|
Na. 052 Jumatano Juni 14 - 20, 2000 |
|
|
|
|
|
Mchango wa taasisi ya Dhiynurayn MOJA ya kazi ya taasisi ya dini yoyote ile ni kutoa hudumu ya kiroho na kimwili kwa waumini wake na jamii nzima kiujumla kama mwandishi KENNETH SIMBAYA wa Iringa anavyoelezea kazi za Taasisi moja ya dini ya Kiislamu ijulikanayo kama Dhi Nureyn Islamic Foundation. Dhi Nareyn Islamic Foundation ni Taasisi ya Kiislamu yenye makao yake makuu mjini Iringa, ilisajiliwa rasmi Wizara ya Mambo ya Ndani mwaka1988 chini ya sheria ya usajili wa vyama ya mwaka 1954. Malengo yake makuu kama yalivyobainishwa katika katiba yake ya Dhi-Nureyn ni kutoa huduma kwa jamii ya Kiislamu na jamii yote ya watu wa Iringa na hatimaye kwa Watanzania wote. Dhi-Nureyn inalenga kuleta umoja miongoni mwa wananchi na maelewano mazuri baina ya dini tofuati ili kujenga taifa imara. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Dhi Nureyn, Sheikh Said Abri , Dhi-Nureyn haikuanzishwa ili iwe dhidi ya Taasisi fulani, bali ilianzishwa ili iwe nazo pamoja katika kutafuta Ufalme wa Mbinguni na maendeleo ya jamii yetu. "Kwa minajali hiyo, Dhi-Nureyn Islamic Foundation imekuwa na mahusiano mazuri na Taasisi zingine za Kiislamu hapa mkoani na nchi nzima kiujumla pia ina mahusiano mazuri na Taasisi za dini zisizo za Kiislamu", anasema Sheikh Said Abri. Tukianza na huduma za kiroho, Dhi Nureyn kwa kuzingatia umuhimu wa misikiti katika kuijenga jamii katika maadili yaliyo mazuri na kuipa jamii ya Kiislamu haki yao ya kikatiba ya kuabudu na kuleta ushirikiano miongoni mwa waumini katika kutafakari kwa pamoja jinsi ya kuboresha hali zao na kutatua matatizo yao kwa njia ya kushauriana, Taasisi imejenga misikiti kumi na tatu katika maeneo tofuati ya Manisapaa ya Iringa na vijijini, (misikiti mingine sita inaendelea kujengwa) na inalenga kutoa huduma hiyo katika sehemu yoyote itakayohitaji huduma hiyo. Miongoni mwa misikiti mipya iliyokwisha kujenga na inayojengwa na Dhi-Nureyn mpaka hivi sasa na maeneo iliyopo katika mabanoni, msikiti wa Dhi-Nureyn (Wilolesi), msikiti wa AL Furqaan (Kihesa), msikiti wa Annour (Kihesa), msikiti wa Rahma (Mkimbizi), msikiti wa Tawheed (Ipogoro) na msikiti wa Al Haramain (Ndiuka). Mingine ni msikiti wa Igumbiro (Igumbiro), msikiti wa Njia panda (Njia panda), msikiti wa Rawdha (Mbigili), hii yote ipo Manispaa ya Iringa. Iliyopo nje ya Manisapaa ya Iringa ni msikiti wa Abdul Ghafur (Mtandika), msikiti wa Sirajudin (Ilula), msikiti wa Al-Hijra (Mazombe), msikiti wa Ansaa (Mtwivila), msikiti wa Bilal (Bwawani), msikiti wa Slaf (Makambako) na msikiti wa Saddya (Migori Mtera). Mingine ni msikiti wa Al Faruuq (Nduli), msikiti wa Kitwiru (Kitwiru), msikiti wa Al-Shaikh (Ruaha Mbuyuni) na msikiti wa Ibn Baaz (Ifunda). Dhi-Nureyn pia inatoa huduma zingine muhimu kwa jamii kama vile elimu ya dini na elimu dunia ili kuwaanda vijana wa kizazi cha kesho kuwa raia wema na viongozi wacha Mungu Kama anavyoelezea katibu mkuu wa Dhi-Nureyn, Bw. Shams Ilim, "Katika kufanikisha azma hiyo tumeweka madrasa katika kila msikiti kwa ajili ya kuwapatia watoto, kinamama, kina baba elimu yadini yao. Sambammba na hilo,Taasisi imeshaanza mpango wake wa kuhakikisha kuwa katika kila msikiti panakuwa na shule ya awali", anasema Bw. Shams, zaidi ya hayo Taasisi imeanzisha chuo cha Kiislamu kiitwacho Dar-al-Uluum Ipogoro mjini hapa ili kuwapata wataalamu wa mambo ya dini wenye maono ya mbali na ambao wanaweza kubuni miundo mbinu ya kuiendeleza jamii katika medani tofuati. Chuo hicho kilianza rasmi mwaka 1996 kikiwa na wanafunzi 25 toka vijiji mbalimbali vya mkoa wa Iringa lakini kwa hivi sasa chuo kina wanafunzi130 toka vijiji vya mkoa wa Iringa na mikoa ya jirani. Vijana katika chuo cha Dar al Uluum wanaandaliwa kwa muda wa miaka miwili. Mbali na kupatiwa Elimu ya dini vijana katika chuo cha Dar al Uluum husomeshwa masomo ya mazingira, kilimo bora na baadaye wataanza kusomeshwa ufundi pia. Taasisi pia ina walipia ada wanafunzi zaidi ya thelathini wasio na uwezo wa kulipa ada. Huduma nyingine ya jamii inayotolewa na Taasisi ni huduma ya afya, taasisi sasa hivi inakamilisha ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Mbigili Iringa vijijini, zahanati ambayo itatoa huduma za afya kwa vijiji vitano vilivyo jirani na Mbigili. Taasisii imefanya hivyo baada ya kuona matatizo makubwa ya huduma ya afya kwa wanachi wa maeneo hayo. Pamoja na zahanati hiyo, Taasisi katika mpango wake wa miaka mitano ijayo imeazimia kujenga kituo cha Afya Iringa mjini, zahanati Ruaha Mbuyuni Iringa (V) na Mkimbizi Iringa (M). Taasisi ya Dhi-Nureyn pia inafanya misafara ya tiba kwa ajili ya kutoa tiba bure kwa wananchi kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa kujitolea kutoka Muhimbili na hopistali ya mkoa Iringa. Huduma nyingine ya jamii inayotolewa na Dhi-Nureyn ni huduma ya maji. Mpaka sasa Taasisi imeshachimba visima sita ndani ya wilaya ya Iringa na kuweka pump katika maeneo ya Mkimbizi, Nduli, Nyololo, Ifunda na Ruaha Mbuyuni. Visima vinavyotarajiwa kuchimbwa mwezi Juni na Julai mwaka huu ni visima vitano katika vitongoji vya Ifunda, visima viwili Ikonongo, visima viwili Itamba, na kisima kimoja kimoja Mtwivila, Migori, Mkimbizi shuleni, Idodi na Mazombe. Taasisi ya Dhi-Nureyn ni mkombozi wa wakina mama hapa Iringa kwani imekuwa ikitoa mikopo midogo midogo kwa vikundi vya kina mama na kuwapa vitendea kazi kama vile vyerehani. Malengo ya baadaye ya Dhi-Nureyn ni kufungua shule ya sekondari ya bweni, kituo cha Afya, kujenga chuo cha Ufundi na kituo cha watoto yatima hivi vyote vinatarajiwa kujengwa Iringa mjini na kuchimba visima 50 Iringa vijijini. |
YALIYOMO
TAHARIRI
Mkapa, Karume wapewa tiketi za CCM kugombea urais Kufuatia
kukamatwa kwa Sheikh Mbukuzi na Ricco:
HABARI
Amiri Mbukuzi ahojiwa na polisi Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi watajwa USHAURI NASAHA
MAKALA
MAKALA
MAKALA
MAKALA
HOJA BINAFSI
Makala maalum ya Maulid
MAKALA
Habari za Kimataifaza Kimataifa Lishe
RIWAYA
MICHEZO
|
|
|
|
|