AN-NUUR
Na.163 Rabiul Thani 1419, Agosti 21 - 27, 1998
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
Maoni

Kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani:

  • Huu ni unazi au sehemu ya mtandao?
  • Tufikiri kwa akili zetu, pamoja na umasikini wetu

  •  


Mara tu baada ya tukio la kulipuka mabomu katika Balozi za Marekani Dar es Salaam na Nairobi; Marekani ilitamka wazi kwamba haitakurupuka na kuanza kunyoshea watu vidole kutokana na fundisho la Oklahoma. Vyombo vya dola 

hapa kwetu navyo vikawataka wananchi watulizane waviache vyombo husika vifanye kazi yake.

Wengi tuliheshimu agizo na maelekezo haya ya vyombo vya Serikali yetu tukufu.

Hata hivyo kadri siku zilivyokuwa zikienda inaonekana jambo hili ama limetawaliwa na unazi au tukio lenyewe lote toka awali na yote yanayoendelea hivi sasa ni kitendawili tata ambacho kuteguliwa kwake kutahitaji watu razini wenye kuyazamia mambo kwa kina na akili huru bila hisia za mapenzi au chuki zisizo na sababu.

Gazeti moja la kila siku katika toleo lake la Jumapili, Agosti 9, likifungua ukurasa wa kutoa habari za watuhumiwa liliandika "Mujahidina akamatwa Kenya’. Nalo gazeti moja la Kiingereza la kila wiki katika toleo lake la Agosti 10-16,lilikuja na taarifa isemayo: "Police in Arusha were at the weekend said to be on the tracks of a group of Muslim fundamentalists who arrived in the town late on Friday, spent the night in a mosque before leaving for the Namanga border post for onward travel into Kenya on Saturday morning; as the investigations into the bomb attacks on U.S. Embassies in Nairobi and Dar es Salaam gained momentum." 

Taarifa za gazeti lingine zikasema kwamba mtu mmoja mwenye asili ya Kiarabu anashikiliwa na polisi kwa kuhusika na tukio hilo. Kwa mujibu wa taarifa za gazeti hilo katika toleo lake Na. 1681 la Agosti 11, Muarabu huyo alikamatwa baada ya kutoka hotelini kwake Arusha na kwenda kuswali msikitini ambako alikaa sana kabla ya kutoka na kuelekea Namanga.

Katika tarehe hiyo hiyo gazeti moja la jioni katika toleo lake Na. 0585 likatoa picha ya Osama bin Laden ikiwa na bango: Hili ndilo Gaidi Lenyewe. Huku pembeni yake kukiwa na habari inayoeleza kwamba Waarabu watatu walionekana wakipiga kwa siri picha za video jengo la Ubalozi wa Marekani mjini Nairobi siku tatu kabla ya tukio.

Gazeti la Daily Nation katika toleo lake No. 11729 la Jumatano Agosti 19, likielezea tukio la kupekuliwa hoteli moja huko Nairobi, kuhusiana na tukio hili liliandika:

FBI scoops on bombers’ hotel kama kichwa cha habari kisha likaanza kwa kusema: "FBI special agents wearing bullet-proof vests and armed with rifles yesterday raided the hotel where the Nairobi bomb was made.’

Wakati hata FBI wenyewe hawajafikia japo hatua tu ya kusema kwamba ushahidi uliopatikana unatosheleza kuwafikisha watuhumiwa mahakamani Daily Nation linasema; "The two rooms at the Hill Top Hotel were rented by four bombers -two Palestinians, an Egyptian and a Saudi Arabian....On that day, they completed the final assembly in pick-up truck and drove the bomb across the city."

Maelezo ya gazeti hili kama yalivyoandikwa na Bw. Stephen Muiruri hayazungumzii tena suala la watuhumiwa na upelelezi bali kauli thabiti ya kuthibiti kuhusika kwa watuhumiwa.

Haya yanafanyika wakati Marekani yenyewe ilisema kwamba haitafanya papara kuwatuhumu watu kutokana na fundisho la Oklahoma.

Kisicho eleweka hapa ni uhusiano wa kauli hiyo ya Marekani na mwenendo wa vyombo vya habari. Kwani toka awali huku Marekani ikitoa tahadhari hiyo; vyombo vya habari navyo ndani ya Markeani kwenyewe na huku kwetu; wakati huo huo vikaanza kuimba kibwagizo cha Osama bin Laden.

Pengine kutokana na kile ambacho chaweza kuitwa sayansi ya Utukizi (Science of coincidence); mtuhumiwa wa kwanza akakamatwa alipotaka kuingia Afghanistan. Na pengine kwa sayansi hiyo hiyo ya utukizi, vyombo vya habari vikatuambia kwamba wenzake wawili walishavuka na kuingia Afghanistan kutoa taarifa ya kazi kwa Osama bin Laden.

Ukirejea nyuma kwa sayansi hiyo ya utukizi (Science of Coincidence); vyombo vya habari ndani ya Marekani na huku kwetu toka mapema kabisa kabla ya uchunguzi kuanza; walishawataja Waarabu; Waislamu Usama bin Laden na Afghanistan.

Sura ya hali hii inaleta utata mkubwa.Kwamba je; v yombo vya habari vinafanya hivyo kwa unazi na ushabikiki tu, au ni sehemu ya mtandao wa vyombo rasmi vinavyohusika na suala hili!

Picha inayojitokeza hapa ni kana kwamba toka awali mkosa alishajulikana na iwavyo vyovyote lazima awe huyo huyo; na pengine hata adhabu atakayopewa ishawekwa.

Uongo, wizi, ujambazi, uzinzi na sifa nyingine mbaya haziwezi kuwa ni sifa za kabila au taifa. Kwa hiyo hata kama itatokea kutokana na mazingira na malezi watu wengi katika jamii fulani wakawa na tabia isiyo njema basi haiwezi kusemwa kwamba hiyo ni moja ya sifa za kabila au taifa hilo. Au kwa mfano ukisemwa wizi ikawa sawa na kusema kabila fulani au ukitaja kabila hilo ikawa ni sawa na kusema mwizi. Uovu si suala la mila ya watu.

Ireland juzi hapa limelipuliwa bomu na kuuwa makumi ya watu. Tukio hilo ni mlolongo wa matokeo ya ugomvi wa muda mrefu kati ya Wakatoliki na Waprotestanti, kutokana na ugomvi huo mamia ya watu walishauliwa, mali kuharibiwa na watu wengi kutiwa vilema.

Hatusikii magaidi hawa wa Ireland wakitajwa kwa dini zao - yaani Wakatoliki au Waanglikana. Bali hutajwa kwa vyama vyao-Republican (Wakatoliki) au Unionists (Waprotestanti). 

Ndani ya Ireland yenyewe si Wakatoliki wala Waprotestanti wanaoitwa magaidi ya Kikatoliki au au magaidi ya Kiprotestanti. Wala haiwi ukisema Mzungu maana yake gaidi au gaidi maana yake Mzungu.Na kwa hiyo vile vile huku kwetu hatuwaiti Wakatoliki au Waanglikana magaidi kutokana na ugaidi unaofanyika Ireland. 

Tunatenganisha kati ya uovu wa Magaidi na Ukristo au Uzungu.

Wazungu walio Wakristo wa Afrika ya Kusini walikuwa wakiendesha ubaguzi, udhalimu na mauaji dhidi ya Waafrika walio wengi. Aidha walikuwa wakiendesha ugaidi dhidi ya nchi huru jirani.

Uovu wao huo haukufanywa sababu ya kulipa kanisa na Wazungu wote nembo ya ugaidi.

Waarabu walikuwa ni watu wa kati katika biashara ya utumwa. Wenyewe walikuwa Wazungu Wakristo. Walipeleka watumwa Amerika na Carribean kwenye mashamba yao. Hata meli zao za kubebea watumwa zilipewa majina matakatifu ya Kikristo. Na wakati mwingine kabla ya meli kuanza safari kupeleka watumwa ilibarikiwa kwanza na kiongozi mkuu wa Kanisa. Lakini leo, hatusikii - ‘Christian Slave Trade’ au hata ‘European Slave Trade’. Limetafutwa jina la kijiografia - "Trans-Atlantic Slave Trade". Ukisema mkristo, mtu hafikirii Uzungu wala ukitaja Uzungu mtu hafikirii utumwa. Kanuni hii hubadilika anapohusika Mwislamu!

Mwaka 1994 yalifanyika mauaji ya kutisha Rwanda. Malaki ya watu waliuliwa. Kwa kuzingatia hadhi ya makanisa na kwamba watu wa kanisa hawawezi kuwa wauaji. Maelfu ya watu walikimbilia makanisani. Lakini huko huko ndani ya kanisa viongozi wa Makanisa walishiriki kupelekea watu hao kuangamizwa. Hatujasikia mtu akisema Ukatoliki ni uuaji. Ukitaja mauaji ya Rwanda watu hawawafikirii Wakatoliki. Wala ukitaja Mkatoliki mtu hajengi taswira ya jitu kali lililojaa damu mikononi likiendesha ‘greda’ juu ya miili ya Wanyarwanda ndani au nje ya Kanisa. Watu hawajengi taswira hiyo kwa sababu propaganda kupitia vyombo vya habari haijawapeleka huko. Ila inapokuja kwa Muislamu busara hii hupotea. Uislamu ndio Uarabu na Uarabu ndio ugaidi, kuuwa na ukatili!

Rais Chiluba wakati anagombea Urais kwa mara ya kwanza aliwakusanya Wazambia na akawataka wampe kura ili wasaidiane kuondoa umasikini wakati huo hali ya uchumi ikiwa mbaya sana. Lakini mara aliposhinda tu na kukalia kiti cha Urais, akatangaza kwamba Zambia ni taifa la Kikristo, agenda ambayo haikuwepo katika kampeni zake. Hakuna aliyesema neno.

Wakati huo huo na katika kipindi hicho hicho chama cha FIS Algeria kiliendesha kampeni kwamba kama kitapewa uongozi kitapiga marufuku pombe, disco, "night clubs", Casino, mashindano ya Miss Algiers na Hijab ndiyo vazi rasmi la wanawake wa nchi hiyo. Vilikuwepo vyama vingine katika kampeni hizo ambavyo vilitoa ahadi kwamba vikiingia madarakani Mini-sketi zitaendelea, mkorogo, madisco na ulevi rukhsa n.k.

Wananchi wa Algeria wakachagua FIS; hilo likawa tatizo Demokrasia kwa viwango vyote vya Ulaya na Marekani vikawekwa kando.

Ugaidi wenye kuteketeza mali na roho za watu ni uovu wa kulaaniwa na kila mtu mwenye chembe ya utu iliyosalia katika ubinaadamu wake. Na hata kama mtu au kundi la watu limeonewa hiyo siyo njia ya kiungwana ya kuwasilisha hisia zao.

Baada ya kuanguka ukomunisti Marekani ilitamka wazi kwamba Uislamu ndiye adui aliyesalia. Juhudi kubwa imefanywa kupitia vyombo vya habari kupandikiza hisia hizo. Matokeo yake nchi zote duniani zinaimba wimbo huo bila kujali ukweli.

Mara tu lilipotokea tukio la kutisha na la kusikitisha la kulipuliwa Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam na Nairobi, kabla hata ya uchunguzi.kuanza vyombo vya habari vikaanza kuhusisha mabomu hayo na Wasudan; Iraq, Waarabu, Waislamu.

Magazeti mengine yakafikia hata kutaja majina ya watu kwa kusema "Hili ndio gaidi lenyewe"; wakati hata uchunguzi wenyewe haujaanza au ndio kwanza unaanza. Gazeti moja nchini katika toleo lake la Agosti 13, Toleo Na. 1684 katika kuitikia kibwagizo cha Wamarekani likaandika kwamba "katika maeneo ya Kariakoo kuna Wairani, Walebanon; na Wapalestina ambao baadhi yao wamejenga majumba makubwa yakiwa na sehemu iliyo chini ya ardhi lakini kazi yao hasa wanayofanya nchini haieleweki." Hii ilikuwa ni sehemu ya habari inayoelezea msako unaoendelea kuwasaka watuhumiwa wa mlipuko wa bomu katika Ubalozi wa Marekani.

Lakini gazeti halioni wasiwasi juu ya zile taasisi za kidini zenye viwanja vya ndege ambavyo ndege toka nje hutua bila kufanyiwa ukaguzi wowote! Kwa nini wasitiliwe shaka hawa kuwa wanahusika na milipuko ile. Halikadhalika Mwandishi hakuona sababu ya kuwa na wasiwasi na zile taasisi zenye tume za majeshi ya vita (armed forces)!

Katika nchi hii Waislamu ni sehemu ya raia ambao kwa uchache waweza kusema kwamba ni nusu ya watu wote (50%). Lakini maadhali imekwishapigwa propaganda kwamba Waislamu ni adui basi hata kama Waislamu walishiriki kumuondoa Mkoloni; na wanakaa vyema kwa salama na amani na ndugu zao wa dini nyingine na wakapiga kura zao kuiweka serikali madarakani; waweza kuuliwa na hata kufanya tu ule uchunguzi juu ya kuuliwa kwao kunapuuzwa.

Juhudi pekee itakayofanyika ni kuwapa jina - Siasa kali.Waislamu wenye kuvuruga amani n.k. Hilo likishafanyika, hakuna wasiwasi tena, kwani Marekani atahoji?

Leo hapa wamedhalilishwa wanawake, lakini si kitu kwani Bwana Mkubwa hatahoji maadhali wamepewa nembo ya Uislamu.

Marekani leo inaishutumu Afghanistan au tuseme Talaban na inaitafutia kila sababu. Moja ya kisingizio ni kwamba inavunja haki za binaadamu. Wanawake lazima hijab (za Niqaab); marufuku shule za mchanganyiko; n.k. uhalali wa sheria za Talaban juu ya namna wanawake wanavyotakiwa wawe ni sawa na Saudia au Saudia ni zaidi. Marekani haina ugomvi na Saudia; kwanini! Hilo hatuhoji. Maadhali Bwana Mkubwa anasema Talaban na sisi huku wimbo ni huo huo. 

Sudan inalea magaidi; kwanza yako wapi na yanafanya nini na yule anayemlea na kumpa John Garang kibri je; hatuna muda wa kufikiri.

Huko nyuma nchi hii iliwahi kuwa na heshima sana. Si kwa mali bali kwa msimamo wetu wa kufikiri na kuyapima mambo sisi wenyewe.

Mwalimu Nyerere hakuamini kwamba masikini hawezi kufikiri. Aliamini kwamba akili ya mtu haitegemei utajiri wake na ubabe wake. Kwahiyo kama nchi hatukufikiri kwa akili ya Marekani au Urusi. Mara kadhaa tulitofautiana nazo; Chambilecho msemo wa masikini jeuri.

Leo tumefikia hatua tunaamua hatuna uwezo wa kufikiri ila wengine wafikiri kwa niaba yetu. Na nchi yenye nguvu kubwa kijeshi na tajiri kama Marekani inaposema kwamba nchi masikini kama Tanzania ni rafiki wanaelewana; maana yake ni kwamba anachosema Marekani ndio msimamo wa Tanzania.
 

Juu

YALIYOMO



TAHARIRI

Milipuko ya mabomu Dar, Nairobi: Waislamu walaani vyombo vya habari
Na Mwandishi wetu

Wanawake Waislamu Tanga waazimia kupigania haki
Na Ibn Masoud, Tanga

Marekani yashambulia Sudan, Afghanistan

Maoni: Kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani:
Huu ni unazi au sehemu ya mtandao?

Nguruwe kuzua tafrani Kibamba
Na Mwandishi Wetu

Sheikh Mbukuzi ataka vijana wajihadhari  na utamaduni wa Magharibi
Na Said Shariff

TAMPRO kuzindua Tawi Iringa
Na Mwandishi Wetu

Tamasha la kusaidia wagonjwa laanza Moro
Rajab Rajab na Mussa Ally, Morogoro

Kambi ya matibabu ya Macho Tanga yaanza
Na Mwandishi Wetu

MAONI: Kanisa mshiriki wa ukandamizaji

Porojo za Ngatara
Na J. Hussein

Ubatizo kupitia TVZ?
Na Salahuddin Ahmad

Waislamu Kosovo waangamizwa

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA 
SHIRIKISHO LA TANZANIA -2

Hoja binafsi: Uhusiano na Marekani usituletee maafa
Na Said Rajab

Darasa la Muhammad (s.a.w)

Wanamume toeni haki  za wanawake kuepusha ufisadi
Na Halima Issa Ndabi,  Mwanza

MAKALA: Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu,  ni uzushi mtupu! - 2
Na Muhibu Said

Mwanaadamu alipofikia
Na Nineka B.N., Geita

Mafunzo ya Quran

Barua za wasomaji

Mashairi

Masomo ya dini ya Kiislam

Chakula na Lishe

Matangazo
 

 

 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org

Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita