|
Na. 043 Jumatano Aprili 12- 18, 2000 |
|
|
|
|
|
Tatizo si jino kwa jino, bali utekelezaji muafaka! NA MAALIM BASSALEH HIVI sasa hali ya Zanzibar inatisha sana! Mfano wake ni kama iliyotegeshewa bomu la masaa; linalongojea wakati wake ufike liripuke! Kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa kulitegua bomu hilo, basi saa hiyo ikifika bomu litaripuka na maafa yake hayasemeki! Njia pekee itakayowezesha kurudisha utulivu na amani ni kuliondoa wingu la hofu na wasiwasi lililotanda hivi sasa, katika anga la visiwa hivyo. Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari watu katika kisiwa cha Unguja wanaishi katika hali ya hofu na wasiwasi. Kwa karibu wiki nzima sasa Polisi wamekuwa wakitembeza mkong'oto dhidiya wale wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa chama cha upinzani cha CUF. Baadhi ya watu wamejeruhiwa, wengine vibaya sana na wamelazwa hospitalini mahututi. Kuna wanaodai kuharibiwa mali zao au kuporwa kabisa. Na wapo wengine waliokamatwa na kuwekwa mahabusu. Watu wanajifungia ndani wanaogopa kutoka nje wakapambana na KOSOVO. Piga piga na kamata kamata hiyo kama Wazanzibari walivyoibatiza jina la KOSOVO! Lakini nini sababu ya hiyo KOSOVO? Sababu mbili kubwa ndizo zinazotolewa. Kuna wanaosema kuwa KOSOVO hiyo imechochewa na kauli ya JINO KWA JINO, iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha CUF, Maalim Seif Shariff Hamadi, katika mkutano wa hadhara huko Unguja. Na kundi la pili, ambalo linajumuisha idadi kubwa ya waandishi na vyombo vya habari, vya ndani na nje ya nchi, wanadhani KOSOVO hiyo ni ulipizaji kisasi wa Polisi dhidi ya wale wanaotuhumiwa kuwapiga Polisi na kuwanyang'anya silaha yao, pale Polisi walipokwenda kuhoji uhalali wa mkutano wa tawi moja la CUF uliokuwa ukihutubiwa na katibu Mkuu wa chama hicho. Hebu kwanza tuanze na ile kauli inayoambiwa ni ya uchochezi na inayoashiria umwagaji wa damu. Hapa imebidi niitafakari ile kauli maarufu ya Bwana Yesu inayosema,"Kabla ya kutaka kutoa kibanzi kilichomo katika jicho la mwenzako, toa boriti iliyomo katika jicho lako!" Haohao wanaomlaumu Katibu Mkuu wa CUF kwa kutangaza JINO KWA JINO ndio waliotangulia kupanda majukwaani na kuwaambia wafuasi wao wakiwaona wanaofuga madevu wawachape bakora! Jee! Huo si uchochezi? Jee! Hiyo si kauli ya kuashiria umwagaji damu? Au kauli ya uchochezi haiwezi kuwa ni ya uchochezi mpaka itamkwe na mpinzani? Ni kweli Maalim Seif alisema kuwa safari hii, chama chake kitaingia katika uchaguzi mkuu ujao kwa sera ya JINO KWA JINO! Lakini nini maana ya usemi huo wa JINO KWA JINO au JICHO KWA JICHO? Hivyo kweli maana yake ni kupita kuwang'oa watu meno yao au kuwatofoa macho yao? Kwa nini tunataka kufanya mlima kutokana na kichuguu? JINO KWA JINO, na JICHO KWA JICHO NI HAKI! Ni usemi uliomo katika vitabu vitakatifu, Kur-ani na Biblia. Hayo ni maneno ya Mungu. Mwenyezi Mungu ameagiza mwenye kutoa jino la mwenziwe na lake litolewe. Hiyo ndiyo sheria ya maumbile tuliyowekewa na Muumba wetu; kwa ajili ya kuzuia dhuluma ulimwenguni.Yeyote atakayekuwa akielewa kuwa akimfanya ubaya mwenziwe naye atalipwa ubaya pia, hatathubutu asilani kuwafanyia dhuluma wenziwe. Mwenye kuikubali sera yaJINO KWA JINO, katu hawezi kuishabikia dhuluma. Hatadhuhumu, lakini pia, hatakubali kudhulumiwa! Basi kwa nini wale wasiokuwa nania ya kudhulumu wengine wawe na hofu na sera ya JINO KWA JINO? Ama kuhusu ile sababu ya pili kuwa Polisi wanatembeza mkong'oto ili kulipiza kisasi cha wenzao waliopigwa katika mkutano wa CUF ina mushkeli kidogo. Hali hiyo inanikumbusha kichekesho kimoja katika katuni za Chakubanga. Polisi kwa kiserikali wanaitwa usalama. Kazi yao kubwa ni kulinda usalama wa raia. Lakini katika kipindi fulani Polisi walicharuka kuwanyanyasa raia. Katika kipindi hicho, siku moja, Chakubanga alikuwa amekaa na marafiki zake kijiweni wanazungumza. Ghafla akawaona Polisi wanakuja. Basi Chakubanga aliwageukia wale wenziwe na kuwaambia, "upesi tuondoke hapa. Wana usalama wale!!! wanakuja. Wasije kutukosesha usalama." Ingawa katuni hiyo ilikuwa inachekesha, lakini ilikusudiwa kutoa ujumbe maalumu. Kwa vyovyote vile Jeshi la Polisi, katika utendaji wake wa kazi halitakiwi lionekane linatumia jazba au nguvu zilizopita mpaka. Polisi hawana haki, ya kisheria ya kumhukumu raia kwa kosa lo lote alilolitenda. Wajibu wao ni kumkamata mtuhumiwa na kumfikisha mahakamani ambapo ndipo pahali pekee mtuhumiwa anaweza kutiwa hatiani na kupewa adhabu inayostahili. Lakinijambolinalosikitisha ni kuwa kiongozi wa Jeshi la Polisi anaagiza Polisi wawape mkong'oto raia! Au Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, anaridhia raia wapigwe na Polisi. Anasema wanajeshi hawachezewi. Amewauliza Watanzania kwani hawaoni kuwa raia wakimpiga askari wa JKT mmoja,jeshi zima litawaelemea raia hao? Swali la kujiuliza jee hivyo wanavyofanya wanajeshi hao ni sawa? Siku zote Jeshi la Polisi limekuwa likiwaagiza raia wasichukue sheria mikononi mwao. Wanapomkamata mtuhumiwa wasimsulubu bali wampeleke Polisi. Kuchukua sheria mkononi nikosa la jinai. Kwa nini basi Jeshi la Polisi liwe ndilo la mwanzo kuvunja sheria hiyo hiyo inayotaka raia waifuate? Mara nyingi viongozi wetu na hata baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikishuighulikia zaidi matokeo na kupuuzia sababu zinazopelekea kutokea matokeo hayo. Hiyo ndiyo jazba! Katika hili sakata linaloendelea huko Unguja chanzo chake ni tawi moja la chama cha CUF lililofanya mkutano katika tawi hilo. Mkutano huo ulihudhuriwa na KatibuMkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamadi. Waandaaji wa mkutano walivyohisi kuwa wanachama wengi wa tawi hilo watahudhuria mkutano huo waliona walizungushie tawi lao ua wa magunia; ili mkutano huo uwe ni wa ndani nasiyo wa hadhara. Kwa sababu wale watakaoingia katika ua huo wa magunia ni wale wanachama wanaohusika tu. Hapo ndipo lilipoanza sokomoko! Polisi walikwenda katika eneo hilo la mkutano na kutakawahusika wawape kibali cha kufanyia mkutano ule. Walijibiwa ule ulikuwa ni mkutanowa ndani, nimkutano wa tawi, kwa mujibu wa sheria za nchi, hauhitaji kibali! Jawabu hilo halikuwaridhisha Polisi hao. Ukazuka ubishi mkubwa baina ya pande mbili hizo. Matokeo yake ni kushikana mashati na kuumizana. Inasemekana katika hekaheka hizo Polisi mmoja alinyang'anywa silaha aliyokuwa nayo. Kweli jambo la kujeruhiwa Polisi si jambo jema. Linafaa likemewe kwa nguvu zote! Lakini jambo la kuzingatia ni kwa nini Polisi hao wajeruhiwe au wanyang'anywe silaha? Mbona Polisi wako wengi tu mitaani, hatukusikia wakivamiwa na kupigwa, na wengi wao wanatembea bila ya kuwa hata na silaha? Kwa nini basi wale, Polisi waliokwenda kule mkutanoni wajeruhiwe? Kwanza, kabla ya kujaribu kulijibu swali hilo, tuangalie mazingira yale yaliyozunguka kadhia yote hiyo. Jee! Mkutano wa ndaniunahitaji kibali? Kama hauhitaji, jee ili mkutano ukubalike kuwa ni wa ndani unahitaji vigezo gani? Hapana shaka mkutano wa ndani ni mkutano utakaofanyika katika ukumbi wa ndani na siyo hadharani. Lakini katika mazingira yetu ya Kitanzania shughuli zinaweza kufanyika nje na zikahesabika kuwa ni shughuli za ndani! Mtu anaweza kustaajabu akisikia hivyo! Lakini huo ndio ukweli ulivyo. Ni kawaida hapa nchini mtu anapofiwa kufunga barabara kwa kuweka mawe au miti barabarani ili kuashiria kuwa barabara ile kwa muda huo, hairuhusiwi kupitiwa na watu wasiohusika na shughuli hiyo. Hata tunapokuwa na harusi au furaha yo yote ndivyo inavyokuwa. Hata tunapokuwa na sherehe za kichama au za kiserikali mtindo ndio huohuo, ziwe ni mbio za mwenge au hata kumpokea kiongozi wa kitaifa wa chama tawala. Wale walioandaa ule mkutano wa CUF wanaielewa desturi hiyo. Wameizoea na hata hao Polisi waliokwenda kuuliza kibali bila ya shaka yo yote kama ni Watanzania, wanalielewa hilo! Ofisi za matawi ya vyama vya siasa, na hasa vyama vya upinzani, mara nyingi, huwa ni chumba kimoja tu, hakitoshi kuchukua hata watu thelathini. Tawi moja la chama linaweza kuwa na wanachama zaidi ya elfu moja. Kwa kuelewa hilo ndio viongozi wa tawi hilo la CUF wakaona bora wajenge ua wa magunia wawepo ndani ya uzio. Sasa Polisi wanapokwenda kutafuta kibali katika pahali kama hapo huwa wamekusudia nini? Hili nafikiri ndilo swali la msingi linalotaka kuulizwa na viongozi wetu kabla hawajatoa lawama kwa wapinzani. Isiwe madamu viongozi wa CUF wamesema safari hii ni JINO KWA JINO, basi lazima waonekane ni watu walionuia kumwaga damu! Hali inaonyesha kuwa zikitokea vurugu pande zote mbili zinaweza kudhurika, raia na Polisi pia. Kama kuwa na silaha ndiyo umwamba mbona watu wasio kuwa na silaha walithubutu kumnyang'anya silaha Polisi na inaonesha kuwa hao waliopora silaha hawakuwa wakijua kuitumia silaha hiyo au siku nyingine matokeo yangalikuwa mengine. Mungu atunusuru! Hali hii ya vurugu huko Zanzibar inasababishwa na kupuuzia utekelezaji wa muafaka. Kila upande baina ya pande mbili zinazozozana huko Zanzibar, CCM na CUF, inautupia lawama upande wa pili. CUF inasema CCM imetekeleza kiasi cha asilimia hamsini tu cha vipengele vilivyokubaliwa katika mwafaka. Lakini CCM inadai imetekeleza karibu asilimia tisini ya mkataba huo. Jawabu hii ya CCM inanikumbusha juu ya kisa kimoja nilichohadithiwa na rafiki yangu mmoja. Alinieleza safari moja alijiwa na matapeli lakini waliojifanya ni watu wa dini. Walimwomba awasaidie kufanikisha maulidi wanayotaka kusoma kwa kuwasaidia kuwapa vifaa vya pilau. Walimwambia wao wamekamilisha kila kitu lakini bado wanahitaji mchele, mafuta ya kula na nyama tu. Yule rafiki yangu akawajibu inaonekana ninyi hamjafanikisha lolote maana huo mchele, mafuta na nyama mnayotaka nikupeni ndiyo hiyo pilau yenyewe. Ninyi mmefanikisha nini? Basi wao wakajibu tumekamilisha asilimia kubwa ya vitu tumenunu kuni, vitunguu, viazi, mdarasini, bizari nyembamba, chumvi n.k. Ni kweli kwa idadi ya vitu wao wamekusanya vitu vingi; lakini vitu vyote hivyo viki changanywa pamoja haviwezi kupika pilau. Pilau hasa ni huo mchele, mafuta na nyama. Kama huna vifaa hivyo vitatu, hata uwe na vifaa vingine vingi sana, hutaweza kupika pilau. Basi na CCM Zanzibar hata kama kweli imetekeleza asilimia tisini ya mwafaka, kama inavyodai, lakini isipokubali kuweka Tume Huru ya Uchaguzi, bado hofu na wasiwasi wa wapinzani na jumuiya ya kimataifa haitaondoka. Hawataridhika kuwa kweli uchaguzi mkuu ujao unaweza kuwa huru na wa haki. Ni tume huru tu ndiyo itakayoleta ridhaa ya pande zote. Kwa nini basi serikali haitaki kujenga mazingira ambayo yatawapa imani washiriki wote kuwa uchaguzi ujao utakuwa wa haki na huru? Jumuiya ya Ulaya imeiambia serikali ya Muungano ifanye juhudi ya kuingilia kati mgogoro wa Zanzibar kwa sababu wao wanaamini kuwa Zanzibar ni sehemu ya Tanzania. Jee! Nini matokeo ya kupuuza
ushauri huo wa Umoja wa Ulaya. Jee! Tanzania imejiweka tayari kwa matokeo
yanayoweza kusababishwa ana kukataa kutekeleza ushauri huo?
|
YALIYOMO
Tahariri
Waislamu waapa kuinyima kura CCM Mkapa
ahutubia Taifa:
Wananchi wamuunga mkono Askofu Kakobe MPASHO NASAHA
SHERIA
Ushauri Nasaha
MAKALA
WAZO LA WIKI
MAKALA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
Makala ya Mtangazaji
Riwaya
Lishe
•••Golikipa Majimaji alia na mabeki |
|
|
|
|