|
Na. 047 Jumatano Mei 10 - 16, 2000 |
|
|
|
|
|
MFUPA ULIOMSHINDA MANCHESTER
WAING'OA MENO BAYERN
Munich, Ujerumani REAL Madrid ya Hispania imefanikiwa kuingia fainali ya ligi ya Mabingwa wa Ulaya baada ya kuishinda Bayern Munich ya Ujerumani kwa jumla ya mabao 3-2. Real Madrid ilipata ushindi huo baada ya kufungwa mabao 2-1 na Bayern Munich katika mchezo wa marudiano uliofanyika mjini Munich, Ujerumani jana. Katika mchezo wa kwanza uliofanyika mjini Madrid, Real walipata ushindi wa bao 2-0. Katika mchezo uliofanyika jana, goli la kwanza la Bayern Munich lilifungwa na mshambuliaji Jancker katika dakika ya 12. Mshambuliaji machachari, Nicholas Anelka wa Real Madrid alisawazisha goli hilo kwa kichwa katika dakika ya 31 baada ya kuunganisha pasi safi toka kwa Savio. Goli la pili la Bayern Munich lilifungwa na mchezaji Elber katika dakika ya 54. Ushindi wa Real Madrid umeifanya timu hiyo kuweka rekodi ya kuwafunga vigogo wa ligi hiyo ya Ulaya ikiwemo mabingwa watetezi, Manchester United ya Uingereza ambao waliwatoa kwa jumla ya magoli 3-2.
Mapunda, Makoye hawafai timu ya Taifa - Kipingu
WASHAMBULIAJI matata, Steven Mapunda 'Garincha' na Ephrain Makoye 'Dogo' wa timu za Simba na Yanga za Dar es Salaam, wameelezwa kuwa hawana sifa za kuchaguliwa timu ya Taifa ya Vijana walio na umri usiopindukia miaka 20. Kanali Iddi Kipingu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) amesema kuwa wachezaji hao wamekosa sifa hizo kwa sababu waliwahi kuchezea timu ya Taifa ya wakubwa wanaochupa umri wa miaka 20. "Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) mchezaji aliyewahi kuichezea timu ya Taifa ya wakubwa haruhusiwi tena katika timu ya Vijana katika msimu mmoja wa mashindano", amedai. Historia inaonesha kuwa Mapunda na Makoye wamewahi kuchezea timu ya Taifa ya wakubwa kwa vipindi tofauti kabla ya kuenguliwa kwa sababu kadhaa. Hata hivyo Kipingu ambaye ni meneja wa timu za Taifa za Vijana chini ya umri wa miaka 17 na miaka 20, amekiri juu ya ubora wa Makoye na Mapunda katika usakataji kabumbu. Aidha Kipingu amesema kwamba timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 ina matatizo kiuchezaji kwa kuwa haichezi kwa ushirikiano japo kwa mchezaji mmoja mmoja wanaonekana kuwa na uwezo mzuri. Timu hiyo iliyo chini ya Makocha Mnigeria Ernest Mokake na Mtanzania Juma Matokeo itapambana na vijana wenzao kutoka Namibia Jumapili wiki hii jijini katika mashindano yaliyoandaliwa na CAF. "Lakini nadhani timu yetu itafanya vizuri dhidi ya Namibia kwa sababu inafundishwa na waalimu wazuri (Mokake na Matokeo) ambao sina mashaka nao hata kidogo" amejigamba.
Tarimba ashinikizwa kujiuzulu Yanga
Na Mwandishi Wetu
IMEFAHAMIKA kuwa Kaimu Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Abbas Tarimba amekuwa akipigwa vita ndani ya klabu hiyo na hata kutakiwa kujiuzulu na baadhi ya wanachama waliomuweka madarakani. Tarimba amekuwa ndani ya tafrani hiyo baada ya kutangaza hadharani hivi karibuni kwamba anakusudia kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba kwa tiketi ya CCM. Imeelezwa kuwa wanachama hao wamekerwa na kitendo cha mwenyekiti wao kutafuta maslahi ya kisiasa kupitia mgongo wa klabu yao ambayo kimsingi haina chama. Kwa mujibu wa habari ambazo NASAHA linazo Tarimba ameombwa kuchagua ama siasa au michezo ili kuepusha mgawanyiko mkubwa ndani ya Yanga ambao unaweza kuibuka. Yanga inaundwa na wanachama wenye itikadi tofauti za kisiasa na inapotokea kiongozi anataka wadhifa wa kisiasa kupitia chama fulani ni budi aache madaraka ya klabu ili kuepusha mgawanyiko klabuni" amesema mmoja wa wanachama kuelezea umuhimu wa Tarimba kujiuzulu. Ikumbukwe kuwa awali ya hapo tayari kuna kundi la wanachama lililoko msituni kupanga mikakati ya jinsi ya kufanikisha mapinduzi dhidi ya utawala wa Tarimba. Kundi hilo sasa limeongeza kasi sasa katika kampeni
yake na kupata zaidi ya wafuasi baada ya Tarimba kutangaza kuingia katika
siasa huku akiwa kiongozi wa klabu.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Wananchi washutumu vyombo vya habari Lipumba awaambia wananchi wasibabaishwe na walioko madarakani Wasomi SUA walaani ‘rushwa’ ya kisiasa Polisi kataeni kutumiwa - Lipumba Maelfu ya tani za matunda yanaoza Tanga Habari za ndani
MPASHO NASAHA
HABARI
Ushauri Nasaha
Makala
MAKALA
MAKALA
Kalamu ya Mwandish
MAKALA
RIWAYA
Lishe
|
|
|
|
|