|
Na. 043 Jumatano Aprili 12- 18, 2000 |
|
|
|
|
|
Ugumu wa maisha kuendelea
RAIS Benjamin Mkapa juzi Aprili 10, alilihutubia taifa ambapo alitangaza kuwa Tanzania itaanza kunufaika na mpango wa kusamehewa madeni, mpango ambao matunda yake yataanza kuonekana miezi 18 baada ya kuanza kutekelezwa msamaha huo. Rais Mkapa aliyasema hayo wakati akitangaza hatua ya Tanzania kusamehewa madeni ya thamani ya dola za Marekani bilioni 2 mashirika ya fedha ya kimataifa na baadhi ya nchi za nje. Hata hivyo Mhe. Rais hakutaja ni lini mpango huo wa msamaha wa madeni utaanza kutekelezwa jambo ambalo linaashiria kuendelea kwa hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi. Mhe. Rais aliendelea kueleza kuwa kiasi hicho cha msamaha ni sawa na nusu ya madeni ambayo nchi hii imekuwa ikidaiwa. Alifafanua kuwa msamaha huo umetolewa kufuatia Tanzania kutekeleza kikamilifu masharti ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Dunia(IMF), ikiwemo kukusanya kodi kwa wingi. Mhe. Rais alisema kuwa kwa msamaha huu nchi itafaidika kutumia kiasi cha shilingi bilioni 80 (dola za Marekani milioni 100)kila mwaka katika kuboreshwa huduma za jamii, pesa ambazo zingetumika kulipa madeni. Hata hivyo alieleza kwamba manufaa hayo ya msamaha wa madeni yatategemea kutekelezwa kwa masharti kadhaa, yakiwemo kukuza demokrasia na kuendelea kusanya kodi kwa wingi. Katika hotuba hiyo Rais Mkapa pia alieleza kuwa serikali itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake ili kuwe na uchaguzi huru na wa haki na akawaonya wale ambao wameanza kudai damu itamwagika na waliotangaza sera za jino kwa jino. Vyombo vingi vya habari vimeonyesha tafsiri ya kuwa onyo hilo la Rais limeelekezwa kwa Chama cha Wananchi (CUF). Wakati huo huo, Kiongozi wa upinzani Bungeni ambaye pia ni Waziri Mkuu kivuli Bi. Fatma Maghimbi amesema kwamba ameshangazwa na kauli hiyo ya Rais ya kuelekeza onyo kwenye chama chake (CUF). Akizungumza na Shirika la Habari la Utangazaji la BBC jana jioni alisema kuwa awali aliposikia kuwa Rais angehutubia Taifa alitegemea kuwa Rais angezungumzia na kuonesha kuguswa na kitendo cha Polisi kuwapiga raia hovyo huko Zanzibar hivi sasa. Alisema kwamba amesikitishwa kuona Mhe. Rais akielekeza lawama kwenye chama chake cha CUF. Alieleza kuwa katika vurugu hizi za polisi wamewashauri wanachama wa CUF kutonyanyua mkono kujibu mashambulizi hayo ya polisi,na kwamba ikiwezekana wakimbie tu. Akizungumzia shutuma za "jino kwa jino" Bi. Fatma Maghimbi alieleza kwamba wao walitangaza kuwa mwaka 1995 Chama cha CUF kilidhulumiwa. Hivyo waliazimia kwamba mwaka huu hawatakubali kudhulumiwa tena na kwamba endapo wataonewa itakuwa "jino kwa jino". Akifafanua usemi huo Mhe. Maghimbi alisema, "...ukianza kuning'oa jino langu nami nitakung'oa lako... na hiyo ni wakati wa uchaguzi mkuu." Alishangaa kuwa kauli hiyo inapewa tafsiri potofu wakati iko wazi katika Kiswahili kilicho fasaha. |
YALIYOMO
Tahariri
Waislamu waapa kuinyima kura CCM Mkapa
ahutubia Taifa:
Wananchi wamuunga mkono Askofu Kakobe MPASHO NASAHA
SHERIA
Ushauri Nasaha
MAKALA
WAZO LA WIKI
MAKALA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Makala ya Mtangazaji
Riwaya
Lishe
•••Golikipa Majimaji alia na mabeki |
|
|
|
|