|
Mashairi
Kheri ya Mwaka Mpya 1421H
Kwa jina lake Mwenyezi,uhai alienipa,
Mwenyewe kiti cha enzi, na yeye ndiye ‘kibopa’,
Ndiye mtoaji kazi, muondoshaji “Ukapa”,
Kheri ya Mwaka Mpya, watoaji wa NASAHA.
Mwenzenu nimefurahi, mwaka mpya kunifika,
Wa zamani baibai, wa nyuma tulikotoka,
Kuzubaa hakufai, sasa dini ni kushika,
Kheri ya Mwaka Mpya, Mwamedi Namkandika,
Mwanahelo dada yangu, wa Mgulani Shuleni,
Pokea salamu zangu, japo upo kitandani,
Nakuombea kwa Mungu, uje pata afueni
Kheri ya Mwaka Mpya, Ndugu Adam Lugomba.
Shemdoe, Mtauni, Jushaka na Kikong’ona,
Wote nawaulizeni, mwaka mpya meuona?
Muhimu kwetu ni nini, kufanya chatakikana?
Kheri ya Mwaka Mpya, ‘Nganenga’ na ‘Chipukizi’.
Mariam Mkombozi, na Jalia Mama Hawa,
Kwenye fani ni wajuzi, kheri nanyi mwatakiwa,
Zidini kuchapa kazi, ndipo mtafanikiwa,
Kheri ya Mwaka Mpya, Muhibu na Kijukuu.
Na siasa nayo pia, humo humo tuchanganye,
Tusije kupuuzia,tukajifanya mamwenye,
Kama dini twaijia, haya na tuyafanye,
Kheri ya Mwaka Mpya, Baby Fumo na Saballa.
Saba ninatamatia, nimefika kituoni,
Endapo nimekosea, chonde nisameheni,
Nilikua nasinzia, wakati nipo tungoni,
Kheriya MwakaMpya, rafikiyangu Sabaya.
MTAGALUKA RASHID -Mtaaluma
S.L.P. 16380,
D.S.M.
Usile bila kunawa
Bisimilahi anzio, kwandika na kutamka,
Mtume wake fatio, kilala na kuamka,
Nisemayo si chukio, ni mambo ya uhakika,
Ndugu yangu uasike, nawa kisha kunuia.
Usile bila kunawa, afyayo itadhurika,
Usitiye kwenye kinywa, mkono usosafika,
Iwe kula hata kunywa, manani sijeudhika,
Maji umebarikiwa, nawa ndo chakula ule.
Chakula ukitafuta, majasho yakakutoka,
Hata ukishakipata, kunawa kwasaulika,
Utahema na kutweta, macho yakikukodoka,
Ulimi wadendadenda, akili ishakuruka.
Hima hima takasike, kwa maji yalosafika,
Matonge na uyashike, ukiwa nayo hakika,
Mdomoni uyaweke, moyo ukiburudika,
Ni amri si utashi, kabla kula kunawa.
Utapata ya kuhara, na maradhi kemkemu,
Ukiifanya papara, mbele sijejilaumu,
Ukadhani masihara, ukala bila nidhamu,
Ukifa wenda jahimu, iepe mbaya bishara.
Kula kwa mkono wako,si kijiko wala uma,
Usahili myeyuko, kwa meno kuuma uma,
Thamani ya kinywa chako, kuepuka vyuma vyuma,
Mkono wende kinywani, japo lifanywe tambiko.
Chakula chende tumboni, maungoni kusambaa,
Kipitize mdomoni, tiba yenye manufaa,
Kamwe sio sikioni, na puwani ni hadaa,
Wamenena ulamaa, ya nini ladha kukhini?
Siige uzungukule, kutumia wa kushoto,
Kuepa ukale kale, kizowa kila kokoto,
Yooo mama tumbole! Uliye kitoto toto!
Kula kwa ule wa tangu, Adamu alotumia.
Kituoni ninatuwa, kalamu haijagoma,
Beti nilizochaguwa, tisa zimetakadama,
Sina haja ya uluwa, ni kutoa taaluma,
Kitaka kujuwa tamu, nawa kwanza ndipo ule.
Z.F.S. Bin Sheikh (Asili Mali),
IUIU, -UGANDA.
Mwaka mpya umejili
Malenga napiga hodi, Mhariri ufahamu,
Ninanena makusudi, tusiwe ni mahmumu,
Na kisha hapana budi, kuwatolea salamu,
Mwaka mpya umejili, kwetu sisi Islamu.
Moja nne mbili moja, sasa huu umetimu,
Kumi na tano si hoja, karne kwetu muhimu,
NASAHA natoa hoja, tushereheke kwa zamu,
Mwaka mpya umejili, kwetu sisi Islamu.
Mtume wetu rasuli, ametumwa kwa kaumu,
Makka akawa dhalili, Hijra memlazimu,
Toka kwa Mola jalali, Madina kwenda hukumu,
Mwaka mpya umejili, kwetu sisi Islamu.
Funzo gani twalipata, sisi tulio wagumu,
Rafikiye alimwita, safari wakajihimu,
Mbona sisi tunasita,kuziendea hukumu,
Mwaka mpya umejili, kwetu sisi Islamu.
Tena zile za Rabuka, aliyetuleta humu,
Uovu umetushika, tumekuwa mahasimu,
Mvinyo twautandika, zinaa nazo zadumu,
Mwaka mpya umejili, kwetu sisi Islamu.
Hakika tutahadhari, hiyo siku ya Kiyamu,
Tufanye yalo mazuri, tuokoke kwa Karimu,
Ukafiri ni kiburi, Allah sijemlaumu,
Mwaka mpya umejili, kwetu sisi Islamu.
Lazima tujihesabu, kabla haijatimu,
Kitadhihiri kitabu, Mola ataturujumu,
Ya nini kujipa tabu, kuingia jahanamu,
Mwaka mpya umejili, kwetu sisi Islamu.
Kalamu naweka chini, naendea majukumu,
Lazimatuwe makini, wala tusije laumu,
Sijitie matatani, turejee kwa Rahimu,
Mwaka mpya umejili, kwetu sisi Islamu.
Rajab Said (Rasaki),
S.L.P. 90329,
D.S.M.
Haya ni maisha gani?
Hodi ndugu washairi, wa Bara na Visiwani,
Nawe ndugu Mhariri, naja kwako gazetini,
Gazeti lako mahiri, niweke japo pembeni,
Haya ni maisha gani, kula kwa kubahatisha?
Kula kwa kubahatisha, haya ni maisha gani,
Ni maisha ya kutisha, hapa kwetu duniani,
Ni maisha ya kuchosha, ndugu zangu sikieni,
Haya ni maisha gani, kula kwa kubahatisha?
Msinione nakonda, mkadhani naugua,
Kunenepa ninapenda, dhiki zinanisumbua,
Njaa kwangu kawaida, kula ni bahati mbaya,
Haya ni maisha gani, kula kwa kubahatisha?
Kipato changu cha chini, ndugu zangu nawambia,
Hakitoshezi nyumbani, haibaki hata mia,
Huniandama madeni, mwana anapougua,
Haya ni maisha gani, kula kwa kubahatisha.
Jamani msinicheke, mwenzenu nitaabuni,
Mtu kuwa peke yake, haya alianza nani?
Kila mtu na mwenzake, ameagiza Manani,
Haya ni maisha gani, kula kwa kubahatisha.
Maisha haya jamani, yameniweka pabaya,
Ndugu hata majirani, thamani wamenitoa,
Wanasema mtu gani, kifo hataki changia,
Haya ni maisha gani, kula kwa kubahatisha.
Mjomba aliugua, akalazwa Muhimbili,
Nami kiguu na njia, kwenda kumjua hali,
Kisa pesa sikutoa, wakanitoa akili,
Haya ni maisha gani, kula kwa kubahatisha?.
Siitwi kwenye vikao, vya ndugu wanapokaa,
Tunamtaka mkeo, na sare ya kutambaa,
Sasa ni lako chaguo, pesa au kitambaa,
Haya ni maisha gani, kula kwa kubahatisha.
Kaditamati watama, kuendelea siwezi,
Natembea nikihema, nywele zangu kama chizi,
Namuachia Karima, yeye ndie muamuzi,
Haya ni maisha gani, kula kwa kubahatisha?
(Mwanafunzi)
Abdallah Omari Sabaya,
S.L.P. 100054,Mbagala, D.S.M.
Hilo ni tunda gani? (Jibu-2)
Mhariri gazetini, makini wa kupangiza,
Shemdoe ana nini, tamu swali kuuliza,
Jawabu alitamani, apasishe watoweza,
Tunda nichama cha CUF.
Sikiliza Shemdoe, swali uloulizia,
Jibu nataka nitoe, tena bila kukawia,
Kisha upige mayowe, ikiwa ndilo sawia,
Tunda nichama cha CUF.
Beti sita kizingiti, beti sita kama nanga,
Kweli umejizatiti, utoe umma ujinga,
Nazipenda zako beti, zinatuonesha mwanga,
Tunda ni chama cha CUF.
Beti ya tatu sikosi, ndipo ulipofungia,
Ulitangaza jeusi, hali nyeupe rangia,
Mtoto sio mgosi, hapo rangi napindua,
Tunda ni chama cha CUF.
CUF tunda adilifu, ndivyo nilivyobaini,
Sera zake yakinifu, usawa ni yake fani,
Uvumi ni maradufu, tokea ile tisini,
Tunda ni chama cha CUF.
CUF mwamko anzishi, haichoshi kitafiti,
Naona ni kiamshi, madhila yalo zatiti,
Hakika huliangushi, halipo kwenye kijiti,
Tunda ni chama cha CUF.
Hapa mbele sitamani, sasa jipumzisheni,
Sahihisha mtihani, Almasi kwa makini,
Lile lililo dhumuni, litangaze gazetini,
Tunda nichama cha CUF.
Mtoto Mtaun (Mtafiti) S.L.P. 4 Kilwa Kiwawa.
Hilo ni tunda gani ?(swali)
Tunda hilo si peasi, si chungwa wala fenesi,
Niwapasheni wagosi, rangi yake ni nyeusi,
Kulikosa ni mkosi, jibule mbona rahisi,
Mwalijua ila basi,basi mna wasiwasi,
Nijibu nawe Rasaki, Asha, Juma nawe Mbiku,
Mtagaluka sihamaki, jibu wote uwapiku,
Tunda hili tunda gani, nilinenalo Mtunzi?
ALMASI H. SHEMDOE “Tunda la Matumaini”,
Kigogo, Dar es Salaam
(NASAHA Jumatano Machi29 -Aprili 4, 2000)
Tunda ni Shemdoe (jibu 3)
MHARIRI nijongeshe, Ofisini niketishe,
Mezani niwasilishe, jibu langu nifikishe,
Almasi nimpashe, mashaka nimuondoshe,
Haraka ulichapishe, Mgosi limshitushe,
Ili alihakikishe, mshindi anipitishe,
Muhimu usinibishe, ‘nikilala niamshe’,
Tunda hilo SHEMDOE, Tunda la matumaini.
Kwa hoja takuonyesha,nikujibu uridhike,
Mi-beti nitakutwisha, hadi shingo uvunjike,
Na hapa sitochemsha, huo ukweli ushike,
Wala sitokuangusha, hivyo usitetemeke,
Hadharani najulisha, tunda nalifahamike,
Jibu zuri takupasha, ili usihuzunike,
Tunda hilo SHEMDOE, ulinenalo Mtunzi.
Tunda hilo si nanasi, mkono ninakuunga,
Si chungwa wala peasi, ninakataa malenga,
Tunda hilo Almasi, Mtunzi usoboronga,
Kwenu waitwa Mgosi, mwenyeji wa kule Tanga,
Kwa kutunga umepasi, huna muda wa kuringa,
Yeyote hatokuasi, Rashidi nitampinga,
Tunda hilo SHEMDOE,tunda la matumaini.
Kweli tunda si nanasi, sasa nakuchambulia,
Tunda ni wewe Mgosi, Wallahi nakuapia,
Kwenye NASAHA, hukosi, ya muhimu kutwambia,
Hilo ni jibu halisi, nadhani nimepatia,
Kwani jibu ni jepesi,kila mtu alijua,
Hakuna cha wasiwasi, sifazo zimeenea,
Tunda hilo SHEMDOE, ulinenalo Mtunzi.
Beti tano ndio mwisho, nimefika kituoni,
Na hapa ni hitimisho, sendi mbele asilani,
Wewe tunda furahisho, tena mwingine sioni,
Mwenye mema mafundisho, utoayo NASAHANI,
Bali fanya sahihisho, beti punguza mtani!
Wale watunzi wa kesho, wawekwe japo pembeni,
Tunda hilo SHEMDOE, Tunda la “matumaini”.
Mtagaluka Rashid - Mtaaluma,
S.L.P. 16380, Dar es Salaam.
|
YALIYOMO
Tahariri
Wanaokemea dhuluma wasinyanyaswe
Waislamu
waapa kuinyima kura CCM
Mkapa
ahutubia Taifa:
Ugumu
wa maisha kuendelea
Wananchi
wamuunga mkono Askofu Kakobe
MPASHO NASAHA
WAKIAMUA,
HATA WAKICHAFUKA WATANAWA!!!
SHERIA
Faida
ya kuwepo kwa sheria za haki kunategemea na wanaozisimamia
Ushauri Nasaha
Namna
ya kumfanya mtoto wako aweze kuzungumza
MAKALA
Sababu
‘1000’ kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani - 2
WAZO LA WIKI
Polisi
acheni ubalakala
MAKALA
Kuporomoka
kwa maadili katika jamii yetu; Sababu na utatuzi wake - 2
Kalamu ya Mwandishi
Tatizo
si jino kwa jino, bali utekelezaji muafaka!
MAKALA
Uchaguzi
Mkuu Mwaka 2000 (6)
Vijana
mjiandikishe kwa wingi na siku ya uchaguzi mjitokeze
Makala ya Mtangazaji
LEO
NI SIKU YA ASHURA
Habari
za Kimataifa
Riwaya
Kisasi
cha mauti -3
Lishe
Ni
kwa jinsi gani wanawake wanapata utapiamlo
MASHAIRI
MICHEZO
Madadi, Jamhuri acheni ‘rusha
roho’ katika soka – Wapenzi
Yanga wakumbwa na kiwewe
Mapunda asema hana bahati ya
kutia mabao
•••Golikipa Majimaji alia
na mabeki |