NASAHA
Na. 052 Jumatano Juni 14 - 20, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
HABARI

Mauaji ya Mwembechai: 
Hatimae inquest yafunguliwa

  • Waislamu wasema isiwe kiini macho cha uchaguzi 
Na Mwandishi Wetu 

Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu imekubali kufunguliwa 'inquest'(uchunguzi) ya mauaji ya Waislamu yaliyotokea katika msikiti wa Mwembechai Februari, 1998.

Inquest hiyo iliyokubaliwa baada ya kilio cha muda mrefu cha Waislamu itasikilizwa katika mahakama ya Kisutu, Juni 20, mwaka huu. 

Kufunguliwa kwa inquest hiyo kunafuatia maombi yaliyotumwa na BARAZA KUU kupitia kwa wakili wake Bw.Said Elmaamry, kwa hakimu mkazi wa mahakama ya Kisutu. Maombi ya Inquest hiyo yalipelekwa tangu Aprili 23, 1998. 

Kiongozi mmoja wa BARAZA KUU aliyeongea na NASAHA ameonyesha wasi wasi wake kuwa huenda inquest hiyo imetolewa kama kiini macho kwa ajili ya uchaguzi Oktoba. 

Kiongozi huyo alisema kwamba huu ni mwaka wa pili tangu Waislamu tuombe Inquest, lakini serikali imekuwa bubu na inaibuka siku chache kabla na uchaguzi. 

Kwa mujibu wa sheria panapotokea kifo cha utatanishi au mauaji, mahakama inawajibika kuandaa inquest bila hata ya kuombwa ili kujua sababu ya kifo cha mauaji hayo. 


DC aishukuru Finland 

Na Rajab Rajab, Morogoro 

MKUU wa wilaya ya Morogoro Bw. Mathew sedoyoka ameushukuru umoja wa wananchi wa Finland kwa kuchangia zaidi ya shilingi milioni Mia sita katika shughuli mbalimbali za maendeleo mkoani Morogoro.

Bw. Sedoyoka alitoa salamu hizo jana wakati akifungua semina ya siku tatu inayovihusisha vikundi mbalimbali vya maendeleo visivyo vya kiserikali mkoani Morogoro .Semina hiyo iliandaliwa kwa ushirikiano kati ya muungano wa vikundi visivyo vya kiserikali (NGO), umoja wa nchi ya Finland na mkoa wa Morogoro (UHUSIANO ) pamoja na shirika la maendeleo lisilo la kiserikali , hapa ­ Finland lenye makao yake mjini hapa. 

Bw. Sedoyoka alisema vijana wa Tanzania wameanza kufaidika na mchango uliotolewa katika kuleta maendeleo kwa njia ya kujitegemea. 

Akizungumza kabla ya ufunguzi wa semina hiyo mwenyekiti wa (NGO ) umoja unaofadhiliwa na Finland Bw. Ndumey Mukama amesema ubinafsishaji nchini umechangia udhaifu katika maendeleo. 

Alisema kama ambavyo vijana wa ufini wanavyopenda shughuli za maendeleo ya kujitegemea , watanzania nao wanapaswa kuwa hivyo hasa kwa kujifunza kupitia kwa vikundi hivyo. 

Semina hiyo ilihusisha jumla ya washiriki sabini kutoka vikundi mbalimbali vya maendeleo vya Finland na Tanzania . hususan Morogoro. 


Amiri Mbukuzi ahojiwa na polisi

Na Mwandishi Wetu 

POLISI walimkamata na kumhoji Amir wa Shura ya Maimamu Sheikh Juma Mbukuzi Jumanne ya Juni 6, mwaka huu. Sheikh Mbukuzi alikamatwa na kuhojiwa kwa zaidi ya masaa manne kufuatia nasaha zake alizozitoa katika Msikiti wa Mtambani Jumapili ya Juni 4, mwaka huu kwenye hafla ya kuwakumbuka na kuwaombea dua Waislamu waliouliwa na polisi Mwembechai.

Akiongea baada ya swala ya Isha katika msikiti wa Mujahidina ulioko eneo la Mburahati jijini, Amir Mbukuzi alidai kuwa alipigiwa simu na polisi mmoja wa kituo Kikuu cha polisi na kumtaka aripoti kituoni hapo. 

Katika taarifa hiyo ambayo aliitoa Jumamosi iliyopita Amir Mbukuzi alisema kuwa baada ya kupokea simu hiyo alimtaka polisi amweleze kile walichomuitia. 

"Askari huyo alimpa simu bosi wake ambaye aliniambia kuwa wanahitaji kunihoji juu ya hotuba niliyoitoa Mtambani", alisema Sheikh Mbukuzi. 

Ameendelea kueleza kuwa baada ya kufahamu sababu ya kuitwa kwake alimweleza polisi yule kuwa ataenda huko baada ya kuswali kwani muda wa swala ulikuwa umekaribia. 

Huku waumini wa Msikiti wakimsikiliza kwa makini, Sheikh Mbukuzi aliendelea kusema kuwa baada ya swala nilienda na polisi wakanitaka nitoe ufafanuzi juu ya hotuba yangu wakitaka kujua eti kwanini nimesema kuwa viongozi wa CCM ni wabovu, kwanini nimesema mwenge sawa na koroboi eti kwanini nawataka wanawake Wa kiislamu wawanunie waume zao wanaong'ang'ania CCM. 

Kuhusu ubovu wa viongozi, Sheikh Mbukuzi amesema, "niliwaambia polisi kuwa, mimi naamini kuwa viongozi hao ni wabovu kwa vile hawatendi uadilifu katika kazi yao", alisema na kusisitiza siyo waadilifu kwa vile wanawabagua Waislamu. 

Juu ya usemi wake wa kufahamisha mwenge na koroboi, Sheikh Mbukuzi akasema kuwa , "nimewaeleza kwamba kauli hiyo niliitoa wakati natoa ufafanuzi wa wanafalsafa kuhusu mambo yanayoleta na kudumisha amani na utulivu katika jamii", kauli hiyo ilikusudiwa kuonesha udhaifu wa mwanga wa mwenge ambao ni sawa tu na ule unaotolewa na koroboi. Akaongeza kuwa lengo lilikuwa kuwazindua wale wanaodhani kuwa hata kama misingi ya kujenga amani na utulivu itavunjwa basi tukiwasha mwenge tutauweka na kuidumisha amani. 

Kuhusu wanawake kuwanunia waume zao wanaong'ang'ania CCM, Sheikh alisema kuwa "nimewaeleza polisi kuwa Uislamu unapinga dhuluma na umeharamisha Muislamu kumsaidia dhalimu, wanaume wanaoishabikia CCM wanasaidia dhuluma hivyo wake zao hawana budi kuwanunia. 

Akiendelea kutoa taarifa, Sheikh Juma amesema kuwa baada ya mahojiano yaliyodumu zaidi ya masaa manne, polisi walimtaka awapelekee ushahidi wa maandishi kutoka kwenye Qur'an unaoruhusu Waislamu kuchanganya siasa na dini. Sheikh alisema kuwa aliwatumia kiasi cha aya 20 zinazothibitisha kuwa Uislamu hautenganishwi na siasa kama ilivyo kwa dini nyingine. 

Alipotaka kujua kutoka kwa polisi endapo akina Pengo walioandika kitabu kuikosoa serikali na huyo Kakobe wameitwa na kuhojiwa, alijibiwa kuwa mambo hayo hufanywa kwa siri na kuwa polisi hawatangazii umma juu ya watu wanaowahoji. 

"Mimi nimewaeleza kuwa amani na utulivu katika nchi hii itatoweka endapo vyombo vya polisi vitashindwa kutenda uadilifu", alimalizia Sheikh Mbukuzi. 

Baadaye Sheikh Mbukuzi alimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa polisi walimwambia kuwa lengo la kumhoji ni kutaka kuona endapo vifungu vya sheria vilivyopo vinawaruhusu kumshitaki Sheikh huyo kwa matamshi yake. 

Waumini kadhaa walionekana kutoridhishwa na hatua hiyo ya kukamatwa Sheikh wao. Mzee mmoja wa makamu aliyejitambulisha tu kwa jina la Fadhili alisema kuwa yeye haoni jambo jipya alilosema Sheikh hadi akamatwe. 

"Haya masuala ya kudhulumiwa kwetu yalishafika hata kwa Rais sasa lipi jipya alilosema Sheikh wetu? Kama ni hili la kutoichagua CCM kwani wao walitaraji nini ikiwa wamekataa kuyashughulikia matatizo yetu?" 

Muumini mwingine aliyejitambulisha kama Ustadh Ally Masoud alisema kuwa lazima serikali ikubali ushauri uliotolewa na Sheikh Mbukuzi ili kudumisha amani na utulivu tulionao. 

"Sheikh wetu alitaja mambo manne ya kuleta na kudumisha amani alipokuwa anaongea pale Mtambani sioni baya hata moja. Sasa kwanini ahojiwe?" aliuliza Ustadh Ally. 

Kwa ujumla hotuba ya Sheikh Mbukuzi aliyoitoa Mtambani ililenga kuwatanabahisha wananchi na watawala juu ya umuhimu wa kuacha propaganda na badala yake wazingatie mambo ya msingi yatakayodumisha amani iliyopo nchini. 

Sheikh Mbukuzi alimnukuu mwanafalsafa wa Kiislamu alitaja misingi minne ya kuleta amani kuwa ni uadilifu wa viongozi, wataalam watakaotumia elimu zao kutumikia jamii, matajiri watakaotoa mali zao kusaidia wasionacho na dua za maskini na mafukara. 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
NASAHA yatimiza mwaka mwaka mmoja

Mkapa, Karume wapewa tiketi za CCM kugombea urais

CCM walilia kiti cha CUF

Kufuatia kukamatwa kwa Sheikh Mbukuzi na Ricco:
Viongozi wa Serikali  watakiwa kuacha udini dhidi ya Waislamu

HABARI
Mauaji ya Mwembechai: Hatimae inquest yafunguliwa

DC aishukuru Finland

Amiri Mbukuzi ahojiwa na polisi

Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi watajwa

USHAURI NASAHA
Mapambano dhidi ya dhuluma ni ya kudumu

MAKALA
Dini na siasa haviwezi kutenganishwa

MAKALA
Mchango wa taasisi ya Dhiynurayn

MAKALA
Sayyidat Fatma:Jumuia iliyosimama dhidi ya dhulma 

MAKALA
Kupiga vita udini zisiwe kauli za kuendeleza udini dhidi ya Waislam

HOJA BINAFSI
Kwa Rafiki yangu Mpendakula

Makala maalum ya Maulid
Kumpenda Mtume Muhammad (s.a.w.)

MAKALA
CCM  na sera za maendeleo

Habari za Kimataifaza Kimataifa

Lishe 
Vyakula vitupatiavyo vitamini C

BARUA

MASHAIRI

RIWAYA
Mapinduzi ya fikra - 4 

MICHEZO
Ongara, Salvatory, Nteze, Mwansasu waenda Ulaya
Mokake aikosoa Yanga


   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita