NASAHA
Na. 043 Jumatano Aprili 12- 18, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MAKALA

Sababu '1000' kwanini tunataka CCM ing'oke madarakani - 2 

Na Mwijilisti Kamara Kusupa

TUNAENDELEA na mada ya sababu elfu moja za kuuondoa utawala wa CCM madarakani. Wakati nikiandika mada hii ,mtu mmoja maarufu aliniuliza, Je, ni kweli Mchungaji unazo sababu elfu moja au ni kichwa cha kuvutia hisia za wasomaji tu sawa na yale mazungumzo ya "Alfu Lela Ulela"? Nami nilimjibu ya kwamba, ni kweli kichwa cha mada yoyote ile ni lazima kwanza kiteke hisia za wasomaji wake ndipo watakapopata hamu ya kusoma yaliyomo, lakini pia sababu elfu moja zipo. Kama kuna Mtanzania huko Mbeya anayo sababu moja ya kutaka CCM ing'oke, na Mtanzania mwingine yuko Iringa, na mwingine Kilimanjaro, Kagera, Mara, Mpwapwa na penginepo basi wakifika elfu tayari hapo kuna sababu elfu moja.

HATA kama itatokea kuwa sababu ya wananchi wa Mbeya ikawa ndiyo hiyo hiyo sababu ya wananchi wa Iringa, Ruvuma, Rukwa, na penginepo maadamu sababu hiyo inawaathiri watu wengi katika ujumla wao basi hiyo sababu moja ni sawa na elfu maana kama moja inaweza kujeruhi maelfu basi hiyo ni moja iliyo ndani ya wingi. Kwa ajili hiyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kusimama katika hiyo sababu yake moja ili tuufikie uamuzi wa pamoja wa kusema CCM ni lazima ing'oke kama alivyong'oka Mkoloni. 

Mpende msipende, mtake msitake ni lazima nitashinda

Mnamo 1995, mgombea mmoja wa kiti cha Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi alifika eneo fulani ambapo aliarifiwa kwamba watu wa eneo hilo karibu wote ni wapinzani na kwamba wamedhamiria kumpa mgombea wa NCCR kura zao. Mara aliposimama kujinadi, badala ya kunadi sera, au sifa zake na mema aliyoyafanya katika kipindi cha miaka mitano ya Ubunge wake, mgombea huyo akatoa "nyodo" ya kufunga milenia, akawaambia wananchi "nasikia hapa ndio ngome kuu ya NCCR sasa nawaambia ya kwamba mpende msipende, mtake msitake, ni lazima nitashinda. Mpige kura au msipige kura mimi bado nitakuwa mbunge tu." Kisha akashuka toka jukwaani kwa jeuri na mikogo, akapanda gari akaondoka na kuwaacha waungwana wakiwa wameduwaa huku baadhi ya wananchi wachache bila shaka washabiki wa CCM wakisema "leo nimeipata freshi yake." 

Nimeyatoa maneno hayo kama mfano hai wa kuthibitisha tatizo lililopo kwa Watanzania, maneno yenye "utemi", "ufedhuli", na "ubinafsi" uliokithiri yanapotoka kwenye kinywa cha mtawala au kiongozi, kwenda kwa wapiga kura au watu wanaoongozwa, basi hapo tatizo siyo huyo "mtu mwovu" bali tatizo halisi ni huo "mfumo mwovu" unaotumika hadi kuwapata watawala wa aina hii. Siku zote. Watawala wabaya au kwa lugha nyingine viongozi wabovu huwa hawashuki toka mbinguni wala hawajiweki wenyewe madarakani, bali huwa wanawekwa na watu kupitia mfumo ambao watu wamekubaliana nao kwamba huu ndio utaratibu wetu wa kuwapata viongozi wetu na watawala wa nchi. 

Sasa mfumo mwovu ni lazima utatoa au utazaa viongozi waovu, sawa na mti mbaya unavyozaa matunda mabaya. Wengi wetu huwa tunaishia kuona ubaya wa mtu binafsi na kuujadili huku tukiufunika kabisa (overlook) ubaya wa mfumo. Huwa tu nashindwa kuona kwamba kiongozi mbovu ni zao au tunda la mfumo wetu, na kwahiyo tunapaswa kuujadili mfumo na kuuchukia kabla ya kumchukia mtu binafsi. Matokeo ya upofu wa kutokuuona uovu ndani ya mfumo yamekuwa ni utamaduni uliopo sasa wa kubadilisha watu mmoja baada ya mwingine yaani anatoka "mbovu huyu" na anaingia "mbovu yule" hadi wengine wanafikia hatua ya kukata tamaa kwamba haiwezekani kupata uongozi bora kumbe sababu yake ni ule ukweli kwamba utaratibu wetu wa kuwapata viongozi ndio haufai na kwahiyo hatuwezi kuwaepuka viongozi wasiofaa kwa kuwa chimbuko lao ni huo mfumo usiofaa, mfumo unaopaswa kuzikwa kama mzoga. 

Tuchukulie mfano hai wa huyu mbunge jeuri anayetembeza utemi hata siku ya kampeni, je, tumaini lake ni nini? Ni wazi kwamba tumaini lake siyo hizo kura za wananchi wa jimbo lake bali ni CCM na zile mbinu zake au mbinu zao CCM ambazo wana hakika nazo kwamba hata kama watu wote watasusa kupiga kura bado mtu wao atashinda tu. Hata kama mtu wao atachukiwa hiyo ni kazi bure kwani bado atashinda tu. Hata kama atazembea kwenye kipindi chote cha miaka mitano ya uongozi wake bado atashinda tu, maana kinachomwezesha kushinda siyo hizo kura za wapiga kura bali ni "mbinu", uwongo na udanganyifu ambao kwa lugha nyingine unaitwa "rigging."

Mnamo mwaka 1995, CCM walifanya "rigging" ya hali ya juu kwa kuwatumia usalama wa Taifa na wakurugenzi wa Wilaya ambao walifanywa kwa makusudi wawe Returning Officers au Wasimamizi wa Uchaguzi na waliweza kuchezea matokeo kama walivyotaka wao. Kwa ,mfano katika kituo kimoja kwenye jimbo langu la uchaguzi la Mpwapwa, kulikuwa na kituo kimoja cha wapiga kura 300, baada ya zoezi la upigaji kura kwisha, ni watu 285 ndio walipiga kura na katika kura hizo mgombea wa kiti cha Urais wa NCCR-Mageuzi wa wakati huo Bw. Mrema alipata 0. 

Baada ya matokeo kubandikwa watu walianza kujiuliza ina maana hata wakala wa Mrema hakumpigia kura? Mmoja akasema mimi nawahakikishia kwamba kura yangu nimempa Mrema, mara ghafla ukatokea kama mkutano wa hadhara watu wengi waliopiga kura pale kwenye kituo hicho wakajitokeaza kukiri hadharani kwamba walimpa "tik" Mrema, wakajihesabu hadi wakafika 160 wakaamua kuandamana hadi Wilayani lakini kwa bahati mbaya wakafika siku ya tatu na kuambiwa na msimamizi (Mkurugenzi wa Wilaya) kwamba tayari kura zimeshajumlishwa na wala zoezi haliwezi kurudishwa nyuma na kuanza tena kuhesabu kura upya ili kuhakiki nani kapata ngapi, zaidi ya yote masanduku yameshachanganywa. 

Katika hatua nyingine msimamizi msaidizi mmoja akawasilisha matokeo yake kwamba mgombea wa kiti chaUrais wa Chama cha TADEA amepata kura nne na kumfanya mkurugenzi huyo awe hoi kiasi cha kumhoji hizo kura za Rais wa TADEA ziko wapi kwani TADEA HAIKUWA IMEWEKA MGOMBEA! Masanduku yalipofunguliwa ikadhihirika kwamba hakuna kura yoyote kwa rais wa CCM alikuwa amezidishiwa kura 26. Hapo ndipo nilipobaini kwamba kumbe matokeo yote yanayowasilishwa pale na wasimamizi wasaidizi ni kitu cha kubuni tu, hizo tarakimu zote ni za kupanga nani apate ngapi, na nani awe mshindi. 

Chini ya mfumo wa namna hii au utaratibu wa jinsi hii tunaweza kuona ni kwanini mgombea anaweza kudiriki kuwatamkia watu maneno yenye fedhuli kiasi hicho kwamba Mpende Msipende, Mtake Msitake bado mimi ni mshindi. Mpige kura msipige bado nitakuwa mbunge! Wabunge wanaochaguliwa na Usalama wa Taifa ni kweli watakuwa na mzigo wowote wa bungeni kutetea matakwa ya Serikal? 

Nasikia mwaka huu utawala wa Mkapa umeagiza kwamba jimbo lolote ambalo CCM itapoteza basi afisa usalama wa wilaya na mkuu wa wilaya watapoteza kazi. Sasa kuna swali jingine kuu la kujiuliza, nalo ni kwamba nchi ambayo viongozi wake wanapatikana kimizengwe namna hii, kweli inaweza kupata maendeleo? Watu tusiishie kuufananisha uchaguzi wetu na ule wa Wamarekani au nchi zingine zilizoendelea ambapo wagombea hupeana mikono ya pongezi na kutakiana heri baada ya kutangazwa nani mshindi na nani mshindwa, kwani uchaguzi wetu watawala wameufanya kuwa "drama", uchaguzi wetu ni sawa kabisa na mchezowa kuigiza. Uchaguzi mkuu unapogeuka kuwa sawa na mchezo wa TAUSI na akina Bishanga, tutarajie nini katika nchi hiyo? 

Ni wazi kwamba kila neno litafanywa kwa namna ya kuigiza, viongozi wataigiza kana kwamba wanaongoza. Wafanyakazi nao wataigiza kana kwamba wanafanya kazi kumbe hakuna kinachofanyika. Wanafunzi wataigiza kana kwamba wanasoma kumbe hali yao ikilinganishwa na wanafunzi wa nchi nyingine wa kwetu ni kama wanakwenda shuleni kupoteza muda, na baada ya miaka saba wanatunukiwa vyetiv ya kuhitimu elimu ya msingi huku wakiwa hawana msingi wowote wa elimu wala kisomo, kwani misingi yote ya elimu imekwisha bomolewa. 

Wakulima nao wataigiza kana kwamba wanalima kumbe mtu makini akitazama anaona ni kichekesho, kwani hakuna kilimo na kwa hiyo atacheka na kusema ngoja tuone mwisho wake. Kweli mwisho wa yote, ni nchi kugeuka kuwa nchi yenye njaa kila mwaka na taifa omba omba wa chakula toka mataifa mengine. Nchi iliyotangaza kwamba siasa yake ni ya ujamaa na kujitegemea na dunia nzima ikaielewa hivyo lakini kinyume chake ikawa nchi tegemezi yenye kuagiza chakula toka nchi zingine wakati yenyewe ina ardhi yake, maji yake, na wakulima wake, hicho ni kitendawili kama siyo mzaha! 

Inabidi wananchi tujiulize Je, huo sio utani? Ama tusema ni mchezo wa kuigiza ambao lengo lake ni kuwapa watu burdani? TX mmoja aliyepata kufanya kazi Tanzania miaka ya 1980 aliwahi kusema "In Tanzania the workers pretend to work and the employers pretend to pay." Akiwa na maana katika Tanzania, wafanyakazi hujifanya kufanya kazi na waajiri wao nao hujifanya kulipa mishahara. 

Ukweli ni kwamba, wenye kazi hawafanyi kazi na hicho wanacholipwa hakistahili kuitwa mishahara. Kwasababu haitoshi kuwafanya watu waishi, na kwa kuwa kipato halali hakitoshi basi pengo lake ni lazima lizibwe na kipato cha haramu. Hapo ndipo muungwana anapolazimishwa kula haramu ili aweze kuishi, kwa sababu mfumo wa maisha haumwezeshi kuishi kwa kipato halali. Hawezi kusomesha watoto kwa mshahara wa kuigiza, wala hawezi kujitibu au kutibu familia kwa mshahara wa kuigiza, wala hawezi kumudu gharama za maisha zinazopanda kila mara kwa mshahara wa kuigiza. 

Kumbe mlalahoi afanye nini? Jibu lililo wazi ni rushwa. Utawala wa CCM hauwezi kuondoa rushwa badala yake utawala ndio unaolazimisha hata wasiopenda rushwa, waitafute kwa udi na uvumba ili kunusuru maisha yao. Vinginevyo mtu anayelipwa mshahara wa kuigiza yaani mshahara wa kumwezesha kutumia kwa siku kumi tu, akiridhika nao ni wazi kwamba atakufa kabla ya kuufikia mwisho wa mwezi. 

Sasa ni nani aliye tayari kuwa mwaminifu hadi kufa? Ni mfanyakazi gani atakayekuwa tayari kusema ee Mungu ipokee roho yangu, ninakufa kwasababu serikali ya CCM haikunipa malipo ya haki kuniwezesha kupata ugali? Ni mkulima gani atakayekuwa tayari kusema ee Mwenyezi Mungu ipokee roho yangu, nina kufa kwasababu Serikali ya CCM imekopa mazao yangu? Ukweli ni kwamba hakuna mtu aliye tayari kuachia maisha yake kirahisi hivyo, ni lazima atafanya kila awezalo. 

Kwa vyovyote vile utawala wa CCM ukubali, usikubali bado ukweli uko pale pale kwamba ndio umewafanya watu kuwa "corrupt" baada ya kuua morali za watu na kuziba kabisa njia za kupata na kuishi kwa halali. Ndiyo maana nasema ziko sababu zaidi ya 1000 za kutaka utawala wa CCM ung'oke madarakani. 

Wiki ijayo CCM nambari wani kwa rushwa, CCM mnyonyaji nambari wani wa walalahoi.

Juu
 

YALIYOMO
 

Tahariri
Wanaokemea dhuluma wasinyanyaswe

Waislamu waapa kuinyima kura CCM

Mkapa ahutubia Taifa: 
Ugumu wa maisha kuendelea

Wananchi wamuunga mkono Askofu Kakobe

MPASHO NASAHA
WAKIAMUA, HATA WAKICHAFUKA WATANAWA!!!

SHERIA
Faida ya kuwepo kwa sheria za haki kunategemea na wanaozisimamia

Ushauri Nasaha
Namna ya kumfanya mtoto wako aweze kuzungumza

MAKALA
Sababu ‘1000’ kwanini tunataka CCM ing’oke madarakani - 2

WAZO  LA  WIKI
Polisi acheni ubalakala

MAKALA
Kuporomoka kwa maadili  katika jamii yetu; Sababu na utatuzi wake - 2

Kalamu ya Mwandishi
Tatizo si jino kwa jino, bali utekelezaji muafaka!

MAKALA
Uchaguzi Mkuu Mwaka 2000 (6)
Vijana mjiandikishe kwa wingi na siku ya uchaguzi mjitokeze

Makala ya Mtangazaji
LEO NI SIKU YA ASHURA

Habari za Kimataifa

Riwaya
Kisasi cha mauti -3

Lishe
Ni kwa jinsi gani wanawake wanapata utapiamlo

MASHAIRI

MICHEZO

  • Madadi, Jamhuri acheni ‘rusha roho’ katika soka – Wapenzi
  • Yanga wakumbwa na kiwewe
  • Mapunda asema hana bahati ya kutia mabao

  • •••Golikipa Majimaji alia na mabeki
     


       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita