NASAHA
Na. 043 Jumatano Aprili 12- 18, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
SHERIA

Faida ya kuwepo kwa sheria za haki kunategemea na wanaozisimamia 

MARA nyingi imekuwa ikisemwa na viongozi wa Serikali kuwa Tanzania ni nchi ya Kidemokrasia yenye utawala unaozingatia, haki, usawa na utawala wa sheria. Na ni mara nyingi zaidi pia tumekuwa tukisikia au kuona wananchi wakilalamikia utendaji wa vyombo vya Serikali kuwa unakiuka misingi ya sheria na haki za binadamu. Je Kwani sheria zinazolinda haki za raia hazipo? Na kama zipo tatizoni nini? MWANDISHI ABU MAUA anafafanua.

SEHEMU ya utangulizi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza wazi kabisa. Kuwa Tanzania ni nchi inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani, na kwamba Tanzania ni nchi yenye mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendele wowote na hivyo kuhakikisha kwamba haki zote za binadamu zinadumishwa na kulindwa na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu. 

Isitoshe kifungu cha 9 (f) cha Katiba hiyo hiyo kinaeleza kwamba heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata kanuni za Tangazo la dunia kuhusu Haki za Binadamu katika uendeshwaji wa shughuli za serikali. 

Tangazo hilo la Dunia yaani Universal Declaration On Human Rights lilikubaliwa na kutiwa saini na serikali mara tu baada ya uhuru 1961. 

Kwa mujibu wa Katiba kifungu 13(I) watu wote mbele ya sheria ni sawa na kwamba ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria. Kifungu cha 13(5) kinafafanua maana ya ubaguzi kuwa ni kutimiza haja, haki au mahitaji mengineyo kwa watu mbali mbali kwa kuzingatia pamoja na mambo mengine kabila, dini, maoni yao ya kisiasa n.k. 

Hapa ndipo mambo yanapoanza kustaajabisha kwa sababu kama Katiba ambayo ndiyo sheria Kuu ya nchi inazingatia na kulinda usawa,haki na undugu kwa kiasi hiki kwa nini basi kila siku tunaona na kusikia wananchi wanalalamika kuwa baadhi yao wanabaguliwa na kunyimwa haki zao za msingi kwa mujibu wa katiba? 

Kwa nini wapinzani hawaishi kula vipigo toka kwa mapolisi? Kwa nini watu wengine wakitofautiana kimawazo iwe kwenye dini zao hata kupelekea watu kutoana ngeu hawapelekwi FFU wala kuitwa wavunjifu wa amani na wanaotumiwa na mataifa ya nje?. Ila tofauti kama hizo zinapotokea kwa watu wengine hufanywa nitofauti kubwa hata kufyatulia watu risasi za moto? 

Watuhumiwa wa makosa ya jinai wanapofika polisi hupigwa vibaya kama nyoka aliyeingia chumbani wakati kifungu cha 13(6)(b) cha Katiba kinasema wazi kuwa ni marufuku kwa mtu aliyeshitakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo. Kama vile haitoshi Kifungu cha 13(6)(d) kinazuia heshima na utu wa mtu kuharibiwa katika shughuli zote zinazohusu upelelezi na uendeshwaji wa makosa ya jinai. Lakini utaona kila siku vijana wanaotuhumiwa na makosa yanayoitwa ya "uzururaji" hufungwa mashati na kuwekwa msururu barabarani kama msafara wa watumwa katika nchi yao huru! 

Kwa upande mwingine sheria ya vyama vya siasa (political parties Act, 1992) kama ilivyorekebishwa na Act, No. 32 ya 1994, Kifungu cha 11(3) inasema kuwa vyama vya siasa vinapohitaji kufanya mikutano ya hadhara au maandamano ya amani wanatakiwa kupeleka taarifa kituo cha polisi kilicho karibu na eneo. Sheria inasema wazi kuwa ni "kupeleka taarifa" na sio "kuomba kibali" kama ama ovyo polisi wanataka iwe. Baada ya kutoa taarifa chama kinaruhusiwa na sheria sio na polisi narudia tena chama kinaruhusiwa na sheria sio na polisi kuendelea na mkutano. 

Vurugu zilizotokea Zanzibar hivi karibuni kwenye ofisi za chama kikuu cha upinzani nchini CUF ni matokeo ya tafsiri mbaya ya sheria niliyoitaja hapo juu. Mkutano ule uliovamiwa na polisi kwa madai kuwa umefanyika bila "ruhusa" ya polisi haukuwa mkutano wa wazi (public meeting). Hivyo hata kama sheria ingetaka polisi watoe kibali cha mkutano, mkutano ule usingehitaji kibali" kwa kuwa ulikuwa ni mkutano wa ndani. 

Mikataba kadhaa ya kimataifa inayoridhia haki za Binadamu mfano, tamko la Dunia la Haki za Binadamu la 1948 (The Universal Declaration On Human Rights, 1948),Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa 1976 (U.N. International Covenant On Civil and Political Rights, 1976), na Mkataba wa Umoja wa Africa wa Haki za Binadamu wa 1981 (African Charter on Peoples and Human Rights, 1981) imetiwa saini na Serikali. Mikataba hii inatambua haki za raia kama uhuru wa kuabudu, kutoa mawazo na kujieleza, kuanzisha, kujiunga, na kushiriki katika siasa kwa usawa bila kujali dini ya mtu, kabila au sehemu anayotoka. 

Sasa ikiwa kama serikali imeridhia mikataba hii ya Haki za Binadamu hoja za Upemba, Uunguja, wahongwa wa kofia na kanzu zinatoka wapi? Hapana shaka sheria nyingi zilizopo ni nzuri tatizo ni hao wanaozisimamia. 

Sheria zote zinakataza ubaguzi lakini wapo watu wanaobaguliwa, katiba inalinda haki za Binadamu lakini haki hizo zimekuwa zikivunjwa kila kukicha. Sheria inatoa uhuru wa kuabudu na kutangaza imani lakini leo wapo watu kwa nafasi zao za kiserikali wanadharau vitabu vitakatifu vya dini za watu hata kudai kuwa vitabu hivyo si lolote si chochote na walioviandika wanapaswa kuburuzwa mahakamani. 

Kwa hiyo hata kama sheria zote zitakuwa ni nzuri kwa kiasi gani kama zinasimamiwa na viongozi wenye choyo na wakandamizaji sheria hizo hazitofua dafu. Ubaguzi, umaskini na mateso kwa raia itakuwa ndiyo sehemu ya maisha yetu ya kila siku! 

Wiki ijayo: Je ni haki mahakama kuahirisha kesi zaidi ya siku sitini bila ya kuanza kuisikiliza? Ujumbe:October 2000 tujiandae kupiga kura. 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Wanaokemea dhuluma wasinyanyaswe

Waislamu waapa kuinyima kura CCM

Mkapa ahutubia Taifa: 
Ugumu wa maisha kuendelea

Wananchi wamuunga mkono Askofu Kakobe

MPASHO NASAHA
WAKIAMUA, HATA WAKICHAFUKA WATANAWA!!!

SHERIA
Faida ya kuwepo kwa sheria za haki kunategemea na wanaozisimamia

Ushauri Nasaha
Namna ya kumfanya mtoto wako aweze kuzungumza

MAKALA
Sababu ‘1000’ kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani - 2

WAZO  LA  WIKI
Polisi acheni ubalakala

MAKALA
Kuporomoka kwa maadili  katika jamii yetu; Sababu na utatuzi wake - 2

Kalamu ya Mwandishi
Tatizo si jino kwa jino, bali utekelezaji muafaka!

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (6)
Vijana mjiandikishe kwa wingi na siku ya uchaguzi mjitokeze

Makala ya Mtangazaji
LEO NI SIKU YA ASHURA

Habari za Kimataifa

Riwaya
Kisasi cha mauti -3

Lishe
Ni kwa jinsi gani wanawake wanapata utapiamlo

MASHAIRI

MICHEZO

  • Madadi, Jamhuri acheni ‘rusha roho’ katika soka – Wapenzi
  • Yanga wakumbwa na kiwewe
  • Mapunda asema hana bahati ya kutia mabao

  • •••Golikipa Majimaji alia na mabeki
     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita