|
Na. 047 Jumatano Mei 10 - 16, 2000 |
|
|
|
|
|
Sababu '1000' kwanini tunataka
CCM ing'oke madarakani - 6
SASA hawana dira, hawana sera, wala hawana
lengo, kwa kifupi wamefilisika. Ingekuwa ni kampuni basi CCM ingekwisha
tangazwa kwamba ni "Mufilisi" na wale wote wanaoidai wasamehe madeni yao
kwakuwa kampuni haina chochote cha kuwalipa na deni lake halilipiki kabisa,
ama ingekuwa ni moja ya mashirika ya umma ingebidi ibinafsishwe na kutafutiwa
tajiri wa kuinunu mara moja. Wala CCM hawana mpango wowote kwa ajili ya
wananchi, hata mtu akiwauliza sasa wako madarakani kufanya nini na kwaajili
ya nani, bila shaka jibu lake litakuwa kwamba tuko madarakani kwa sababu
madaraka ni matamu. Wala hawana kile walichozea kuita mshikamano kwani
kila mmoja yuko madarakani kwasababu zake binafsi.
KUNA wengine wapo madarakani ili kulinda utajiri wao maana siku watakapoachia madaraka utakuwa ndio mwanzo wa kufilisika kwakuwa ni madaraka ndiyo yaliyowatajirisha na siyo bidii ya kazi na maarifa ya kuutafuta utajiri. Kuna wengine wamefanya makosa mengi ya jinai kiasi kwamba wanaogopa siku ya kuachia madarakal abda watashitakiwa, ndiyo maana wakati mwingine wamediriki kutunga miswada kwa madhumuni ya kuweka sheria za kujihami wasifikishwe mahakamani baada ya kuachia ngazi. Kuna wengine ambao kwasababu ya ulevi tu na kula huduma kwenye madaraka kwa muda mrefu wamelemaa kiasi cha kuona haya kuishi bila ya wadhifa wowote, hawa ndio wenye ndoto za kufia madarakani kama walizokuwa nazo akina Idd Amin, Mathias Nuema, Bedel Bokasa, Kamuzu Banda, Mobutu Sese Seko na wale waliojiita "rais wa maisha." Hapa Tanzania wapo "Mawaziri wa Maisha", "Wabunge wa maisha", "mabalozi wa maisha" n.k. Hawa hawawezi kupisha damu mpya, au kizazi kipya hadi kifo kitakapowatenganisha na madaraka yao. Pamoja na kwamba mkusanyiko wao ni katika msingi wa ubinafsi wa kila mtu na lwake, lakini bado katika ubinafsi wao CCM wanaunganishwa na neno moja kuu nalo ni nguvu za dola. Tumaini lao lote ni katika mapolisi na magereza. Siyo siri kwamba CCM imelipindua jeshi la Polisi na kuligeuza kuwa jeshi la kichama ambalo liko kulinda maslahi ya Chama Cha Mapinduzi, na siyo maslahi ya raia. Sababu za Polisi kuuvaa U-CCM ziko nyingi na nitazieleza kwa ufasaha katika toleo lijalo. Ili kulinda maslahi ya Chama Cha Mapinduzi inabidi Polisi ipambane na yeyote yule atakayejionyesha kuleta upinzani dhidi ya CCM na hasa ule upinzani makini unaoelekea kuing'oa CCM madarakani. Siku za nyuma upinzani ulipojitokeza kwa waandishi wa habari ambao kalamu zao zilikuwa hazichoki kuandika mabaya ya watawala, mapambano kati ya Polisi na wanahabari yalikuwa makali na ya mara kwa mara, wengi bado wanakumbuka sakata za Polisi kuwapiga virungu waandishi na kunyang'anya kamera zao au kuziharibu. Wengi bado wanakumbuka jinsi mwandishi Mwaibabile alivyofungwa (gerezani) katika mazingira ya kutatanisha kwa sababu tu alisimama kinyume na maslahi ya mkubwa fulani. Nguvu za dola zilitumika. Lakini hatimaye CCM ikatambua kwamba haiwezi kuzimisha nguvu ya uandishi kwa kutumia nguvu ya dola, nasikia walichokifanya ni kuwaita baadhi ya Wahariri, Wakuu wa magazeti na kuwalambisha "hongo ya mamilioni" ili magazeti yao yaandike kile ambacho dola inataka. Na kweli yapo magazeti ambayo yamebadili misimamo ghafla na kuanza kuuponda upinzani wowote dhidi ya CCM kwa namna ambayo haijakuwako siku za kale za magazeti hayo. Yupo mwandishi mmoja ambaye nasikia alikataa hongo hiyo na baadaye gazeti lake likasakamwa kwa kufunguliwa mashitaka mengi tu na yeye mwenyewe kuwekwa rumande kwa makosa ya jinai lakini makosa yakubuni kwa muda mrefu na sasa gazeti hilo limekufa. Mambo haya ya kulambishana hongo yalifanyika katika kipindi ambacho Wizara inayoshughulikia magazeti ilikuwa chini ya "kingunge" maarufu wa CCM. Mara upinzani wa magazeti ulipopoozeshwa, ukaibuka upinzani wa Waislamu wanaoisema wazi wazi serikali ya CCM na maovu yake, ni wakati huo huo ndipo mapambanao makali yakaibuka kati ya Polisi na Waislamu, wakati mwingine Mahakama nazo zikajihusisha kwa kutoa maamuzi ya ajabu ajabu kama vile ya kuwanyima washitakiwa dhamana hata pale walipostahili. Naam magereza yakatumika kama kiboko cha CCM dhidi ya upinzani lakini hilo likawa si suluhisho, kwani haukupita muda chama cha wananchi (CUF) kilipojipanga vizuri na kuimarisha uongozi wake hadi kuufufua tena upinzani wa kisiasa ambao CCM ilidhani imeua kwa kutumia mamluki wao iliowapandikiza ndani ya chama cha NCCR-Mageuzi. Upinzani wa kisiasa safari hii ukaibukia kwenye chama cha CUF, wakajitahidi sana kuupaka matope kwa kukipa chama hiki dosari ya "udini" na "upemba" lakini wananchi wamepuuza, na kwahiyo CCM wameamua kuirudia silaha yao ya asili yaani mapolisi, mahakama, na magereza. Sasa mapambano ni kati ya Mapolisi na CUF. Kila mara Polisi wanapoanzisha fujo matukio yanayoonyeshwa kama madhara ya fujo hizo ni yale tu yanayohusu Polisi kujeruhiwa lakini siyo yale ya maelfu ya wananchi walioumizwa ama kujeruhiwa na mapolisi. Wengi watakumbuka jinsi magazeti yaliyolambishwa asali ya "kingunge" yalivyokazana kumwonyesha Inspekta ukurasa wa mbele tena kwa wiki nzima kana kwamba ndiye majeruhi pekee, baya zaidi ni hicho kitendo cha wapiga debe wa CCM wengine wakijificha kwenye majoho ya Uaskofu wanapokazana kuunganisha matukio hayo na hicho wanachodia eti sera ya CUF ya jino kwa jino. Ukweli ni kwamba jino kwa jino ndiyo msimamo wa CUF siyo sera na utabaki hivyo hadi CCM itakapoanguka. CUF katika nchi hii yanaweza kuwa ya muda mrefu kuliko wengi wanavyodhania, ni sawa tu na mapambano kati ya Wazalendo na Polisi wa Makaburu yalivyochukuwa muda mrefu nchini Afrika Kusini. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wananchi wamekwisha amua kwamba "enough is enough!" liwalo na liwe lakini haki ni lazima ipatikane. Wananchi wamekwishaona na kufikia uamuzi kwamba dola ya sasa haina faida yoyote kwao. Dola inapobinafsishwa na kugeuka kuwa ipo kwa manufaa ya wachache, basi walio wengi hawatashindwa kuisambaratisha. CCM ina dola, na CUF ina wananchi sasa tuone nani zaidi? Wanaolaani msimamo wa jino kwa jino kabla ya yote wajiulize ni msimamo wa nani? Je ni wa chama cha CUF au ni msimamo wa wananchi? Fujo zilozotokea Zanzibar na sehemu nyingine za Tanzania bara Dares Salaam, Kigoma na Tabora, hasa kwenye mikutano ya CUF hazijafikia hata nusu ya fujo zilizotokea pale Mwembechai 1998, miaka miwili kabla ya "falsafa" ya jino kwa jino kuingia CUF, Je, hapo kilichokuwa kinatekelezwa ni nini hasa? Ukweli ni kwamba ni serikali ndiyo iliyoanzisha matumizi ya nguvu dhidi ya raia wasiokuwa na silaha na hivyo ikaamsha utamadauni wa wananchi kujihami na kupigania haki zao kufa na kupona. Chama Cha Mapinduzi ambacho kimsingi kilipaswa kudumu katika nia na madhumuni ya TANU yaani kiwasemee watu, kipiganie haki za wanyonge mara serikali "inapokengeuka" na kuanza kudhulumu haki za watu, kinyume chake CCM ndiyo kwanza inajigeuza kuwa "dude" lililo kinyume na wanyonge. Je ilitarajia nini? Kwamba wanyonge watadumu katika utulivu ule ule wa enzi za TANU wakati wanyonge hawa hawana wakili wa kuwatetea!! Ikumbukwe ya kwamba, Serikali kimsingi haina dini pia haina chama badala yake ina "ethics", kanuni, miongozo ya siku kwa siku, sheria za nchi, na katiba ya nchi. Katika utekelezaji wa miongozo ya siku kwa siku ndipo hutokea serikali kuteleza, kupotoka, na kufanya makosa yatokanayo na upungufu wa kibinaadamu (maana wanaoiendesha siyo malaika), sasa inapotokea hivyo hapo ndipo chama cha siasa kinapotakiwa kuchukuwa jukumu la kuwa upande wa wananchi ili kuhakikisha haki inatendekea. Ninaposema chama cha siasa kuchukua jukumu ninamaana chama chochote cha siasa kiwe chama tawalaau chama chaupinzani kutokana na ukweli kwamba chama cha siasa hakishiriki katika operesheni za kiserikali hata kama chama hicho ndicho kinachoshika serikali na kwahiyo siyo vibaya chama kupinga mambo ya serikali yake. Enzi za mfumo wa chama kimoja na hasa enzi za TANU, chama kiliweza kuketi kama chama na kujadili mambo ya serikali, ndiyo maana mauaji ya wachawi ya Shinyanga na Mwanza (1974-77) yalipingwa hadi kupelekeza Waziri wa Mambo ya Ndani wa enzi hizo Alhaji Ali Hassan Mwinyi kujiuzulu, na baadhi ya wahusika kufikishwa mahakamani. Kwajili hiyo hata sakata la Mwembechai laiti kama CCM ingefuata nyayo za TANU ikasimama upande wa wananchi na kupinga mauaji yale, basi watu wasingekuwa na uchungu kama walio nao sasa. Lakini kinyume chake chama tawala na Serikali vimefanywa kitu kimoja, kumbe raia akionelewa na serikali iliyoko madarakani aende wapi kuitafuta haki yake? Je aende mbinguni kwa Mungu? Au akae akilia tu kama yatima? Hapo ndipo watu hufikia hatua ya kusema "yaliyotukuta yametosha enough is enough liwalo sasa na liwe; lakini haki tunaitaka. Walifikia uamuzi wa namna hiyo walalahoi wa Afrika Kusini na wakafanikiwa kuondosha utawala wa Makaburu uliodumu kwa miaka zaidi ya mia tatu. Walifikia uamuzi wa namna hiyo Walalahoi wa Angola, Zimbabwe na Namibia, katika nchi hizi zote dini ya Kikristo ilikuwa na nguvu sana, na watawala pamoja na mawakala wao, walitumia sana maandiko ya Biblia kama hayo ya kudai ":akupigaye shavu la kushoto mgeuzie na shavu la kuume." Lakini wasia wa maandiko hayakufaulu kuuokoa "ubeberu wa watawala" kwa sababu tangu mwanzo YESU hakumaanisha hivyo wala hakuja duniani kuhalalisha udhalimu wa watawala bali alikuja "kuokoa" na kwahiyo YESU atabakia kuwa YESU mwokozi na utakatifu wake, na watawala nao watabakia watawala waonezi na udhalimu wao, hakuna udugu kati ya YESU na wakandamizaji wala uhusiano uwao wote hadi mtu aliyeitwa kuzitangaza fadhili za Bwana kama vile Askofu, mchungaji mwinjilisti au nabii kugeuka kuwa mpiga debe wa serikali au mtetezi wa utawala dhalimu. Afanyaye hivyo anapoteza muda wake, kwani mwisho wa mambo yote dola ya kidhalimu ni lazima itaanguka wala hatakuwepo yeyote wa kuinusuru iwe kwa sala na maombezi, au kwa dua, uganga na matambiko. Wala CCM isijidanganye kwamba kuigeuza Tanzania kuwa dola ya kipolisi kutaisaidia la hasa! Kwasababu mapolisi jumla yao wako 60,000 kwa nchi nzima hivyo upinzani ukishawishi walalahoi milionni moja tu kati ya wananchi milioni 30, basi polisi ndio watakaokwenda na maji. Wala serikali haina magereza ya kufunga watu 1,000,000. Kwahiyo isithubutu kuendelea kupambana na upinzani kwa "gia" hiyo ya Polisi na magereza. Zaidi ya yote ikumbuke ya kwamba baada ya 'redundance" askari wengi sana wako vijiweni, wanataaluma wengi na wenye uzooefu wako vijiweni, hawa wako upande wetu wa wapinzani na mwisho kuna jeshi la vijana wasio na kazi, wasio na maliwala wasio na chochote cha kupoteza endapo wataamriwa kuingia kwenye mapambano ya ana kwa ana na dola ya kionezi. CUF ina nguvu za wananchi na CCM ina nguvu za dola sasa iendelee na tabia yake ya kutangaza vita dhidi ya upinzani na mwisho tuone nani ataibuka mshindi. Wiki ijayo "CCM, Mene mene tekeli na peresi".
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Wananchi washutumu vyombo vya habari Lipumba awaambia wananchi wasibabaishwe na walioko madarakani Wasomi SUA walaani ‘rushwa’ ya kisiasa Polisi kataeni kutumiwa - Lipumba Maelfu ya tani za matunda yanaoza Tanga Habari za ndani
MPASHO NASAHA
HABARI
Ushauri Nasaha
Makala
MAKALA
MAKALA
Kalamu ya Mwandish
MAKALA
RIWAYA
Lishe
|
|
|
|
|