|
Na. 052 Jumatano Juni 14 - 20, 2000 |
|
|
|
|
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mwishoni mwa wiki iliyopita kiliwapitisha Rais Benjamin Mkapa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bw. Amani Karume kugombea urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu utakovishirikisha vyama vingi vya siasa unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu. Rais Mkapa alipitishwa na Mkutano Mkuu Maalmu wa CCM uliofanyika Dodoma Jumamosi Juni 10, ambapo katika kura 1497 zilizopigwa kumkubali au kumkataa, kura za ndio zilikuwa 1485, kura 7 zilimkataa na kura 5 ziliharibika. Rais Mkapa alikuwa ni mwanaCCM pekee aliyegombea nafasi hiyo. Awali, Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM katika kikao chake cha Ijumaa Juni 9, kilimchagua Bw. Karume kuwania urais wa Zanzibar. Bw. Karume ambaye ni Waziri wa Mawasiliano wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) alipata kura 111 na kuwashinda wanaCCM Zanzibar Dk. Mohamed Gharib Bilal ambaye ni Waziri Kiongozi wa SMZ aliyepata kura 61, Bw. Abdisalaam 15 na Bi. Amina Salum Ali 9 . Bw. Abdisalaam ni Naibu Waziri wa Fedha katika serikali ya Muungano wakati Bi. Amina ni Waziri wa Fedha wa SMZ. Kupitishwa kwa Rais Mkapa kunafanya idadi ya wanowania urais wa jamhuri ambao wamepitishwa rasmi na vyama vyao kufikia wawili. Mwingine ambaye amepitishwa na chama chake kugombea nafasi hiyo kubwa zaidi nchini ni Profesa Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi. Watanzania wengine ambao wanakusudia kuwania nafasi hiyo kwa tiketi ya vyama vyao ni pamoja na Bi. Edith Munuo (NCCR), Bi. Anna Komu (CHADEMA), Bw. Augustine Mrema (TLP), Bw. John Cheyo (UDP) Hata hivyo mchuano mkali unatarajiwa kuwepo kati ya Rais Mkapa ambaye amekuwa madarakani kwa miaka mitano sasa na Profesa Lipumba ambaye ni mtaalamu mahiri wa Uchumi na ambaye imekuwa ikielezwa kuwa anaongea kwa ufasaha na anao uwezo mkubwa wakuchambua masuala. Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wamekuwa wakieleza kuwa Profesa Lipumba ambaye katika uchaguzi wa 1995 "alijitokeza katika dakika za mwisho" safari hii ameonesha kuwa kivutio kikubwa cha wananchi hasa kufuatia ziara zake ambazo anaendelea kuzifanya mikoani kuonana wananchi. Wasemaji hao wamemulezea Profesa huyo kuwa nafasi ya kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kubwa kwa vile ana umri mdogo kuliko Rais Mkapa jambo amblo limefanya akubalike zaidi kwa vijana ambao mwaka huu wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi huo. Wamesema sehemu ya vijana hao hawakushiriki kupiga kura mwaka 1995 kwa vile walikuwa hawajafikia umri wa miaka 18 ambao kwao wanaruhusiwa kupiga kura halali. Kwa upande wa Rais Mkapa mmoja wa wachunguzi hao wa masuala ya kisiasa na kijamii ameeleza, "Mkapa ni mgombea mzoefu na ameiongoza serikali kwa miaka mitano sasa..." Hata hivyo, wameeleza wataalamu hao, "yapo mambo ambayo yanaelekea kumporomosha (Rais) Mkapa". Wamedai kuwa katika kipindi cha utawala wa Rais Mkapa utoaji wa huduma za jamii umepungua sana kiasi cha kumwamcha mwananchi wa kawaida, ambaye ndiye mpiga kura, katika hali ngumu ya maisha. Aidha, wamedai kuwa kitendo cha Rais Mkapa kuchangiwa shilingi milioni moja na matawi ya CCM nchini kote kumwezesha kuchukua fomu ya kuomba kugombea urais wa Jamhuri kwa tiketi ya CCM "kuliwalazimisha wanaCCM wengine waliokuwa na nia ya kuwania nafasi hiyo washindwe kutimiza haki zao za kichama kutokana na utaratibu ambao ni nje ya utamaduni wa CCM" Wameendelea kudai kuwa ilikuwepo mizengwe ndani ya CCM ambayo ilipelekea hata Mama Getrude Mongela kushidwa kujitokeza kuwania nafasi hiyo ambayo kwayo aliwahi kutamka kwamba yupo tayari kuigombea mwaka 2000. "Kubanwa kwa (Mama) Mongela ambaye amewahi kuonesha uwezo mkubwa kitaifa na kimataifa lazima kumeacha jeraha kubwa katika jamii ya wanawake wa Tanzania ...mwaka huu ni mwaka wao wanawake, UN (Umoja wa Mataifa) ilitangaza (kuwa) ni mwaka wa wanawake na uongozi. Aidha, wataalamu hao wa masuala ya siasa na jamii wamenasibisha kunywea kwa Mama Mongela na kauli ya Katibu Mkuu wa CCM Bw. Philip Mangula ambaye anadaiwa kuwaambia wanawake wajitokeze kugombea udiwani na ubunge tu lakini sio urais. Taarifa zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa takribani vikundi 20 vya akina wanawake tayari vimemwandikia Katibu Mkuu huyo wa chama tawala juu ya kauli yake hiyo ya 'kuwabana wanawake'. Aidha, imeelezwa kuwa kauli za vitisho za Mwenyekiti wa Vijana wa CCM, Bw. Emmanuel Nchimbi ziliwanyima demokrasia wanaCCM waliotaka kuomba kugombea urais. Ilidaiwa Bw. Nchimbi alitamka kuwa mwanaCCM atakayechukua fomu kuomba kugombea urais na hivyo kutaka kuchuana na Rais Mkapa angetengwa. Wachunguzi hao wa masuala ya kisasa waliendelea kudai kuwa "CCM imejipunguzia mapenzi" kwa watanzania walio wengi ambao ni masikini kwa uwamuzi wake wa kutoza shilingi milioni moja kama ada ya kuchukulia fomu ya kuomba kugombea urais wa Jamhuri. Wamesema mbali na mizengwe ya akina Mangula na Nchimbi, ada hiyo iliwanyong'onyeza wanaCCM. Uchambuzi wa wataalamu hao umeendelea kuonesha kuwa CCM inao wakati mgumu pia katika uchaguzi wa rais wa Zanzibar ambapo mgombea wake Bw. Karume atamenyana na mwanasiasa mkongwe Bw. Seif Sharif Hamad ambaye anawania kiti hicho kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF). Wakielezea mazingira magumu yanayomkabili mgombea huyo wa CCM, wachunguzi hao wa masuala ya kisasa wamesema wapenzi wa CCM visiwani humo wamegawanyika kutokana na harakati za uteuzi wa Bw. Karume. Mbali na wanaCCM wanne ambao majina yao yalifikishwa katika halmashauri Kuu ya taifa ya CCM, pia walijitokeza Bw. Hassan Diria na Bw. Mohammed Raza kutaka kuwania kiti kinachoachwa wazi na Dk. Salmini Amour. Wawili hawa walijitoa katika hatua za awali za uteuzi kwa namna walivyokuwa wakitajwa kwa rangi na kabila zao jambo ambalo wachunguzi hao wa mambo wanadai litaigharimu CCM katika uchuguzi wa Oktoba 29 mwaka huu. Kwa upande mwingine wamedai "kutupwa" kwa Dk. Bilal kumeleta mgawanyiko mkubwa miongoni mwa wanaCCM visiwani humo. Wameeleza kundi kubwa la Wazanzibar lilionesha kumuunga mkono Dk. Bilal kiasi cha kuweza kuongoza katika kura za maoni katika Kamati Maalum ya CCM Zanzibar. Dk. Bilal pia alipata mamia ya watu kumuunga mkono kwa kusaini fomu yake ya kuomba kugombea nafasi hiyo, tofauti na Bw. Karume ambaye wapiga debe wake wamejaa Bara badala ya Viswani ambako ndiko atapigiwa kura. Aidha, wamedai kwamba kutopitishwa kwa Dk. Bilal kumewanyima Wazanzibar kiongozi msomi. Habari zilizopatika kutoka visiwani zinadai kuwa CUF wametamba kwamba mchuano wa kuwania urais wa Zanzibar umerahisishwa sana kwao kwa CCM kumpitisha Bw. Karume na hivyo "wataibwaga CCM". Wakichambua hali ya mambo visiwani humo wachunguzi hao wa mambo wamedai Bw. Karume hatarajiwi kupata kura kisiwani Pemba na kwamba kundi la Dk. Bilal lina kila dalili ya 'kupiga kura ya hasira'. Wameendelea kudai kuwa CCM pia huenda ikapoteza kura nyingi za wanawake kwa "kumuwekea ngumu Waziri Amina Salum Ali". Wamedai kuwa Waziri huyo mwanamke alishawishiwa ajitoe katika kinyang'anyiro hicho lakini 'sapoti' kubwa ya wanawake wa Zanzibar ilimtaka aendelee ili wanawake hao waone iwapo ni kweli wao hawapewi nafasi ndani ya CCM. Imeelezwa kuwa nyufa hizo zinaelekea kumpa Bw. Maalim Seif nafasi kubwa ya kushinda kiti cha Urais wa Zanzibar. Lakini wachunguzi wa mambo wamedai mbali na nyufa hizo ndani ya CCM, Maalim Seif ameonesha uwezo mkubwa wa kusimamia amani visiwani humo bila nguvu ya dola. Wameeleza katika uchaguzi wa mwaka 1995 Maalim Seif alitangazwa kushidwa na Dk. Salmin kwa chini ya asilimia moja ya kura zilizopigwa na kwamba CUF haikuwa radhi na matokeo hayo kwa madai kuwa haki haikutendeka. Wamedai upevu wa hekima wa Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa Waziri kiongozi wa SMZ ulisaidia kuwapoza wanaCUF visiwani humo kutovuruga amani kutokana na madai ya dhuluma dhidi yao. "(Maalim)Seif aliwatuliza wanaCUF, kisha akaongea na jumuiya ya kimataifa, nao wakamwelewa na Commonwealth (Jumuiya ya Madola) ikaingilia kati"' alidai mmoja wa wataalamu hao na kuongeza kuwa jambo hilo lilimpa heshima kubwa kwa Wazanzibar. |
YALIYOMO
TAHARIRI
Mkapa, Karume wapewa tiketi za CCM kugombea urais Kufuatia
kukamatwa kwa Sheikh Mbukuzi na Ricco:
HABARI
Amiri Mbukuzi ahojiwa na polisi Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi watajwa USHAURI NASAHA
MAKALA
MAKALA
MAKALA
MAKALA
HOJA BINAFSI
Makala maalum ya Maulid
MAKALA
Habari za Kimataifaza Kimataifa Lishe
RIWAYA
MICHEZO
|
|
|
|
|