NASAHA
Na. 047 Jumatano Mei 10 - 16, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Barua 
 
 

Barua ya wazi kwa Sheikh Suleiman Gorogosi



Asslam Alaykum

NIANDIKAPO barua hii natumaini hali yako sheikh ni nzuri kabisa na Mwenye Enzi Mungu anaendelea kukupa rehma zake.

Mimi ni miongoni mwa watu ambao hufuatilia kwa karibu sana vipindi vyako vya dini unavyoendesha katika vyombo vya habari na hasa Radio Tanzania (RTD) na sasa katika Television ya Taifa (TVT). Kwa hakika dhima uliyopewa ya kufikisha ujumbe kwa umma ni kubwa sana na hasa ukizingatia ni yenye kuulizwa siku ya kiama. Binafsi ninafurahishwa sana kwa umma wa Kiislam kupata nafasi hii ambayo ujumbe wake huwafikia watu wengi kwa muda mfupi bila kujali dini zao na mahali walipo. 

Nafasi hiyo pia wanayo viongozi wa dini nyingine ili nao wafikishe ujumbe kuhusu imani ya dini zao. Mnachotofautiana ni namna tu ya kufikisha ujumbe huo. 

Kama nilivyo sema kuwa nafasi hiyo uliyopewa ni muhimu sana katika taifa letu na hasa kwa umma wa Kiislam. Ukitumia kama inavyo stahili utailetea jamii ya Kiislam manufaa makubwa na hatimaye vipindi hivyo vitakuwa ni vya kheri na neema. Lakini kama nafasi hiyo haitatumika vilivyo, basi itakuwa ni hasara na fedheha kwa jamii na umma wa Kiislam kwa ujumla. 

Sheikh, linalonipelekea mimi kuandika waraka huu ni jinsi unavyo ipoteza nafasi hii muhimu ya kufikisha ujumbe kwa jamii kwa muda mfupi na haraka. Mategemeo ya Watanzania walio wengi na hasa Waislamu ni kuona mandalizi ya uhakika ya vipindi vitakavyo iwezesha jamii si tu kuuelewa Uislam, bali pia kuupenda na hatimaye kutekeleza amri zake vilivyo. Lakini cha kusikitisha ni kuwa vipindi unavyo tuandalia si vya kuujenga Uislam bali kuudhalilisha na kuutia aibu mbele za Watanzania na walimwengu kwa ujumla. Dakika hizo chache unazopewa katika television sikutegemea kama ungezitumia kwa DHIKRI na QASWIDA, tena huku watu wa dini zote wakiwaangalia badala ya kuzitumia kuuelekeza umma wa Watanzania na jamii ya Kiislam namna ya kujenga maisha yao hapa duniani kwa kuishi kama alivyotutelekeza ALLAH (S.W.). Jamii yetu imezungukwa na madhila mbalimbali kama vile ulevi, uzinzi, wizi, utovu wa nidhamu, uonevu, kutokuwa na aibu (hasa wanawake na mavazi) na baya zaidi hakuna uadilifu kati ya mtu na mtu na viongozi na wananchi wao. Haya ndiyo mambo ambayo ungekuwa unajaribu kuyapa kipaumbele ili, kwa kutumia uwezo na kipaji ulichopewa na Molla wako, jamii hii ijione inafanya makosa na hatimaye kujirekebisha. 

Bila shaka umeona au kusikia jinsi viongozi wenzako wa dini nyingine walivyo zitumia nafasi zao kama hizo unazopata na hasa katika siku hizi za sikukuu ya Pasaka. Wamejaribu kwa nguvu zao zote kuionesha jamii maovu yatokanayo na matendo yao na kuwaelekeza namna ya kuyaendea maisha ya dunia na hasa suala la kuwaweka viongozi madarakani kwa kutumia nguvu ya kura. Wanaelewa vizuri mfumo mzuri wa maisha katika jamii kwanza huanza na suala la kuwa na viongozi wadilifu ambao watakemea maovu na kusimamia ujenzi wa mazingira ya maendeleo ya kimaada, kiakili, kifikra na kiroho kwa uadilifu bila kuleta hisia za uonevu. 

Hivyo, ni matumaini yangu kuwa utaweka mipango mizuri ya kuandaa programu zenye kuipelekea jamii kufaidika na vipindi vya dini tunavyopata badala ya kuendesha programu ambazo zinaweza kufanyika misikitini badala ya kwenye TV na Radio. Unaweza pia kushiriana na masheikh wenzako ambao kwa pamoja mnaweza kutoa DAW'A yenye kujenga jamii hapa duniani na siku ya kisimamo na hasa suala la kuwapata viongozi wadilifu na kuondoa maovu katika jamii. 

Nakutakia mafanikio mema katika Dhima hii uliyopewa ili utakapoulizwa namna ulivyotumia muda wako uwe na jibu madhubuti la kumweleze ALLAH (S.W.). 

Ust. Jamal Athman Nchula, 
Dodoma.


TANESCO hata nyie mnatudhulumu pia? 



Ndugu Mhariri

NAPENDA kukushukuru kwa kunipa nafasi kidogo katika gazeti lako kutoa dukuduku langu lenye majonzi juu ya dhulma kubwa tunayofanyiwa ama na wafanyakazi wa Tanesco au na uongozi mzima hasa wa mkoa wa Dar es Salaam.

Mimi nikiwa mkazi wa Tabata hapa Dar es Salaam ambaye nimekuwa mteja mtiifu na mwenye kuthamini huduma ninayopewa ingawa kwa matatizo na shirika hili, nimejitahidi kulipa bili mpaka ya mwezi Aprili, 2000. Lakini ipo bili ya nyuma anbayo sio mimi peke yangu bali pia na baadhi ya majirani zangu zimeletwa kwetu kimakosa kiasi cha kudaiwa zaidi ya laki mbili kwa mtu mmoja kwa mwezi!! Ni maajabu mno. Nimefuatilia kwa makini mpaka katika ofisi zao na wamesema inawezekana kuwa makosa yamefanyika na wameniambia watafuatilia. Cha ajabu na kusikitisha mno ni pale ufuatiliaji walioufanya ni ule wa kuja kutukatia umeme. Jamani ni dhulma gani hii mnatufanyia hata nyie pia ?? Naomba uongozi wa shirika hili ufuatilie kwa karibu mno kilio chetu na isiwaachie wafanyakazi wa kawaida wakija kusisitiza tulipe tu hizo pesa na pesa zaidi za kuwarudishia umeme kama faini zao ,Inauma sana kwa kweli. Tumechoka jamani kunyanyaswa.

Samwel Jonas
TABATA,
Dar es salaam.


Kuchanganyadini na siasa nani kaanza?



Ndugu Mhariri,

NAOMBA nafasi katika gazeti lako nitoe machache kuhusu kuchanganya dini na siasa. Mara kadhaa nimesikia viongozi wa serikali na wa chama tawala (CCM) wakiwakemea Waislamu juu ya suala la kuchanganya dini na siasa. Hivi ni nani anayechanganya dini na siasa? 

Ni serikali au Waislamu? Siku zote tunawaona viongozi wa serikali wakila kiapo kwa kutumia vitabu vya dini. Je huko sio kuchanganya dini na siasa? Serikali ya Jamhuri ya Muungano ina katiba yake kwanini hawa viongozi wasiape kwa katiba ya nchi? 

Mara nyingi viongozi wa serikali wamekuwa wakihudhuria shughuli za kidini na kutoa maelekezo, je hii sio kuchanganya dini na siasa? Vile vile hatuwasikii viongozi wa serikali kuwakemea viongozi wa Kanisa kuhusu kuchanganya dini na siasa. 

Hivi karibuni Kanisa Katoliki limetoa maelekezo ya kisiasa na kuahidi kufuatilia uchaguzi mkuu ujao. Hili viongozi wa serikali wamelikalia kimya!!. 

Viongozi wa serikali waache unafiki kuhusu suala hili la kuchanganya dini na siasa. Mimi naona viongozi wa serikali ndio walioanza kuchanganya dini nasiasa. 

Lioche Abbas Lioche, 
S.L.P. 14, Kilwa Masoko.


Hongera Lipumba



Ndugu Mhariri,

NACHUKUA nafasi hii kumpongeza Mwenyekiti wa CUF Prof. Lipumba kwa kuwaacha solemba waandishi wa habari kuhusu sherehe za Muungano!

Wengi tunafahamu kuwa katibu mkuu wa CUF Maalim Seif alisema hawatahudhuria sherehe hizo kupinga unyanyasaji unaofanywa na jeshi la polisi huko Zanzibar. Tunajua kabisa wapo waandishi wa habari ambao wao hupenda kuiandika vibaya CUF ambao walishanoa kalamu zao ili kulihusisha suala hilo na CUF kutoutambua Muungano! Tunaelewa hata CCM ilishapata agenda hapo. Tumeshuhudia baadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa "wakijipendekeza" kwa kusema eti kususia sherehe za muungano nikuwasaliti Watanzania! Hii inaonesha kuwa kamasiyo "chenga ya kisigino" ambayo Prof. Lipumba amewapiga wanafiki hao ,leo tungesikia mengi kwenye vyombo vya habari na chama tawala! 

Tunafahamu Lipumba na Seif waliliona hili ndio maana wakaamua Prof. ahudhurie na si kumsaliti kama wanavyojaribu kulipotosha. Kwa hili napenda kuwapongeza viongozi wa CUF na nawaeleza kuwa hapo wameshinda mbili bila (2-0)!!! 

Mvungi M.F., Morogoro.


Waislam tuamke 



Ndugu Mhariri,

WAISLAM wa Tanzania wamekuwepo wakilalamika kuwa serikali yetu haitutendei haki.

Malalamiko hayo yameshapelekwa kwa Mheshimiwa Rais na majibu alioyatoa hayaridhishi. 

Waislam wamehoji kwanini wavamiwe ndani ya nyumba yao ya ibada na wauawe na chombo cha dola na serikali isifanye uchunguzi?. 

Waislamu wanalalamika uhalali wa kukosa kwao nafasi za juu serikalini hali inayoonesha upendeleo wa dhahiri. 

Kuna mambo mengi ambayo Waislam wanayakosoa ikiwa pamoja na uhuru wa kutangaza dini kwa mujibu wa katiba kifungu No. 19: 1 na19:2 lakini wahubiri wa kiislam ovyo hukamatwa kwa madai ya kashfa. 

Waislam wamekuwa wakiambiwa wasichanganye dini na siasa yaani wasiwe wanazungumza mambo ya siasa misikitini lakini makanisani hawawasemi kabisa!!. 

Mbaya zaidi kuna Waislamu ambao bado wapo usingizini wanaiunga mkono kauli hiyo. 

Hawajui kuwa kauli hiyo ina lenga kumfanya Muislam asiwe na uhuru wa kulalamika au kulaumu mabaya wanayotendewa na serikali. 

Kama Muislam kuzungumza siasa msikitini haifai. Je! Muisilam anaweza kuilaumu serikali kwa maovu yake akiwa juu ya jukwaa la kisiasa yanayohusu dini? 

Hapa jibu litakuwa hapana ukifanya hivyo utaambiwa unazungumzia udini. 

Unapoeleza kuwa msikitini usizungumzie siasa hiyo ni katiba inayokataza au ni Aya ya Quran. 

Waislamu ni ndugu ni watu wanaopenda Amani kisha Mungu ametuhimiza tusidhulumu na tusikubali kudhulumiwa. 

Kwa maana hiyo Mungu ametutaka tutendeane haki na tupige vita dhulma. 

Ikiwa mtu anakudhulumu unamueleza "Bwana unanidhulumu haki zangu naye hakujali unadhani utamwelewa vipi?. 

Lazima mtu huyo atakuwa amekudharau na anajuwa hauna chochote utakacho mfanya. 

Ndugu zangu Waislamu yafaa kwanza tujipongeze kwa kuwa watu wenye subira tumevumilia maovu yote tunayotendewa na serikali yetu. 

Ni imani tumekubali yote kwa ajili ya kuitakia mema nchi yetu. 

Yafaa tuitumie njia hii ya Amani kuionesha serikali kwamba tumechoshwa na maovu inayotutendea. 

Hatuwezi kufanikiwa katika hili bila ya kuiondoa CCM madarakani. 

Wakristo wao wameshatunga vitabu wanavyosambaza mikoani vinavyowataka Wakristo wawachaguwe wenzao. 

Wameahidi kuufuatilia uchaguzi mkuu ujao. 

Wakati wenzetu wanafanya hayo sisi tunaambiwa tusichanganye dini na siasa hamuoni kuwa tunafanywa mishumaa ambapo thamani yetu mpaka umeme ukatike?. 

Wito wangu mimi tuungane Waislamu tuchague chama chochote cha upinzani tukiunge mkono na tukipigie debe tulete mabadiliko. 

Yusuph Ahmadi Saabi, 
S.L.P. 31775, 
Dar es Salaam.

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Mazingira ya uchaguzi huru na haki yasivurugwe

Wananchi washutumu vyombo vya habari

Lipumba awaambia wananchi wasibabaishwe na walioko madarakani

Wasomi SUA walaani ‘rushwa’ ya kisiasa

Polisi kataeni kutumiwa - Lipumba 

Maelfu ya tani za matunda yanaoza Tanga

Habari za ndani
Uondoeni ‘ukoloni’ wa CCM- Mbukuzi

MPASHO NASAHA
WABONGO HAWANA NYONGO !

HABARI
Nchi wafadhili wataka upinzani,  CCM yalalama

Waislamu Musoma walalamika

Habari za Kimataifa

Ushauri Nasaha
Jukumu la wazazi, walimu kwa wanafunzi wanaomaliza masomo

Makala
Madhara ya ulevi kwa binadamu

MAKALA
Sababu ‘1000’ kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani - 6

MAKALA
Kiini macho cha msamaha wa deni

Kalamu ya Mwandish
Kama CUF ni chama cha Waislamu 
Jee, CCM ni chama cha Wakristo?

MAKALA
Chama cha Mapinduzi na sera za maendeleo (2)

RIWAYA
Mapinduzi ya fikra

Lishe
Jinsi ya kuzuia utapiamlo kwa wanawake

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Real Madrid yaingia fainali
  • Mapunda, Makoye hawafai timu ya Taifa - Kipingu
  • Tarimba ashinikizwa kujiuzulu Yanga

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita