AN-NUUR
Na.163 Rabiul Thani 1419, Agosti 21 - 27, 1998
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
Porojo za Ngatara
Na J. Hussein

Juma lililopita niliahidi kuzijadili hatua kwa hatua "hoja" za Bwana Ngatara; ambazo hata hivyo mimi nilichagua kuziita porojo. Swali la kujiuliza ni je, ni ushabiki wa kidini (mimi ni Muislam-Alhamdulilah) ulioniongoza kuziita juhudi za Bwana Ngatara ‘porojo" au kuna kigezo kingine? Wahenga wamesema: bila utafiti huna haki ya kuzungumza na ukilazimisha kuzungumza basi usije ukakasirika iwapo utakachozungumza kitaitwa ‘porojo’. Kwa kifupi ni kwamba namtuhumu Bwana Ngatara kwa kutofanya utafiti kabla ya kuzungumza.

Baada ya kutoa utangulizi huu, hebu sasa tuone ni zipi hizo porojo za Bwana Ngatara na ni kwa nini ziitwe hivyo!

Moja kati ya sera kuu za kitaifa za Tanzania, tangu uhuru, ni ile inayohakikisha kwamba nchi inabakia kutokuwa ya kidini, ambayo kikatiba inalinda haki ya watu ya kuabudu na kuamini dini waipendayo. Ni msingi huu imara wa kijamii na kisiasa ulioiwezesha Tanzania kubakia "Kisiwa cha amani" ndani ya bara linalokabiliwa na misuguano na migongano ya hatari ya kila aina..." - Bwana Ngatara.

Awali ya yote inanipasa kutafautiana na Bwana Ngatara kuhusu dhana ya Amani. Kwa mujibu wa Bwana Ngatara Tanzania kuna amani. Bila shaka uwezo wa kufikiri wa Bwana Ngatara ungekuwa ni mkubwa kuliko alionao angeona kuwa ‘kuwepo na amani’hakutafsiriwi na kukosekanakwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yenye mweleko wa kitikadi au kuondoa mamlaka iliyopo.

Tafsiri sahihi zaidi ya ‘kuwepo kwa amani’ ni kushamiri kwa hali ya usalama wa maisha ya watu na mali zao kunakoambatana na utii kwa sheria na kuthaminiwa kwa haki za binadamu.

Swali ni je, hali hii inapatikana ndani ya nchi hii? Jibu ni hapana. Jibu lingekuwa ni ndiyo, tusingeshuhudia kila anayajenga nyumba kuigeuza gereza kwa hiari yake mwenyewe kwa kuhakikisha milango na madirisha yote vinaimarishwa kwa ngao za chuma. Wanachoogopa ni nini na wao wanaishi kwenye kisiwa cha amani? Ni amani ya aina gani hiyo ambapo kama huna kitambulisho cha ajira polisi wanahaki ya kukubandika lebo ya mzembe na uzururaji na kama huna ‘kitu kidogo cha kuwakatia’ unahukumiwa kuwa huna haki ya kuwa huru? Mifano ya aina hii ni mingi. Tena mingi sana. Cha msingi ni kuzingatia kuwa kuzuka kwa makampuni mengi ya ulinzi; uhamasishaji wa ulinzi wa sungusungu; kupitishwa kwa haraka haraka kwa sheria ya ubakaji; ukatili wa kutisha unaoonyeshwa na wananchi kwa wanaodhaniwa kuwa vibaka; wananchi kugoma kuendelea kulipa kodi mpaka waonyeshwe mchanganuo wa matumizi ya kodi zao za awali; serikali kugoma kufuta zile sheria arobaini za ukandamizaji kama ilivyoshauriwa na tume ya Nyalali miaka saba iliyopita; n.k. yote haya yanaonyesha kutoweka kwa amani katika jamii kwa kiwango cha hali ya juu.

Hata kama tutajaalia kuwa kweli Tanzania kuna amani bado nalazimika kumtuhumu BwanaNgatara kwa uzushi kwa kuingiza ghilba paleanapojaribu kuhusisha amani hiyo na sera za kidini zilizopo. Kwanza kabisa sera ya nchi kutoongozwa na dini yoyote na mtu kuwa na haki ya kuabudu kupitia dini aitakayo, iko kwenye makaratasi tu na si katika utekelezaji. Katika utekelezaji utafiti unaonyesha kuwa Wakristo wanapewa haki zaidi katika jamii na miongoni mwao Wakatoliki wanahadhi zaidi. Kwa kuwa jambo hili limeshazungumzwa na kuandikiwa sana, sioni sababu ya kujichosha kwa kulizungumzia kwa undani. Hata hivyo kabla sijaliruka labda tuingie huko mitaani tutizame mfano mmoja au miwili itakayotuwekea bayana utekelezaji wa sera hii.

Hivi karibuni vyombo vya habari vimepasha kwamba kijana mmoja wa Kiislamu alikamatwa na polisi huko mjini Korogwe na kufunguliwa mashtaka kwa kuandika katika baiskeli yake kuwa Yesu si Mungu. Ni nini tafsiri ya kitendo hiki? Tafsiri yake ni kuwa kwa mujibu wa serikali (jeshi la polisi ni idara nyeti na muhimu katika serikali) Yesu ni Mungu! Bila shaka msimamo huu ni wa kutia mashaka makubwa kwa serikali inayojitangaza kuwa haiongozwi na dini yoyote. Msimamo huu wa serikali umetiliwa nguvu na yaliyojiri katika mhadhara mkubwa ulioendeshwa hivi karibuni Jijini na Mwinjilisti wa Kijerumani Rainhard Bonke ambao pia ulihudhuriwa na baadhi ya watu mashuhuri wakiwamo Makamu wa Rais Dk. Omari Ali Juma, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Lt. Yusuph Makamba na mke wa Waziri Mkuu Bibi Esther Sumaye. Katika mhadhara huo tulibwagizwa kwa mapana na marefu kuwa Yesu ni Mungu wa Tanzania. 
 


Inaendelea toleo lijalo
 

Ubatizo kupitia TVZ?


 


Na Salahuddin Ahmad

KWA kipindi kirefu sasa Wazanzibari tumepigwa na bumbuwazi kutokana na vipindi pamoja na maneno ya watangazaji wa TV ya Zanzibar.

Bumbuwazi hili linazidi tunapowakuta Waheshimiwa Wawakilishi na Viongozi mbali mbali pasipo na kuelewa wakisemacho au wakiwa na malengo yao ya siri wakivisifu vipindi hivyo pamoja na sera ya TVZ.

Kwanza, kabla sijaielekea TVZ na vipindi vyake napenda kuwaelekea wale tunaowaitakidi kuwa viongozi wanaopaswa kuishauri serikali ambao hudai kuwa vipindi visivyo na muruwa vizuri vya TVZ ni "maendeleo’.

Kwa kweli kutarajia maendeleo kutoka kwa mtu asiyefahamu maendeleo ni sawa na kutaraji kuwa iko siku mbingu zitainyeshezea Zanzibar au pahala pengine mvua ya dhahabu na almasi!!

Wanasaikolojia na wanasosholojia wa Kimagharibi na sehemu nyingine za dunia hivi sasa wanalaumu utamaduni wa ngono (sex-culture) kuwa ni sababu kubwa ya maovu mbali mbali, ukosefu wa maadili na utu, mauaji, ubakaji, udhalilishaji wa watoto (n.k.) ambayo hivi sasa nchi za Kimagharibi zinataka kujinasua nayo bila ya mafanikio. 

Aidha inaaminiwa kuwa utamaduni huu utakuwa ndilo chimbuko kubwa la kuanguka kwa utamaduni huu kama ilivyokuwa huko nyuma kwa Ugiriki na dola ya Kirumi.

Leo waheshimiwa wanatwambia kuwa utamaduni wa ngono ni maendeleo!! Unatarajia nini kwa Mwakilishi anayeita maangamizi kuwa ni maendeleo kama si maangamizi makubwa zaidi?

TV Z mbali na vipindi vyake vichafu mbali mbali ambavyo hivi majuzi imejionesha wazi inakotuelekeza, imekuwa ikidai kuwa ikibinda nkoi ni utamaduni wa Mzanzibari sawa na maneno ya Mheshimiwa mmoja alipolinganisha ngoma hiyo na unyago.

Lakini hiyo nani aliyewahi kuona au kusimuliwa kuwa unyago ulikuwa ukichezwa hadharani penye machanganyiko wa wanawake na wanaume au watoto na wazee?

Siku ya tarehe 27 Julai, 1998 Jumatatu wakati wa baina ya saa 1.20-1.30 TVZ ilifikia onyesho lake la kuwaka (sijui kama litatokea jingine au la) ambapo picha za uchi na watu waliokuwa wakifanya liwati zilionyeshwa bila ya kificho wala woga. 

Kipindi ambacho kilikuwa kinaonyeshwa wakati huo kilipewa jina One World ambacho kilikuwa cha mada mbali mbali za sanaa na mambo ya mazingira.

Pamekuwepo na wasiwasi (wenye msingi madhubuti)kwamba nguvu za Ukristo zimekuwa zikiongezwa kwa upande wa Zanzibar. Wasiwasi huu sasa unachukua picha halisi baada ya TVZ kutumika kutoa vipindi maalum vya Kikristo kwa jina la Vipindi Maalum vya Mabadiliko (Turning Point).

Vipindi hivi ambavyo vimepelekea kufanyiwa mabadiliko programu ya vipindi vya kawaida vya TVZ vinavyooneshwa baina ya saa 1.00 na 2.000 usiku ni zawadi kutoka Shirika la Kimataifa la Utangazaji la Kikristo (CBN- Christina Broadcasting Network International).

Haijulikani pana kitu gani maalum kuanzia tarehe 2 Agosti hadi 9 kilichopelekea vipindi hivi kupatiwa nafasi maalumu kwenye TV za Serikali.

Jambo ambalo limewashangaza wengi ni kwanini TVZ ibadili ratiba yake nzima ya wiki ili kutoa nafasi kwa vipindi hivi ambavyo vimelengwa kwa watu wa rika tofauti (watoto hadi watu wazima) wakati siku ya Jumapili ina kipindi cha kawaida cha Kikristo - "Tumuabudu Mungu".

Hii ni sawa n a Waislamu kutengewa Ijumaa kwa vipindi vinavyoaminiwa na TVZ kuwa ni vya Kiislamu (kulingana na aina yaUislamu wa SMZ).

Hali hii mara nyingi inahusishwa na ahadi ya Mkurugenzi wa TVZ Hassan Mitawi kuwa ana nia ya kuifanya TVZ kuwa katika hali ya "ushindani" na TV nyingine na ndio maana hata watangazaji wa kike wote wakatakiwa kuvua vitambaa vya kichwa ukiwacha siku ya Ijumaa ambayo huvaa vitambaa hivyo. Kwa kuwa ni vigumu kuuvua Ukristo na mila au utamaduni wa Magharibi tuna wasiwasi kuwa ushindani wa mitawi usije ukawa ni kuibatiza Zanzibar kwa kutumia chomo cha umma.
 

Juu

YALIYOMO



TAHARIRI

Milipuko ya mabomu Dar, Nairobi: Waislamu walaani vyombo vya habari
Na Mwandishi wetu

Wanawake Waislamu Tanga waazimia kupigania haki
Na Ibn Masoud, Tanga

Marekani yashambulia Sudan, Afghanistan

Maoni: Kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani:
Huu ni unazi au sehemu ya mtandao?

Nguruwe kuzua tafrani Kibamba
Na Mwandishi Wetu

Sheikh Mbukuzi ataka vijana wajihadhari  na utamaduni wa Magharibi
Na Said Shariff

TAMPRO kuzindua Tawi Iringa
Na Mwandishi Wetu

Tamasha la kusaidia wagonjwa laanza Moro
Rajab Rajab na Mussa Ally, Morogoro

Kambi ya matibabu ya Macho Tanga yaanza
Na Mwandishi Wetu

MAONI: Kanisa mshiriki wa ukandamizaji

Porojo za Ngatara
Na J. Hussein

Ubatizo kupitia TVZ?
Na Salahuddin Ahmad

Waislamu Kosovo waangamizwa

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA 
SHIRIKISHO LA TANZANIA -2

Hoja binafsi: Uhusiano na Marekani usituletee maafa
Na Said Rajab

Darasa la Muhammad (s.a.w)

Wanamume toeni haki  za wanawake kuepusha ufisadi
Na Halima Issa Ndabi,  Mwanza

MAKALA: Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu,  ni uzushi mtupu! - 2
Na Muhibu Said

Mwanaadamu alipofikia
Na Nineka B.N., Geita

Mafunzo ya Quran

Barua za wasomaji

Mashairi

Masomo ya dini ya Kiislam

Chakula na Lishe

Matangazo
 

 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org

Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita