|
Na. 047 Jumatano Mei 10 - 16, 2000 |
|
|
|
|
|
Chama cha Mapinduzi na sera za maendeleo (2)
JAMBO hili si geni hapa nchini, miaka yote imekuwa ni kawaida kwetu kumsikia Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali akitutangazia wizi na ubadhirifu wa fedha za wananchi ndani ya Mawizara na idara mbali mbali za serikali ambao huwa haushughulikiwi kisheria. Katika kuhakikisha kuwa viongozi wabadhirifu hawashughulikiwi ipasavyo, hata ofisi ya maadili ya viongozi wa umma iliyoanzishwa mwanzoni mwa mwaka 1996, ili kudhibiti mienendo ya viongozi wa umma nayo pia umewekewa vizingiti vya kisheria ili ishindwe kufanya shughuli zake sawa sawa. Katika sheria inayohusika na maadili ya viongozi, kifungu cha 23 kinamtaka raia yoyote mwenye malalamiko dhidi ya kiongozi wa umma anaehusika kwa mujibu wa sheria hiyo, awasilishe malalamiko yake kwa maandishi yaliyowekewa sahihi, jina na anuani ya mlalamikaji. Kwa sababu ya hofu ya kuchukuliwa hatua kali na vigogo wenye nchi wala nchi inakuwa ni vigumu kwa watumishi wa serikali, idara za serikali, mashirika ya umma (ambayo bado hayajauzwa kwa sasa) na hata wananchi wa kawaida, kutoa taarifa ili hatua zichukuliwe mapema. Mwaka huo huo wa 1998 kulipata kutokea ubishi makali ndani ya Bunge baada ya fedha kiasi cha shilingi milioni 154.5 za mgawanyo wa dharura kutoka katika bajeti ya serikali ya mwaka 1997 kutumika bila ya kutolewa maelezo ya kuridhisha. |Akichangia muswada wa sheria wa kuidhinisha matumizi ya serikali ya mwaka 1997 uliowasilishwa bungeni na Naibu Waziri wa Sheria, kwa ajili ya kupitishwa bila kupingwa, mbunge wa viti maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Thabita Siwale alieleza wazi kuwa madaraka aliyopewa Waziri wa Fedha kisheria ya kuweza kugawa upya fedha za bajeti bila ya kupatiwa na kikao chochote ni hatari. Kimantiki, sheria kama hizi ndio hasa NI mianya ya rushwa au ufujaji wa fedha za serikali, sote tunafahamu sababu iliyomfanya Profesa Mbilinyi, aliyekuwa Waziri wa Fedha kabla ya huyu wa sasa kujiuzulu. Ilikuwa ni tuhuma ya ulaji wa rushwa, kwa kusamehe ushuru (kodi) ya minofu ya samaki, kwa mamlaka aliyopewa kinyume cha sheria za bunge. Hili ni tatizo la msingi kabisa linaloikabili nchi yetu, bila ya kuwa na mfumo wa utawala bora, utakaowezesha malalamiko ya wananchi kuhusu utendaji na mamlaka waliyopewa watendaji wakuu katika taasisi mbali mbali nchini, ikiwa ni pamoja na Polisi, na mahakama, ambayo mara nyingi hapa nchini hutumika kukidhi matakwa ya wanasiasa, demokrasia ya kweli nchini itabaki kuwa ni nadharia isiyotekelezeka. Ufujaji na ubadhirifu wa mapesa ya umma umekithiri mno nchini, umeenea karibu katika idara na wizara zote za serikali, hasa kwa kutumia kasma ya masurufu. Takwimu zilizokusanywa kutoka vyanzo mbali mbali zinaonyesha kwamba mpaka kufikia Desemba mwaka 1999, Wizara ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilikuwa bado haijarejesha masurufu kiasi cha shilingi bilioni 4.329. Sayansi, teknolojia na elimu ya juu, milioni 543, tume ya taifa ya uchaguzi milioni 415, mfuko wa pembejeo katika wizara ya kilimo, ulikopesha kiasi cha shilingi bilioni 5.765, zilizorejeshwa ni bilioni 1.242 tu. Wananchi walitegemea kusikia serikali ikitangaza kusimamishwa kwa utoaji zaidi wa masurufu katika wizara husika, lakini wapi, vigogo wanaendelea kuchota kama kawaida. Hali inatisha, tabia ya serikali ya ChamaCha Mapinduzi kutenga kiasi kikubwa cha fedha katika bajeti za kila mwaka kwa ajili ya matumizi ya kawaida, badala ya matumizi ya maendeleo ya nchi, ni ushahidi kuwa maslahi ya wananchi si katika sera za Chama Cha Mapinduzi. Wananchi wana msemo kwamba "ada ya mja ni kunena lakini muungwana ni vitendo. Huu ni msemo wenye mantiki kali, maana itakuwa ni kichekesho kuamini eti anaekupiga kofi ni kwamba kafanya hivyo kwa sababu anakupenda. Biashara za baadhi ya wananchi zinakufa, na watoto wao wanakufa njaa kwa sababu serikali imekataa kulipa madeni ya ndani kwa kisingizio cha kuhakiki usahihi wa madeni hayo. Ni jambo la kusikitisha, idara ya magereza peke yake inadaiwa shilingi bilioni 9.8, kilimo shilingi 693,759,323 na ofisi ya Makamu wa Rais shilingi 276,730,756. Madeni ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi si ya nje peke yake, humu nchini serikali inadaiwa kiasi cha shilingi bilioni 15 na shirika la umeme la Tanzania (TANESCO), hili ni deni hadi kufikia mwezi Desemba 1999. Kama deni hilo limeongezeka au limelipwa hakuna ajuae. Wananchi wanataka kujua, kama serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 939 kwa ajili ya matumizi ya mwaka 1999/2000, ni matumizi gani hayo ambayo hayana fungu kwa ajili ya matumizi yake ya umeme? Na je siku shirika la umeme litakapokuwa ni la mtu binafsi atakubali kudai kiasi hicho cha fedha na bado aendelee kutoa umeme? Ushauri kwamba tuwape viongozi wa Chama Cha Mapinduzi
nafasi tena ya kuongoza nchi kwa matumaini kwamba huenda wakajirekebisha
ni uwendawazimu.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Wananchi washutumu vyombo vya habari Lipumba awaambia wananchi wasibabaishwe na walioko madarakani Wasomi SUA walaani ‘rushwa’ ya kisiasa Polisi kataeni kutumiwa - Lipumba Maelfu ya tani za matunda yanaoza Tanga Habari za ndani
MPASHO NASAHA
HABARI
Ushauri Nasaha
Makala
MAKALA
MAKALA
Kalamu ya Mwandish
MAKALA
RIWAYA
Lishe
|
|
|
|
|