NASAHA
Na. 043 Jumatano Aprili 12- 18, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Waislamu waapa kuinyima kura CCM
  • Wasema Ikulu anatakiwa kiongozi muadilifu 
  • Wanadai haki sio upendeleo 
Na Mwandishi Wetu 

WITO umetolewa kwa Waislamu nchini kutokipigia kura Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi Mkuu ujao kwa kile kilichoelezwa na Waislamu hao kuwa ni hatua ya kukomesha dhuluma inayofanywa na CCM na serikali yake dhidi ya Waislamu nchini.

Wito huo umetolewa na Waislamu waliojumuika jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita kuadhimisha sherehe za mwaka mpya wa Kiislamu wa 1421 ambapo ilifafanuliwa kuwa ni haramu kwa muislamu kumchagua yule ambaye amekuwa akimzuia kufanya ibada kama alivyoagizwa na Mola wake. 

"Ni haramu kujiunga katika chama kinachokuzuia kuifuata dini yako... Waislamu chagueni wanaomtambua Mwenyezi Mungu, msichague mtu atakayewakamata kwa kusema Yesu si Mungu", alisema Sheikh Bakari Mkali katika sherehe hizo zilizofanyika katika viwanja vya Msikiti wa Tungi Temeke. 

Aidha Sheikh Mkali aliwataka Waislamu nchini wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na hatimaye kupiga kura kwa vile utaratibu wa kupiga kura si jambo la haramu katika dini ya Kiislamu. 

Akifafanua kauli yake hiyo, Sheikh Mkali aliiambia hadhara ile kuwa utaratibu wa kupiga kura katika kupeana majukumu umethibiti katika matukio kadhaa katika historia ya ulimwengu wa Kiislamu. Alitolea mfano kura zilizopigwa ili kumpata mtu ambaye angemlea Bi Maryam, mama wa Mtume Issa bin Maryam. 

Mtume Issa ndiye anayefahamika kama Yesu katika dini ya Kikristo. 

Akizungumza katika sherehe hizo, aliyekuwa Imamu wa Msikiti wa Mwembechai, Sheikh Omari al-Bashir alizidi kuwasisitiza Waislamu kutoipa kura CCM katika uchaguzi Mkuu ujao kwa kusema kwamba wakati wa kufanya hivyo umefika. 

"Waislamu na wasiokuwa Waislamu,na wenye kutaka salama umefika wakati wa kufanya hijra... wote walioko CCM wayatupe makadi yao na kuhama huko ili wapate salama", alisema Sheikh Al-Bashir na kuongeza kwamba Muslamu yeyote anayemuunga mkono dhalimu ili hali akijua kuwa huyo ni dhalimu basi huyo huwa katoka katika Uislamu. 

Hijra, kwa mujibu wa Ustaadh Salim Mohammed aliyeombwa na NASAHA kulieleza neno hilo, ni neno la Kiarabu lenye maana ya kuhama toka sehemu moja kwenda nyingine mara nyingi ili kutafuta unafuu fulani 

Naye Amir wa Shura ya Maimamu, Sheikh Juma Mbukuzi, akizungumza na umati mkubwa wa Waislamu uliokusanyika msikitini hapo kuukaribisha mwaka mpya wa Kiislamu aliwataka Waislamu wasirudi nyuma kwa vile tayari yapo matumaini ya ushindi dhidi ya dhuluma wanazofanyiwa. Aliwaambia Waislamu kuwa kinachotakiwa ni kuongeza juhudi na kuzidi kumtegemea Mwenyezi Mungu. 

"Lilikuwepo giza lau koloni, (lakini)ikaja nuru ya uhuru, sasa lipo giza la ukoloni mamboleo lakini Mwnyezi Mungu si dhalimu", alisema Amir Mbukuzi na kuongeza, "hivyo dhuluma haitadumu lakini kazi ifanyike." 

Amir huyo wa Shura ya Maimamu aliwakumbusha Waislamu kwamba walikuwepo watawala dhalimu kiasi cha kujitangaza wao ni miungu lakini mwisho wao ulipofika waliondoshwa." 

Kiongozi mwingine wa Waislamu, Sheikh Swalehe Ngowi, akizungumza katika hafla hiyo iliyoandaliwa kwa pamoja na jumuiya na taasisi mbalimbali za Waislamu, aliwataka Waislamu "wachunge" kura zao na wachague utulivu, amani na uadilifu. 

"Chagueni utulivu na amani siyo CCM... Kura yako ichunge isije ikawa sabahu ya kuajiri madhalimu", alisema Sheikh Ngowi. 

Akikumbusha madai ya CCM na Serikali yake kukosa uadilifu, Sheikh Ngowi alisema kuwa chama hicho tawala na serikali yake vimekataa kuunda tume ya kuchunguza mauaji ya Mwembechai lakini viliunda tume kuchunguza kuuliwa kwa mbwa aliyekuwa kapewa jina la migration huko Sumbawanga. 

"Waondoeni (CCM na serikali yake) tuwaoneshe namna ya kutawala kwa uadilifu", alisema Sheikh Ngowi huku akipigiwa Takbir. 

Aidha,ilielezwa katika maadhimisho hayo ya mwaka mpya wa Kiislamu kwamba Waislamu nchini hawajadai kupewa upendeleo dhidi ya raia wengine na wala hawataomba upendeleo huo hapo baadaye. Wamesema madai yao yote yametokana na haki ambazo wamekuwa wakipunjwa. 

"Madai yetu tumeyataja waziwazi na jinsi ambavyho serikali imekuwa ikituminya tumeeleza pia; sisi hatujataka upendeleo bali kila kundi la raia lipewe haki linayostahiki", alieleza msemaji wa kamati ya maandalizi ya sherehe hizo na kisha akahoji, "... Sasa hao wanaovumisha sisi tunataka upendeleo wamepata wapi uzushi huo?" 

Katika siku za hivi karibuni, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hasani Mwinyi, aliwaambia Waislamu kwamba wasitake upendeleo kwa vile nchi hii inatoa haki sawa kwa watu wote. Mzee Mwinyi alitoa salaam zake hizo baada ya Sala ya Idd el Hajj iliyofanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, vilivyoko Kawe, jijini Dar es Salaam. 

Katika hadhara hiyo pia zilitolewa salaam za wanafunzi wa Kiislamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambazo ziliwataka Waislamu nchini kuutumia uchaguzi Mkuuwa mwaka huu kuondoa ubaguzi wa kidini. 

Katika salaam zao hizo zilizotolwa kupitia Jumuiya yao ya MSAUD, wanafunzi hao wamesema muda mrefu umepita sasa tangu Waislamu watoe madai yao hadharani. 

Katika waraka wao, ambao NASAHA inayo nakala wanafunzi hao wamekumbusha kuwa Waislamu wamekuwa wakilalamikia, pamoja na mambo mengine, "mgandamizo dhidi yao katika maeneo ya elimu na utawala. 

Ili kuoneshamgandamizo huo katika utawala dhidi ya Waislamu, wasomi hao wameorodhesha jumla ya wilaya 90 za Tanzania Bara ambapo katika hizo wilaya 80 wakuu wake ni Wakristu na Waislamu ni kumi tu. 
 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Wanaokemea dhuluma wasinyanyaswe

Waislamu waapa kuinyima kura CCM

Mkapa ahutubia Taifa: 
Ugumu wa maisha kuendelea

Wananchi wamuunga mkono Askofu Kakobe

MPASHO NASAHA
WAKIAMUA, HATA WAKICHAFUKA WATANAWA!!!

SHERIA
Faida ya kuwepo kwa sheria za haki kunategemea na wanaozisimamia

Ushauri Nasaha
Namna ya kumfanya mtoto wako aweze kuzungumza

MAKALA
Sababu ‘1000’ kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani - 2

WAZO  LA  WIKI
Polisi acheni ubalakala

MAKALA
Kuporomoka kwa maadili  katika jamii yetu; Sababu na utatuzi wake - 2

Kalamu ya Mwandishi
Tatizo si jino kwa jino, bali utekelezaji muafaka!

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (6)
Vijana mjiandikishe kwa wingi na siku ya uchaguzi mjitokeze

Makala ya Mtangazaji
LEO NI SIKU YA ASHURA

Habari za Kimataifa

Riwaya
Kisasi cha mauti -3

Lishe
Ni kwa jinsi gani wanawake wanapata utapiamlo

MASHAIRI

MICHEZO

  • Madadi, Jamhuri acheni ‘rusha roho’ katika soka – Wapenzi
  • Yanga wakumbwa na kiwewe
  • Mapunda asema hana bahati ya kutia mabao

  • •••Golikipa Majimaji alia na mabeki
     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita