NASAHA
Na. 047 Jumatano Mei 10 - 16, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Kalamu ya Mwandishi 
 

Kama CUF ni chama cha Waislamu
Jee, CCM ni chama cha Wakristo?

NA MAALIM BASSALEH

GAZETI moja la Kikristo linalotoka kila Jumapili, katika toleo lake la wiki iliyopita, Jumapili, Mei 7-13, 2000, limedai kwamba, "CUF ni chama cha Waislamu!" Mwandishi wa makala hayo ametaja sababu tatu zinazokifanya chama hicho kiwe ni chama cha Waislamu.

Kwanza, amedai kuwa viongozi wakuu wa CUF ni Waislamu. Pili, amesema kuwa chama hicho kikishika madaraka kitatumia SHARIA badala ya SHERIA. Na mwisho amedai kuwa chama cha CUF kinaendesha kampeni misikitini.. 

Japokuwa mwandishi wa makala hayo anataka wasomaji wake waamini kuwa maelezo aliyoyaandika yametokana na uchunguzi wa kina alioufanya, lakini kwa msomaji aliye mahiri hataacha kugundua kuwa makala hayo si ya kichunguzi, hata kidogo, bali ni makala yenye kudhihirisha chuki alizonazo mwandishi juu ya Uislamu na Waislamu kwa jumla. 

Kwa mujibu wa sheria ya usajili wa vyama vya siasa hapa nchini, chama cho chote cha kisiasa hakiwezi kupata usajili wa kudumu mpaka kwanza Msajili wa vyama vya kisiasa afanye uchunguzi kuhakikisha kuwa chama kinachoomba usajili wa kudumu ni chama cha kitaifa; nasiyo chama cha kimkoa, kikabila au kidini. 

Ni dhahiri kuwa chama cha CUF kimetimiza shuruti hizo ndiyo kikapewa usajili wa kudumu. Usajili wa kudumu uliopewa chama cha CUF ni uthibitisho tosha kuwa ofisi ya Msajili wa vyama vya kisiasa imeridhika kuwa chama hicho ni cha kitaifa na siyo cha kidini, kama mwandishi huyo anavyodai. Kwa hivyo madai ya mwandishi huyo hayana msingi wo wote. 

Ama kudai CUF kuwa ni chama cha Waislamu eti kwa sababu tu viongozi wake wakuu ni Waislamu, hiyo ni hoja butu, iliyokosa mantiki. Ni kweli Mwenyekiti wa CUF, kitaifa, ni Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye ni Mwislamu, Naibu Mwenyekiti ni Bwana Shaaban Mloo", ambaye pia ni Mwislamu; na Katibu Mkuu wa chama hicho ni Maalim Seif Shariff Hamadi ambaye, kadhalika,ni Mwislamu, lakini hiyo haiwezi kuwa sababu tosha ya kukifanya chama cha CUF kiwe ni chama cha Waislamu! 

Ikiwa mantiki aliyoitumia mwandishi wa makala hayo kuwa kama chama cha kisiasa viongozi wake wakuu ni waumini wa dini fulani basi lazima chama kama hicho mwelekeo wake utakuwa ni wa dini ya viongozi hao, jee hatuoni kuwa vyama vingi vilivyokwisha pata usajili wa kudumu vitakuwa ni vyama vya Wakristo, kwa sababu viongozi wake wakuu, takriban, wote ni Wakristo? 

Tuchukue mfano wa kile chama kikongwe cha CCM. Mwenyekiti wake wa Kitaifa ni Mheshimiwa William Benjamin Mkapa, ambaye ni Mkristo. Makamo Mwenyekiti, Bara, ni Mheshimiwa John Samweli Malecela, ambaye pia ni Mkristo. Na Katibu Mkuu wa chama hicho ni Mheshimiwa Phillip Mangula, ambaye kadhalika ni Mkristo. 

Isitoshe Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuia ya Vijana ya chama hicho ni Ndugu Emmanuel Nchimbi ambaye ni Mkristo na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake ya CCM ni Mheshimiwa Anna Abdala ambaye naye hivyo hivyo ni Mkristo. Jee! Kwa mujibu wa mantiki ya mwandishi wetu na CCM ni chama cha Wakristo, kwa vile viongozi wake wa ngazi za juu ni Wakristo? 

Na hali hiyo ndiyo iliyoenea katika vyama vyote. Angalia chama cha NCCR-Mageuzi. Mwenyekiti wake kitaifa ni Mheshimiwa James Mbatia. Makamu Mwenyekiti ni Bibi Edith Lucina. Na Katibu Mkuu Taifa, ni Mheshimiwa Polisya Mwaiseje wote hao ni Wakristo. Kwa mantiki ya mwandishi wa makala hayo basi na NCCR-Mageuzi ni chama cha Wakristo! 

Na chama cha TLP, Mwenyekiti wake kitaifa ni Mheshimiwa Augustine Lyatonga Mrema, ambaye ni Mkristo. Katibu wake Mkuu ni Mheshimiwa Harold Jaffer na Katibu Mwenezi wa chama hicho ni Bwana Thomas Ngawaiya ambao wote ni Wakristo. Jee! Chama cha TLP ni cha Wakristo? 

Chama kingine kilichopata usajili wa kudumu na ambacho kina wabunge katika Bunge la Tanzania ni UDP. Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho ni Mheshimiwa John Momose Cheyo na Katibu Mkuu wake ni Mheshimiwa Richard Kasella Bantu. Wote hao ni Wakristo. Jee! Tuseme chama hicho cha UDP ni cha Wakristo? 

Vyama vyote hivyo japokuwa viongozi wake wote wa ngazi ya juu ni Wakristo mwandishi wetu hakudai kuwa vyama wanavyoviongoza ni, vya Wakristo. Lakini chama kimoja tu cha CUF kimetokezea kuwa na viongozi Waislamu tayari anakipakazia kuwa ni chama cha Waislamu! 

Kama chama cha CUF kweli ni cha Waislamu mbona katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Temeke ambalo wakazi wake wengi ni Waislamu, hakikuweka mgombea Mwislamu; lakini kilimsimamisha Bwana Tambwe Hiza ambaye ni Mkristo? 

Aidha kama CUF ni chama cha Waislamu vipi baadhi ya viongozi wake wa ngazi ya juu ni Wakristo? Kwa vile zaidi ya asilimia 95 ya Wazanzibari ni Waislamu, bila ya shaka yoyote wanachama wengi wa CUF na hata CCM huko Zanzibar watakuwa ni Waislamu; lakini mbona bara ambako kuna machanganyiko wa Waislamu na Wakristo chama cha CUF kina wafuasi kutoka katika dini zote mbili kuu? 

Hivi sasa wapiga debe wakubwa wa CUF bara ni Bwana Kasella Bantu ambaye ni Mkristo, Bwana Tambwe Hiza ambaye pia ni Mkristo na ndiye aliyesimama kidete kupinga shutuma za udini ndani ya CUF. Na kadhalika yupo Ndugu Kamara Kasupa ambaye yeye mwenyewe ni Mwinjilisti. Jee! Mwinjilisti kujiunga na chama cha Waislamu anatafuta nini? Au anataka kuwavua Waislamu waliomo katika CUF waingie Mkristo? 

Huu si wakati wa majungu na fitina! Huu ni wakati wa ukweli na uwazi. Kila mtu ana uhuru wa kusema na kuandika. Ule wakati wa kusema watu, fulani tu au wa kuwa na ukiritimba wa magazeti fulani umepitwa na wakati. Anayesema anajibiwa kwa hivyo mtu achunge sana anachokisema au kukiandika. Atakayesema ovyo, bila ya ushahidi atasutwa tu! 

Chuki za mwandishi wetu zimempofua macho hata haoni kuwa takriban vyama vyote vya kisiasa vilivyopata usajili wa kudumu, vile vya upinzani na hata chama tawala, vinaongozwa na Wakristo, lakini chama kimoja tu kuwa na viongozi Waislamu imekuwa nongwa? Jee! Waislamu hawana haki ya kuongoza katika nchi hii? 

Inaonekana ili mwandishi wetu akubali kuwa chama au taasisi fulani haina udini au si ya Kiislamu basi lazima chama au taasisi kama hiyo iongozwe na Wakristo tu, ikiongozwa na Waislamu imekwishageuka kuwa ni chama au taasisi ya Waislamu! 

Mwandishi wetu hakufanya hivyo kwa bahati mbaya; bali inaelekea kuna mkakati maalum uliolenga katika kuwatisha na kuwavunja moyo Waislamu nchini wasishiriki katika siasa na wala wasijitokeze katika kushika nafasi za uongozi katika vyama vya siasa na taasisi za kitaifa, ili siku zote wawe ni watu wa kuongozwa na kuburuzwa na Wakristo. 

Ndiyo maana akasema kuwa CUF inafanya kampeni zake misikitini. Lengo la kauli yake hiyo ni kuwatisha Waislamu wasizungumzie siasa misikitini. Lakini, kila siku, tunawasikia mapadre na Maaskofu wakitoa kauli za kisiasa na hata kushutumiwa na wanasiasa wakiwamo makanisani na siyo katika majukwaa ya kisiasa. Vipi basiviongozi wa dini ya Kikristo wawe na haki ya kuzungumzia siasa makanisani lakini viongozi wa dini ya Uislamu wasiwe na haki kama hiyo misikitini? 

Ama madai ya kwamba CUF ikishika madaraka nchini itaweka SHARIA badala ya SHERIA; hiloni jambo lisilo na ushahidi wowote. Ni chuki tu ya mwandishi huyo kuichukia SHARIA YA KIISLAMU!!! CUF, kikiwa ni chama cha kisiasa na si cha kidini; na hasa kwa vile baadhi ya viongozi wake wakuu pamoja na wafuasi wake wengi ni Wakristo hakiwezi kabisa kufanya lengo lake pindi kikishinda uchaguzi na kuingia madarakani eti sharia za Kiislamu. 

Kwanza, Uislamu si dini ya kulazimishana. Ni dini ya hiari. Kur-ani Tukufu inasema wazi wazi, "Hakuna kulazimishana katika (kufuata) dini (ya Uislamu)." Kwa hivyo fikra kuwa Mwislamu akishika uongozi wa nchi atawalazimisha watu wa dini nyingine waache dini zao na kuufuata Uislamu; au kwamba ataweka SHARIA badala ya SHERIA hazina ukweli wo wote. 

Lakini inachofaa mwandishi huyo aelewe ni kuwa Mwislamu yeyote, mwenye imani kamili na dini yake, anaitakidi kuwa dini ya haki mbele ya Allah (S.W.) ni Uislamu tu. Na kwamba Mwislamu ye yote atakayeridhia kwa nafsi yake mwenyewe, bila ya kulazimishwa, kuhukumu au kuhukumiwa kwa sheria isiyokuwa ya Allah (S.W.) basi huyo ni mharibifu, ni dhalimu na ni kafiri hasa! 

Na jambo hilo halina CUF, CCM, NCCR-Mageuzi, TLP au UDP. Kila Mwislamu awe mwanachama wa chama cho chote cha kisiasa mapenzi yake ni kutaka kuona si nchi hii tu bali ulimwengu mzima unafuata SHARIA na siyo SHERIA!!! 

Mimi sitaki kuwa msemaji wa chama cha CUF; lakini sitakaa kimya na kuridhia Uislamu ushutumiwe. Niwajibu wa kila Mwislamu anapoona watu, hasa wale wa dini nyingine, wanaipakazia au kuishutumu dini ya Uislamu waitetee dini yao kwa hali yo yote iwayo. Itikadi za kisiasa haziwezi kuwa ni sababu ya kumziba mdomo Mwislamu wa kweli asiitetee dini yake inaposhutumiwa na mkereketwa mwenziwe wa chama chake. 

Hakuna Mwislamu wa chama chochote kiwacho atakayekubali kuona SHARIA inavunjwa naye akaridhia. Ndiyo maana Waislamu wote wanakataa SHARIA ya Kiislamu ya mirathi kubadilishwa. Hakuna cha BAKWATA wala CCM, au TLP, au UDP au CUF, wote kwa pamoja wanapinga SHARIA ya Mirathi kubadilishwa! 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Mazingira ya uchaguzi huru na haki yasivurugwe

Wananchi washutumu vyombo vya habari

Lipumba awaambia wananchi wasibabaishwe na walioko madarakani

Wasomi SUA walaani ‘rushwa’ ya kisiasa

Polisi kataeni kutumiwa - Lipumba 

Maelfu ya tani za matunda yanaoza Tanga

Habari za ndani
Uondoeni ‘ukoloni’ wa CCM- Mbukuzi

MPASHO NASAHA
WABONGO HAWANA NYONGO !

HABARI
Nchi wafadhili wataka upinzani,  CCM yalalama

Waislamu Musoma walalamika

Habari za Kimataifa

Ushauri Nasaha
Jukumu la wazazi, walimu kwa wanafunzi wanaomaliza masomo

Makala
Madhara ya ulevi kwa binadamu

MAKALA
Sababu ‘1000’ kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani - 6

MAKALA
Kiini macho cha msamaha wa deni

Kalamu ya Mwandish
Kama CUF ni chama cha Waislamu 
Jee, CCM ni chama cha Wakristo?

MAKALA
Chama cha Mapinduzi na sera za maendeleo (2)

RIWAYA
Mapinduzi ya fikra

Lishe
Jinsi ya kuzuia utapiamlo kwa wanawake

BARUA

MASHAIRI

MICHEZO

  • Real Madrid yaingia fainali
  • Mapunda, Makoye hawafai timu ya Taifa - Kipingu
  • Tarimba ashinikizwa kujiuzulu Yanga

  •  

     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita