NASAHA
Na. 052 Jumatano Juni 14 - 20, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA

Dini na siasa haviwezi kutenganishwa: 
Sheria ya Musa ilikuwa 'Dini' pia ilikuwa 'siasa' 

Na Mwinjilisti Kamara Kusupa 

MTUME na Nabii Mussa alikuwa na sura mbili, yeye kama Mtume na Nabii mkuu, alikuwa kiongozi wa dini. Lakini pia Mussa kama "Administrator" alikuwa mtawala na kiongozi wa kisiasa. Anayepingana na ukweli huu labda ana tafsiri yake ya siasa, na pengine ana tafsiri yake ya dini iliyo tofauti kabisa na tafsiri yangu.
 

MUSSA alikuwa na sura mbili alikuwa na sura ya dini na upande mwingine sura ya siasa. Sheria yake Mussa pia ilikuwa na sura mbili, sura ya dini na sura ya siasa, lakini vyote viwili vilichanganyikana pamoja. Hakuna ambaye angeweza kutenganisha wala ambaye angeweza kusema mimi natekeleza sheria ya Mussa kama dini tu lakini kisiasa nina kitu kingine cha kutekeleza ambacho ni tofauti na hii sheria. Wala hakuna ambaye angeweza kusema mimi nitaitekeleza sheria ya Mussa kwasababu ya manufaa ya kisiasa tu lakini nitakuwa na dini yangu iliyo tofauti na hii sheria. Sheriaau Torati ya Mussa ilikuwa ndiyo mtawala wa mambo yote yanayohusu maisha ya Myahudi kama mwanadamu yaani kuanzia maisha yake ya kiroho na maisha yake ya kimwili pia. Sheria ya Musa ilifanya kazi mbili, kwanza ilimwezesha mtekelezaji au mtendaji wa sheria hiyo akiwa kama binaadamu aweze kuhesabiwa kwamba ni mwenye haki mbele za Mungu, yaani sheria ilimfanya mtu kuwa "upright with God"

Lakini pia sheria ilimfanya mtu kuwa mwenye haki mbele ya mtu mwingine na papo hapo kuwa mwenye haki mbele ya jamii kwa ujumla. Kwa kifupi sheria ilisimamia haki ya Kimungu na haki ya Kijamii yaani "Social justice." Ni hii "social justice", ndiyo inayozaa amani katika nchi na katika jamii. Amani si kitu kishukacho kama zawadi kutoka kwa Mungu bali ni tunda la haki. Pasipo haki hakuna amani. Lakini sheria ya Mussa ilikuwa ni nini hasa? Kwa tafsiri rahisi sheria ilikuwa ni mfumo, sheria ulikuwa ulikuwa ni mpango wa uhakika wa maisha sheria iliongoza maisha ya mtu kiroho na kimwili pia, na kwa maana hiyo sheria ilisimamia uhusiano mwema kati ya mtu na mtu, kwani maslahi ya kila mmoja katika jamii yalilindwa na sheria. 

Yatima hakustahili kuhisi anapungukiwa na kitu cha kumwondolea furaha yake katika maisha maana sheria ilichukua majukumu ya Baba au mama aliyekufa na kumlea mtoto wa Kiyahudi, wala mjane hakupaswa kuhuzunika ama kuhisi upungufu utokanaona kufiwa na mumewe kwani sheria ilichukua majukumu yote ya mume aliyekufa na kuziba pengo hilo kwa mjane. 

Kwajili hiyo, kwa mtazamo wa ndani, sheria ya Mussa ilikuwa na "morals" ndiyo maana mwenye kuifuata alibarikiwa na Mungu na mwenye kuipuuza alilaaniwa. Hii ndiyo tofauti kubwa kati ya sheria ya Mussa kama kitu kitokacho kwa Mungu, na sheria za wanadamu ambazo mara nyingi zinakuwa "immoral" kutokana na ukweli kwamba zinatungwa kwa lengo la kukidhi maslahi ya binafsi ama wakati mwingine zinatungwa kwa lengo la kukomoana, kupambana n.k. 

Matatizo ya kijamii hayawezi kutatuliwa na sheria ambazo lengo kuu ni kupambana na wahusika, badala yake matatizo ya kijamii yatatatuliwa na sayansi au mfumo ulio sahihi utakao hakikisha haki ndiyo inayotawala katika jamii. Matatizo yanayotokea hapa nchini na katika nchi nyingi za Kiafrika ni kukosekana kwa mfumo sahihi wa kuhakisha nchi inaendeshwa katika misingi ya haki. Na mara inapokosekana haki, hapo ndio huwa mwanzo wa mtafaruku katika jamii maana lazima yatainuka makundi ya kuipigania haki ama kuzipigania haki zao, na dola nayo huinuka kupambana na wapigania haki kwa nguvu zake zote kwa kisingizio cha kulinda usalama wa taifa au kulinda amani. 

Haujapatikana bado mfumo utakaofanya kazi mbili kwanza kukidhi matakwa ya kiroho na kisha matakwa ya kijamii. Kinachofanyika sasa ni ubabaishaji mtupu. Ubabaishaji wa kutenganisha madarakaya dola na utawala wa Mungu, wakati huyo raia ambaye dola ina mamlaka juu yake ana uhusiano wa moja kwa moja na Mungu ambaye dola kwa namna moja au nyingine huyo Mungu haimtambui. 

Mtu ambaye kwa njia ya roho ameungamanishwa na Mungu na kwa njia ya mwili ameungamanishwa na dola atajikuta anayo kazi ya kuchukuliana na mabwana wawili, mmoja yuko juu mbinguni anataka maagizo yake yafanyike na mwingine yuko hapa duniani lakini kajiweka juu sana kwa njia za kikatiba na kisheria, naye huyu Bwana wa duniani anataka hilo alitakalo yeye lifanyike. 

Kwa vyovyote utawala wa nchi, ambao kimsingi umemwasi Mungu kama ilivyokuwa utawala wa nchi za Kikomunisti, na nchi zingine za kijamaa kama Tanzania ambazo ziliendana katika uasi ule ule wa kikomunisti ingawaje zilijifanya kuruhusu dini, siku zote umewatia raia zake majaribuni. 

Hapo ndipo wengine walipoona ni heri watafute hekima ya kuwawezesha kuchukuliana na uasi wa dola ili tu waishi vizuri duniani kuliko kuchukuliana na Mungu lakini wafarakane na dola iliyoasi, wakakubaliana kimsingi kwamba hawatachanganya dini zao na siasa za nchi. Naziita dini zao kwa sababu najua wazi kwamba Mungu kamwe hawezi kuafiki unafiki. 

Unafiki unakuja ama unadhirika kwa njia hii:-chukulia kwamba kuna mhubiri ambaye yeye amekubaliana kwa dhati na dhana ya kutokuchanganya siasa na dini ya kisha anawaendea waumini ili kuwahubiria maneno ya Mungu, anafungua kitabu kitakatifu na kunukuu andiko kutoka kitabu cha Mussa kiitwacho Kumbukumbu la Torati 281. Pasipo kujali kwamba Torati ya Musa ulikuwa ni mfumo, bali yeye anaendelea kuwasomea watu maneno haya, "Na itakuwa hapo utakapoisikiza sauti ya Bwana Mungu wako, na kuyafanya kwa bidii maagizo yote nikuagizavyo hivi leo, ndipo baraka hizi zitakapokufuata, utabariki wa uingiapo, utabariki wa utokapo ...n.k. 

Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya Bwana Mungu wako usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake kukupata. Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani. Litalaaniwa kapu lako na chombo chako cha kukandia. Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. Utalaaniwa uingiapo, utalaaniwa utokapo. Bwana atakuletea mashaka na kukemewa katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya. Nawe siku zote utaonewa na kutekwa nyara wala hapatakuwa na mtu wa kukuokoa.....Mgeni aliye kati yako atazidi kupaa juu yako nawe utazidi kushuka chini. Yeye atakukopesha wala wewe usimkopeshe. Wewe utakuwa mkia yeye kichwa. Watu wanaweza kumwamini wasikiapo habari za baraka na laana kwakuwa tu hali halisi ya maisha yao na mazingira ya nchi wanayoishi yanafanana na hayo yaliyoandikwa. 

Kwa nchi maskini kama Tanzania ambayo uchumbi wake hauko huru na wala hauko mikononi mwa wananchi badala yake uko mikononi mwa wageni, ni rahisi mtu kujionea maisha yake yanaangukia katika mstari mmojawapo wa hayo anenayo Mussa, labda analima pamba na pamba yake inakwenda nje ya nchi kutengeneza nguo na mavazi mengine lakini yeye mwisho wa yote anaambulia mitumba,watu wengine wanazivaa kwanza nguo hizo wakiisha zichoka ndipo analetewa yeye (aliyelaaniwa) azivae. 

Maana yake ni kwamba analima pamba lakini hafaidi matunda ya jasho lake. Ama kwa mfugaji ambaye anauza mifugo yake, inachinjwa, lakini yeye na wanawe wanakata mwaka mzima bila ya kula nyama, kisha ngozi za ng'ombe, mbuzi, kondoo na wanyama pori zinapelekwa nje ya nchi huko zinatengenezwa viatu lakini wengine wanavivaa kwanza viatu hivyo na wakiisha vichoka ndipo yeye analetewa kama mitumba anunue na kuvaa, Je, ni kitu gani kitakachomfanya asiamini kwamba amelaaniwa? 

Nchi inayofikia hatua ya watu wake kuvaa mitumba kuanzia nguo za nje hadi nguo za ndani kama chupi, sidiria, soksi na gagulo n.k. taifa hilo likihubiriwa habari za baraka na laana litaachaje kusikiliza kwa makini wakati mahubiri yanagusa hali halisi ya maisha ya watu wake? Hapo ndipo watu wengine wanaweza kulia, au kutubu lakini kinachowasukuma kufanya yote hayo siyo ile hali ya roho zao kumpenda Mungu bali ni kule kuelemewa na matatizo ya kiuchumi ambayo kimsingi yamesababishwa na mfumo mbaya wa uchumi katika ngazi ya kimataifa na pia mfumo mbaya wa uchumi ndani ya nchi yenyewe. 

Mifumo ambao kabisa Mussa hahusiki nayo, wala Mungu hahusiki kwa namna yoyote ile badala yake wahusika wakuu ni yeye mhubiri, watawala wa nchi, tabaka la wadhulumaji, na tabaka la hao wadhulumiwa. Mambo kama hayo ya kulia na kutubu yanapofanyika katika mzunguko wa kila wiki yaani "routine", ni rahisi watu kujidanganya kwamba wanamwabudu Mungu na pia kujidanganya kwamba wanao uhuru wa kuabudu, kwa kuwa wanayo dini yao, au dhehebu lao ambalo halina matatizo na serikali lakini kumbe wakipimwa katika maana halisi ya "Religio", hawa hawana uhusiano wowote mzuri na Mungu wao na pia hawana uhusiano mzuri baina yao ndani ya nchi badala yake wana uhusiano wa mtu kumla mtu wala hawana uhusiano ulio hai na Mungu wao kama alivyokusudia mwandishi wa andiko hilo yaani Nabii Mussa. 

Kilichofanyika hapo ni kuchanganya mambo yasiweza kuchanganyika pamoja na yakaliwa na binaadamu ama yakamfaa mtu katika maisha yake. Udhalimu ulioko duniani + udhalimu ulioko nchini + uasi wa dola + unafiki wa Mhubiri = na kilio, toba ya kijinga, na kukata tamaa kwa waumini. Kwasababu mfumo wa sheria ya Mussa haukuruhusu utapeli wa taifa moja kutapeli taifa jingine, wala kundi moja ndani ya taifa kwasababu ya nguvu zake kiuchumi basi liweze kutapeli kundi jingine na kusababisha tofauti kubwa ya mapato na ya maisha. 

Kwahiyo tatizo hapo ni kuchanganya dini (ya kweli ya Nabii Musa) na matokeo ya siasa mbaya ya zilizoshindwa kulinda haki ndani ya nchi hadi kuwaletea watu maafa ya umaskini wa kutisha ambao kutokana na watu kukosa jibu basi watu hao wanaamua kujifariji kwa kukimbilia kwenye maandiko ili wapate majibu rahisi na yasiyoweza kupingwa na yeyote. Katika torati ya Mussa ilielezwa bayana Baraka na Laana. Sasa katika habari ya laana,sheria au falsafa ya Mussa inaeleza kwamba mtu (au mwamini) anageweza kulaaniwa na kupatwa na madhara ya aina tatu; ambayo yalijulikana kwa laana ya torati:- 

(a) Kwanza mtu ambaye hakutii sheria, aliweza kulaaniwa na Mungu na kufa papo hapo mara atendapo hiyo dhambi yake kama ilikuwa ni kubwa sana. 

(b) Pili mtu aliweza kulaaniwa akapatwa na ugonjwa usiotibika ama usiosikia dawa. Ugonjwa wowote ambao zamani ulikuwa hauna dawa ulihesabiwa kama pigo kutoka kwa Mungu. 

(c) Tatu mtu aliweza kulaaniwa akawa maskini. Hata angefanya kazi kupindukia mtu aliyelaaniwa hangeweza kuondoa umaskini wake kwasababu iliaminiwa kwamba ni pigo kutoka kwa Mungu. Watu wa aina hii ndio ambao mfalme Suleimani katika mahubiri yake au katika kitabu chake cha mhubiri anasema Mungu amewapa taabu wanadamu, taabu ya kututa na kukusanya ili kumwekea yeye ambaye Mungu amemridhia. 

Sasa kwa kuyatumia maandiko ya Musa wakati ambapo nchi, au taifa haliendeshwi kwa torati ya Mussa hicho peke yake ni kitendo cha kitapeli kwasababu ni kuchanganya mambo mawili yasiyoweza kuchanganyika pamoja na kutoa matunda mema ya kuliwa na watu. Ni kuchanganya torati (iliyotolewa kwa nia safi) na uliokuwa mfumo wa haki na kuuchanganya na madhara ya mifumo mibovu ya wanadamu waliomwasi Mungu na kisha kumfanya mwathirika au victim awe ndiye mwenye hatia ya kutokuisikiza kwa bidii sauti ya Mungu. Kama watu wanaamua kulitumia neno la Mungu katika maisha yao basi itawapasa kukubali kwamba Mungu ndiye anayetawala vyote na anahusika na yote yanayohusu maisha yetu kama wanadamu yaani kuanzia kiroho, kiuchumi, kisiasa, kijamii. 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
NASAHA yatimiza mwaka mwaka mmoja

Mkapa, Karume wapewa tiketi za CCM kugombea urais

CCM walilia kiti cha CUF

Kufuatia kukamatwa kwa Sheikh Mbukuzi na Ricco:
Viongozi wa Serikali  watakiwa kuacha udini dhidi ya Waislamu

HABARI
Mauaji ya Mwembechai: Hatimae inquest yafunguliwa

DC aishukuru Finland

Amiri Mbukuzi ahojiwa na polisi

Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi watajwa

USHAURI NASAHA
Mapambano dhidi ya dhuluma ni ya kudumu

MAKALA
Dini na siasa haviwezi kutenganishwa

MAKALA
Mchango wa taasisi ya Dhiynurayn

MAKALA
Sayyidat Fatma:Jumuia iliyosimama dhidi ya dhulma 

MAKALA
Kupiga vita udini zisiwe kauli za kuendeleza udini dhidi ya Waislam

HOJA BINAFSI
Kwa Rafiki yangu Mpendakula

Makala maalum ya Maulid
Kumpenda Mtume Muhammad (s.a.w.)

MAKALA
CCM  na sera za maendeleo

Habari za Kimataifaza Kimataifa

Lishe 
Vyakula vitupatiavyo vitamini C

BARUA

MASHAIRI

RIWAYA
Mapinduzi ya fikra - 4 

MICHEZO
Ongara, Salvatory, Nteze, Mwansasu waenda Ulaya
Mokake aikosoa Yanga


   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita