|
Na.163 Rabiul Thani 1419, Agosti 21 - 27, 1998 |
|
Tunataka kiwanja chetu Bagamoyo
Ndugu Mhariri KWA kipindi kirefu sasa, nimekuwa nikifuatilia utekelezaji wa habari zinazotolewa katika gazeti letu tukufu la AN-NUUR. Mara nyingi dhulma dhidi ya Uislamu na Waislamu huondoshwa baada ya kutolewa habari yake katika gazeti hili. Pia wakati mwingine sisi wenyewe tunapojisahau kutekeleza majukumu yetu mbalimbali, huwa tunayatekeleza baada ya kukumbushwa na chombo hiki. Yapo matukio mengi, lakini nayatolea mfano machache. Tulijisahau kufanya Da’awah khususan Vijijini mpaka baadhi ya vijiji kuathirika vibaya kama vile kijiji cha Tae. Iliporipotiwa tu, Da’awah ilianza tena huko na kwingineko. Tunataraji kuwa tutafanya Da’awah vijijini kote Inshallah bila kungoja kukumbushwa tena na AN-NUUR. Kulitolewa agizo la Rais kuwa watuhumiwa katika kesi ya Mwembechai wakiwemo wazee, watoto, wagonjwa na wanawake waachiwe, Wizara husika ikakalia agizo hilo kwa kipindi kirefu. Iliporipotiwa tu, wazee wote waliachiwa isipokuwa Mzee Kipochi aliyeachiwa kwa dhamana. Pia Chuki Athumani naye alifunguliwa pingu na kufutiwa mashitaka. Pia Sheikh Mwazige aliachiwa baada ya Sheikh Pandukizi kuhoji ni vipi alihusika na kile kinachoitwa "vurugu" katika eneo la Mwembechai hali ya kuwa anaishi Bagamoyo? Tunashukuru sana hata ule Msikiti wa Ijumaa Bagamoyo ambao ulifungwa katika mazingira yasiyoeleweka, sasa umefunguliwa tena tangu Julai 31, 1998 baada ya kuripotiwa humu gazetini. Mimi ninachotaka kwa uongozi wa Msikiti huo, watoe maelezo, tena ikiwezekana katika gazeti hili, kile kiwanja cha Msikiti huu kilichowekewa uzio ambacho kinasadikiwa kupewa Mfadhili aliyejenga Msikiti wa Ramiya kinaanza kujengwa! Je, jengo hilo linahusiana vipi na Msikiti/Waislamu? Kama bado wana nia ya kumpa yule mfadhili, basi kabla hajapata khasara zaidi, asiendelee na ujenzi wa jengo lake binafsi, bali tunawataka hao viongozi na huyo mfadhili wakikabidhi kiwanja hicho kwa Waislamu ili kijengwe shule ya Kiislamu hapa Bagamoyo. Kama itatolewa hoja kuwa shule itakuwa karibu na bahari, basi hata shule za Mwambao, Mwanamakuka, Magambani na Ufundi zote ziko karibu na bahari. Pia majengo yote ya "kutanua" yapo karibu na bahari. Majengo mashuhuri kama Boma, Posta, Chuo cha Sanaa, Chuo cha Uvuvi, Idara ya Mambo ya Kale (zamani ilikuwa Magereza kisha ikawa polisi), Mahakama, Idara ya Elimu n.k. yote yapo karibu na bahari. Kwa hiyo, kabidhini kwanja bila kutoa hoja, kwani mmedhulumu mali ya Waislamu. Mwisho kabisa naomba AN-NUUR iendelee kututolea nuru ili tuweze kuona udhalimu na kuuondoa. Pia tuweze kuiona njia ya sawa itakayotuongoza katika salama Duniani na Akhera Insha Allah. Ummu Khansaa,
Kumfyeka Kapuya ni uduni wa fikra
Ndugu Mhariri TANGU kwisha kwa Maulid kule Bagamoyo tumekuwa tunasoma maoni tele kwenye magazeti yahusuyo hutuba ya Waziri Kapuya. Wengi wa wasomaji wamedhihirisha kutokubaliana na mawazo ya msemaji huyu ambaye ni mja tu kama waja wengine ambao pia wana mawazo kama ya Bwana huyu au kinyume chake. Lakini kilichonisukuma kuandika barua; Ndugu Mhariri, nikuwa wasemaji wote wameibuka na mkupuko wa kujenga mlima kwenye kichuguu. Ama sisemi kuwa nidharau au kashfa kwa Uislamu kwa yale aliyotoa Waziri pale Maulidini la, bali yale ni mawazo yake ambayo kama angepata nafasi mtu kumuuliza nini awazacho juu ya Waislamu wa nchi hii basi yale ndiyo majibu yake. Sasa ndugu zangu hapa hakuna haja ya kuanza kumsakama ndugu yetu hadi wengine wamefikia kudodosa ukweli wa imani yake kama ni Muislamu kweli. Allah Akbaru. Jamani huyu ni mja kama sisi ndugu zangu, na alichosema hakiwezi kutanzua lolote katika nyoyo za wale ambao hawakubaliani na aliyoyasema, bali cha maana ni kuangalia katika yale aliyosema ni yepi yenye muelekeo katika kuendeleza dini hapa nchini. Kuendelea kumsakama Kapuya sio kujenga bali ni kuzidisha mwanya kwenye ufa. Tuna mambo mengi sana ya kuhojiana hapa nchini ambayo sijui njia ipi tutumie Waislamu tupate nusra. Hivi sasa Waislamu hawana hata shule za msingi ambazo ni zao, wala hawana zahanati ambayo ni yao, wala kampuni ambayo itasaidia kuendeleza jumuiya za Kiislamu, vyote hatuna, sisi hatuwezi hata kuchanga shilingi mia mia kila mtu ili tuweze kuwasaidia wenzetu waliopatwa na mikasa ya kusema kuwa Yesu si Mungu, wengine wako nje kwa dhamana, na mawakili wanasubiri malipo, haya yote hatuna sisi kazi yetu kungoja kaneno kama kale alikosema Kapuya basi hapo tena iwe nongwa. Kapuya ni mtu tu wa Kiislamu hapa duniani, au kwa kusema hakuna dira kwa Waislamu, basi amekana kitabu chake yaani Qur’an laa, sivyo, ndugu zangu, hebu tutazame yale mambo yanayotukabili kila siku kabla ya kuelekeza nguvu zetu kwa Waislamu wenzetu ambao tunategemeana. Uislamu ni dini ya nasaha, dini ya amani, dini ya rehema, dini ya salama, ni dini pekee yenye mwongozo swafi, kwani Kapuya pia kasema wazi siku ile kuwa hii dini yetu ni njia ya maisha, yaani Uislamu ni njia ya maisha ya walimwengu wote. Nasi tuwe kama dini yetu ilivyo, na pindi tutapotatizana
baina yetu, ubora tuitane ili tuweze kukanyana kwa njia ya kitabu na sunna
za Mtume wetu (s.a.w) Nguvu zetu ni umoja; ni hatari kutengana. Basi tukae
kwa amani na salama tupate kufaulu. Amin.
J.S. Elmarjeby,
Si hoja bali ni agizo la Mwenyezi Mungu
Ndugu Mhariri NINAYO heshima mbele yako na mbele ya Muislamu mwenzangu Abbas Machano wa Zanzibar kuhusu barua yake iliyomo katika gazeti la AN-NUUR Na. 159 la Julai 24-30, 1998, yenye kichwa cha habari "Polisi kujenga Msikiti si hoja". Namkumbusha Abbas kwamba kujenga Msikiti si hoja bali ni moja ya maagizo ya Mwenyezi Mungu (s.w.) kwa watu wote bila kujali itikadi, rangi au nyadhifa zao. Jengo la Msikiti haliwezi kuwa la watu bali ni jengo la Mwenyezi Mungu japo watu wanaweza kujenga jengo la Msikiti. Kilicho cha Mungu haki na hoja kwa wanadamu ila kilicho cha wanadamu kina hoja kwa wanadamu kwa waanadamu. Abbas wewe kuwa Muislamu si hoja, hoja itakujia kama hutakufa katika Uislamu. Ustadh Abbas ndani ya wazuri hutokea wabaya sana na ndani ya wabaya wamo wazuri zaidi, na mtu halipwi kwa ubaya ila sawa ubaya wake na mtu kamwe hatachukua mzigo wa mwingine kila mmoja sambamba na furushi lake mwenyewe. Kwa Muislamu kumkatisha tamaa Muislamu mwenzake kwa kufanya yale ayaridhiayo Mungu ni kosa, kwani pia kwa kufanya hivyo, ni kuwakatisha tamaa Waislamu wengine pale wanaotaka kuiga mfano huo mzuri, aliye mbora kati ya watu hakika Moka ndiye amjuaye. Mtu hulaaniwa pale afanyapo laana na hushukuriwa pale anapotekeleza, kuyanusuru, na kuyatetea maagizo ya Mwenyezi Mungu. Abbas unatoa hukumu kwa wajenzi wa Msikiti ili hali wewe ni Muislamu, tena bila kujua thamani ya jengo, mahala lilipo na bila ya kuwajua walioshiriki kulijenga, idadi yao, na limeanza kujengwa mwaka gani. Hayo majengo uliyoyataja ni tofauti kabisa na hili la hapa, na si kibanda kama ulivyohisi na hukupaswa kuita kibanda jengo la Mwenyezi Mungu kwa kufanya hivyo unaufedhehesha Uislamu wako. Sisi wazalendo wa Newala tunawapongeza wananchi wote wa Newala wale walioshirikiana na askari wetu wa polisi na Magereza kulijenga jengo hilo ambalo kwa kiasi fulani litasaidia kupunguza msongamano kwenye Misikiti mingine ya hapa na tunawaomba askari wa majeshi yote hapa nchini kuiga mfano huu mzuri. Jabiri Juma,
Tumeuawa ndio basi?
Ndugu Mhariri NAPENDA kujitokeza kwa mara ya kwanza katika gazeti lako. Kwanza nawapa pongezi nyingi katika kuupigania Uislamu na kupigana na dhulma dhidi ya dini ya haki kwa kupitia gazeti lako la AN-NUUR. Kwa kweli inasikitisha sana kuona Waislamu tunadhulumiwa na tumebaki kimya tu kana kwamba tunaridhika na dhulma tunayotendewa. Kwanza napenda kuwapa pole Waislamu wote waliopata tabu, karaha, maonevu ya wazi hapo Mwembechai, tumeona wazazi wetu wa kike (akina mama) kadhia walioipata pale walipokamatwa na kupelekwa Keko. Huko wamevuliwa nguo mbele ya watu rika mbalimbali kewli inasikitisha sana. Iweje Waislamu wameuawa kwa kupigwa risasi na askari halafu serikali imekaa kimya au ukweli na uwazi wenyewe ndiyo huo. Hao askari waliofanya mauaji watachukuliwa hatua lini? Kama askari ameua jambazi ambalo linadhuru raia wema anachukuliwa hatua, iwaje anaeua watu walio katika moja ya mikutano ya kidini hawachukuliwi hatua zozote? Mwisho napenda kutoa pongezi zangu kwa akina mama wa Songea kufanya maandamano ya amani kuonyesha vazi la hijabu. Nashauri wanawake wa mikoa mingine tuige mfano huo. Tunu Ibrahimu,
Hongera Katibu wa BAKWATA mkoa wa Tanga
Ndugu Mhariri NAOMBA unipe nafasi katika gazeti lako ili nitoe zangu pongezi kwa Katibu wa Bakwata mkoa wa Tanga. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuletea kiongozi mwadilifu Katika mkoa wetu huu wa Tanga kwani hajafikisha hata miezi mitano tangu ateuliwe kushika wadhifa huo. Hapa kwetu Mombo katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa kulikuwa na mgogoro uliozaa jamaa mbili. Pamoja na shutuma walizopelekewa viongozi wa Bakwata mkoa, kwamba walianzisha jamaa ya nyuma ni vijana wa Ansar Sunna wanaotaka kuuteka Msikiti na wanaotaka kuvuruga amani katika eneo la Mombo, lakini Katibu huyu wa mkoa alichofanya ni kwamba alikuja kuhakikisha maneno hayo kama yalikuwa ni ya kweli au si ya kweli. Kitu ambacho viongozi wa Bakwata Wilaya walishindwa kufanya. Yeye alivyokuja alisikiliza malalamiko ya pande zote mbili zinavutana, ndipo akagundua kwamba chanzo cha jamaa mbili ilikuwa ni Imamu asiyefaa. Amechaguliwa anayefaa mgogoro wa Mombo umekwisha na Waislamu wanaswali pamoja. Tunamuoma Mwenyezi Mungu akuzidishie maisha marefu na akuwezesha kuendelea na uadilifu huo huo. Abdulrahamani Omar,
Maulidi na kujenga Misikiti hatufiki mbali
Ndugu Mhariri NINAOMBA unipe nafasi katika gazeti lako nizungumze machache kama atakavyoniwezesha Allah (s.w.). Rejea nukta zifuatazo: Misikiti haiwezi kujenga Hospitali na Shule, bali Hospitali na Shule zinaweza kujenga Misikiti. Hivyo kutokana na nukta hiyo Waislamu wote nchini tunajifunza kuwa tujitahidi kujenga shule na mahospitali badala ya kukaza mishipa kusoma Maulidi na kujenga Misikiti. Je, ni Muislamu gani katika nchi hii amekosa nafasi
ya kusalia eti Misikiti michache? Je, ni Waislamu wangapi wanakosa nafasi
za masomo kwa ukosefu wa shule?
Haddi Gonce
|
Milipuko ya mabomu Dar, Nairobi: Waislamu
walaani vyombo vya habari
Wanawake Waislamu Tanga waazimia kupigania
haki
Marekani yashambulia Sudan, Afghanistan Maoni: Kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani:
Nguruwe kuzua tafrani Kibamba
Sheikh Mbukuzi ataka vijana
wajihadhari na utamaduni wa Magharibi
TAMPRO kuzindua Tawi Iringa
Tamasha la kusaidia wagonjwa
laanza Moro
Kambi ya matibabu ya Macho Tanga
yaanza
MAONI: Kanisa mshiriki wa ukandamizaji Porojo za Ngatara
Ubatizo kupitia TVZ?
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA
Hoja binafsi: Uhusiano na Marekani
usituletee maafa
Wanamume toeni haki za
wanawake kuepusha ufisadi
MAKALA: Hoja za kutofautisha Yesu
na Issa ni udhaifu, ni uzushi mtupu! - 2
Mwanaadamu alipofikia
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org