|
Na. 047 Jumatano Mei 10 - 16, 2000 |
|
|
|
|
|
Na Mwandishi Wetu WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Kilimo-Sokoine kilichopo Morogoro, wamelaani kile walichodai kuwa ni rushwa ya kisiasa ambayo inalenga kuwarubuni wanafunzi kwa vitisho na'hongo' ya ahadi za kutafutiwa ajira na chama tawala pindi watakapokiunga mkono. Wakizungumza kwa nyakati tofauti na NASAHA kuhusu madai hayo, wanafunzi hao walitoa mfano wa wimbi la wanafunzi wa chuo hicho kujitokeza hadharani katika sherehe za kukabidhiwa kadi za uanachama wa CCM jambo ambalo linavunja masharti ya mkopo wa masomo kwa wanafunzi hao wanapjiunga na chuo hicho kwa masomo yashahada ya Kwanza. "Sisi tunapojiunga na chuo hutakiwa kusaini kukubali masharti ya mkopo wa kudhaminiwa na serikali masomo ya shahda", alisema mmoja wa wanafunzi hao ambaye aliomba asitajwe jina lake gazetini. Mwanafunzi huyo aliongeza kwa kusema "moja ya masharti hayo ni kuwa mwanafunzi asijihusishe na masuala ya siasa wakati akiwa masomoni, na kwamba akienda kinyume na masharti hauyo, udhamini huo utafutwa!! Wanafunzi hao walikuwa wakitoa maoni yao kufuatia kile walichodai kukithiri kwa harakati za kisiri siri za kushawishi wanafunzi chuoni hapo ili wajiunge na chama tawala, kwa madai kuwa wanachama hao watawasaidia kutafutiwa ajira pindi wamalizapo masomo yao. Walieleza kuwa harakati hizo hushamiri pindi wanapotarajiwa kutembelewa na viongozi wa chama na serikali ngazi ya mkoa au taifa. Mara baada ya ziara hizo, wanafunzi walioshawishika husafirishwa na magari ya chuo hadi mjini ambako sherehe za kukabidhiwa kadi za uanachama hufanyika mbele ya viongozi hao. "Mwaka juzi baadhi ya wanafunzi walisafiri hadi Dodoma ambako walikabidhiwa kadi mbele ya Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Mhe. Mkapa", alisema mwanafunzi mwingine ambaye naye alikataa kuandikwa jina lake gazetini kwa hofu ya "kuandamwa" na wale watakaochukizwa na habari hizi. Hivi karibuni Waziri Mkuu Mhe. Frederick Sumaye alifanya ziara mkoani Morogoro ambako alitembelea Mzumbe na Chuo cha Sokoine ambako alishiriki hafla ya upandaji miti. Mara baada yaziara hiyo Mhe. Waziri Mkuu alikabidhi kadi za CCM kwa wanachama wapya. Hafla hiyo ilifanyika katika ofisi za CCM Wilaya ya Morogoro mjini. Gazeti moja litolewalo kila siku jioni, katika toleo lake la tarehe 4 Mei mwaka huu lilichapisha picha iliyowaonesha baadhi ya wanachama wapya waliokabidhiwa kadi ambao walitajwa kuwa ni "vijana na chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo Morogoro". Mwanafunzi mmoja wa kike ambaye alisema kuwa yeye simiongoni mwa waliochukua kadi hizo za CCM alidai kwamba alifuatwa na rafiki aliyejaribu kumshawishi kwenda kuchukua kadi kwa maelezo kwamba wangalipatiwa ajira na chama hicho mara tu watakapomaliza masomo yao. "Nilimuuliza; CCM wangetuajiri wapi wakati nasikia SUKITA iliishafilisika na kuuzwa", alisema mwanafunzi huyo ambayenae pia alionesha woga wa kutajwa jina lake gazetini. "Hivyo", aliendelea kueleza mwanafunzi huyo, "huyo rafiki yangu hakuwa na majibu yaliyoeleweka nami sikushawishika na propganda hizo." Akitoa maoni yake juu ya madai hayo, mwanafunzi mmoja anayesoma shahada ya juu chuoni hapo alisema kuwa propaganda hizo bila shaka zina lengo la kuwapata wanafunzi vijana ambao wengi wao wamejiunga chuoni hapo baada ya kumaliza kidato cha sita sekondari. Hata hivyo alieleza kuwa, mwenendo huo kama ni kweli unatumika kupata wanachama si mzuri, maana unaweza kuwafundisha kuamini kuwa njia za vishawishi ni muhimu katika maendeleo ya maisha yao. "Vijana kama hawa wakianza kushawishika mapema katika maisha yao ipo hatari huko mbele kuzoea mwenendo huu wa kurubuniwa", alisema msomi huyo na kumalizia "tabia hii kama ni kweli ipo inaweza ku-'create potential corrupt elements' katika system" akimaanisha, uwezekano wa kuwaandaa wala rushwa katika taasisi zetu. Mwanafunzi mwingine anayesomea shahada ya juu katika chuo hicho aliielezea hali hiyo kuwa ni "rushwa" ya kisiasa". Msomi huyo alilaani kitendo cha kuwatisha wanafunzi wanaoonesha hisia zao za kisiasa kuunga mkono upande wa upinzani na vitendo vya baadhi ya washabiki na viongozi wa siasa kutaka kuwalazimisha kuunga mkono siasa za chama tawala. Pamoja na hali hiyo, kulikuwepo na taarifa katika baadhi ya vyombo vya habari zilizodai kuwa wanafunzi wa shule za sekondari Tabora walisimamishwa masomo kama adhabu kutokana na tuhuma kuwa walihudhuria mkutano wa hadhara uliokuwa ukihutubiwa na Mwenyekiti wa Chama cha CUF Prof. Ibrahim Lipumba. Wakati huko Kilimanjaro ilidaiwa kuwa wanafunzi wa shule ya sekondari walisimamishwa masomo kwa kutokuhudhuria mapokezi na mkutano wa Waziri Mkuu Frederick Sumaye ambaye pia ni kiongozi katika chama cha CCM. Aidha, kiasi cha miezi miwili iliyopita gazeti hili liliripoti habari za wanafunzi wa Kiislamu wa shule moja ya sekondari jijini waliohojiwa na waalim wao kwa madai ya kufanya 'kosa' la kuhudhuria khitma iliyoandaliwa na Halmashauri Kuu ya Waislamu kwa ajili ya wale waliouliwa Mwembechai Februari, 1998. Katika maoni yao, wanafunzi hao na Sokoine walisema kuwa mwenendo huu, mbali ya kuwa na mtazamo wa kuwarubuni kirushwa, umeambatana na mtazamo wa vitisho ambavyo vinawanyima haki yao ya kidemokrasia ya uhuru wa mawazo na mtazamo wa kisiasa wautakao. |
YALIYOMO
TAHARIRI
Wananchi washutumu vyombo vya habari Lipumba awaambia wananchi wasibabaishwe na walioko madarakani Wasomi SUA walaani ‘rushwa’ ya kisiasa Polisi kataeni kutumiwa - Lipumba Maelfu ya tani za matunda yanaoza Tanga Habari za ndani
MPASHO NASAHA
HABARI
Ushauri Nasaha
Makala
MAKALA
MAKALA
Kalamu ya Mwandish
MAKALA
RIWAYA
Lishe
|
|
|
|
|