|
Na. 043 Jumatano Aprili 12- 18, 2000 |
|
|
|
|
|
Polisi acheni ubalakala NA RAJAB NKAWA NI FARAJA ilioje kwangu kukutana tena nanyi wasomaji wapendwa wa safu hii kwa minajili ya kutafakari yale yanayojiri hivi sasa katika nchi yetu,ambayo kama tusipokuwa makini tutashuhudia nchi yetu iliyotulivu na yenye amani ikilazimishwa kwa nguvu kuingia katika maangamizi ya kumwaga damu. Leo wasomaji wapendwa tunaangalia na kutafakari na hatimaye kuukemea uovu unaofanywa na polisi wa serikali ya CCM dhdi ya raia wasiokuwa na hatia, ambao kosa lao ni kule kuwa kwao kinyume na itikadi ya kisiasa ya watawala. Jeshi la polisi linasheria zake ambazo pia zinatambua kuweko kwa haki za binadamu. Na kwa kuwa nchi yetu ni mwanachama wa Jumiuiya mbalimbali za kimataifa, ambazo kwenye mikataba yao kuna kipengele cha kulinda na kuthamini haki hizo, basi ni matarajio yetu kuwa hapawezekani kuwapo na chombo chochote kile ndani yaserikali ya nchi hii ambacho kitakuwa na uwezo wa kuvunja haki hizo pasi na amri na maelekezo ya watawala. Yale yanayofanywa na polisi hivi sasa huko kwenye visiwa vya marashi ya karafuu, ya kamata kamata, pigapiga na umizaumiza tena kwa risasi za moto raia kwa kule tu kuwa kwao upande wa chama cha CUF ni hatari kwa amani yetu. Tunapenda polisi wawe na ufahamu wa kuwa wapo hapo kwa mujibu wa katiba ya nchi ambayo inabainisha kazi yao kuwa ni ulinzi wa raia na mali zao. Sio yale wanayoyafanya sasa ya kutumikia watu walionufaishwa na mfumo uliopo ambao umewanyima wananchi walio wengi wakiwemo hao polisi wenyewe,hata ule uwezo tu wa kujikimu kimaisha. Fahamuni kuwa wale waliopo kwenye vyama vya upinzani wawe ni viongi, wanachama au wapenzi ni raia sawa na raia wengine, ni sawa na viongozi wa CCM, wanachama na wapenzi wake. Hakuna aliyebora kati yao mbele ya sheria au mbele yenu ninyi polisi. Na kwa kuwa upepo wa demokrasia umekwisha anza kuvuma kwa kishindo hivi sasa basi fahamuni kuwa CCM itaondoka kama zilivyoondoka tawala nyingine zilizo jichimbia kwa zaidi ya miaka 40, zaidi ya muda ambao CCM imejichimbia hapa nchini kwetu. Na muda huo ukifika basi mtafute pa kukimbilia kwani historia lazima iwahukumu kutokana na unyama wenu. Polisi fahamuni kuwa hivi sasa tupo katika vita vya kitabaka baina ya wale walionufaishwa na mfumo uliopo na wale walioumizwa na mfumo huu. Ni vita kati ya wadhulumu na wadhulumiwa. Na kwa kuwa hawana hoja zenye mashiko juu ya madhila wayapatayo wananchi, basi ninyi polisi kama chombo cha dola mnatumika kuwakandamiza wananchi wenzenu ilhali hapana tofauti kati ya ninyi na sisi. Hivi nyumba mnazoishi nyinyi polisi na mabanda ya kuku ya Interchick kipi kina hadhi? Nyumba mnazoishi ni vichekesho vitupu. Hazifai si tu kwa makazi ya binadamu bali hata ukitaka kufuga kuku itabidi uzifanyie marekebisho maana waweza kuua kuku wote kwa joto hasa kuku wenyewe wakiwa ni 'broiler'. Mishahara yenu ndiyo hiyo hiyo ya kawaida,labda mnatushinda kwa kuwa mnapanda mabasi ya daladala bure! Tumieni akili acheni ubalakala. Mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi ni kwa ajili yetu sisi sote na ninyi mkiwemo. Hebu fikirieni mnapomlenga mwananchi mwenzenu na hatimaye kuachjia 'triger' huku ukishuhudia kutapatapa kwa raia huyo wakati roho yake ikitoka; mnajisikiaje? Kwa kweli ni lazima tuwafikisheni mbele ya vyombo huru vya sheria ili mjibu dhambi hizi mnazotufanyia. Jueni kuwa hivi sasa dunia imeshikamana dhidi ya uovu, na popote utapokimbilia utarudishwa nchini kwako ili upambane na haki katika mahakama huru. Kwa wale wasio na uwezo hata wa kukimbia ndio na washangaa zidi. Kwa upande wa wananchi wale mliojitoa kuhakikisha kuwa nchi inaingia kwenye mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi kwa manufaa yetu na hata wale wenye kutupinga, fahamuni kuwa haya yanayofanywa dhidi yenu ndio machungu katika kutafuta haki. Kumbukeni kuwa daima haki haitolewi kama keki kwenye kisahani, bali hupiganiwa. Hatuna njia rahisi na ya mkato isipokuwa ikibidi kupoteza nguvu zetu, viungo vyetu na hata uhai wetu. Lakini lazima haki isimame na pasiwepo mtu kunyanyaswa kwa rangi yake, dini yake, kabila lake au kwa njia yoyote ile nyingine. Hakikisheni haki sawa kwa wote inasimama na kamwe basiwepo tena misamiati kama kile chama cha Waislamu au kile chama cha Wapemba, tunataka vyama vyote viitwe vyama vya siasa sawa na vile iitwavyo CCM, TLP au TPP, pamoja na ukweli kuwa miongoni mwa vyama hivyo upo mlundikano wa viongozi wa ama dini moja au kabila moja. Kwa upande wa serikali tunapenda kukufahamisheni kuwa si vyema kufumbia macho mambo ya aibu yanayofanywa na jeshi la polisi hivi sasa hasa kule upande wa Zanzibar, ukizingatia kuwa chanzo cha vurugu ni polisi kuingilia mkutano wa ndani wa CUF na kufuatiwa na amri ya kamanda mkuu wa polisi aliyepata u-alhaji hivi karibuni Mhe. Mahita, kutaka polisi wafanye hayo wanayoyafanya. Na inasemekana kuwa hayo yote yanabaraka toka kwa rais wa Jamhuri na rais wa Zanzibar, kwani kamada Mahita aliongea nao kabla ya kuzungumza na polisi. Tunapenda kukufahamisheni kuwa machafuko yakitokea Zanzibar ndiyo yametokea Tanzania, damu ikimwagika Zanzibar ndiyo imemwagika Tanzania na vita vya ndani vikianza Zanzibar ndiyo vimeanza Tanzania. Sina hakika kama kutakuwako mmnufaikaji wa jambo hilo. Panapo majaaliwa tukutane
wiki ijayo.
|
YALIYOMO
Tahariri
Waislamu waapa kuinyima kura CCM Mkapa
ahutubia Taifa:
Wananchi wamuunga mkono Askofu Kakobe MPASHO NASAHA
SHERIA
Ushauri Nasaha
MAKALA
WAZO LA WIKI
MAKALA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Makala ya Mtangazaji
Riwaya
Lishe
•••Golikipa Majimaji alia na mabeki |
|
|
|
|