|
Na.163 Rabiul Thani 1419, Agosti 21 - 27, 1998 |
|
TAHARIRI
Milipuko katika Balozi za Marekani: Uwigo wa upelelezi uachwe wazi GAZETI moja nchini hapa katika maoni yake ya toleo la Agosti 13, likizungumzia upelelezi wa waliohusika na ulipuaji wa bomu katika ubalozi wa Marekani lilishauri kwamba uwigo wa upelelezi upanuliwe. Nayo Serikali ya Tanzania kupitia wasemaji mbalimbali wa Serikali wameihakikishia Marekani kwamba itasaidiana nayo katika kuwasaka wahusika na kupiga vita ugaidi wa kimataifa. Tunadhani suala hapa si kupanua wigo wa upelelezi, bali kuuacha wazi; yaani nyanja zote ziwe wazi kutizamwa na zaidi ili kuleta ufanisi hapana budi kushirikisha vyombo na wataalamu wa aina mbali mbali. Hii ni pamoja na polisi, wataalamu wa mabomu, vyombo vya usalama, wataalamu wa masuala ya siasa hasa za Marekani halikadhalika historia n.k. Hii ni muhimu kwani yamekwishawahi kutokea matukio mbali mbali duniani yaliyowatatiza watu wengi na ikawa vigumu kupata hakika yake. Bw. Hitler alivyopambana na wapinzani wake na mazingira ya kuuliwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israel, Bw. Rabin ni miongoni mwa matukio yaliyoleta utata mkubwa kujua hakika yake. Lakini hata katika hili utata mwingi umeshaingia tayari. Mara tu baada ya tukio vyombo vya habari vikaanza kuimba habari za Usama bin Laden kiasi cha kufikia hatua ya kusema, "Hili ndilo Gaidi lenyewe." Sayansi ya utukizi, tayari Afghanistan na Sudan zimeshambuliwa hata kabla ya watuhumiwa kufikishwa Mahakamani. Kama suala ni Sudan kulea maharamia au magaidi, kwenda kuua watu ovyo kwa mabomu sio uharamia. Kama suala ni udikteta kama ilivyosemwa kwa Saddam je, kwenda kuua watu zaidi ya nusu milioni huo ndio uungwana na Ustaarabu kwa vipimo vya Marekani. Kama lipo kosa kwa nchi hizi basi itakuwa ni msimamo wao wa kutokusalimu amri kwa Marekani. Inachofanya Marekani hivi sasa ni kujitafutia maadui, ili ipate kuonyesha mabavu yake. Lingine la kuzingatia hapa ni kwamba, kashfa ya Monica Lewinsky ilipoibuka kwa mara ya kwanza Rais Clinton alianzisha vagi la kutaka kuipiga mabomu Iraq. Imeibuka tena, mabomu yanalipuka katika balozi za Marekani; Sudan na Afghanistan zinashambuliwa. Ni yale ya wakati wa Regan, wamarekani wanahoji kipi cha kufia Lebanoni, Regan anatuma Jeshi kuvamia Grenada. Lakini suala lingine la kuzingatia ni lile alilolitaja Profesa Ali Mazrui, wakati akitoa mhadhara juu ya vita vya Ghuba 1991 ambalo alilipa jina la ‘Linkage’yaani kiunganishi au kisingizio. Mwaka 1956,Ufaransa na Uingereza zilishiriki kuishambulia kijeshi Misri. Lakini kwavile zisingeweza kuingia moja kwa moja, ilikuwa muhimu kipatikane kisingizio. Zikaichochea Israel iivamie Misri ili waweza kupigana nyuma yake. Mgogoro ulikuwa kati ya Jamal Abd Naser na Kampuni ya Wazungu iliyokuwa inamiliki Mfereji wa Suez. Kwamba Abdul Naser aliitaifisha. Hapakuwa na mgogoro wowote kati ya Israel na Misri. Lakini Israil ikaishambuliaMisri ili kipatikane kiunganishi. Mwaka 1982 lilifanyika jaribio la kumuua Mwanadiplomasia mmoja wa Israel huko London, Uingereza, na hicho kikawa kisingizio Israel ikaishambulia Lebanon na kuua maelfu ya Walebanoni. Tukio ndani ya London lilitoa kisingizio kwa Israel kuivamia Beirut maelfu ya maili kutoka eneo la tukio na kuangamiza maelfu ya roho za watu. Ni kwa kuyazingatia yote haya tunasisitiza kwamba, ili kuupata ukweli wenyewe juu ya suala hili ni lazima wigo uwe wazi na wataalamu mabingwa wa fani mbali mbali wahusishwe. Tukirejea kwenye suala la kufanya juhudi kuwapata wahusika na kupiga vita ugaidi wa kimataifa; kila mmoja wetu anaunga mkono juhudi hizo. Lakini tunadhani ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili si kupiga vita tu ugaidi na kuwasaka wahalifu, lakini kubwa zaidi ni kuondoa sababu zinazopelekea kuibuka kwa ugaidi. Kwamba wakati tunaungana leo na Marekani kuomboleza na kuwasaka magaidi walio dhidi ya Marekani, tuyatafakari pia yale ambayo Marekani imewahi kuyafanya dhidi ya nchi nyingine ambayo yaweza kuwa sababu ya kufanyiwa vitendo vya kigaidi. Toka baada ya vita kuu ya pili Marekani ama imeingilia kijeshi; kuvamia au kupiga mabomu nchi nyingine mara nyingi zaidi kuliko nchi yoyote duniani. Mfano imefanya hivyo huko Korea, Dominica, Vietnam, Cambodia, Cuba na Laos. Mahali pengine ni Lebanon, Chile, Panama, Libya, Nicaragua, Grenada, Iran na Iraq. Wakati wa Rais Truman Marekani iliangusha bomu la Atomiki huko Hiroshima na Nagasak, Rais John F. Kennedy akaendesha operesheni iliyoitwa ‘Bay of Pig’ huko Cuba na Johnson akaingia vitani na Vietnam. Richard Nixon akaendesha vita dhidi ya Cambodia na Vietnamu. Wakati wa Rais Reagan na George Bush, Amerika ikashiriki vita vya wenyewe kwa wenyewe Lebanon na kuipiga mabomu Beirut kutokea baharini. Amerika ilipiga vita miji ya Bengaz na Tripol huko Libya. Ikavamia Grenada na Panama. Ikatungua ndege ya abiria ya Iran na kuua abiria wote kwa mamia. Lakini zaidi ikaishambulia Iraq katika kiwango cha kutisha kwa hoja ya kuilazimisha itoke Kuwait. Mfalme Haile Selase alivyoichukua Eritrea hakuna aliyemshambulia kijeshi. Kosa la Saddam likapelekea maelfu ya raia wa Iraq kuuliwa na bado leo wanateswa kutokana na vikwazo vya kibiashara, kisingizio kikiwa upekuzi wa silaha. Lakini hakuna anayehoji juu ya silaha za nyukilia na zile za maangamizi makubwa za Israeli. Kwa hiyo tunadhani ni muhimu katika kulitizama tatizo hili, pengine kuzichimbua sababu zinazochochea baadhi ya nchi kujengewa uadui na nchi nyingine au baadhi ya makundi ya watu. Pamoja na kuyasema yote haya tungependa kutoa tahadhari kwa Waislamu juu ya jambo hili. Kadhia hii ya mabomu imeshaingia unazi hivyo chukueni hadhari kwa kauli zenu. Wengine waweza kusema watakavyo ikiwa ni pamoja na kuwatia watu uhalifuni kabla hata ya uchunguzi, sio nyinyi, Waislamu. Kweli yenu si sawa na urongo wa wengine.Kweli yaweza kuwaponza na urongo wa wengine ukachukuliwa ndio kweli maadhali umeelekezwa dhidi yenu. Na hili halihitaji ushahidi wa kutoka mbali. AN-NUUR imepewa ilani ya kufungiwa wakati wowote kwa kudumu kwake kusema ukweli kwamba polisi wameua Waislamu pale Mwembechai na juu ya udhalimu mwingine wanaofanyiwa Waislamu. Kwa kuyakariri hayo na kuripoti kauli za viongozi wa serikali waliodai kwamba ‘askari sio mbwa na hakuna haja ya kuunda tume kufanya uchunguzi’; basi huo umeitwa uchochezi. Aliyeua si mchochezi, aliyesema piga yule si mchochezi wala aliyesema polisi si mbwa; si mchochezi. Pamoja na ukweli wa tuliyoyaandika na utetezi wetu, lakini haijasaidia kitu. Kama alivyosema Prof. Ali Mazrui kisingizio kimetafutwa; "Mmeandika uchochezi" kwa sababu kusema "hatutaki mseme ukweli" haiwezi kusemwa hivyo. Tunasisitiza; Waislamu chukueni hadhari zenu. Jambo hili limeingia unazi. Kweli yenu itawaponza. Kwa bahati mbaya sana kwa nchi yetu, chuki za kidini dhidi ya Waislamu zimetufikisha hapa. |
Milipuko ya mabomu Dar, Nairobi: Waislamu
walaani vyombo vya habari
Wanawake Waislamu Tanga waazimia kupigania
haki
Marekani yashambulia Sudan, Afghanistan Maoni: Kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani:
Nguruwe kuzua tafrani Kibamba
Sheikh Mbukuzi ataka vijana
wajihadhari na utamaduni wa Magharibi
TAMPRO kuzindua Tawi Iringa
Tamasha la kusaidia wagonjwa
laanza Moro
Kambi ya matibabu ya Macho Tanga
yaanza
MAONI: Kanisa mshiriki wa ukandamizaji Porojo za Ngatara
Ubatizo kupitia TVZ?
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA
Hoja binafsi: Uhusiano na Marekani
usituletee maafa
Wanamume toeni haki za
wanawake kuepusha ufisadi
MAKALA: Hoja za kutofautisha Yesu
na Issa ni udhaifu, ni uzushi mtupu! - 2
Mwanaadamu alipofikia
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org