|
Na. 047 Jumatano Mei 10 - 16, 2000 |
|
|
|
|
IMEELEZWA kwamba hali iliyojitokeza hivi sasa katika baadhi ya vyombo vya habari nchini kuhusu nani atagombea urais wa Tanzania na Zanzibar kwa tikiti ya CCM ni mbinu ya kutaka kupotosha demokrasia nchini. Hayo yameelezwa na wananchi mbali mbali waliozungumza na NASAHA kwa nyakati tofauti. Wananchi hao wakizungumzia hali hiyo iliyojitokeza ambapo baadhi ya vyombo vya habari vinataja majina na kuendesha kura ya maoni kwa wanaotarajiwa kugombea urais hasusan Zanzibar, ni sawa na kupotosha demokrasia ya uchaguzi wa vyama vingi. "Tanzania kuna vyama vingi vya siasa, haieleweki ni kwa nini vyombo hivyo vya habari havitoi fursa kama hiyo kwa vyama vingine zaidi ya CCM?" alihoji mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Makame kutoka Zanzibar. Kuhusu nafasi ya mgombea urais wa Tanzania, fursa inatolewa na vyombo vya habari kwa Chama cha Mapinduzi tu, ambapo imeelezwa hatua ya Rais Mkapa ya kuchukua fomu na kuzungumzia malumbano ya kuweka wigo au la kwa wengine wanaotaka kujitokeza kuchukua fomu kutoka katika chama hicho. Lakini uzito kama huo hautolewi kwa vyama vya upinzani na wale wanaotarajiwa kugombea kwa kupitia vyama hivyo. Wakati huo huo, Mwenyekiti wa UDP, Bw. John Cheyo, amesema tukitazama hali ilivyokuwa katika miaka karibu mitano ya Serikali ya Awamu ya Tatu, ambapo misiba imekuwa mingi, kama vile ajali, ukame, njaa na mafuriko, kwa mila za Kisukuma ingetosha kwa chifu kujiuzulu. Bw. Cheyo anashangaa kwa nini viongozi wengine hawaigi mfano kama huo. Mheshimiwa Cheyo aliyasema hayo katika ukumbi wa Maelezo, jijini alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, hivi karibuni. Naye mwenyekiti wa TLP, Bw. Agustino Mrema akizungumza katika viwanja vya shule ya Msingi ya Ukombozi, Manzese, jijini, mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema anashangazwa na hatua ya Rais Mkapa ya kuchukua fomu za kugombea Urais, na kudai kuwa anataka kumalizia kazi yake iliyobaki. "Jamani kuna kazi ipi ambayo anataka kumalizia? Na kama ipo basi ni kutufanya tuwe maskini zaidi,.....tangu atawale hali zenu zinazidi kuwa mbaya, sasa anataka ziwe mbaya kiasi gani", alishangaa, Bwana Mrema. Aidha, Mwenyekiti wa TLP, Bw. Mrema amezungumzia umuhimu wa wapinzani kuweka mgombea mmoja na namna ya kumpata. Bw. Mrema alipendekeza kigezo cha kumpata mgombea huyo wa upinzani. Kigezo kilichopendekezwa na kiongozi huyo wa kitaifa wa TLP ni kumtazama kiongozi wa upinzani aliyepata kura nyingi katika uchaguzi wa 1995. Kwa kigezo hicho Bw. Mrema alisema yeye ndiyo anayestahili kuwa mgombea kwa kambi ya upinzani katika Uchaguzi wa Oktoba 29,mwaka huu. Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamesema hoja ya Mhe. Mrema ina lengo la kumpigia debe Mkapa, kama mgombea wa CCM. Wananchi hao walioongea na mwandishi wa habari hii, walisema kama kigezo ni kura nyingi, basi nafasi hiyo angeachiwa Bw. Mkapa. Wananchi hao walizidi kusema kuwa mazingira ya 1995 ni tofauti kabisa na 2000, na kwamba hivi sasa tunahitaji Rais msomi. "Hivi sasa tumeingia katika karne ya 21 ya sayansi na teknolojia, hivi wenzetu duniani watatuelewa kweli,tukiwa na Rais mwenye elimu ya darasa la 8?" aliuliza mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mzee Dilunga wa Manzese. Wananchi hao pia walishangazwa na kauli ya Askofu Methodius Kilaini, ambaye ni msaidizi wa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, kusema kwamba wapinzani hawana nafasi ya kuingia Ikulu. Wananchi hao wamedai kuwa kauli hiyo ni sawa na kujipendekeza na kuipigia debe CCM. "Juzi juzi hapa Maaskofu hawa wa Kikatoliki kupitia
tume yao walitoa kitabu kilichoeleza kuwa viongozi walioko madarakani hawafai,
leo tena wanawaponda wapinzani", alisema mwananchi mmoja aliyekataa kuandikwa
jina lake gazetini.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Wananchi washutumu vyombo vya habari Lipumba awaambia wananchi wasibabaishwe na walioko madarakani Wasomi SUA walaani ‘rushwa’ ya kisiasa Polisi kataeni kutumiwa - Lipumba Maelfu ya tani za matunda yanaoza Tanga Habari za ndani
MPASHO NASAHA
HABARI
Ushauri Nasaha
Makala
MAKALA
MAKALA
Kalamu ya Mwandish
MAKALA
RIWAYA
Lishe
|
|
|
|
|