| KULIKONI
BUNGENI?
1. Bismillah Rahmani, kalamu naichukua,
Lengo nifike Bungeni, Meshindwa kuvumilia,
Pesa ni mamilioni, naona yateketea,
Waziri Mambo ya Ndani, nini amewagawia?
2. Waheshimiwa Bungeni, Bajeti mnapitia,
Mliipitisha lini, Bajeti ya kutuua,
Naya kutusweka ndani, waja tuso na hatia,
Waiziri Mambo ya Ndani, nini amewagawia?
3. Kwa taifa masikini, kama letu Tanzania,
Kuwaweka watu ndani, karibu thalatha mia,
Kwa makosa ya kubuni, pale mkijisikia!
Atayezalisha nani, pesa zinateketea!
4. Akiulizwa Bungeni, sababu ajizulia,
Leo wa Uarabuni, na kesho Watanzania,
Wameichoka amani, chuki wamemtumia,
Karatasi mfukoni, siye tumemlipua!
5. Kweli Wabunge jamani, hivi mlimsikia?
Na mlikuwa makini, au mlipata sinzia!
Kwani mlishindwa nini, Gwanda kumshikilia,
Mengi machozi machoni, Luanda yamezidia.
6. Mnapokuwa Bungeni, nyie twawategemea,
Kutotazama usoni, ukweli kupigania,
Mtatuambia nini, kwetu mtaporejea,
Waziri Mambo ya Ndani, mmeshindwa mzomea!!
7. Helikopta Jijini, wote tumejionea,
Tishio kiasi gani, kwa watu waso hatia,
Kusema waongezeni, damu wakaifukia,
Waheshimiwa semeni, enyi mloshangilia.
8. Kwa kweli sikuamini, pale niliposikia,
Wizara hii haini, pesa mmeipatia,
Tena ni mamilioni, iweze tumalizia,
Lo Bungeni kulikoni, mmeshangaza jamia.
9. Aliyehukumu nani, Chuki kumfyatulia,
Risasi ya kifuani, na mwingine kumuua,
Ni Swalehe masikini, nanyi mkashangilia,
Omari kafia ndani, mahabusu Segerea.
10. Huu udhalimu gani, hapa kwetu Tanzania,
Aloua hadharani, mapesa mwampatia,
Wenzetu mlo Bungeni, haya mwayafurahia?
Kama sisi ni wageni, haki yetu kutuua!!!
11. Kina mama masikini, wote tumewasikia,
Mabomu gani nguoni, adabu mewakosea,
Kuwaanika juani, sawa mlijionea?
Tume jama iundeni, wenyewe twagharimia.
12. Tamati kubwa huzuni, Luanda nimekomea,
Malenga Bara na Pwani, Luanda nisaidia,
Ni hoja nzito jamani, haki yetu kutetea,
Iundwe tume yakhini, kwa kodi tunazotoa!!
WABILLAH TWAUFIIQ
k.s. luanda (Nolo),
dar es salaam.
Twadhalilika na Amanda
1.Bismillah taala kwajina naanzilia,
Na Mtume wa taala, salam kumfikia,
Kwani yeye mtawala, wa akhera na dunia,
Kwa sabuni ta Amanda kwa kweli twadhalilika.
2.Najitoa uwanjani, uchungu kuueleza,
Kutazama sitamani, Amanda yaniumiza,
Amanda siitamani, hata mwenyekuigiza,
Pale asipojithamini, mwiliwe kuutangaza.
3. Hili ni dhehebu gani? lisilo jua aibu,
Au ni kabila gani? linalopenda aibu,
Au wewe mpagani? pia unao wajibu,
Mapajayo na mabegani? kwetu kuwe ni dhahabu.
4. Kutoka kwa biashara, hebu hili zingatia,
Kwategemea ubora, si aibu kujijengea,
Kwa kujitoa sitara, heshima kuvunjia,
Kwa sabuni ya Amanda, kwakweli twadhalilika.
5. Uchungu umenijaa, mkono wanitetema,
Namuomba Mola jaa, kwani yeye ni karima.
Atuepushe balaa, atupe yaliyo mema.
Kwa tangazo la Amanda, kwa kweli twadhalilishwa
Fatma Ally,
S.L.P. 1895, Dar es Salaam.
Nyoka Mleleka -2
1. Bi-ismika ya Allah, kwa jina lenye baraka,
Ndugu yangu Abdallah, Salamuzo zimefika,
Siyo utumwa Hewallah, kwa wito kuuitika,
Nyoka kutuingilia, haya shime tumtoe.
2.Haya shime tumtoe, katuingilia nyoka,
Japo kutatubomoe, ili aweze kutoka,
Lazima tumuondoe, kama salama twataka,
Nyoka katuingilia, haya shime tumtoe.
3. Abdillahi Azizi, Rashid, Mtagaluka,
Tusidhani hatuwezi, kama nia tutaweka,
Malenga wa Unyamwezi, juu yenu kuitika,
Nyoka katuingilia, haya shime tumtoe.
4. Saballah bin Jihadi, Shinyanga umejiweka,
Onyesha zako juhudi, wa Mwanza waje haraka,
Saphia Musa Mweledi, lete mkuki na shoka,
Nyoka katuingilia, haya shime tumtoe.
5. Mengi tusiulizane, "Eti vipi Alifika?
La awali tuungane, kwa wito wake Rabbuka,
Kwa umoja tupambane, kukomboa Tanganyika,
Nyoka katuingili, haya shime tumtoe.
6. Ninyi nyote mwakumbuka, kadhia ya huyu nyoka,
Ni pale alipofika, porini alikotoka,
Akawa ahangika, baridi atetemeka,
Nyoka katuingilia, haya shime tumtoe.
7.Wazee aliwakuta, moto wao wamekoka,
Pembeni kajikunyata, kwa heshima kajiweka,
Moto kaanza kukoka, mwili ukachangamka,
Nyoka katuingilia, haya shime tumtoe.
8. Wazee wa Tanganyika, ndipo tunawakumbuka,
Hisani waloiweka, leo wadharaulika!!
Tangu lini Mwana nyoka, akawa mfadhilika??
Nyoka katuingilia, haya shime tumtoe.
9. Jambo linalonisonga, ni hili nalitamka,
"Nyoka ukimpa unga", "Mwili atanenepeka",
Hatoki atajijenga, na hatamu atashika,
Nyoka katuingilia, haya shime tumtoe.
10. Hayo ya kale si ndwele, tugange yatayofika,
Wala isiwe kelele, taratibu atatoka,
Shime tutazame mbele, nyuma mwiko kugeuka,
Nyoka katuingilia, haya shime tumtoe.
11. Ninashukuru jamia, adui katambulika,
Lengo alilopania, atugonge mwana nyoka,
Penye nia pana njia, na Inshallah atatoka,
Nyoka katuingilia, haya shime tumtoe.
12. Nyoka hapigwi mwilini, bure tutahangaika,
Tena hata mkiani, kifo hakitamfika,
Ila apigwe kichwani, asagike mwana nyoka,
Nyoka katuingilia, haya shime tumtoe.
Saidi M. Said Linze,
Masjid AN-NUUR,
S.L.P. 116, MPANDA
SAFARINI DAR ES SALAAM.

|
YALIYOMO
TAHARIRI
Milipuko ya mabomu Dar, Nairobi: Waislamu
walaani vyombo vya habari
Na Mwandishi wetu
Wanawake Waislamu Tanga waazimia kupigania
haki
Na Ibn Masoud, Tanga
Marekani yashambulia Sudan, Afghanistan
Maoni: Kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani:
Huu ni unazi au sehemu ya mtandao?
Nguruwe kuzua tafrani Kibamba
Na Mwandishi Wetu
Sheikh Mbukuzi ataka vijana
wajihadhari na utamaduni wa Magharibi
Na Said Shariff
TAMPRO kuzindua Tawi Iringa
Na Mwandishi Wetu
Tamasha la kusaidia wagonjwa
laanza Moro
Rajab Rajab na Mussa Ally, Morogoro
Kambi ya matibabu ya Macho Tanga
yaanza
Na Mwandishi Wetu
MAONI: Kanisa mshiriki wa ukandamizaji
Porojo za Ngatara
Na J. Hussein
Ubatizo kupitia TVZ?
Na Salahuddin Ahmad
Waislamu Kosovo waangamizwa
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA
SHIRIKISHO LA TANZANIA -2
Hoja binafsi: Uhusiano na Marekani
usituletee maafa
Na Said Rajab
Darasa la Muhammad (s.a.w)
Wanamume toeni haki za
wanawake kuepusha ufisadi
Na Halima Issa Ndabi, Mwanza
MAKALA: Hoja za kutofautisha Yesu
na Issa ni udhaifu, ni uzushi mtupu! - 2
Na Muhibu Said
Mwanaadamu alipofikia
Na Nineka B.N., Geita
Mafunzo ya Quran
Barua za wasomaji
Mashairi
Masomo ya dini ya Kiislam
Chakula na Lishe
Matangazo
|