|
Na. 043 Jumatano Aprili 12- 18, 2000 |
|
|
|
|
|
Kuporomoka kwa maadili katika jamii yetu; Sababu na utatuzi wake - 2 Na H. Sulayman "Jihadharini na vikao vya kijiweni- ,Muhammad S.A.W. TULIONA katika toleo lililopita vipi mazoea ya kupenda kuiga kila kitokacho kwa Wazungu bila kukifanyia uchambuzi wa kina, inavyochangia kwa kiasi kikubwa kuharibu maadili yetu. Tabia nyingine inayochangia kuporomoka kwa maadili yetu, ni mazoea ya vijana wetu kuweka mabaraza katika vikao vijulikanavyo kama "kijiweni". Katika vikao hivyo hupigwa shule juu ya namna ya kutenda uhalifu na kuvunja maadili mema katika jamii. Mafaili ya watu mbali mbali hushushwa zikitajwa aibu zao na sifa kemkem kuwapa wavunjao maadili ya jamii kwa kisingizio cha uhuru wa mtu binafsi. Yote hayo huzungumzwa sio kwa lengo la kurekebisha tabia zao au ya muhalifu, isipokuwa ni kwa lengo la kuonesha ushujaa wa watu hao wanaopaswa kuigwa! Ushujaa gani huo! Pengine ushujaa wao ni wa kumuasi Mola wao mbele ya macho yake!! "Vijiwe" hivi hutumika pia kama vituo vya kusambazia bangi na madawa ya kulevya, na hivyo kuharibu akili na siha za vijana wengi na hatimae kupatikana jamii dhaifu, chovu na ya uvivu uliopindukia. Kwa hakika anayeangalia kasi ya kuporomoka maadili kwa vijana wetu, atabashiri kupatikana jamii ya kesho iliyo dhalili na dhaifu legelege katika kila upande; upande wa maendeleo ya jamii, kisiasa, kiuchumi na kimaadili sawia. Vile vile, "vijiwe" hivi, hutumiwa na wanachama wake kama vituo vya kupangilia harakati na sakanati za kufanya uhalifu kama vile wizi, ubakaji kunajisi n.k. Zile tabia za ajabu kutoka Ulaya kama ile ya watu "wa kaumu luti na mithili yao" kudai watambuliwe na katiba za nchi zao kama kundi lenye haki sawa ya mume na mke (wa jinsia moja), zimekuwa zikienezwa katika jamii yetu kupitia kwenye vikao vya kijiweni, kama lilivyoripiti gazeti moja la hapa nchini siku ya Ijumaa Aprili 7, 2000, habari za watu hao wa jinsia moja kwa picha na maelezo, likiashiria kushamiri kwa tabia hii. Haya yote na Ya mithili yake yanachangia sana katika kuharibu maadili yetu mazuri yaliyosisitizwa na dini zote na akili iliyosawia. Uislamu katika kutoa mwongozo wake kwa mwanadamu, umekata kabisa mizizi ya fitina kwa kukemea vikali vikao vya kijiweni, na pindi hapana budi kuwepo basi viwepo kwa masharti. Hebu na tumsikilize mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad S.A.W: "Jihadharini/Jiepusheni na vikao vya (kijiweni) karibu na njia wapitamo watu. (Maswahaba) wakasema: Hayo ni majlisi (vikalio) yetu ambayo hatuna budi nayo. Akasema (S.A.W.): Kama hapana budi ila makae katika majlisi yenu hayo, basi ipeni njia haki yake. (Maswahaba) wakasema: Ni zipi haki za njia ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu? Akasema S.A.W. (haki za njia) ni:- (1) kuinamisha chini macho (ikiwa ni ishara ya kutokodolea macho sehemu, au yale aliyoharamisha Mwenyezi Mungu kuyaona pasina haki). (2) Kujizuia na kusababisha maudhi ya aina yeyote kwa watu na vitu. (3) Kujibu salamu (za wapita njia) - kama ishara kuwa nyinyi ni watu wa amani. (4) Kuamrisha na kuusia mambo mema (yenye faida kwa jamii) (5) Kukataza maovu. Hadithi hii imepokelewa na kukuabalika kwa wapokezi wetu. Na hii huenda ikawa ni tafsiri ya kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema. "Vikao vyao vingi (watu walio wengi) havina faida wala kheri (kwa jamii) isipokuwa vile vyenye kuhimiza kutoa sadaka na kuamrisha kufanya mema au kufanya suluhu baina ya watu (waliogombana)...." Ewe kijana jihadhari na vikao vya kijiweni visivyo na faida kwako duniani na akhera. Kwanini usijadili na wenzako njia na sababu mbali mbali za kukupelekea kufaulu mitihani yako ya shule au ya maisha badala ya kumjadili fulani nyendo zake ili umuige! Nini msijadili mambo ya kimaendeleo kwa mtaa wenu na jamii yenu badala ya kujadili vimbwanga vya changudoa na stori za Maradona! Amka kijana wakati ndio huo. |
YALIYOMO
Tahariri
Waislamu waapa kuinyima kura CCM Mkapa
ahutubia Taifa:
Wananchi wamuunga mkono Askofu Kakobe MPASHO NASAHA
SHERIA
Ushauri Nasaha
MAKALA
WAZO LA WIKI
MAKALA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Makala ya Mtangazaji
Riwaya
Lishe
•••Golikipa Majimaji alia na mabeki |
|
|
|
|