|
Na. 047 Jumatano Mei 10 - 16, 2000 |
|
|
|
|
|
Mauaji ya Kanisa la Kurejesha
Amri Kumi za Mungu:
Kampala, UGANDA MAUAJI ya hivi karibuni yanayohusianishwa na lile dhehebu la Kikristo la Uganda, yawezekana ni mbinu ya kuficha mauaji ya Waislamu yaliyofanywa na utawala wa Uganda. Kulingana na habari kutoka Kampala, Uganda, kiasi cha miili 40 ya watu ambao wamefukuliwa kutoka katika makaburi ya halaiki, imetambuliwa kuwa ni ya Waislamu. Viongozi kutoka nchi nzima wameitaka serikali kutoa taarifa juu ya zaidi ya Waislamu 1000 ambao wametupwa jela katika kipindi cha miaka michache iliyopita bila kushitakiwa. "Ninahofia kwamba baadhi ya miili iliyofukuliwa ni ya Waislamu hawa waliokamatwa na kutiwa kizuizini kama wafungwa wa kisiasa", alisema Imamu mmoja wa Kampala kulieleza jarida la Cresent International. "Ni jambo ovu kabisa maiti za Waislamu na dhehebu ambalo hawakuwaza hata kulikaribia", aliongeza. Imam huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema, kwamba Waislamu wote wa Uganda walistushwa sana na ugunduzi wa maiti za Waislamu. "Tulifahamu kwamba mambo yalikuwa mabaya, lakini siyo kwa kiasi hiki". Mashaka yaliyokuwepo ya kwamba sio zote katika maiti 1000 zilizofukuliwa toka kwenye makaburi ya halaiki ni wafuasi wa dhehebu hilo, yalitiwa nguvu na Aggrey Amori, Mbunge wa Chama cha upinzani aliliambia Bunge kwamba "maiti zilizofukuliwa toka mojawapo ya makaburi ni za Waislamu, pengine ni miongoni mwa wale waliofungwa kwa kuipinga serikali hapo kabla". Bw. Amori, ambaye sio Muislamu na ambaye ni Mbunge wa Samia Bungwe, aliliambia jarida la Cresscent International kwamba ipo haja ya kuundwa Tume Huru mara moja ili kufahamu nini hasa kilitokea Uganda kuhusiana na mauaji hayo. Vinginevyo tutaishia na upotoshaji mkubwa wa ukweli, habari za uzushi zenye ukweli nusunusu na uongo mwingi ambao ni kashfa kubwa kwa watu wasiokuwa na hatia walioangamia katika uendawazimu huo". Ukatili mkubwa wa hivi karibuni dhidi ya Waislamu nchini Uganda, na ukimya wa Jumuiya ya Kimataifa, sio jambo geni na halitofautiani na matukio kama hayo katika historia ya Uislamu Uganda. Wakati wa ukoloni, Waislamu waligandamizwa kwa kiwango cha kutisha, na hali hiyo iliendelea chini ya watawala tangu mwaka 1992. Na hivi majuzi, Rais wa sasa Bwana Yoweri Museveni ameondokea kuwa mpinzani mkubwa wa Uislamu katika bara lote la Afrika na hivyo kujizolea umaarufu mkubwa katika nchi za Magharibi. Wakati habari hizi za mauaji na ukatili zikidhihirishwa jijini Kampala, Museveni alikuwa London, Uingereza akila na kunywa na wanasiasa na viongozi wa Kanisa. Na wakati nchi za Magharibi zikiomboleza waathiriwa wa dhehebu la Kikristo, Waislamu wa Uganda wanajiuliza ni maiti ngapi za ziada za Waislamu zitakazopatikana tena na mambo yepi mengine ya kutisha yanayongoja kugunduliwa. Wakati huo huo, polisi wa Uganda wamekanusha madai ya Mbunge Aggrey Awar (Samia Sugwe) kwamba maiti za wanaume waliotahriwa zilizopatikana toka kwenye kaburi la halaiki zilikuwa za Waislamu. Polisi nao walidai kwamba hata makabila ya Bakonzo na Bamba wanatahiri wanaume wao hivyo madai ya Awari hayana msingi wowote. Habari hizo zilizopatikana toka katika gazeti la The Monitor la Uganda zilisema kwamba kwa mujibu wa mkuu wa wilaya ya Bundibugyo, Charles Tumwesigye, watu zaidi ya 20 toka katika eneo lake waliuawa na dhehebu hilo. Hata hivyo, Bwana Tumwesigye alipingana na polisi pale aliposema; "pamoja na wafusai waliotahiriwa wa kabila la Bamba, niliona maiti ya mfuasi mmoja aliyejulikana kwa jina la Abubakar ambaye ni Muislamu". Inafahamika kwamba maelfu ya Waislamu wapo katika
jela za Uganda kwa sababu za kisiasa na wengi wao wamefungwa bila kufunguliwa
mashitaka.
Mtuhumiwa wa kirusi cha kompyuta 'LOVE BUG' akamatwa
WAENDESHA mashtaka nchini Phillipines siku ya Jumanne walisema kwamba polisi hawakuwa na ushahidi wa kutosha kuendelea kumshikilia mtu anayeshukiwa kuwa ndiye aliyekitengeneza kirusi cha kompyuta kilichoitwa 'love bug' na kuamuru aachiwe huru. Reonel Ramones (27), ambaye ni mfanyakazi wa benki alitiwa mbaroni na polisi nchini Phillipines siku ya Jumatatu kwa tuhuma za kuvunja sheria inayohusiana na "maneno ya siri" (passwords), sheria ambayo msingi wake ni kulinda maneno ya siri (passwords) kwa ajili ya kadi za malipo (credit cards). Tuhuma hizo zilitokana na malalamiko kutoka kwenye makampuni yanayotoa huduma ya mtandao wa kompyuta (Internet Service Providers-ISPs) kwamba kirusi ambacho kiliziingia kompyuta nyingi duniani wiki iliyopita kilianzia kwenye nyumba anamoishi Ramones pamoja na rafiki wake wa kike, Irene de Guzman. Uharibifu uliosababishwa na kirusi cha "Love Bug" umefikia dola bilioni 5 na inakadiriwa kwamba unaweza kufikia dola bilioni 10, zilisema taarifa kutoka katika shirika moja la Marekani, Computer Economics. Kirusi asilia ambacho kina ujumbe unaosema "nakupenda" (ILOVEYOU) kinafanya kazi kwa kumshawishi mwenye kupokea ujumbe-umeme (email) wake afungue faili linaoambatana na ujumbe huo. Pindi mtu anapofungua tu faili hilo basi kirusi hicho huvuruga mfumo mzima wa kompyuta hiyo (Hard-Disk). "Ushahidi hautoshi," alisema mwendesha mashitaka mkuu, Severino Gana kuwaambia waandishi wa habari baada ya kutolewa matokeo ya uchunguzi wa awali kabla ya kufunguliwa mashitaka ya jinai. "Bado kuna baadhi ya 'diskettes' zinatakiwa kukaguliwa." Alisema kuwa Ramones ameachiwa huru wakati ushahidi zaidi ukiendelea kutafutwa na anatarajiwa kujibu mashitaka ya awali tarehe 19 mwezi wa tano mwaka huu. Ramones alisema kuwa yeye ni mhanga wa "kufananishwa," lakini hakufafanua. Siku ya Jumatatu wapelelezi waliipekua nyumba yake na kumkamata Ramones; lakini de Guzman hakuwepo nyumbani. Baadaye aliiambia idara ya upelelezi kuwa atajisalimisha lakini alikana kuhusika. "Ni wazi kwamba hahusiki kwa vyovyote," alisema Rolando Quimbo ambaye ni mwanasheria wa de Guzman kuwaambia waandishi wa habari wakati alipozitembelea ofisi za idara ya upelezi. Wapenzi hao wawili wote walisoma katika chuo cha AMA Computer College (AMACC) mjini Manila na ofisa mmoja wa upelelezi, Elfren Meneses, alisema kuwa kuna watu wengine wanane ambao wana mahusiano na chuo hicho na wanashukiwa kuhusika na usambazaji wa kirusi cha "Love Bug." Aliwaambia waandishi wa habari kuwa kuna majina 10 yaliyokutwa kwenye kirusi hicho. "Kulikuwa na taarifa kutoka idara ya upelezi ya Marekani, FBI, kwamba majina hayo yanaelekea kutoka katika shirika liitwalo AMACC," alisema na kuongeza kuwa chuo hicho kiliahidi kutoa msaada katika uchunguzi huo. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, AMACC ilisema kuwa inafahamu kwamba kuna watu wenye kuhusiana na chuo hicho ambao wanatuhumiwa kuwa ndiyo waliokibuni kirusi hicho. Mkuu wa idara ya upelelezi, Federico Opinion alisema kuwa ingawaje hakuna kompyuta iliyokutwa kwa Ramones, kuna ushahidi kwamba ilikuwepo na kwamba iliondolewa. "Hapakuwa na kompyuta lakini kulikuwa na dalili kwamba vitu viliondolewa, kulikuwa na vifaa vya kompyuta," alisema. Idara ya upelelezi imeiweka nyumba ya Ramones chini ya uangalizi tangu Jumamosi mara tu baada ya taarifa kwamba kirusi kile kilianzia hapo. Idara hiyo haikuweza kuchukua hatua yoyote kwa sababu uharibifu kwa kutumia kompyuta siyo kosa kwa sheria za Phillipines na haikuweza kupata hati ya kupekua mpaka Jumatatu. "Love Bug" ni kirusi cha hatari kabisa kilichopata kuundwa. Mara tu mtu anapofungua barua-umeme inayokibeba na kukifanya kifanye kazi kwa kukibonyeza (double-clicking), kirusi hicho husambaa kupitia kwenye anuani zote zilizopo kwenye programu ya kutuma barua-umeme (email), MS OutLook Express, kisha huharibu mafaili kadhaa yaliyopo ndani ya kompyuta iliyoathiriwa kabla ya kusambaa katika mtandao (network) iwapo kompyuta hiyo imeunganishwa na nyinginezo.
Russia yakiri kupoteza ndege ya kivita Chechnya
TAARIFA za kijeshi za Russia zimethibitisha kupotea kwa ndege ya kivita aina ya SU-24 ndani ya Chechnya Jumapili iliyopita. Jeshi la Russia linaendelea kuitafuta ndege hiyo pamoja na marubani wake. Russia haijathibitisha kama ndege hiyo imeangushwa na wapiganaji wa Chechnya. Lakini taarifa iliyotolewa na msemaji wa wapigianaji wa Chechnya Morladi Udogov amesema kuwa wapiganaji hao wameangusha ndege mbili za Russia mwisho wa wiki iliyopita. Udogov amesema ndege moja aina ya SU-24 iliangushwa katika eneo la Vedeno muda mfupi baada ya Vladmir Putin kuapishwa kuwa Rais wa Russia. Ndege nyingine iliangushwa kwenye mpaka na Jamhuri ya Dagestan. Udogov pia amesema kuwa askari 12 wa Kirusi wameuawa katika shambulio lililofanywa kwenye treni. Russia imesema kuwa imeongeza usalama ndani ya Chechnya kuepusha athari kwa utawala mpya wa Putin. Wakati huo huo, Rais wa Russia Bw. Vladmir Putin jana alikagua gwaride la jeshi katika siku ya kuadhimisha miaka 55 ya ushindi dhidi ya NAZI wa Ujerumani walioongozwa na Adolf Hitler. Putin amesema, japokuwa ni siku nyingi zimepita lakini bado kumbukumbu hiyo ni muhimu ili kuwadhihirishia maadui kuwa agenda ya kutawala nchi nyingine kwa kutumia nguvu za kijeshi haikufanikiwa na haitafanikiwa. Miaka 55 iliyopita Ujerumani ilipambana na Urusi katika kampeni yake ya kutawala ulimwengu, kampeni iliyopelekea kutokea vita vya kwanza na vya pili vya dunia ambapo Ujerumani ilishindwa vibaya dhidi ya mataifa washirika. Vladimir Putin anakamata rekodi ya Russia kwa kuwa Rais kijana zaidi katika historia ya Urusi inayodumu kwa karne moja.
Mbunge wa Kenya ataka mashamba ya Wazungu yavamiwe
NAIROBI, Kenya MBUNGE wa Chama cha upinzani cha Social Democratic Party nchini Kenya, Bw. Stephen Ndicho ametoa wito kwa Wakenya wasio na ardhi kuvamia mashamba yanayomilikiwa na Wazungu. Mbunge huyo amemtaka Rais Daniel Arap Moi kuiga mwenendo wa Rais Mugabe wa Zimbabwe na pia kuwaunga mkono Wakenya wasio na ardhi kuchukua mashamba yanayomilikiwa na wageni. Amenukuliwa na gazeti la East African Standard akisema, wageni na Wazungu wana siku 90 tu za kuyawacha mashamba yao na kuyakabidhi kwa walalahoi wa Kenya. "Wazee wetu walipigana dhidi ya wakoloni katika miaka ya 1950 na wangeweza kuchukua ardhi lakini wageni mpaka leo wanaendelea kumiliki mashamba makubwa wakati watu wetu wamebaki bila ardhi", alisema. Ndicho ameyataja mashamba yanayomilikiwa na makampuni ya Chai na Kahawa ya Kakuzi na Socfinaf kuwa ni mashamba ya kwanza kuvamiwa. Mashamba hayo yote yanamilikiwa na Wakenya wenye
asili ya Kizungu na Kiasia.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Wananchi washutumu vyombo vya habari Lipumba awaambia wananchi wasibabaishwe na walioko madarakani Wasomi SUA walaani ‘rushwa’ ya kisiasa Polisi kataeni kutumiwa - Lipumba Maelfu ya tani za matunda yanaoza Tanga Habari za ndani
MPASHO NASAHA
HABARI
Ushauri Nasaha
Makala
MAKALA
MAKALA
Kalamu ya Mwandish
MAKALA
RIWAYA
Lishe
|
|
|
|
|