|
Na. 052 Jumatano Juni 14 - 20, 2000 |
|
|
|
|
|
Viongozi wa Serikali watakiwa kuacha udini dhidi ya Waislamu
VIONGOZI wa chama tawala na serikali hususan Wakatoliki wanaoshikilia nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali ndani ya Chama cha Mapinduzi na serikali wametakiwa kuacha kupenyeza udini wao dhidi ya Uislamu ambao imedaiwa tayari umeifikisha nchi pabaya. Hayo ni majumuisho ya pamoja ya maoni yaliyotolewa na wananchi mbali mbali waliozungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki kufuatia kukamatwa kwa Kiongozi wa Shura ya Maimamu, Sheikh Juma Mbukuzi na Kiongozi wa kikundi cha Mihadhara ch Almalid International, Ustaadh Said Ricco, baada ya kutoa maoni kuhusu dhulma dhidi ya Waislam nchini katika hafla ya kumbukumbu ya mauaji ya Mwembechai iliyofanyika Msikiti wa Mtambani hivi karibuni. Katika maoni hayo wananchi hao wamedai kuwa Kanisa Katoliki ndio chanzo cha sababu zilizopelekea mauaji ya Mwembechai. Sheikh Mbukuzi na Ustaadh Ricco walikamatwa na kuhojiwa katika Kituo cha Kati cha Polisi jijini kwa masaa kadhaa na kisha kuachiwa. Wameeleza wazungumzaji hao kwamba kauli zilizotolewa na Paroko mmoja wa Kanisa Katoliki Mburahati, Dar es Salaam, "ziliichagiza serikali" mkoani Dar es Salaam na hatimaye polisi walitumwa kwenda kuuvamia Msikiti wa Mwembechai kwa kile kilichoelezwa na serikali kuwa ni kumkamata kiongozi wa mihadhara ya Kiislam iliyokuwa ikiendelea msikitini hapo ambayo ilidaiwa ilikuwa ikiukashifu Ukristo. Wazungumzaji hao pia wamelishutumu Bunge na chama tawala cha CCM kwamba vyombo hivyo vilichukua misimamo yao juu ya suala hilo kwa kupuuza madai ya Waislam ya walioua wachukuliwe hatua na iundwe tume kuchunguza madai ya Waislamu. "Bunge ndicho chombo tunachokitegemea kulinda haki za raia, lakini cha ajabu likagoma hata kuunda tume yake ya uchunguzi kwa madai hakuna pesa, na hii CCM nayo katika kikao chake mashuhuri kabisa ikapongeza kitendo kile cha polisi kuwaua Waislamu", alisema mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Abdillah Kassige, mkazi wa Mtoni, Temeke. Hata hivyo imedaiwa na mmoja wa wananchi waliozungumza na Nasaha kwamba mbali na kuwepo madai kuwa Wakatoliki wanaendeleza udini dhidi ya Waislamu, Wakristo wengi wasio Wakatoliki hawalielewi hilo na wamekuwa 'wakishirikishwa bila ya wao kujua'. "Ukisoma kitabu cha (Dk.) Sivalon utaona kuwa Wakatoliki hapa Tanzania wanasema kuwa maadui zao wakuu ni wawili; Uislamu na Umarx na wakaweka mikakati ya kupinga kuenea kwa Uislamu", alisema Mzee Farahani ambaye alidai "taarifa" hiyo ipo katika sura za mwanzo za kitabu cha Kanisa Katoliki na Siasa Tanzania 1953 Hadi 1985 kilichoandikwa na Dr. John C. Sivalon. "waprotestant wakikisoma kitabu hicho ndio watajua Wakatoliki wamefanya nini na wanafanya nini nchi hii kuna sehemu (ya kitabu hicho) inaeleza jinsi Wakatoliki walivyofanikiwa kujaa Bungeni baada ya mikakati yao na (Dk.) Sivalon kanukuu taarifa ya kanisa hilo kwamba bunge lilikuwa na asilimia 75 Wakristo na katika hao asilimia 70 ni Wakatoliki",aliendelea kufafanua Mzee Farahani. Amedai kwamba kwa maana hiyo Wakristo wasio Wakatoliki walio madarakani wapo kwa muda tu na kwamba ni mpango wa Kanisa hilo kuwaondoa kidogo kidogo baada ya kuwakandamiza waislam. "Hao Waanglikana na Walutheri na wengine wote wasio Wakatoliki wanashikilia vyeo hivyo katika kipindi cha mpito tu baadaye wataanza kuenguliwa mmoja mmoja", alisema. Aidha, imedaiwa na watoa maoni hao kwamba katika siku za hivi karibuni kanisa hilo limekuwa likitoa mwelekeo wa siasa za Zanzibar na pia limetunga kitabu mahususi kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao. "Lakini cha ajabu", alishangaa mwananchi mmoja, "wakati (Wakatoliki) wanafanya hivyo, serikali inawadhibiti Waislamu; tena kwa kufanya propaganda za kuwatisha wasiingie katika vyama vinavyoongozwa na Waislamu". Mwananchi huyo aliongeza kufafanua madai yake kwamba vipo vyama vingine mbali na CCM ambavyo viongozi wake ni Wakatoliki lakini hivyo haviguswi na kwamba kipo kingine ambacho mbali ya kuwa kiongozi wake alikuwa ni Mkatoliki chama hicho kilijaa viongozi na wanachama wa kabila fulani lakini pia hakikuguswa kwamba kina ukabila kwa sababu aliyodai mwananchi huyo kuwa ni "cha kwao Wakatoliki". Hata hivyo, mwananchi huyo ambaye aliomba asitajwe gazetini hakukitaja chama hicho kwa jina. Akiongea kuhusu madai ya propaganda ya kuwadhibiti Waislamu wasishiriki siasa , Mzee Majaliwa wa Temeke Mwisho amedai kuwa wazee wa Kiislamu ndio walioanzisha TANU na ndio iliyoleta Uhuru wa nchi hii. "hii ada (mazoea) ya viongozi wa CCM kupiga kelele dhidi ya Waislamu katika siasa ni unafiki unaopingana na historia ya nchi hii", alieleza Mzee Majaliwa ambaye anakadirika kupindukia umri wa miaka 70. Amedai kuwa wakati wa kupigania uhuru TANU ilijaa Waislamu na kwamba Wakatoliki wengi walikuwa wakiwatumikia wakoloni. "Waislamu ndio walioilea TANU na hilo linajulikana na Wakristo wote wasiokuwa wanafiki ndani ya CCM", amedai Mzee Majaliwa. Akisimulia kwa uchungu mzee huyo alisema Waislamu wa wakati huo walikuwa wakipigana kumng'oa mkoloni kutoka nchini na kwamba jambo hilo halikufanyika kwa sababu ya dini au rangi ya uzungu ya mkoloni yule. Akifafanua kwamba TANU haikuwa na ubaguzi wa kidini, Mzee Majaliwa alisema: "Waislamu walijaa TANU ili kuondoa dhuluma ya mkoloni, ndio maana Wakristo walijiunga na chama (TANU) bila kutajwa kwa dini zao, alikuja (Mwalimu) Nyerere (ambaye alikuwa ni) Mkatoliki, akaja (John) Rupia (ambaye alikuwa) ni Muanglika". Mzee mwingine alidai kwamba "tabia" ya viongozi wa CCM kuwasakama Waislamu ni utekelezaji wa sera za udini dhidi ya Waislamu. "Huu ni mpango mahsusi wa kutuondoa Waislamu katika siasa ili wapate kutukandamiza katika nchi yetu kama ambavyo tayari wamekwisha tukandamiza katika kisomo kizuri (elimu ya juu), na vyeo makazini Bungeni wamejaa wao na hata udiwani wanataka wajae wao tu", alisema mzee huyo ambaye aliomba asitajwe gazetini kwa vile wanae wawili wanaofanya kazi shirika la reli wanaweza "kuharibiwa kazi zao". Katika kile kilichoonekana ni kuzidi kuonesha jinsi Kanisa 'linavyopenyeza mkono' wake serikalini wananchi wamehoji mkengeuko wa Rais Benjamin Mkapa katika kuyashughulikia matatizo ya Waislamu aliyopelekewa mwanzoni mwa mwaka jana. "Mwezi wa kwanza (Januari) mwaka jana Waislamu tulipomsomea Rais (Mkapa ) risala yetu, majibu yake (Rais Mkapa) yalikuwa mazuri, lakini kuja mwezi wa nane (Agosti) tulipokumbushia Rais katugeukaanasema yeye ni rais wa wote na hawezi kuwapuuza wasiokuwa Waislamu", alieleza Bw. Maulidi wa Buguruni Sokoni. Bw. Maulidi na wenzake wamedai kwamba Rais Mkapa alibadili mwelekeo katika masuala yale ya Waislamu baada ya kuwasikiliza viongozi wa kanisa. "Kwa mfano sisi tunataka Tanzania ijiunge na OIC, (Kardinali) Pengo ametuambia Waislamu tulipeleke jambo hili Bungeni kwa hiyo Pengo alikwishazuia OIC isisshughulikiwe katika ofisi ya Rais sasa anatusukumia Bungeni ", alichangia mwananchi mwingine aliyekuwa jirani ya Bw. Maulidi akiuza matunda katika soko hilo la Buguruni. "...Waislamu tutegemee nini ikiwa mshitakiwa ni mbuzi na hakimu ni mbwa mwitu?", alihoji mwananchi huyo. |
YALIYOMO
TAHARIRI
Mkapa, Karume wapewa tiketi za CCM kugombea urais Kufuatia
kukamatwa kwa Sheikh Mbukuzi na Ricco:
HABARI
Amiri Mbukuzi ahojiwa na polisi Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi watajwa USHAURI NASAHA
MAKALA
MAKALA
MAKALA
MAKALA
HOJA BINAFSI
Makala maalum ya Maulid
MAKALA
Habari za Kimataifaza Kimataifa Lishe
RIWAYA
MICHEZO
|
|
|
|
|