|
Na. 047 Jumatano Mei 10 - 16, 2000 |
|
|
|
|
|
Kiini macho cha msamaha wa deni KWA muda wa siku tatu mfululizo za wiki ya
kwanza ya mwezi huu, waandamanaji walipambana na polisi katika Jiji la
Washington DC, wakitaka kuvuruga mkutano wa Shirika la Fedha Duniani (IMF)
na Benki ya Dunia. Madai yao ni kuwa, Mashirika hayo ni majambazi wakubwa
yanayozitia umasikini nchi changa. Wakati hayo yakijiri, vyombo vya habari
nchini vimekuwa vikipongeza hatua ya Tanzania kusamehewa sehemu ya madeni
yake na mashirika hayo. Pamoja na pongezi hizo, vyombo hivyo vimeeleza
kuwa serikali imetakiwa itumie unafuu huo kuboresha hali za wananchi kutokana
na tamaa wanayopewa kinyume cha hali halisi ya msamaha wenyewe. K. ABDULLAH
afanya uchambuzi wa kitaalamu dai hilo la msamaha wa madeni.
KWANZA, hakuna Tanzania ilichokipata kutokana na msamaha huo. Na kama imepata 'hakuna' haiwezi kutumia senti tupu kuboresha hali za wananchi. Mashirika haya ya fedha IMF, Benki ya Dunia na nchi wahisani yanachofanya ni utapeli wa kuzitia utumwani nchi changa. Utaratibu wao ni kutoa mkopo kwa riba ambao kwa mahesabu yake baada ya muda deni (deni halisi pamoja na riba) huwa kubwa ambalo nchi haiwezi kulilipa mpaka kiama. Kwamba nchi hata kama ingetaka itumie pato lake lote la mwaka kwa miaka mingi tu kulipa deni hilo, bado deni lisingekwisha. Jaalia deni lako limefikiadola x ukasamehewa kiasi cha dola y kwa vile umekuwa mlipaji mzuri wa deni. Lakini x-y=z ambayo ni salio la deni ambalo unatakiwa uendelee kulilipa. Na huna uwezo wa kulimaliza kwa miaka 100 ijayo, kwa vile, kwanza ni kubwa sana, pili kwa tabia yako nzuri unaendelea kukopeshwa na tatu riba inaendelea kutozwa. Katika hali hiyo zile dola y ulizosamehewa kama sehemu ya deni, haitakusaidia kitu kwa vile msamaha huo haujakutoa kitanzi cha deni. Pili hakuna tamaa kwa siku za karibuni utaepukana kulipa deni kwa deni kumalizika. Msamaha haumaanishi umepewa kitu, wala si kuwa sasa hutalipa deni kwa hiyo fedha ulizokuwa unalipa deni, sasa utazitumia kwa maendeleo. Chukua mfano mwepesi ambapo Mtu kakukopesha shilingi 10. Kutokana na mfumo wa viwango vya riba, baada ya miaka 30 deni hilo likafikia shilingi 50. Iwapo uwezo wako ni kulipa senti 20 kwa mwaka itakuchukua miaka 250 kumaliza deni hilo, hata likisimama bila kuongezeka. Sasa ukiambiwa umesamehewa deni la shilingi 20, bado una deni la shilingi 30 ambalo litakuchukua miaka 150 kulilipa. Kwa hiyo utakufa, watoto, wajukuu na vitukuu wataendelea kurithi kitanzi cha deni. Kwa ajili hiyo, huo msamaha wa shilingi 20 haukusaidii chochote. Lakini msamaha wenyewe na salio la deni linaonekana kuwa ni kiini macho na utapeli mtupu. Wewe ulikopa shilingi 10 tu. Huu msamaha wa deni lashilingi 20 unatoka wapi! Utapeli wenyewe ni kuwa ushalipa zaidi ya fedha ulizokopa lakini bado unaambiwa unadaiwa. Sina hakika deni la awali la Tanzania kwa IMF na Benki ya Dunia ni shilingi ngapi. Lakini ni utapeli huo huo wa kupewa shilingi 10 ukadaiwa shilingi 50 na kusamahewa shilingi 20, ukabakiwa na deni la shilingi 30 ambalo huwezi kulimaliza kulilipa hata kwa miaka 150. Taarifa zinasema deni tulilosamehewa ni shilingi trilioni 1.6 (1,600,000,000,000) Msamaha huo unaelezwa kuwa ni kiasi cha nusu ya madeni ambayo Tanzania inadaiwa na mashirika ya fedha ya kimataifa. Kama hesabu hiyo ni sahihi, ina maana jumla ya deni ni shilingi trilioni 3.2 (3,200,000,000,000). Jambo moja la hakika ni kuwa Tanzania haijawahi kupewa huduma, bidhaa au fedha taslimu za kiasi hicho cha shilingi trilioni 3.2 kutoka IMF au nchi wahisani. Kinachofanyika ni utapeli wa kucheza na namba kwa kutumia kanuni ya FV=PV (1+r)^n ambpo FV huwakilisha thamani ya denikwa sasa (au baadaye). PV = Thamani ya deni la awali (au sasa hivi) r = Kiwango chariba. n = Muda (deni limedumu miaka mingapi). Kwa kanuni (formula) hii, kama deni la Tanzania kwa sasa ni shilingi trioni 3.2, mkopo wa awali miaka thelathini iliyopita ulikuwa bilioni 740 tu. Tukijaalia fedha hizo zilikopwa mwaka 1970 na hatujakopa tena wala kulipa. Ziada hutokana na utapeli huu wa kucheza na namba ni trilioni 2.46 (2,460,000,000,000) kwa kutukopesha shilingi 740,000,000,000. Vipi mtu akutapeli trilioni 2.46 aseme anakusamehe kukutapeli trilioni 1.6. Wanaotutapeli hawana ujuha wala wema wa kutoa sadaka ya trilioni 1.6. Wanaelewa vyema kiini macho cha kinachoitwa misamaha ya deni. Ni kwa sababu hiyo, mashirika hayo ya fedha hayaoni taabu kusema tumewasamehe trilioni 1.6. Wanajua trilioni 1.6 haiwakilishi mali halisi waliyowapa kwa mikopo. Ukichukulia kuwa uwezo wetu wa kulipa deni ni shilingi bilioni 20 kwa mwaka, tunahitaji miaka 160 kumaliza deni la trilioni 1.6. Baada ya miaka hiyo 160, au badala yake, mtu akisema msamaha wa kodi utumike kupambana na umaskini inaingia akilini. Lakini leo wakati deni la trilioni 1.6 lipo na serikali inalazimika kulipa sehemu katika pato lake kila mwaka; nini mantiki ya kauli - serikali itumie fedha za msamaha wa kodi vizuri! Kwani kufutwa kwa deni hilo maana yake ni serikali kuwa na fedha hizo taslimu? Kwanza hazikuwa mali halisi bali namba za mchezo wa hesabu tu!! Lakini pili, bado deni lipo na serikali inaendelea kulipa. Suala la msingi ni wananchi kuelimishwa juu ya utapeli huu unaofanywa na mashirika ya fedha ya Kimataifa sio kuwapa matumaini hewa wananchi. Hakuna unafuu wowote wananchi watakaoupata kwa kiini macho hiki cha kusamehewa madeni yatokanayo na mchezo wa namba usiowakilisha mali. Wananchi waelezwe mipango ya serikali inayoingia akilini, ya kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa chakula, tatizo la ajira linapungua na huduma za kijamii zinaboreshwa na hii si kutokana na kiini macho cha kusamehewa riba au sehemu ya mzao hewa wa madeni. Inawezekana propaganda hii ikatumika kuonesha kuwa serikali inafanya vizuri, lakini haitakuwa na 'matunda' ya kudumu kwa sababu huo unafuu hautaonekana na bado deni litakuwa pale pale. Kufikia mwaka 1989 Marekani ilikuwa na deni la Dola trilioni 3 (3,000,000,000,000 UD Dollars)ambapo malipo ya riba ya likuwa Dollar 240 bilioni sawa na zaidi ya nusu ya pato lote litokanalo na kodi. Maana yake ni kuwa Marekani haitakaa imalize kulipa deni hilo. Lakini Marekani inadaiwa na nani? Hudaiwa na Benki Kuu yake iitwayao Federal Reserve Bank ambayo imepewa watu wachache binafsi waiendeshe. Na ilivyo,sio kuwa Benki hiyo ina mali nyingi ya thamani ya trilioni za Dola. Bali huchapisha noti ikaipa serikali ikaanza mchezo wa namba. Kwa mchezo huo wa kiini macho wa kucheza na namba, kinaibuka kikundi cha watu wachache wenye nguvu sana ambao ndio huikokota Marekani watakako. Mjumbe mmoja wa Bunge la Congress miaka ya 1960 Bw. Wright Patman aliwahi kusema: In the United States today we have in effect two governments.... We have the duly constituted Government.....Then we have an independent uncontrolled and uncoordinated government in the Federal Reserve System operating the money powers which are reserved to Congress by constitution." Akimaanisha kuwa Marekani sasa hivi kama ina serikali mbili. Ile iliyowekwa kisheria na serikali katika mfumo wa Benki inayodhibiti hata hiyo serikali yenyewe kutokana na nguvu za kifedha. Panapokuja katika kiwango cha serikali za nchi maskini na mahusiano yake na IMF, Benki ya Dunia na nchi wahisani, hali ni hiyo hiyo. Nchi zinatiwa utumwani kwa deni lisilolipika. Kutokana na kutiwa kitanzi hicho cha deni la kitapeli, hupokonywa uhuru na uwezo wa kupitisha maamuzi juu ya mambo yake yenyewe. Kwa mfano, hamtaki kuuza Benki yenu, mnaambiwa lazima muuze. Hamuoni ulazima wa kubinafsisha mashirika ya umma au kuuza viwanda vyenu na migodi yenu ya dhahabu na almasi, mnalazimishwa uzeni na wakati mwingine kulazimishwa hata mumuuzie nani. Ni vyema wananchi wakaelimishwa juu ya ukweli huu wa mashirika ya fedha ya kimataifa na athari ya kitanzi cha madeni ambayo nchi yetu ishanasa. Lakini muhimu pia wananchi waelezwe bayana kiini macho hiki cha msamaha wa madeni. Wasipewe tamaa hewa. Hakuna kilichopatikana kwa kusamehewa trilioni 1.6 na bilioni 320. Deni lipo pale pale tunalazimika kulipa. Na msamaha huo haumaanishi kuongezeka senti moja katika pato la nchi. Kwa mwendo huu wa mfumo wa uchumi wetu, tutaendelea kulipa deni mpaka siku ya kiama na deni katu hatutalimaliza. |
YALIYOMO
TAHARIRI
Wananchi washutumu vyombo vya habari Lipumba awaambia wananchi wasibabaishwe na walioko madarakani Wasomi SUA walaani ‘rushwa’ ya kisiasa Polisi kataeni kutumiwa - Lipumba Maelfu ya tani za matunda yanaoza Tanga Habari za ndani
MPASHO NASAHA
HABARI
Ushauri Nasaha
Makala
MAKALA
MAKALA
Kalamu ya Mwandish
MAKALA
RIWAYA
Lishe
|
|
|
|
|