuia kongwe na nguzo madhubuti ya maendeleo ya Waislamu. Jumuia hiyo imekuwa ikiwaunganisha wanawake wa Kiislamu wa ndani na nje ya mkoa wa Kilimanjaro hata kuweza kutetea maslahi yao binafsi na yale ya jamii kwa ujumla. Historia yake inaanzia miaka ya 1930, muasisi wake akiwa ni mama Mabrouk (marehemu). Mama huyu alikuwa ni mhamiaji wa Moshi akitokea Mombasa, Kenya. Huko Mombasa alikotokea, tayari wanawake wa Kiislamu walikuwa na umoja wao. Hivyo mama Mabrouk akaiona haja ya kuundwa kwa umoja wa aina hiyo miongoni mwa wanawake wa mjini Moshi. Kwa mujibu wa maelezo ya Sheikh Mussa ambaye ndiye Sheikh wa mkoa, wito wa mama Mabrouk uliitikiwa mara moja ambapo zaidi ya wanawake 30 waliungana. Umoja ukaanza shughuli za kidini kama vile kuandaa maulidi ya mfunguo sita kwa kuzishirikisha wilaya zote za mkoa huo. Kutokana na mipango na uendeshaji mzuri wa Maulidi, sifa za jumuia zikazagaa hivyo ikaanza kupokea wanachama wengi kutoka ndani na nje ya Moshi mjini. Wingi huo wa wanachama ukaifanya jumuia kufahamika zaidi na kupata hadhi. Mbali na kuandaa Maulidi, Sayyidat Fatma pia ilifungua madrasa za watoto wadogo. Zilizokuwapo zikaboreshwa kwa kuzipatia nyenzo za kufundishia, mikeka na hata waalimu. Madrasa katika misikiti maarufu ya mjini Moshi, riadha na ule wa Ijumaa zilianzishwa na kuendeshwa na wanajumuia. Aidha wanajumuia walihamasishwa kuchangia ujenzi wa shule ya msingi Muslim (shule ya msingi Mwenge) pamoja na ukumbi wa shuleni hapo. "Lengo letu kubwa ni kuiendeleza dini ya Allah.Tukiandaa maulid na kusomesha wanetu. Sisi ndio wapokeaji wageni wa wapishi katika hafla zote za kidini",amasema mama Fatuma Makurie. Uongozi ndani ya jumuia hii ni wa kurithi kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Watoto wa waasisi ndio wanaokuja kushika hatamu za uongozi, wakifuata taratibu na mipangilio ya uendeshaji kama walivyowaona wazazi wao. Viongozi hawa huitwa WAKUU. Wakuu hupita nyumba hadi nyumba kutoa taarifa za mikutano. Mara nyingi mikutano hufanyikia nyumbani kwa mkuu mmojawapo. Mama Halima Serengia anaelezea: "Mwaka1954 sisi tulikuwa tayari jumuia madhubuti. Kutokana na umaarufu wetu hapa mjini, ikawa rahisi sana kushirikiana na viongozi wa TANU katika kuwashawishi watu wajiunge na chama. Wale wanajumuia vijana wakajiunga na umoja wa vijana wa TANU(TANU Youth League) wakati wale wenye umri mkubwa basi wakawa ndio wanachama waanzilishi wa TANU hapa mjini." Wapo pia baadhi ya wanajumuia waliojitolea nyumba zao za kuishi zikawa zikitumika kama ofisi za chama. "Nyumba yangu iliyoko Mawenzi ?Road tena na mtaa wa Liwali niliitoa itumike kama ofisi ya TANU.Julius akilala humo,na sisi tunalinda usiku kucha maadui wasijemdhuru",anabainisha mama Makurie. Wanasema pia, Mwalimu Nyerere alipokuwa akipanga safari ya kwenda UNO,Sayyidat Fatma walichangishana thumni thumni kwa ajili ya kuifanikisha safari hiyo. Walijitolea muda wao mwingi kuwapikia wageni wa chama cha TANU WANAPOTEMBELEA MKOANI MWAO. Hapa hawaachi kuutaja mkutano mkuu wa PAFMECA uliofanyika mkoani Kilimanjaro mwaka1962, kwani wapishi pia walikuwa ni wao. Hawakuishia jikoni tu. Walitoka nje ya hapo. Wanasema waliwahi kutembea kwa miguu kutoka Moshi hadi Arusha kuunga mkono uchaguzi huru wa kwanza Tanganyika uliofanyika katika miaka ya 1960. Hata hivyo harakati hizi za kudai uhuru wanazielezea kwa uchungu mkubwa.Tukio ambalo wanajumuia hawatalisahau katika historia ya harakati zao ni kifo cha mtoto Sija, mtoto wa mmoja wa waasisi, Mama Sija Athumani. Kwa mujibu wa Mzee Ally Dobi, baba mzazi wa marehemu Sija,kifo cha mwanae kilitokea baada ya kugongwa na gari ya Mwalimu Nyerere. Dereva wa gari alikuwa katika mwendo wa kasi akielekea nyumbani kwao Sija kuchukua nguo za Mwalimu zilizokuwa zikipigwa pasi na yeye Mzee Ally. Kwa imani kubwa waliyokuwa nayo wazee hawa nakiu ya kutaka kujitawala, hawakufungua kesi yoyote.Walimzika mtoto wao. "Nilisamehe kwa kuchelea kudhoofisha harakati za kupata uhuru. Kesi ingetuchukulia muda mwingi mno. Halafu ukizingatia gari iliyomgonga ni ya kijana wetu (Julius wa Nyerere)nilitupilia mbali mambo ya kesi."Anasema Mzee Ally Dobi. Uhuru kupatikana, Sayyidat Fatma ikatupwa kando. Hawakujulikana tena. "Hata katika hafla ya kuupokea uhuru hatukualikwa. Jumuia ilisahauliwa kabisa." Anasisitiza mama Halima. Sayyidat Fatma imejizatiti katika masuala ya kidini. Safari hii ni kwa mtazamo wa umoja wa Waislamu wote hata nje ya mipaka ya Kilimanjaro. Katikati ya mwaka jana waliandaa kongamano la ujirani mwema kati ya wanawake wa Kiislamu wa Moshi na wenzao wa Arusha. Kongamano lililoamsha udugu wa kidini baina ya pande hizi mbili. Likasisitiza umoja na kuzivunjilia mbali tofauti za madhehebu. Hapana shaka yoyote kutamka kuwa kongamano hili ndilo lililozaa umoja wa vikundi vya wanawake wa Kiislamu Manispaa ya Arusha. Uko mpango kamambe wakujenga hosteli ya wasichana kwa ajili ya kuwapa fursa nzuri ya kujisomea. Ndani yake,zitakuwepo pia ofisi za jumuia. Wataalamu wa fani mbalimbali zikiwemo zile za afya, elimu, uchumi na jamii watapatiwa nafasi nzuri ya uongozi kwa lengo la kuikwamua jamii ya Waislamu. Wahisani wanakaribishwa kuchangia ujenzi wa hosteli hii. Kadhalika jumuia imebeba jukumu la kuwalipa posho waalimu watakaofundisha vipindi vya dini mashuleni. Kila kata imeagizwa kulishughulikia suala hilo kwa wanajumuia wenyewe kuchangishana. Sayyidat Fatma inayapokea mabadiliko yenye kulenga
maendeleo. Ina mpango wa kufanya mkutano mkubwa wa wanajumuia wake, mkutano
ambao utachagua viongozi na kuunda katiba itakayowezesha jumuia kusajiliwa.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Mkapa, Karume wapewa tiketi za CCM kugombea urais Kufuatia
kukamatwa kwa Sheikh Mbukuzi na Ricco:
HABARI
Amiri Mbukuzi ahojiwa na polisi Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi watajwa USHAURI NASAHA
MAKALA
MAKALA
MAKALA
MAKALA
HOJA BINAFSI
Makala maalum ya Maulid
MAKALA
Habari za Kimataifaza Kimataifa Lishe
RIWAYA
MICHEZO
|
|
|
|
|