NASAHA
Na. 043 Jumatano Aprili 12- 18, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA
 
 

Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (6)
Vijana mjiandikishe kwa wingi na siku ya uchaguzi mjitokeze 

KWA kawaida hakuna mabadiliko yoyote ya kisiasa yanayoweza kutokea popote ulimwenguni kwa wananchi kutamani, bali mabadiliko hayo hutokea baada ya wananchi kuchukua hatua moja baada ya kuchukua hatua moja baada ya nyingine ili kutimiza azama hiyo. Malalamiko yaliyopo katika kila pembe ya nchi, kufuatia hali duni ya maisha ya wananchi, hasa kuanzia kipindi cha serikali ya awamu ya tatu ni dalili kuwa sasa wananchi wamechoshwa na serikali ya Chama cha Mapinduzi na wanataka mabadiliko. Makala hii inakusudia kuwakumbusha wananchi, hususan vijana kuzingatia hatua muhimu ya kwanza katika kuleta mabadiliko ya serikali kwa njia ya kidemokrasia. Mwandishi RAJAB KANYAMA anaendelea zaidi.
 

KUJIANDIKISHA kwa ajili ya kupiga kura ni jambo lenye umuhimu wa pekee, kwa sabahu kufanya hivyo ndio njia pekee itakayomuwezesha mwananchi mwenye sifa zinazokubalika kupiga kura siku ya uchaguzi itakapowadia. 

Bila ya kujiandikisha kama mpiga kura, wewe kama mwananchi tayari utakuwa umepoteza haki yako ya msingi kabisa ya kumchagua kiongozi unaemtaka. 

Katika uchaguzi mkuu ujao ambao unategemewa kufanyika mwezi Oktoba nchini kote wewe kama mwananchi miogoni mwa wengi, katika jimbo lenu la uchaguzi utashindwa kuwakataa viongozi wabovu, waliodumaza maendeleo ya nchi yetu kwa muda mrefu au utashindwa kuchagua viongozi wazuri unaofikiri kwamba wanaweza kubadilisha hali hii mbaya inayoikabili nchi yetu kama hutojiandikisha na baadae kushiriki kupiga kura. 

Ni muhimu sana ukawa mwangalifu, ukifanya kosa la kuchagua viongozi wabovu, itabidi uvumilie kwa uchungu mkubwa matatizo yote yatakayosababishwa na viongozi hao kwa kipindi cha miaka mitano tena kabla hujapata fursa nyingine ya kufanya mabadiliko. 

Tunatoa tahadhari hii kwa vile kumezuka watu, ambao bila shaka ni mamluki wa Chama cha Mainduzi wakipata huku na huko wakiwakatisha tamaa wananchi wasishiriki uchaguzi, kwa kisingizio kuwa hata kamawatafanya nini, ni Chama Cha Mapinduzi tu ndicho kitakachoshinda uchaguzi kwa vile ndio chama chenye nguvu zote za dola ukiachilia mbali mapesa. 

Mamluki wanasahau kwamba wananchi wakiamua kufanya jambo lao, nguvu za dola hugeuka na kuwa nguvu za soda. 

Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, matokeo ya uchaguzi nchini Senegal siku za hivi karibuni na matokeo ya uchaguzi nchini Taiwan yanaunga mkono hoja yetu kuwa uwezo wa kweli wa kuleta mabadiliko uko kwa wananchi. 

Jambo la muhimu ni kwa wananchi husika kuamini kwamba wanaweza kuleta mabadiliko na kisha kuchukua hatua zinazofaa. 

Ni jambo la muhimu wananchi tukashiriki kupiga kura kwa sababu viongozi wabovu wanaweza wakarudishwa madarakani na kura za wenzetu wachache, ambao kwa namna moja au nyingine kuendelea kuwepo kwa viongozi hao madarakani kuna manufaa kwao. 

Tunahitaji kuweka historia mpya katika nchi yetu, kupiga kura ndio njia ya pekee ya kidemokrasia na amani inayofaa na inayotoa fursa kwa wananchi kuwekana kuondoa viongozi madarakani, iwapo watakuwa hawakuridhishwa na utendaji wao katika kipindi kilichopita. 

Vigezo vya kuipima Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kama inafaa au la ni vingi. 

Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imeshindwa kusimamia haki, imeshindwa kuboresha maisha ya jamii, watu wanazidi kuwa maskini, imeshindwa kupambana na rushwa na ufujaji wa mali ya umma, na sasa inaanzisha vurugu nchini kwa kuwaruhusu askari polisi kushambulia wananchi wanaopaswa kuwalinda kwa sababu za kisiasa pamoja na kuendesha kampeni za vitisho dhidi ya vyama vya upinzani na wafanya biashara wanaokataa kuchangishwa mapesa. 

Demokrasia ni njia ya kufikia muafaka pale panapokuwa na hali fulani ya kutokuelewana au kutofautiana kimsimamo na kifikra juu ya jambo fulani kama ilivyotokea huko Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995. 

Baada ya malumbano ya muda mrefu, hatimae Chama cha Wananchi na Chama Cha Mapinduzi wakafikia muafaka na hatua za kuchukua ili muafaka huo uwe na maana zikatajwa. 

Kinyume chake Chama Cha Mapinduzi hakitaki kutekeleza na badala yake, viongozi wa chama hicho na serikali yake wameamua kutumia maguvu ya dola kuendeleza ukiritimba ambao kwa kweli umepitwa na wakati na kwa kufanya hivyo wanahatarisha amani na utulivu wa nchi yetu. 

Hizi ni dalili mbaya ambazo ni lazima wananchi wawe na hadhari nazo hata katika uchaguzi ujao. 

Hatua ya kwanza ni lazima wananchi wawe macho wakati wa uandikishaji wa wapiga kura maana hapo ndio maandalizi ya wizi wa kura yanapoanza. 

Na jambo linalostahili kupewa kipaumbele ni kwa kila mwananchi kulifahamu vema jimbo lake, hasa wakazi wanaokaa katika eneo la kituo cha kujiandikishia na baadae eneo la kupigia kura ili kuepuka kuwa na wapiga kura wanaotoka nje ya mipaka au wageni ambao kimsingi wasingestahili kupiga kura na kuchagua viongozi. 

Hatua ya pili ni kwa wanachi kutokubali kuuza shahada zao za kupigia kura maana kufanya hivyo ni kujidhalilisha kupita kiwango kwa kukubali kuja kudhalilishwa kwa kipindi cha miaka mitano kwa kupokea shilingi elfu tano ambazo zinatosha kwa mlo wa siku moja. 

Mkondo bora wa Kidemokrasia katika jamii maana yake ni kwa wananchi kuwa na uwezo wa kujiamulia wenyewe kuhusu kiongozi wanaemtaka na njia yakutimiza azma hii ni kwa kushiriki katika kupiga kura, fursa hii isiachwe. 

Ni muhimu kwa wananchi wote kufahamu kuwa kushiriki kwetu katika zoezi zima la kupiga kura siku ya uchaguzi ni haki yetu ya kiraia katika kuweka uongozi bora. 

Ni kwa njia hiyo pekee ndipo tutafanikiwa kuwa na sauti juu ya mipango ya maendeleo yetu. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Wanaokemea dhuluma wasinyanyaswe

Waislamu waapa kuinyima kura CCM

Mkapa ahutubia Taifa: 
Ugumu wa maisha kuendelea

Wananchi wamuunga mkono Askofu Kakobe

MPASHO NASAHA
WAKIAMUA, HATA WAKICHAFUKA WATANAWA!!!

SHERIA
Faida ya kuwepo kwa sheria za haki kunategemea na wanaozisimamia

Ushauri Nasaha
Namna ya kumfanya mtoto wako aweze kuzungumza

MAKALA
Sababu ‘1000’ kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani - 2

WAZO  LA  WIKI
Polisi acheni ubalakala

MAKALA
Kuporomoka kwa maadili  katika jamii yetu; Sababu na utatuzi wake - 2

Kalamu ya Mwandishi
Tatizo si jino kwa jino, bali utekelezaji muafaka!

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (6)
Vijana mjiandikishe kwa wingi na siku ya uchaguzi mjitokeze

Makala ya Mtangazaji
LEO NI SIKU YA ASHURA

Habari za Kimataifa

Riwaya
Kisasi cha mauti -3

Lishe
Ni kwa jinsi gani wanawake wanapata utapiamlo

MASHAIRI

MICHEZO

  • Madadi, Jamhuri acheni ‘rusha roho’ katika soka – Wapenzi
  • Yanga wakumbwa na kiwewe
  • Mapunda asema hana bahati ya kutia mabao

  • •••Golikipa Majimaji alia na mabeki
     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita