NASAHA
Na. 043 Jumatano Aprili 12- 18, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MPASHO NASAHA
 

WAKIAMUA, HATA WAKICHAFUKA WATANAWA!!! 

Na Abu Halima Sa Changwa

NILIKUWA nafuatilia kipindi cha Malumbano ya Hoja wiki zilizopita, na kulikuwa na mjadala kuhusu taarabu na lugha chafu. Watu wengine walikuwa wakisema taarabu haina matusi, wengine wakasema yamo, wengine wanalosema halieleweki, ili mradi aonekane tu kwenye luninga kwamba na yeye alikuwa yumo, n.k.

Nionavyo mimi, taarabu ni sanaa, kama sanaa nyingine. Kwa vile ni sanaa inayotumia lugha, basi tunaiita "fasihi" (literature) na imo katika tapo la "fasihi simulizi" (oral literature au orature). 

Kama ilivyo sanaa yoyote ile, taarabu ni kitu kiko pale kwa ajili ya matumizi ya jamii. Sasa huwezi ukasema taarabu ni mbaya au ni nzuri kabla hujaitumia, au kabla haijawekwa kwenye matumizi, au kabla haijaimbwa, kama ambavyo huwezi kusema kisu au moto ni mbaya kabla havijatumika. Kisu ni kizuri kikitumika kukatia vitu tunavyotaka kukata, au kumenya, lakini kinaweza kuwa kibaya kikitumika kwa mfano kuulia. Vile vile moto ni mzuri ukikuivishia chakula, au ukikupashia joto maji ya kuoga, au ukikupa joto wakati wa baridi, lakini unakuwa ni mbaya ukikuunguzia nyumba, au ukitumika na watu kama akina Kibwetere kuteketeza wenzao, tena makanisani. 

Taarabu nayo ni nzuri ikitumiwa na watu wenye busara, kwa kuimba nyimbo ambazo hata mtu na heshima zake anaweza akaimba akiwa popote, au hata Rais anaweza kuunukuu kwenye hotuba zake, kama ambavyo Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi alivyowahi kumnukuu Siti binti Saad. Lakini taarab ni mbaya ikiwa itaimbwa na mtu domo kaya, asiyeona tabu kuharisha kwa kupitia mdomoni. Kuharisha ni kutokwa na kitu katika hali ambayo si ile ya kawaida. Tumbo likichafuka utaharisha, kwa maana ile haja kubwa itatoka bila ya mpangilio. Vile vile ubongo ukichafuka, basi maneno nayo hutoka bila ya mpangilio. Mtu akila uchafu, tumbo huchafuka naye huharisha. Vile vile mtu akinywa uchafu (mfano pombe), ubongo huchafuka, naye pia huharisha kupitia mdomoni, maana maneno yake hutoka bila ya mpangilio. 

Nilichogundua mimi ni kwamba taarab imevamiwa na watu wasio na ubongo uliotulia. Watu wasio na la kuwaambia watu zaidi ya kuchukua choko choko za mtaani na kuzifanya ndio maudhui ya simulizi zao, kama ambavyo fasihi andishi ilivyovamiwa na watu wasio na falsafa za kuipa jamii. Leo meza za magazeti zimejaa trashes zenye mambo ya kijinga, utakuta vijarida vimeandikwa uharo mtupu; sijui "Mtandao wa mapenzi", "Hadithi za Chumbani", "Shemeji Kula", n.k. Utashangaa leo, hata shuleni, katika somo la Kiingereza, kwa mfano, vitabu vingi vinavyosomwa vimeandikwa na watu wa Afrika ya Magharibi tu, akina Achebe, Armah, Sembene, n.k. Kutoka Afrika Mashariki yuko Ngugi (Kenya) na p'Bitek (Uganda). Wabongo wachache na vitabu vyao havisomwi. Hao niliowataja hapo juu, vitabu vyao vina mafundisho mazuri sana, lakini vinasomwa kwa kulazimishwa, kwa vile kuna mtihani. 

Tatizo ni kwamba, narudia, taarabu imevamiwa na watu wasio na asili nayo. Taarabu ina wenyewe, kama Marehemu Kolimba nilivyomsikia wakati fulani akisema C.C.M. ina wenyewe. Akina ustadhi na akina Al-Anissa ndio walikuwa wakiimba taarab, sasa hivi hata wa-kuja nao eti wanaimba. La kuimba hawana ni kumnukuu Onyango tu, "Mambo iko huku eeeh mambo iko kule", basi! 

Kwenye taarabu watu wastaarabu walikuwa wanakwenda kutulia kupata burdani, leo walevi nao taarabu imekuwa yao. Kwenye taarabu kumeshaingizwa utamaduni wa pombe, na raha ya kilabuni, muziki uwe na fujo na ghasia na matusi ndio panakuwa na "raha". Hili ndilo tatizo la kwanza la kuharibiwa kwa taarabu, starehe ya waungwana imevamiwa na watu waso haya wala haiba. 

Pili, jamii nayo inalikaribisha hili. Ndio maana nasema, mafunza hustawi kwenye kinyesi. Pakiwa na kinyesi lazima funza watastawi. Taarabu chafu sasa hivi imeshamiri kwa sababu wachafuzi wa mazingira wamefanikiwa sana kuyachafua. Jamii imeoza. Jamii yetu si jamii tena bali ni kinyesi, na ndio maana mafunza, yale yanayoandika na kuimba upuuzi, ujinga, matusi, yanastawi. Unadhani kama pasingekuwepo na watu wanaopenda mambo ya kipuuzi yaandikwayo, au yaimbwayo, waandishi hawa na waimbaji hawa wangekuwepo? Au hata kama wangekuwepo, wangepata pa kuuzia uharo wao? 

Jingine ni utawala. Watawala nao wanaona ni sawa tu, kwa sababu wao wana uwezo mkubwa wa kupiga stop ujinga wowote ule. Lakini tabia ya watawala wengi ni kwamba kama linalofanyika halihatarishi kuwa kwake mtawala, halishughulikii, hata kama ni baya. Na pakitokea lolote ninalohatarisha kuwa kwake mtawala, atalishughulikia, hata kama ni zuri. Kwa mfano, wavamizi wa taarabu, mimi huwaita "wa kuja", wanatukanana (wenyewe wanaita kulumbana), wanatupiana kashfa, fedheha, matusi, lakini utawala wala hauyashughulikii. Ndio kwanza na viongozi nao "wanarusha roho". Rusha roho ya taarabu, aka! kwao haina tabu, lakini rusha roho ya kisiasa, si mikong'oto hiyo watu wanayopata. Vyama vingi imekuwa tabu, hadi sisi tusio na vyama nao tumo mashakani. Twasikia tu, huko Homampepaka askari wamepiga wafuasi wa chama fulani, mara huko Ujimoto askari wametandikwa bakora. Tafrani si tafrani ilimradi hakuna amani. Vyama vingi mmevileta wenyewe, leo huu uadui watoka wapi? 

Kama taarabu ilivyovamiwa, na siasa nayo imevamiwa na watu waso haya wala haiba. Nenda kasikilize hotuba kwenye majukwaa ukawasikie watu. Sera hamna, bali utasikia tu "fulani akiwa kiongozi ataleta udini, ataleta waarabu, ataleta vita, atapiga marufuku pombe, hakutakuwa na saluni za nywele , blah blah blah" Wengine utasikia, "si mnamuona, ana kitambi kama mtungi, ana ndevu kama gunzi la mhindi, kipara kama". Ni yale yale ya taarabu ya "Hana nywele kichogoni kapigwa pasi haendi saluni fyoko fyoko fyoko" 

Kolimba alisema, C.C.M. ina wenyewe. Na mimi nasema, taarab ina wenyewe. Siasa nayo ina wenyewe. Wenyewe wanajua kuwa upinzani sio uadui. Mmojawapo ni Mzee Mandela. Alipopata Urais, alimchukua mpinzani wake, Chief Buthelezi kuongoza naye nchi. Na Mandela alikuwa akiondoka nchini kwake, Buthelezi alikuwa ndio anaishika kuiongoza Mandela akiwa hayupo. Kule ndio mambo iko. 

Huku kwetu sio hivyo. Ni kosovo tu, rafu tu, kutokupendana, kufanyiziana, kusimangana, kutukanana, na kila aina ya uharo ndio tunauita siasa. Lakini hata uharo nao hukauka ukapoteza harufu. Bado tuna matumaini kuwa siku moja wataibuka watu wanaojua taarabu nzuri na mbaya. Wakaondoa mbaya ikabaki nzuri. Vile vile watatokea watakaojua siasa nzuri na mbovu. Wataondoa mbovu, na kuweka nzuri. Mzee mmoja, baada ya kusikia polisi wamepiga watu, aliuliza swali: "Hivi lile gongo analotumia askari, nikimnyang'anya, halafu nikambamiza nalo yeye mwenyewe, litambusu tu badala ya kumuumiza?" Mwingine akasema: "Hivi sio hapa Mwarabu alipokurupushwa na wananchi kwa mawe tu na magongo?" 

Wananchi watakuja tu kugundua kwamba mafunza hustawi kwenye kinyesi, na dawa ya mafunza ni kuondoa kinyesi. Kukizoa na kukitupilia mbali, kwa vyovyote vile, na kwa lolote lile, iwe kwa chepe, kwa jembe, au hata kwa mikono, wakiamua, hata wakichafuka watanawa. 

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Wanaokemea dhuluma wasinyanyaswe

Waislamu waapa kuinyima kura CCM

Mkapa ahutubia Taifa: 
Ugumu wa maisha kuendelea

Wananchi wamuunga mkono Askofu Kakobe

MPASHO NASAHA
WAKIAMUA, HATA WAKICHAFUKA WATANAWA!!!

SHERIA
Faida ya kuwepo kwa sheria za haki kunategemea na wanaozisimamia

Ushauri Nasaha
Namna ya kumfanya mtoto wako aweze kuzungumza

MAKALA
Sababu ‘1000’ kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani - 2

WAZO  LA  WIKI
Polisi acheni ubalakala

MAKALA
Kuporomoka kwa maadili  katika jamii yetu; Sababu na utatuzi wake - 2

Kalamu ya Mwandishi
Tatizo si jino kwa jino, bali utekelezaji muafaka!

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (6)
Vijana mjiandikishe kwa wingi na siku ya uchaguzi mjitokeze

Makala ya Mtangazaji
LEO NI SIKU YA ASHURA

Habari za Kimataifa

Riwaya
Kisasi cha mauti -3

Lishe
Ni kwa jinsi gani wanawake wanapata utapiamlo

MASHAIRI

MICHEZO

  • Madadi, Jamhuri acheni ‘rusha roho’ katika soka – Wapenzi
  • Yanga wakumbwa na kiwewe
  • Mapunda asema hana bahati ya kutia mabao

  • •••Golikipa Majimaji alia na mabeki
     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita