|
Mashairi
Cha pwaga kijungu gani? (Swali)
Kuna kitu chanitinga, jibule sijabaini,
Naomba wote malenga, jawabu nipatieni,
Songea hata Iringa, naomba nitajieni,
Cha pwaga kijungu gani?
Kijungu si cha udongo, pia si cha kiwandani,
Hiki chaumiza bongo, mijini na vijijini,
Msijitie mikogo, chungu hiki nambieni,
Cha pwaga kijungu gani?
Kijungu hakina huba, kuvuja yake tabia,
Ukipika kilo saba, kitonge taambulia,
Kwetu hiki ni msiba, kila nikiangalia,
Cha pwaga kijungu gani?
Chungu hiki cha wenyewe, wenyewe wasio shiba,
Ukijitia na wewe, utakupata msiba,
Ni nani hao wenyewe, eleza nipate shimba,
Cha pwaga kijungu gani?
Mtoto Mtauni (Mtafiti),
S.L.P 4,
Kilwa Kiwawa.
Sera gani (Jibu-4)
Sera ninazosikia, hazitatekelezeka,
Ajabu wamepania, madaraka kuyashika,
Hivi nini yao nia, hebu eleza Jushaka,
Sera hizo sera gani, Sabaya toboa siri.
(NASAHA na. 044 Jumatano Aprili 19,2000) _
Kijana Mtagaruka, umakini naamini,
Sikia ninatamka, maneno weka kichwani,
Sera alizo tamka, zakututia shimoni,
Leo natoboa siri, ni sera za chinja ua.
Kwani mimi nazijua, sera zao kwa makini,
Lisha niwakia jua, nilipo kuwa kambini,
Ni sera zinazo ua, wanyonge walo nchini,
Leo natoboa siri, ni sera za chinja ua.
Niliyavua magwanda, nikatoka ulingoni,
Serazo zimenishinda, za hawa mamumiani,
Za vijana kuwakwida, wanapo kuwa hakini,
Leo natoboa siri, ni sera za chinja ua.
Leo natubia kwenu, vijana nisameheni,
Nilipotea mwezenu, haya siku yabaini,
Watu hawa wanambinu, Mwenyezi nawapieni,
Lao natoboa siri, ni sera za chinja ua.
Beti tano naishia, ukweli nimewapeni,
Sera zimewaishia, wamefika ukingoni,
Mchumi twamngojea, alete nema nchini,
Leo natoboa siri, ni sera za chinja ua.
(Mwanafunzi),
Abdallah Omari Sabaya,
S.L.P. 100054,Mbagala,
Dar es Salaam
Ni fani ya mlaghai
Sitomvika kikuba, cha thamani mlaghai,
Nabatili langu huba, kumuenzi haifai,
Atenguaye katiba, kwangu ni kama adui,
Ni fani ya mlaghai, kuuvunja mkataba.
Bado natoa hotuba, madamu ningali hai,
Namuapiza kidhaba, ili awe goi goi,
Apotoaye katiba, na akifa sishangai,
Ni fani ya mlaghai, kuuvunja mkataba.
Kuuvunja mkataba, ni tabia ya laghai,
Kwake dhara na misiba, ni kama havikinai,
Bali tendo la haiba, huchochea halifai,
Ni fani ya mlaghai, kuuvunja mkataba.
Japo muunde nasaba, kwa hima na matumai,
Umfanye mahabuba, pasipo urai rai,
Atafuja lako heba, akidhani hung’amui,
Ni fani ya mlaghai, kuuvunja mkataba.
Alo jaliwa haiba, husasa awe nisai,
Umtakapo mahaba, hujidai hakatai,
Mwisho huzua kalaba, kuibera yako rai,
Ni fani ya mlaghai, kuuvunja mkataba.
Na akiwa ni kahaba, kwa lengo humgundui,
Atajifanya sahiba, kwa mbwembwe na hoi hoi,
Kume ni kama murumba, ana pendo la jinai,
Ni fani ya mlaghai, kuuvunja mkataba.
Mimi sivunji katiba, kwa hila na utatai,
Nitalinda mkataba, siku zote za uhai,
Japo awe na ujuba, laghai hani zuzui,
Ni fani ya mlaghai, kuuvunja mkataba.
Isamail A. Mbayani (Babu Mandevu),
S.L.P. 872, Bukoba.
Riziki katoa Mungu
Hodi ndugu washairi, wa Bara na Visiwani,
Nawe ndugu Mhariri, usiniweke kapuni,
Naleta langu shairi, ninene yalo moyoni,
Riziki katoa Mungu, vipi kwangu yakimbia?
Riziki katoa Mungu, kisha shusha duniani,
Kila mtu lake fungu, alivyopanga Manani,
Iweje kwangu ni chungu, isikae mawindoni,
Riziki katoa Mungu, vipi kwangu yakimbia?
Nimelima langu shamba, hekari ishirini,
Nikaipanda migomba, asubihi na jioni,
Nguruwe waja isomba, nikabaki taabani,
Riziki katoa Mungu, vipi kwangu yakimbia?
Nikakodi baskeli, nikaingia porini,
Na gunia zangu mbili, panga langu mkononi,
Pori nikalikabili, kwa nguvu zake Manani,
Riziki katoa Mungu, vipi kwangu yakimbia?
Kisha minika rejea, kutoka kule porini,
Mkaa usha enea, narudi zangu nyumbani,
Mabwana waningojea, kunipora masikini,
Riziki katoa Mungu, vipi kwangu yakimbia?
Kisha nikawa utingo, kutwa nashinda njiani,
Nikakipata kifungo, Myezi sita gerezani,
Kisa cha hicho kifungo, sare kuweka begani,
Riziki katoa Mungu, vipi kwangu yakimbia?
Nambieni waungwana, sasa nifanye nini?
Serikali imebana, kazi hazipatikani,
Nchi yapewa mabwana, kwa jina lawahisani,
Riziki katoa Mungu, vipi kwangu yakimbia?
Au kosa si kusoma, elimu sina kichwani!!
Wazazi Baba na Mama, walikuwa masikini,
Ni uwezo wa karima, lawama ni mpe nani,
Riziki katoa Mungu, vipi kwangu yakimbia
Nalimaliza shairi, nenda tulia nyumbani,
Nijuzeni washairi, mwezenu nitaabuni,
Lakini si kwa ramli, eti nina mashetani,
Riziki katoa Mungu, vipi kwangu yakimbia?
(Mwanafunzi)
Abdalah Omari Sabaya,
S.L.P 100054, Mbagala,
Dar es Salaam.
Nakulilia Lipumba
Mimi ndiye Tanzania, tabani hoi nalia,
Kifo kimeniwadia, ni mashaka kubakia,
Magoti nakupigia, Lipu uje nitibia,
Lipumba nakulilia, niokoe Tanzania.
Tibani wewe najua, wengine wananiua,
Wanipenda ninajua, niradhi kunichukua,
Tiba yangu waijua, nakulilia tambua,
Lipumba nakulilia, niokoe Tanzania.
Ninazidi angamia, KIDUMU wananiua,
Kazi kuning’ang’ania, MALI ZOTE wang’amua,
Masikini najifia, hawa Lipu waniua,
Lipumba nakulilia, niokoe Tanzania.
Mimi sio MASIKINI, wasomi wananijua,
Ni TAJIRI UCHUMINI, wachache wananiua,
MBUGA, MISITU, MADINI, wageni vyawainua,
Lipumba nakulilia, niokoe Tanzania.
Inayoniponza mbovu, siasa inaniua,
KIDUMU kina MAOVU, kimepanga kuniua,
MCHUMI na MTULIVU, LIPU njoo niinua,
Lipumba nakulilia, niokoe Tanzania.
Umefuzu uchumini, gonjwa linonisumbua,
Nitapona naamini, LIPU ukinichukua,
Kwa mfano mpakani, UGANDA umeinua,
Lipumba nakulilia, niokoe Tanzania.
Watu wangu fikirini, wanangu Watanzania,
Kabila na zote DINI, LIPU nimemridhia,
OKTOBA chaguzini, LIPU wakumpigia,
Lipumba nakulilia, niokoe Tanzania.
LIPU bora duniani, Ulaya wakutambua,
Wafundisha Ulayani, Uchumi ukichambua,
Unaheshima Swideni, Marekani wakujua,
Lipumba nakulilia, niokoe Tanzania.
LIPU wewe mwaadilifu, hata Mungu atambua,
Lipu wewe mwaminifu, kamwe hutanikamua,
Lipu HAKI unasifu, mwiko kwako kubagua,
Lipumba nakulilia, niokoe Tanzania.
Tanzania ndio mimi, kwako nimeshasaini,
Unaninua uchumi, DAKTARI simuoni,
Tiba tosha kwangu mimi, Lipu kwako naamini,
Lipumba nakulikia, niokoe Tanzania.
DAKTARI umewini, Lipumba nakuamini,
Kutibu umasikini, kutibu kwangu nchini,
Uchumi mganga nani? “kama siwe Lipu nani?”
Lipumba nakulilia, niokoe Tanzania.
Wengine kwao maneno, walichosomea MENO,
Yao maneno maneno, amani yao waneno,
Waongo waso mfano, Lipu kwakosina neno,
Lipumba nakulilia, niokoe Tanzania.
Wengine hawaridhishi, wamefuzu uandishi,
Abadani hawatoshi, mimi hawa niridhishi,
Wazuri kimatamshi, wabaya kiutumishi,
Lipumba nakulilia, niokoe Tanzania.
Wengineo ni walimu, Tiba kwangu haitoshi,
Wangineo madhalimu, kwangu ni waangamishi,
Wengineo wahujumu, wewe pekee ridhishi,
Lipumba nakulilia, niokoe Tanzania.
Ni mwishoni shairini, baba ninakutamani,
Nijulike duniani, Tanzania mipakani,
Niangaze kileleni,juu Kilimanjaroni,
Lipumba nakulikia, niokoe Tanzania.
Almasi H. Shemdoe,
“Tunda la Matumaini”,
Dar es Salaam.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Mazingira ya uchaguzi huru
na haki yasivurugwe
Wananchi
washutumu vyombo vya habari
Lipumba
awaambia wananchi wasibabaishwe na walioko madarakani
Wasomi
SUA walaani ‘rushwa’ ya kisiasa
Polisi
kataeni kutumiwa - Lipumba
Maelfu
ya tani za matunda yanaoza Tanga
Habari za ndani
Uondoeni
‘ukoloni’ wa CCM- Mbukuzi
MPASHO NASAHA
WABONGO
HAWANA NYONGO !
HABARI
Nchi
wafadhili wataka upinzani, CCM yalalama
Waislamu
Musoma walalamika
Habari
za Kimataifa
Ushauri Nasaha
Jukumu
la wazazi, walimu kwa wanafunzi wanaomaliza masomo
Makala
Madhara
ya ulevi kwa binadamu
MAKALA
Sababu
‘1000’ kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani - 6
MAKALA
Kiini
macho cha msamaha wa deni
Kalamu ya Mwandish
Kama
CUF ni chama cha Waislamu
Jee,
CCM ni chama cha Wakristo?
MAKALA
Chama
cha Mapinduzi na sera za maendeleo (2)
RIWAYA
Mapinduzi
ya fikra
Lishe
Jinsi
ya kuzuia utapiamlo kwa wanawake
BARUA
MASHAIRI
MICHEZO
Real Madrid yaingia fainali
Mapunda, Makoye hawafai timu
ya Taifa - Kipingu
Tarimba ashinikizwa kujiuzulu
Yanga
|