NASAHA
Na. 043 Jumatano Aprili 12- 18, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Ushauri Nasaha

Namna ya kumfanya mtoto wako aweze kuzungumza

NA KHADIJA IDD

KUWEZA kuzungumza au kujifunza lugha kwa ujumla ni mojawapo ya mambo ambayo aghalabu tunayachukulia juu juu kama ilivyo katika kucha jua na kuchwa. Siku zote tunatarajia tu kuwa kutakucha na tutaamka halafu jioni jua litakuchwa tutalala kama ambavyo tunatarajia kuwa mtoto akizaliwa atajua kuzungumza afikiapo umri fulani. Wazazi huwa hawafanyi lolote hadi mtoto anapoonyesha dalili za kushindwa kuzungumza kama vile 'bubu'au mwenye kigugumizi.

HATA hivyo mzazi au mlezi nafasi yake ni muhimu sana katika kumsaidia mtoto ili aweze kuzungumza kwa usahihi, na katu si kama ya "zima moto" kama wengi wetu tunavyofanya. 

Mtoto anapofikia umri wa mwaka mmoja anatamka neno moja moja, anasikiliza na vile vile anaiga yanayosemwa na wengine. Katika kipindi hiki cha kujifunza kuzungumza, wazazi wanapata fursa ya kusikia yale mtoto anayoyafikiria. Wazazi wanaweza pia kumuuliza mtoto maswali au kumuelekeza huku mtoto akiwajibu kwa mdomo(verbally) ili aweze kujifunza na kujua kuzungumza. Watoto wanatakiwa wawe na stadi(skills) za aina mbili; zalishi (productive) na pokezi(receptive). Kuwepo kwa stadi hizi mbili huwawezesha watoto kuendelea na mazungumzo stadi zalishi, kwa mfano, huwawezesha watoto kuyaweka mawazo yao katika maneno na kuyatamka wakati stadi pokezi huwawezesha kuelewa yale yanayosemwa na watu wengine. 

Hata hivyo stadi hizi hazianzi kwa pamoja kwasababu watoto wanaelewa kwanza wanachoambiwa kabla ya kuweza kuzungumza. Hii ina maana kwamba anakuwa na stadi pokezi kwanza kabla hawajaweza kuzalisha maneno yake. Kwa mfano mtoto Asmaa analifahamu jina lake na akiulizwa kama yeye ni Asmaa husema ndio. Lakini katika kutamka mtoto huyo mwenye umri wa miaka miwili na nusu, atasema 'athima.' 

Pamoja na kukosea katika utamkaji mtoto huyu anajua hasa herufi sahihi za jina lake lakini bado hawezi -kuzitamka. Kwa mfano mtu akiulizwa kama yeye anaitwa 'Athima' atakataa na kusema 'hapana', ni'athima' Mtoto huyu anajua vyema kwamba jina lake halina herufi'th' na katika utamkaji wake anaelewa kuwa anatamka herufi's'. 

Sisi kama wazazi na walezi, tunatakiwa tumsaidie mtoto kama huyu kwa kutamka maneno kwa usahihi na si kuiga yeye anavyotamka, tukifanya hivyo tutarudisha nyuma jitihada zake za kujifunza kuzungumza. 

Vile vile, ili mtoto aweze kuzungumza anatakiwa aimudu midomo yake (lips), kinywa (mouth),ulimi, n.k., ili aweze kutamka vizuri sauti za lugha. Hali hii husaidiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya makuzi ya mtoto katika mwaka wa kwanza,mfano kuota meno, kukomaa misuli ya ulimi n.k. Hata hivyo mtoto anaweza kusaidiwa kwa kumzoesha kutamka maneno yenye herufi zitakazoshughulisha ulimi (herufi, l, ra mfanolala, barbara), midomo.Kwa mfano baba, mama, papa, 'kinywa,yeye, wewe, n.k. 

Baada ya kujua sauti za lugha yao,kwa kuzisikia na kuziiga watoto wataanza kujifunza maana ya maneno. Katika hatua hii watoto hujifunza kutamka majina ya watu waliowazoea mfano baba, mama, dada,babu. Wazazi na walezi, katika hatua hii, hatuna budi kumsaidia mtoto katika kumfundisha kutamka majina ya watu tunaoishi nao,na kuwatofautisha. Tumsaidie mtoto ili aepuke kuita watu wote mama, au wanyama wote mbuzi. 

Mtoto pia hujifunza viungo vya mwili kama vile macho, pua n.k.; majina ya wanyama kama vile paka, mbuzi,n.k. Tunaweza kuwasaidia watoto kwa kuwaonyesha wanyama tofauti na kuwatajia majina yao. 

Pamoja na hayo yote njia ya kumfundisha mtoto kuzungumza ni kwa kuzungumza nae. Kama vile kutumia lugha katika kumuekeza vitu mbalimbali. 

Wakati wa kuoga mzazi ongea na mtoto wake na anaweza kumwambia "sasa hivi ninaosha mguu wako",kauli hii itamsaidia mtoto kuelewa na kushika maneno"minaosha mguu." 

Wakati wa kula chakula mtoto anaweza kusema "mchicha",katikakumsaidia mtoto kama huyo mzazi anaweza kuongeza "ndio mchicha ni nzuri kwa afya yako." Kwa wale wanaosoma 'chekechea', nyimbo zinaweza kutumika kumfundishia mtoto kuzungumza. Mzazi pia anaweza kutumia mada zilizomo katika nyimbo hizo na kumfundisha mtoto. Kwa mfano wimbo wa "Paulo usije kucheza nasisi, una mikono michafu", mzazi mfundishe mtoto ajue kuzungumza juu ya usafi na kunawa vizuri kwa kutumia sabuni. 

Dereva hujifunza udereva kwa kukalia kiti cha dereva na si kile cha abiria, vivyo hivyo mtoto hujifunza kuzungumza kwa kuzungumza. Ni juu yetu kuzungumza na watoto wetu ili wawe wazungumzaji wazuri. Katu tusiwaambie 'nyamaza' kwani na sisi hatuja nyamaza na hatuwezi kunyamaza. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Wanaokemea dhuluma wasinyanyaswe

Waislamu waapa kuinyima kura CCM

Mkapa ahutubia Taifa: 
Ugumu wa maisha kuendelea

Wananchi wamuunga mkono Askofu Kakobe

MPASHO NASAHA
WAKIAMUA, HATA WAKICHAFUKA WATANAWA!!!

SHERIA
Faida ya kuwepo kwa sheria za haki kunategemea na wanaozisimamia

Ushauri Nasaha
Namna ya kumfanya mtoto wako aweze kuzungumza

MAKALA
Sababu ‘1000’ kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani - 2

WAZO  LA  WIKI
Polisi acheni ubalakala

MAKALA
Kuporomoka kwa maadili  katika jamii yetu; Sababu na utatuzi wake - 2

Kalamu ya Mwandishi
Tatizo si jino kwa jino, bali utekelezaji muafaka!

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (6)
Vijana mjiandikishe kwa wingi na siku ya uchaguzi mjitokeze

Makala ya Mtangazaji
LEO NI SIKU YA ASHURA

Habari za Kimataifa

Riwaya
Kisasi cha mauti -3

Lishe
Ni kwa jinsi gani wanawake wanapata utapiamlo

MASHAIRI

MICHEZO

  • Madadi, Jamhuri acheni ‘rusha roho’ katika soka – Wapenzi
  • Yanga wakumbwa na kiwewe
  • Mapunda asema hana bahati ya kutia mabao

  • •••Golikipa Majimaji alia na mabeki
     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita