NASAHA
Na. 043 Jumatano Aprili 12- 18, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Riwaya

Kisasi cha mauti - 3 

MTUNZI: Juma S. Katanga (Jushaka)

"LAZIMA afe! Lazima afe!" Komandoo Mlasi Kasanura Bamba alirudia tena kujiapiza. Damu ilikuwa imetapakaa sakafuni chumba kizima. Maiti kumi zisizo na vichwa zilikuwa mbele ya macho yake na nyingine zilikuwa zimetapakaa hovyo nje. Grand Kapakacha alikuwa bado kajificha nyuma ya mlango bunduki mkononi ,jambia kiunoni. Ni operesheni kabambe kweli kweli. Je, mambo haya yakoje? Ungana na mwandishi katika riwaya hii ya kusisimua.
 

BAADA ya kusikia ishara za sauti ya upande wa pili wa simu Bwana Ziro aliridhika kwamba huyo kweli alikuwa ni Grand K. 

"Sasa Bwana Ziro fanya upesi sana uje hapa kwa Somji kuna ishu nyeti nnakuhitaji, OK, Paka mweusi!", alimaliza Grand K. katika simu. "Ok Nnakuja, Paka mwanga", alijibu Bwana Ziro na kukata simu. 

Muda mfupi tu baada ya kumaliza kuongea katika simu mara Somji na Grand K. waliona mlango ukifunguliwa pale sebuleni na mara Bwana Ziro akaingia. Somji na Grand K. waliinuka wote wawili na kumkumbatia Bwana Ziro kwa furaha kweli kweli. "Paka mweusi hakosi nyama... Paka mweusi hakosi nyama !", Bwana Ziro alirudiarudia kusema maneno hayo huku amemkumbatia Grand K. 

Baada ya kusalimiana na kukumbatiana wote watatu waliketi na kuanza rasmi mazungumzo yao. Walijadiliana sana kwa muda mrefu na inaonekana kwamba walifikia muafaka juu ya jambo fulani hivi kwani walipeana mikono na ishara za kukubaliana na mara Somji aliingia chumbani na kutoka na briefcase nyeusi. Briefcase hiyo ilikuwa imejaa fedha taslim. Somji aliifungua na kumwaga mabulungutu ya pesa mezani na wote watatu wakaanza kuhesabu kwa pamoja."Elfu saba...elfu kumi...laki saba...Milioni moja...Milioni kumi..." hadi wakafika mwisho. Walipomaliza kuhesabu walizirudisha zile fedha ndani ya ile briefcase na Somji akawakabidhi hiyo briefcase kisha wakapeana mikono na kuagana. 

Grand K. na Bwana Ziro kila mmoja alikuwa amekuja na gari lake hivyo wakaamua kwamba wote wawili waondoke pamoja kwa gari la mmojawapo. Wakaafikiana kwamba watumie gari la Bwana Ziro. Hivyo Grand K. alimfuata dereva wake na kumruhusu arudi nyumbani wao wana safari nyingine. Kutokana na uchovu wa kusubiri kwa muda mrefu pale nje kwa Somji, yule dereva wa Grand K. alipitiwa na usingizi akalala fofofo juu ya usukani kama alivyofanya yule dereva mwenzake aliyezimia asubuhi baada ya kupigwa na Grand K. Basi Grand K alipomkuta huyu nae kalala hasira zilimpanda ghafla na kabla hajafungua mlango wa gari ili kumtandika vibao vya moto alisita na kukumbuka kile kilichotokea nyumbani kwake asubuhi. Maana mpaka dakika hiyo alikuwa hajui kama yule dereva aliyemuacha kazimia nyumbani kwake amepona kifo au la. Hivyo kuzusha songombingo lingine pale ingekuwa balaa lingine, halafu mbele ya marafiki zake na tena ni ugenini. Kwa hiyo akaamua kumezea tu na kumaliza hasira zake kimoyomoyo. 

Basi Grand K. na Bwana Ziro waliingia katika hiyo Land Cruiser ya Bwana Ziro wakaondoka na ile Briefcase huku Somji akiwapungia mkono wa kwaheri. 

"Leo ni siku njema sana. Lazima tukatumbue kishenzi Sheraton au sio Paka mwanga!" alitamba Grand K. akimwambia Bwana Ziro. "Ah! Mie si unanijua mwenyewe Paka mweusi? We kaanga mbuyu tu ,mie meno ninayo!" alijibu Bwana Ziro huku akinyonga sukani ya gari na kuingiza gia moja baada ya nyingine. 

Sasa walikuwa njiani wakichoma mafuta kuelekea nyumbani kwa Grand K. kabla hawajenda huko Sheratoni kutanua na fedha za mauzo ya nyumba ya urithi ya Marehemu Kasanura Bamba, kaka yake Grand K. 

***************** 

BABA yao mzazi kina Grand K ,Mzee Bamba, alikuwa ni tajiri mkubwa sana katika jiji hili la Darisalama. Hakuna mtu asiyemjua mzee Bamba kwa utajiri wake. Alikuwa ni mzee mashuhuri kwelikweli. Alikuwa na makampuni mengi ya biashara, viwanda, magari na miradi mingine chungu mzima ambayo yote ilimwingizia fedha nyingi na kumfanya awe "kibopa" na miongoni mwa watu wanaogopwa na kuheshimiwa sana katika mtaa wake kule Msasani. 

Kati ya wanawe hao wawili,yaani Kapakacha au Grand K na Kasanura, Mzee Bamba alimpenda sana huyo mkubwa, Kasanura. Kapakacha yeye alikuwa ni mtoto asiyependwa na baba yake tangu angali mdogo kutokana na vitendo vyake viovu na vya kihuni ikiwemo kuvuta bangi na madawa ya kulevya. Mzee Bamba alipiga kelele we kila siku kumkanya lakini wapi alishindwa na kuamua kumuacha aje afunzwe na Ulimwengu. Kasanura yeye kwa upande wake alishirikiana bega kwa bega na baba yake na kumsaidia katika kusimamia na kuendesha miradi yake. Hivyo maelewano kati ya Grand K. na baba yake mzazi yalikuwa ni madogo sana. 

Siku moja katika zamani hizo, Grand K. alimtaka kaka yake Kasanura amwombee pesa za mtaji kwa baba yao ili aweze kufanya biashara zake mwenyewe. Kasanura kwa sababu ya kumpenda mdogo wake kitinda mimba huyo hakupinga bali alienda moja kwa moja kwa baba yao na kumwambia kuhusu ombi la mdogowe. 

Mzee Bamba alikataa katakata. "Sikiliza Kasanura, mimi siko tayari kabisa kupoteza fedha zangu kumpa mvuta unga, habithi wa amali! Siko tayari!", alisisitiza Mzee Bamba. Lakini pamoja na jibu hilo kali alilolitoa Mzee Bamba Kasanura kwa mapenzi aliyokuwa nayo kwa mdogo wake, hakukata tamaa bali alizidi kumsihi baba yake hata mwisho Mzee Bamba akakubali. Mzee Bamba akampatia mwanawe huyo kitinda mimba Grand K. pesa taslim shilingi milioni kumi ili afungue miradi yake mwenyewe. Basi Grand K akaanza biashara kati ya Italy na Tanzania. Lakini ajabu ni kwamba kila alivyozidi kwenda Italy ndivyo pesa zilivyozidi kumwishia na mwishowe akafilisika kabisa. Ukweli ukaja kujulikana kwamba Grand K. alikuwa akienda Italy si kwa ajili ya biashara bali kufanya starehe na wanawake na kuvuta unga na marafiki aliowapata huko Italy. 

Ikawa kila anapokwenda safarini huko Italy anaambatana na wanawake tofauti tofauti wa kila aina. Mwenyewe akawa anatamba kwamba anatesa na dunia! Basi baada ya kufilisika Grand K. akarudia katika hali yake ya mwanzo bali sasa alizidisha kuvuta bangi na madawa ya kulevya. 

Akawa "teja" kamili haswa! Na katika kuzidi ufirauni wake hapo mtaani akamchukua msichana mmoja changudoa aitwae Joyce akawa hawara wake. Mwenzake Kasanura yeye alimposa binti mmoja mtulivu aitwae Maisara na baadae akafunga ndoa kwa harusi kubwa kweli kweli ambayo haijawahi kutokea kwenye jiji hili la Darisalama kwa miaka hiyo. Ilikuwa ni harusi kubwa ya kifahari ya kukata na shoka kweli kweli. Baada ya ndoa hiyo Kasanura na mkewe Maisara walibahatika kupata watoto wawili, wote wa kiume. Wa kwanza walimuita Njarika ,na wa pili walimpa jina la Mlasi. Baadae Maisara alijifungua tena mtoto mwingine wa tatu lakini ikawa bahati mbaya akafariki. Hivyo wakabaki na watoto hao hao wawili, wajukuu wa Mzee Bamba. Nao ni Njarika bin Kasanura Bamba na kitinda mimba Mlasi bin Kasanura Bamba. 

Huku nyuma, uhusiano kati ya Grand K. na Changudoa Joyce ukazidi kupamba moto huku kila mmoja akibadilisha wapenzi kila siku utafikiri nguo. Ukiachilia mbali Changudoa Joyce, pia alikuwa na wanawake wengine chungu mzima. Joyce nae akasema hapana,na yeye hawezi kubaki nyuma! Yeye ndio usiseme, uhuni alioupata katika kazi ya uchangudoa kule barabara ya Kinondoni na mtaa wa Ohio ulimfanya awe na wanaume lukuki mbali na Grand K. Hivyo ikawa kana kwamba wanashindana vile. Balaa lilioje, ikafikia Joyce akatembea na rafiki wa kaka yake Grand K., Kasanura , aitwae George Fataki. George Fatak alikuwa ni rafiki mkubwa sana wa Kasanura. Hivyo mara kwa mara alikuwa akifika hapo nyumbani kwa Mzee Bamba kuja kumtembelea Kasanura. 

Basi Joyce na George Fataki wakawa vipenzi wakubwa kwelikweli. Hatimaye siku ya siku ikafika. Za mwizi arobaini! Habari zikamfikia Grand K. kwamba Joyce ana uhusiano wa karibu na George Fataki. Grand K. kupata taarifa hiyo, mwiliwote ulikufa ganzi, meno yakamzizima na taswira za madimbwi ya damu zikawa zinampitia mbele ya macho yake. "George Fataki amechokoza moto, sasa atakiona cha mtema kuni. Lazima aiage hii dunia kabla jua halijazama!" Grand K. alijiapiza kwa uchungu huku akichomeka jambia refu ndani ya suruali yake. Hiyo ilikuwa yapata saa kumi na moja jioni. Kabla hajamaliza kuchomeka sawa sawa jambia hilo, mara akamwona George Fataki akija taratibu kuelekea hapo nyumbani kwao. 

Mambo sasa ndio yanapamba moto. Je itakuwaje ndugu msomaji ? Usikose toleo lijalo.
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Wanaokemea dhuluma wasinyanyaswe

Waislamu waapa kuinyima kura CCM

Mkapa ahutubia Taifa: 
Ugumu wa maisha kuendelea

Wananchi wamuunga mkono Askofu Kakobe

MPASHO NASAHA
WAKIAMUA, HATA WAKICHAFUKA WATANAWA!!!

SHERIA
Faida ya kuwepo kwa sheria za haki kunategemea na wanaozisimamia

Ushauri Nasaha
Namna ya kumfanya mtoto wako aweze kuzungumza

MAKALA
Sababu ‘1000’ kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani - 2

WAZO  LA  WIKI
Polisi acheni ubalakala

MAKALA
Kuporomoka kwa maadili  katika jamii yetu; Sababu na utatuzi wake - 2

Kalamu ya Mwandishi
Tatizo si jino kwa jino, bali utekelezaji muafaka!

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (6)
Vijana mjiandikishe kwa wingi na siku ya uchaguzi mjitokeze

Makala ya Mtangazaji
LEO NI SIKU YA ASHURA

Habari za Kimataifa

Riwaya
Kisasi cha mauti -3

Lishe
Ni kwa jinsi gani wanawake wanapata utapiamlo

MASHAIRI

MICHEZO

  • Madadi, Jamhuri acheni ‘rusha roho’ katika soka – Wapenzi
  • Yanga wakumbwa na kiwewe
  • Mapunda asema hana bahati ya kutia mabao

  • •••Golikipa Majimaji alia na mabeki
     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita