|
Na.163 Rabiul Thani 1419, Agosti 21 - 27, 1998 |
|
Wauaji, wanyanyasaji Mwembechai washitakiwe Na Ibn Masoud, Tanga WANAWAKE wa Kiislamu mkoani Tanga wameazimia kuanza upya harakati za kudai haki za Waislamu nchini kama ambavyo walishiriki kuupigania uhuru wa nchi hii. Wamesema pamoja na kushiriki kwao katika kuupigania uhuru, na kuwa chimbuko la Jumuiya ya kwanza ya akina mama katika siasa, bado haki za wanawake Waislamu na Waislamu kwa ujumla zinahujumiwa kinyume na Katiba ya nchi. Aidha, wameungana na wenzao kuitaka serikali iwafichue wale wote walioshiriki mauaji ya Waislamu na madhila mengine kwenye Msikiti wa Mwembechai mapema mwaka huu. Hayo yalikuwemo kwenye tamko la wanawake hao mwishoni mwa kongamano la siku nzima lililofanyika Jumapili ya Agosti 16, 1998 kwenye ukumbi wa shule ya Sekondari ya Usagara mjini hapa. Katika tamko hilo, wameshangazwa kuona idadi kubwa ya polisi ikimwagwa Ngorongoro kuwasaka majambazi waliomuua Afisa wa Polisi wa Wilaya, huku polisi ikiahidi kuwapata wauaji hao wakiwa hai au wamekufa. Wamesema wauaji wa Waislamu pale Mwembechai ni polisi wenye kujulikana. Suala la kuwafichua tu na kuwashughulikia ipasavyo iweje wanafichwa? Ilitamkwa kwa ukali na msomaji wa tamko hilo, Bi. Asia Shekimweri. Alisema hakuna subra katika hili na akaitahadhrisha serikali juu ya kupuuza madai yote ya Waislamu, na akaelezea hofu yake juu ya kupuuzwa huko. Akiendelea na malalamiko hayo, amekumbusha mchango mkubwa wa wanawake wa Kiislamu kwa nchi hii katika kuleta uhuru na baada ya uhuru; kutokana na kudhalilishwa kwa wanawake na mauaji hayo, ameonya uwezekano wa kusimama tena kidete kudai haki za Waislamu kama zilivyohakikishwa kwenye katiba ya nchi, pindi kupuuzwa kwa madai hayo kukiendelea. Akinamama mbalimbali waliochangia kwenye mada za kongamano hilo; walitoa mapendekezo na maazimio tofauti kwa serikali na akinamama wenzao wa Kiislamu. Mchangiaji wa mwanzo aliwataka wazazi wa Kiislamu kupunguza kasi ya kuenea kwa maovu kwa kurahisisha ndoa za mabinti zao hasa katika suala la mahari na akawataka wanawake wa Kiislamu kutokutoa dharura pasipohitajika dharura katika suala zima la kujikwamua kutoka madhila ya aina kwa aina. Mwingine aliitaka serikali iwache kupotosha sheria za Kiislamu hasa ya mirathi, na kwa upande mwingine akazipongeza sana baadhi ya taasisi za Kiislamu kwa kusaidia miradi mbalimbali ya jamii. Dada mmoja ambaye hakutaja jina lake na ambaye ni mwalimu wa shule, alikasirishwa na upotoshaji wa maadili ya Kiislamu katika masomo ya historia na sayansi. Alitoa mifano ya hoja zitolewazo juu ya kuumbwa kwa binadamu ati alianza kuwa nyani, kuwa ni uwongo, pia akakemea kuhusishwa kwa biashara ya utumwa na Uislamu. Mchangiaji ambaye alitia fora zaidi ni binti wa miaka kama 15 ambaye alikuwa akizungumza huku akilia bila kuathiri usikivu wa sauti yake. Alisema "mauaji ya Mwembachai ni unyama, nayalaani. Wanawake wenzetu walionekana tupu zao ni kama tumeonekana tupu zetu Waislamu wote", alilalama. Baada ya kufoka kwa dakika kadhaa na kuwaliza wenzake alimalizia kwa kusema "Niko tayari kwa lolote". Katika kuonesha masikitiko yao zaidi, akinamama hao waliofurika katika pembe zote walizotengewa, hatimaye walitoka kwa pamoja kwa takbira na kuzunguka mitaa mitatu ya jirani na shule hiyo; kabla ya sala ya Alasiri huku wakibeba bango linalodai walioua Mwembechai wakamatwe. Pamoja na mada mbalimbali pia kulikuwa na maonesho na mauzo ya bidhaa mbalimbali . Kabla ya kufunga shughuli, iliundwa kamati ya akinamama
kuwaunganisha wanawake wa Kiislamu kutoka taasisi mbalimbali ili kuratibu
mijumuiko ya aina hiyo mara kwa mara na kila itakapohusu jamii ya Kiislamu
Tanga na Tanzania kwa ujumla.
|
Milipuko ya mabomu Dar, Nairobi: Waislamu
walaani vyombo vya habari
Wanawake Waislamu Tanga waazimia kupigania
haki
Marekani yashambulia Sudan, Afghanistan Maoni: Kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani:
Nguruwe kuzua tafrani Kibamba
Sheikh Mbukuzi ataka vijana
wajihadhari na utamaduni wa Magharibi
TAMPRO kuzindua Tawi Iringa
Tamasha la kusaidia wagonjwa
laanza Moro
Kambi ya matibabu ya Macho Tanga
yaanza
MAONI: Kanisa mshiriki wa ukandamizaji Porojo za Ngatara
Ubatizo kupitia TVZ?
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA
Hoja binafsi: Uhusiano na Marekani
usituletee maafa
Wanamume toeni haki za
wanawake kuepusha ufisadi
MAKALA: Hoja za kutofautisha Yesu
na Issa ni udhaifu, ni uzushi mtupu! - 2
Mwanaadamu alipofikia
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org