AN-NUUR
Na.163 Rabiul Thani 1419, Agosti 21 - 27, 1998
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
MAKALA

Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu, ni uzushi mtupu! - 2


 






Na Muhibu Said

UKOO WA YESU

BW. Augustine anasema Qur’an inasema Mariamu aliyemzaa Isa ni binti Imrani (3:35 na 66:12). Pia inaongeza kuwa Mariamu alikuwa dada ya Haruni (19:28). Biblia inasema dada ya Haruni ni Miriamu wala siyo Mariamu. (Kutoka 15:20). Biblia bado inaeleza kuwa Miriamu dada yake Haruni hajawahi kuzaa maisha yake yote". Mwisho wa kunukuu.

Ni kweli Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndani ya Qur’an Tukufu amewanukuu Wayahudi kumuita Bi. Mariamu kuwa ni dada ya Haruna. Pamoja na hivyo, "udada" unaokusudiwa hapo ni wa:

Kiukoo kwa kuwa Bi. Mariamu na Haruna wote wanatoka katika ukoo wa Lawi. Ushahidi wa hili tunaupata katika Injili ya Luka 1:36 inayoeleza uhusiano wa Mariamu na Elizabeti (mama yake Nabii Yohana Mbatizaji) ambaye ni mmojawapo wa uzao wa Haruni wa ukoo wa Lawi (Luka 1:5).

Kiutumishi wa kazi za Mungu, kwa kuwa Bi. Mariamu na Haruna wote walikuwa ni watumishi wa Mungu hasa kwa vile ukoo wao (Walawi) ndivyo Mungu alivyokwishamteua maalum kwa kazi hiyo (Kutoka 40:12-16 na Luka 1:38).

Kiucha Mungu. Kwa kuwa Bi. Mariamu alikuwa ni mcha Mungu neema aliyopewa na Mungu (Luka 1:30) kama vile Haruna pia. Na hii inafanana na ile kauli ya Bwana Yesu au Nabii Isa (a.s.) aliyosema:

"Kwa maana yeyote atakayefanya mapenzi ya Baba yangu aliye Mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, umbu langu na mama yangu". (Mathayo 12:50).

Hapa haina maana kwamba eti kwa vile Bw. Augustine ataamua kufanya mapenzi ya Mungu basi ndio atakuwa ndugu ya Yesu wa kuzaliwa. Hapana! Lakini atakuwa ni ndugu yake kiimani (kiucha Mungu) tu.

Kwa mantiki hiyo, maelezo ya Qur’an Tukufu juu ya "udada" wa Mariamu kwa Nabii Haruna bado haujatofautisha Yesu na Isa. Lakini maana yake ni yule yule mmoja, Bikira Mariamu anayetajwa na Qur’an na Biblia kama tulivyoona hapo juu.

KUUMBWA

Bw. Augustine anasema, Qur’an inasema Isa aliumbwa na Mwenyezi Mungu sawa na alivyoumbwa Adam (3:59). Hii ina maana kuwa Isa aliumbwa toka katika udongo. Biblia inasema Yesu alikuwako tangu milele yote kama nafsi ya Mungu (Yohana 17:5 na 1 Petro 1:20). Vile vile Biblia inasema alishuka toka mbinguni na kutwaa umbo la mwanadamu (Yohana 1:14). Yesu mwenyewe anasema yeye si wa ulimwengu huu bali ametoka kwa Baba (Yohana 8:23 na 16:28). Hii huoni kuwa ni tofauti? Mwisho wa kunukuu.

Qur’an kusema Nabii Isa au Yesu aliumbwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) sawa na alivyoumbwa Nabii Adamu (a.s.):-

Mosi: Ni kuthibitisha (hakika) kwamba Bwana Yesu naye kama viumbe wengine aliumbwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwani ni Mwenyezi Mungu pekee yake ndiye aliyeumba kila kitu (Isaya 44:24 na Qur’an 6:101-1020.

Pili: Yesu au Nabii Isa (a.s.) aliumbwa kwa tamko tu la Mwenyezi Mungu la kusema "kuwa na akawa" kama Adamu (a.s.) (3:59).

Tatu: Kwa kuwa Nabii Adamu (a.s.) (ndiye mtu wa kwanza kuumbwa) aliumbwa kwa udongo, vile vile Nabii Isa au Yesu (a.s) naye kwa kuwa alikaa tumboni mwa mama yake Bi. Mariamu kwa muda kadhani wazi kuwa naye amerithi mwili ambao asili yake ni udongo kupitia mama yake. Hivyo, naye Yesu pia ni udongo kama Nabii Adamu (a.s.).

Biblia haijaeleza mahali popote kwamba Yesu ni nafsi ya Mungu kama anavyopotosha Bw. Augustine. Pia suala la kuwepo kabla ya ulimwengu si kwa Yesu peke yake bali ni kwa wanadamu wote (rejea Zaburi90:1-2, Waefeso 1:4 na Warumi 8:29-30) kwa shuhuda hizo, ni dhihiri kuwa binadamu wengine wote wana haki ya kusema "walitoka kwa Mungu", wakimaanisha kwamba "Muumbaji wao ni Mwenyezi Mungu".

Ama Bwana Yesu kusema kwamba yeye si wa ulimwengu huu haina maana nyingine yoyote zaidi ya kuonyesha ni jinsi gani asivyothamini maisha ya kidunia na vishawishi vyake vyote badala ya maisha ya akhera. Na hii hata Mtume Muhammad (s.a.w) alikwishaambiwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwamba:

"…Na maisha ya dunia (hii) si kitu ila ni starehe idanganyayo (watu)". (3:185).

Kwa hali hiyo, Yesu ndiye yule yule Nabii Isa bin Mariamu aliyeumbwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t) bila ya baba kama Qur’an na Biblia vinavyoeleza.

Kuzaliwa

Bw. Augustine anasema Qur’an inasema Isa alizaliwa chini ya mtende tena wakati wa mchana (19:25). Qur’an haitaji mji aliozaliwa Isa. Biblia inasema Yesu alizaliwa katika mji wa Bathlehem wakati wa usiku katika zizi la ng’ombe (Luka 2:7). Je, huoni hiyo kuwa ni tofauti? Mwisho wa kunukuu.

Ni kweli Qur’an inaonyesha Nabii Isa alizaliwa chini ya mtende lakini hajaeleza kwamba siku hiyo ilikuwa ni mchana au usiku, pia Biblia haijaeleza kwamba Bwana Yesu alizaliwa katika zizi la ng’ombe kama anavyozua Bw. Augustine.

Mstari huo wa Luka 2:7 alioutaja Bw. Augustine hapa juu) ulichoeleza ni kwamba baada ya Bi. Mariamu kumzaa Yesu alimlaza katika hori la kulia ng’ombe! Na hori siyo zizi la ng’ombe bali ni "mkondo wa bahari" (soma maelezo ya maneno katika Biblia, Uk. 1223). Hivyo, ni upotoshaji wa wazi wa maandiko kuzua kwamba Bwana Yesu alizaliwa katika zizi la ng’ombe!

Mara nyingi Qur’an Tukufu huzungumza msingi wa jambo tu kisha humwachia Mtume (s.a.w) atoe uchambuzi (16:44) kwa mantiki hiyo, Qur’an ilivyokwishabainisha kwamba Nabii Isa au Yesu (a.s) amezaliwa na Bikira Mariamu, siyo lazima ieleze na mji aliozaliwa kwani siyo kitabu cha historia bali ni kitabu cha mwongozo na mazingatio kwa yote kinayoyaeleza n.k. (2:185 na 12:111).

Isipokuwa la kuzingatia hapa ni kuwa katika nchi ya Kiyahudi alikozaliwa Yesu au Nabii Isa (a.s) kama Qur’an Tukufu ilivyoeleza ni mashuhuri sana mitende (Yohana 12:12-13). Kwa hiyo, Qur’an kuonyesha kwamba Nabii Isa au Yesu alizaliwa chini ya mtende ilikuwa ni sahihi kabisa.

Kwa hali hiyo, Biblia kutoeleza ni sehemu gani Yesu (Isa) alikozaliwa bado hakujatofautisha Yesu na Isa.

Na hii ni sawa na wanavyoamini Wakristo wenyewe kwamba Injili ya Yohana Mtakatifu kutoeleza kabisa historia ya kuzaliwa kwa Yesu bado hakujatofautisha na Yesu yule yule anayeelezewa na Injili ya Luka Mtakatifu iliyoeleza kwa kirefu historia ya kuzaliwa kwake (Yesu).
 

Juu

YALIYOMO



TAHARIRI

Milipuko ya mabomu Dar, Nairobi: Waislamu walaani vyombo vya habari
Na Mwandishi wetu

Wanawake Waislamu Tanga waazimia kupigania haki
Na Ibn Masoud, Tanga

Marekani yashambulia Sudan, Afghanistan

Maoni: Kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani:
Huu ni unazi au sehemu ya mtandao?

Nguruwe kuzua tafrani Kibamba
Na Mwandishi Wetu

Sheikh Mbukuzi ataka vijana wajihadhari  na utamaduni wa Magharibi
Na Said Shariff

TAMPRO kuzindua Tawi Iringa
Na Mwandishi Wetu

Tamasha la kusaidia wagonjwa laanza Moro
Rajab Rajab na Mussa Ally, Morogoro

Kambi ya matibabu ya Macho Tanga yaanza
Na Mwandishi Wetu

MAONI: Kanisa mshiriki wa ukandamizaji

Porojo za Ngatara
Na J. Hussein

Ubatizo kupitia TVZ?
Na Salahuddin Ahmad

Waislamu Kosovo waangamizwa

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA 
SHIRIKISHO LA TANZANIA -2

Hoja binafsi: Uhusiano na Marekani usituletee maafa
Na Said Rajab

Darasa la Muhammad (s.a.w)

Wanamume toeni haki  za wanawake kuepusha ufisadi
Na Halima Issa Ndabi,  Mwanza

MAKALA: Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu,  ni uzushi mtupu! - 2
Na Muhibu Said

Mwanaadamu alipofikia
Na Nineka B.N., Geita

Mafunzo ya Quran

Barua za wasomaji

Mashairi

Masomo ya dini ya Kiislam

Chakula na Lishe

Matangazo
 

 

 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org

Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita