|
Na.163 Rabiul Thani 1419, Agosti 21 - 27, 1998 |
|
THE REGISTERED TRUSTEES
OF THE SOCIAL POLITICAL DEVELOPMENT TRUST (AFORD)
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA -2
Uhuru wa mtu kwenda atakako 15. (1) Kila raia wa Shirikisho anayo haki ya kwenda kokote katika Shirikisho na kuishi katika sehemu yoyote , kutoka nje ya nchi na kuingia, na pia haki ya kutoshurutishwa kuhama au kufukuzwa kutoka katika Shirikisho. (2) Sheria yoyote yenye madhumuni ya- kuweka mipaka kwa matumizi ya uhuru wa mtu kwenda anakotaka ili- (a) kuwezesha upelelezi wa kosa la jinai; (b) kutekeleza hukumu au amri ya mahakama; au (c) kumlazimisha mtu kutimiza kwanza wajibu wowote anaotakiwa na sheria kuutimiza; au (d) kulinda manufa ya umma kwa jumla au kuhifadhi maslahi fulani mahususi au maslahi ya sehemu fulani ya umma, ambayo yataelezwa bayana kwenye Sheria hiyo haitahesabiwa kuwa ni batili au ni kinyume cha ibara hii. Haki ya Uhuru wa Mawazo Uhuru wa Maoni 16. (1) kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati. (2) Kila raia anayo uwezo wa kutafuta na haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na dunia kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii. Uhuru wa mtu kuamini dini atakayo 17.(1) Kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru kubadilisha dini au imani yake. (2) Bila ya kuathiri sheria za kulinda amani za Shirikisho, kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi; na shughuli na uendeshaji wa Jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za Mamlaka ya Nchi. (3) Kila palipotajwa neno "dini" katika ibara hii ifahamike kwamba maana yake ni pamoja na madhehebu ya dini, na maneno mengineyo yanayofanana au kuambatana na neno hilo. Uhuru wa mtu kushirikiana na wengine 18. (1) Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za kulinda amani, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo. (2) Bila ya kujali masharti ya ibara ndogo ya (1) haitakuwa halali kwa chama cha siasa kuandikishwa ambacho kutokana na Katiba au sera yake- (a) kina kusudia kukuza au kupigania maslahi ya- (I) imani au kundi lolote la dini; (ii) kundi lolote la kikabila, pahala watu watokeapo, rangi au jinsia; (iii) eneo fulani tu katika sehemu yoyote ya Shirikisho; (b) kinapigania kuvunjwa kwa Shirikisho; (c) kinakubali au kupigania matumizi ya nguvu au mapambano kama njia za kufikia malengo yake ya kisiasa; (d) kinapigania au kina kusudia kuendesha shughuli zake za kisiasa katika sehemu moja tu ya Shirikisho. (e) hakiruhusu uongozi wake kuchaguliwa kwa vipindi na kwa njia za kidemokrasia. (3) Bunge laweza kutunga sheria inayoweka masharti yatakayohakikisha kuwa vyama vya siasa vinazingatia mipaka na vigezo vilivyowekwa na masharti ya ibara ndogo ya (2) kuhusu uhuru, haki ya watu kushirikiana na kujumuika. (4) Bila kuathiri ibara ndogo ya (2) ni marufuku kwa mtu yeyote kulazimishwa kujiunga na chama chochote cha Siasa, au chama chochote cha siasa kukataliwa kusajiliwa kwa sababu tu ya itikadi au falsafa. (5) Itakuwa ni marufuku kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa Mahakama ya Shirikisho, Jaji wa Mahakama Kuu, Hakimu wa ngazi yoyote kujiunga na chama chochote cha Siasa, isipokuwa tu kwamba atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara ya 19 ya Katiba hii. Haki ya kupiga kura 19.(1) Kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka kumi na minane anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofanywaTanzania na wananchi. Haki hii itatumiwa kwa kufuata masharti ya ibara ndogo ya (2) pamoja na masharti mengineyo ya Katiba hii na ya Sheria inayotumika nchini Tanzania kuhusu mambo ya uchaguzi. (2) Bunge laweza kutunga sheria na kuweka masharti yanayoweza kuzuia raia asitumie haki ya kupiga kura kutokana na yoyote kati ya sababu zifuatazo, yaani raia huyo- (a) kuwa na uraia wa nchi nyingine; (b) kuwa na ugonjwa wa akili; (c) kutiwa hatiani kwa makosa fulani ya jinai; (d) kukosa au kushindwa kuthibitisha au kutoa kitambulisho cha umri, uraia au uandikishwaji kama mpiga kura. Mbali na sababu hizo hakuna sababu nyingine yoyote inayoweza kumzuia raia asitumie haki ya kupiga kura. (3)Bunge litatunga Sheria ya Uchaguzi na kuweka masharti kuhusu mambo yafuatayo- (a) utaratibu wa kuandikisha wapiga kura katika uchaguzi wa Rais wa Shirikisho, Wabunge, majimbo ya uchaguzi wa Tanganyika na Zanzibari, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. (b) kutaja sehemu na nyakati za kuandikisha wapiga kura na kupiga kura; (c) utaratibu wa kumwezesha mpiga kura aliyejiandikisha sehemu moja kupiga kura sehemu nyingine na kutaja masharti ya utekelezaji wa utaratibu huo; (d) Kutaja kazi na shughuli za Tume za Uchaguzi na utaratibu wa kila uchaguzi ambao utaendeshwa chini ya uongozi na usimamizi wa Tume za Uchaguzi katika Shirikisho, Tanganyika na Zanzibar. Uhuru wa kushiriki shughuli za umma 20. (1) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ya 19, ya 39 na ya 65 ya Katiba hii kuhusiana na masharti ya kuchagua na kuchaguliwa, au kuteua na kuteuliwa kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi , kila raia wa Shirikisho anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa. (2) Kila raia anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomhusu yeye, maisha yake au yanayolihusu Taifa. Wajibu wa kufanya kazi Wajibu wa Haki ya kufanyakazi 21. (1) Kila mtu anayo Wajibu wa kufanyakazi. (2) Kila raia anastahili fursa ya haki sawa, kwa masharti ya usawa, ya kushika nafasi yoyote iliyo chini ya Mamlaka ya Nchi. Haki ya kupata ujira wa haki 22. (1) Kila mtu, bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote, anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake, na watu wote wanaofanya kazi kulingana na uwezo wao watapata malipo kulingana na kiasi na sifa kazi wanayoifanya. (2) Kila mtu anayefanya kazi anastahili kupata malipo ya haki. Haki ya kumiliki mali 23.(1) Kila mtu anayo haki ya kumiliki mali na haki ya hifadhi kwa mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria. (2) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (1), ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang’anywa mali yake kwa madhumuni ya kuitaifisha au madhumuni mengineyo kwa manufaa ya Taifa bila ya idhini ya sheria ambayo inaweka masharti ya kutoa fidia inayostahili. Wajibu wa Jamii Wajibu wa kushiriki kazini 24. (1) Kazi pekee ndiyo huzaa utajiri wa mali katika jamii, ndilo chimbuko la ustawi wa wananchi na kipimo cha utu. Kila mtu anao wajibu wa- (a) kushiriki kwa kujituma na kwa uaminifu katika kazi halali na ya uzalishaji mali; na (b) kutimiza nidhamu ya kazi na kujitahidi kufikia malengo ya uzalishaji ya binafsi na yale ya pamoja yanayotakiwa au yaliyowekwa na sheria. (2) Bila ya kujali masharti ya ibara ndogo ya (1), hakutokuwapo na kazi ya shuruti katika Shirikisho. (3) Kwa madhumuni ya ibara hii, na katika Katiba hii kwa jumla, ifahamike kwamba kazi yoyote haitahesabiwa kuwa ni kazi ya shuruti endapo kazi hiyo, kwa mujibu wa sheria ni- (a) kazi inayobidi ifanywe kutokana na hukumu au amri ya mahakama. (b) kazi inayobidi ifanywe na askari wa jeshi lolote katika kutekeleza majukumu yao; (c) kazi ambayo mtu yeyote inabidi aifanye kutokana na kuwapo hali ya hatari au baa lolote linalotishia uhai wa ustawi wa jamii; Wajibu wa kutii sheria za nchi 25. (1)Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii Katiba hii na sheria za Shirikisho. (2) Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria za nchi. (3) Bila kuathiri masharti ya Ibara hii kila mtu ana haki ya kupinga kufutwa kwa Katiba hii kinyume na utaratibu uliowekwa na Katiba hii. Kulinda mali ya umma 26.(1) Kila mtu ana wajibu wa kuiheshimu mali ya mtu mwingine, kulinda mali asilia ya Shirikisho, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi. Ulinzi wa taifa 27. (1) Kila raia ana wajibu wa kulinda, kuhifadhi na kudumisha uhuru, mamlaka , na umoja wa taifa. (2)Bunge laweza kutunga Sheria zinazofaa kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kutumikia katika majeshi na katika ulinzi wa taifa. (3) Kwa mujibu wa katiba hii ni marufuku kwa mtu yeyote kutia sahihi mkataba wa kukubali kushindwa vita na kulitoa taifa kwa mshindi, wala kuridhia au kutambua kitendo cha uvamizi au mgawanyiko wa Shirikisho au wa sehemu yoyote ya ardhi ya eneo la Taifa na; (4) Bila ya kuathiri Katiba hii hakuna mtu atakayekuwa na haki ya kuwazuia raia wa Shirikisho kupigana vita dhidi ya adui yeyote anayeshambulia nchi. (5) Uhaini kama unavyofafanuliwa na Ibara ndogo ya 6 ya Ibara hii utakuwa ni kosa la juu kabisa dhidi ya Shirikisho. (6) Uhaini maana yake ni kitendo cha raia wa Shirikisho (a) Kuonyesha nia ya kutenda vitendo vinavyokusaidia kuigawa Tanzania katika nchi tofauti. (b) Kumuua, kujaribu kumuua au kula njama ya kumuua Rais wa Shirikisho , Waziri Mkuu wa Tanganyika ama Waziri Mkuu wa Zanzibar au (c) Kuanzisha vita au kusaidia adui katika vita dhidi ya Shirikisho ama sehemu yoyote ya Shirikisho. Masharti ya Jumla Haki na wajibu muhimu 28. (1) Kila mtu katika Shirikisho anayo haki ya kufaidi haki za msingi za binadamu, na matokeo ya kila mtu kutekeleza wajibu wake kwa jamii, kama zilivyofafanuliwa katika ibara ya 10 hadi ya 27 za sehemu hii ya sura hii ya Katiba. (2) Kila mtu katika Shirikisho anayo haki ya kupata hifadhi sawa chini ya Sheria za Shirikisho. (3) Raia yeyote wa Shirikisho hatakuwa na haki, hadhi au cheo maalum kwa misingi ya ubaguzi. (4) Ni marufuku kwa sheria yoyote kutoa haki, hadhi inayotumika katika Shirikisho au cheo maalum kwa raia yeyote wa Shirikisho kwa msingi wa ubaguzi. (5) Ili watu wote waweze kufaidi haki na uhuru vilivyotajwa na Katiba hii kila mtu ana wajibu wa kutenda na kuendesha shughuli zake kwa namna ambayo haitaingilia haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma. 29. (1) Ifahamike kwamba masharti yaliyomo katika sehemu hii ya Katiba hii, yanayofafanua misingi ya haki, uhuru na wajibu wa binadamu, haibatilishi sheria yoyote iliyotungwa wala kuzuia sheria yoyote kutungwa au jambo lolote halali kufanywa kwa mujibu wa sheria hiyo, kwa ajili ya- (a) kuhakikisha ulinzi, usalama wa jamii na amani katika jamii; (b) kuhakikisha utekelezaji wa hukumu au amri ya mahakama iliyotolewa katika shauri lolote la madai au kesi ya jinai; (c) kulinda sifa, kutunza heshima, mamlaka na uhuru wa mahakama; (d) kuweka vigezo vya uanzishaji, uendeshaji na shughuli za vyama na mashirika ya watu binafsi nchini; (2) mtu yeyote anayedai kuwa sharti lolote katika sehemu hii ya sura hii au katika sheria yoyote inayohusu haki yake au wajibu kwake, limevunjwa, linavunjwa au inaelekea litavunjwa na mtu yeyote popote katika Shirikisho, anaweza kufungua shauri katika Mahakama ya Shirikisho au Mahakama Kuu ya Tanganyika au Mahakama Kuu ya Zanzibar. (3) Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii, Mahakama ya Shirikisho au Mahakama Kuu ya Tanganyika au Zanzibar itakuwa na mamlaka ya kusikiliza kwa mara ya kwanza na kuamua shauri lolote lililoletwa mbele yake kwa kufuata ibara hii; na Bunge laweza kuweka sheria kwa ajili ya kusimamia utaratibu wa kufungua mashauri kwa mujibu wa ibara hii; (4) Endapo katika shauri lolote inadaiwa kwamba sheria yoyote iliyotungwa au hatua yoyote iliyochukuliwa na Serikali au mamlaka nyingine inafuta au inakatiza haki, uhuru na wajibu muhimu zitokanazo na ibara ya 10 hadi 27 za Katiba hii, na Mahakama ya Shirikisho, Mahakama Kuu ya Tanganyika au Zanzibar inaridhika kwamba sheria au hatua inayohusika, kwa kiwango inachopingana na Katiba ni Batili au kinyume cha Katiba basi Mahakama ya Shirikisho au Mahakama Kuu ya Tanganyika au Mahakama Kuu ya Zanzibar itatamka kuwa sheria au hatua hiyo ni batili. Madaraka ya Pekee ya Mamlaka ya Nchi Ukiukaji wa haki na uhuru 30. (1) Mbali na masharti ya ibara ya 29(1), sheria yoyote iliyotungwa na Bunge haitakuwa batili kwa sababu tu kwamba inawezesha hatua kuchukuliwa wakati wa hali ya hatari, ambazo zinakiuka masharti ya ibara ya 12 na ya 13 za Katiba hii. (2) Ni marufuku kwa hatua zilizotajwa katika ibara ndogo ya (1) ya ibara hii kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria yoyote wakati wa hali ya hatari, isipokuwa tu kwa kiasi ambacho ni lazima na halali kwa ajili ya kushughulikia hali iliyopo wakati wahali ya hatari. (3) Ifahamike kwamba masharti yaliyomo katika ibara hii hayataidhinisha mtu kunyang’anywa haki yake ya kuwa hai. (4) Kwa madhumuni ya ibara hii na ibara zifuatazo za sehemu hii "wakati wa hali ya hatari" maana yake ni kipindi chochote ambapo Tangazo la Hali ya Hatari, lililotolewa na Rais kwa kutumia uwezo aliopewa katika ibara ya 31, linatumika. Madaraka ya kutangaza hali ya hatari 31. (1) Bila ya kuathiri Katiba hii, au sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo, Rais aweza kutangazahali ya hatari katika Shirikisho au katika sehemu yake yoyote. (2) Rais aweza tu kutangaza kuwa kuna hali ya hatari iwapo (a) Shirikisho liko katika vita; au ((b) kuna hatari hasa kwamba Shirikisho linakaribia kuvamiwa na kuingia katika hali ya vita; au (c) kuna hatari dhahiri na kubwa, kiasi kwamba amani ya jamii itavurugika na usalama wa raia kutoweka katika Shirikisho au sehemu yake yoyote ambayo haiwezi kuepukika isipokuwa kwa kutumia mamlaka ya pekee; au (d) karibu kutatokea tukio la hatari au tukio la balaa au baa la kimazingira ambalo linatishia jamii au sehemu ya jamii katika Shirikisho. (3) Endapo inatangazwa kwamba kuna hali ya hatari katika Shirikisho nzima, au katika Tanganyika nzima au Zanzibar nzima, Rais atatuma mara moja nakala ya tangazo hilo kwa Spika wa Bunge ambaye ataitisha mkutano wa Bunge, ndani ya siku zisizozidi kumi na nne, ili kuitafakari hali ya mambo na kuamua kupitisha au kutopitisha azimio, litakaloungwa mkono na kura za wajumbe wasiopungua theluthi mbili ya wajumbe wote, la kuunga mkono tangazo la hali ya hatari lililotolewa na Rais. (4) Tangazo la hali ya hatari lililotolewa na Rais kwa mujibu wa ibara hii litakoma kutumika. (a) wakati wowote ambapo mkutano wa Bunge utalitangua tangazo hilo kwa azimio litakaloungwa mkono na kura za wajumbe wasiopungua theluthi mbili ya wajumbe wote. (b) endapo zitapita siku kumi na nne tangu tangazo lilipotolewa kabla ya kupitishwa azimio lililotajwa katika ibara ndogo ya (3); (c) iwapo litafutwa na Rais; (d) baada ya kupita muda wa miezi mitatu tangu tangazo hilo lilipotolewa; isipokuwa kwamba kikao cha Bunge chaweza, kabla ya muda wa miezi mitatu kupita, kuongeza mara kwa mara muda wa tangazo hilo kutumika kwa vipindi vya miezi mingine mitatu kwa azimio litakaloungwa mkono na kura za wajumbe wa kikao hicho wasiopungua theluthi mbili ya wajumbe wote, isipokuwa kwamba kipindi cha hali ya hatari hakitazidi miezi kumi na mbili. (5) Bunge laweza kutunga sheria inayoweka masharti kuhusu nyakati na utaratibu ambao utawawezesha watu fulani wenye kusimamia utekelezaji wa mamlaka ya Serikali katika sehemu mahususi za Shirikisho kumuomba Rais kutumia madaraka aliyopewa na ibara hii kuhusiana na yoyote kati ya sehemu hizo endapo katika sehemu hizi kunatokea yoyote kati ya hali zilizotajwa katika aya ya (c) na (d) za ibara ndogo ya (2) na hali hiyo haivuki mipaka ya sehemu hizo; na pia kwa ajili ya kufafanua utekelezaji wa mamlaka ya Serikali wakati wahali ya hatari. (6) Kwa madhumuni ya kuondoa mashaka juu ya ufafanuzi au utekelezaji wa masharti ya ibara hii, masharti ya sheria iliyotungwa na Bunge inayohusu utangazaji wa hali ya hatari kama ilivyotajwa katika ibara hii, yatatumika tu katika sehemu ya Shirikisho ambapo hali hiyo ya hatari imetangazwa. SURA YA PILI MADARAKA YA UMMA 32 1. Mamlaka yote ya nchi yatakuwa mikononi mwa wananchi na kila serikali itakayoundwa itatokana na ridhaa ya wananchi; ikumbukwe kuwa itakuwa ni marufuku kuwa na Serikali ya Mapinduzi katika shirikisho, Tanganyika na Zanzibar. 2. Kwa mujibu wa Katiba hii itakuwa marufuku kwa mamlaka yoyote katika shirikisho kutoa hati ya uraia kwa mtu mgeni bila kibali cha mkutano mkuu wa kijiji au mtaa wa mwombaji anakoishi au kukusudia kuishi. 3. Kutakuwepo mabaraza ya wananchi katika kijiji/mtaa, Wilaya na Mkoa ambayo yataitwa MABARAZA YA WAWAKILISHI ,yatakayo kuwa na mamlaka kamili ya kiutendaji, ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa Katiba hii hapatakuwepo na utendaji wa kitarafa katika Serikali ya shirikisho, Tanganyika na Zanzibar. 4. Kila mwananchi watakuwa na haki ya kuchagua kiongozi anayemtaka pia atakuwa na haki ya kuchaguliwa kuwa kiongozi hata kama si mwanachama wa chama cha siasa ikumbukwe pia wanaichi watakuwa na haki ya kumwondoa kiongozi yeyote waliomchagua endapo atathibitika kushindwa kutimiza wajibu wake . 5. Kutakuwa na vyombo vya Serikali za Mitaa katika kila mkoa, wilaya, mji na kijiji, katika Shirikisho,ambavyo vitakuwa vya aina na majina yatakayowekwa na sheria iliyotungwa na Bunge husika. 6. Bunge , litatunga Sheria itakayofafanua utaratibu wa kuanzisha vyombo vya Serikali za Mitaa, miundo na wajumbe wake, njia za mapato na utaratibu wa utekelezaji wa shughuli za vyombo hivyo. 7. Madhumuni ya kuwapo Serikali ya Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi. Vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki kuwashirikisha wananchi katika mipango na shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao na nchini kote kwa jumla. 8. Bila ya kuathiri maelezo ya jumla yaliyomo katika ibara ndogo ya (1) ibara hii, hiki chombo cha Serikali za Mitaa, kwa kuzingatia masharti ya sheria iliyokianzisha, kitahusika na shughuli zifuatazo:- (a) kutekeleza kazi za Serikali za Mitaa katika eneo lake; (b) kuhakikisha utekelezaji wa Sheria na ulinzi wa wananchi; na (c) kuimarisha demokrasi katika eneo lake na kuitumia demokrasi kuhakikisha maendeleo ya wananchi. 9. Mbali na Serikali za Mitaa wananchi watakuwa na haki kuanzisha na kuandikisha vyama vya hiari vyenye kukidhi maslahi ya makundi mbalimbali kama vyama vya wafanyakazi, vyama vya shirika, vyama vya hiari n.k. 10. Bila kuathiri masharti yoyote ya Katiba hii, wananchi watakuwa na haki ya kuwachagua wakuu wa mikoa ambao pia watakuwa wabunge wa Bunge la Shirikisho, Wakuu wa Wilaya, Wabunge wa Majimbo ya uchaguzi ambao watakuwa ni wajumbe wa mabunge ya Tanganyika na Zanzibar, madiwani na viongozi wa Serikali za Mitaa. (a) Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya watakoma kuwa viongozi wa sehemu zao na nafasi zao kuwa wazi endapo (I) Rais wa Shirikisho atamteua kuwa waziri au Naibu Waziri wa Serikali ya Shirikisho. (ii) Ameteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho kwa mujibu wa Katiba hii (iii) ataonekana kushindwa kumudu kazi zake kwa mujibu wa Ibara 129 (7) ya Katiba hii. 11. Kwa mujibu wa Katiba hii Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya hawataruhusiwa kuchaguliwa kuwa Mawaziri au Naibu Waziri katika Serikali za Tanganyika au Zanzibar isipokuwa Serikali ya Shirikisho tu. 12. Wananchi watakuwa na haki kwa mujibu wa Katiba hii kumwondoa kiongozi huyo kushindwa kutimiza wajibu wake kwa wananchi waliomchagua, Bunge linaweza kutunga sheria na kuweka utaratibu utakaotumika. 13. Kwa mujibu wa Katiba hii ni marufuku kwa mtu yeyote asiyechaguliwa na wananchi kufanywa au kujifanya kuwa Mbunge wa Shirikisho au kuwa Mbunge wa Tanganyika au Zanzibar, vikao vyote vya Bunge la Tanganyika na Zanzibar vitahudhuriwa na wabunge wa majimbo husika wa kuchaguliwa isipokuwa tu kwenye Bunge la Shirikisho ambapo mawaziri na manaibu Waziri wasiokuwa wabunge wataruhusiwa kuingia bungeni kwa mujibu wa Ibara ya 56 (4) ya Katiba hii. Serikali 34.Kutakuwa na Serikali ya Shirikisho ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yote ya shirikisho katika Shirikisho. (2) Mamlaka ya Serikali ya Shirikisho yatahusu utekelezaji na hifadhi ya Katiba hii na pia mambo yote ya Shirikisho. (3) Mamlaka yote ya Serikali ya Shirikisho juu ya mambo yote ya Shirikisho yatakuwa mikononi mwa Rais wa Shirikisho pamoja na vyombo vya Shirikisho vilivyoundwa na Katiba hii. (4) Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba hii, madaraka ya Serikali ya Shirikisho yatatekelezwa ama na Rais mwenyewe moja kwa moja au na vyombo vya Shirikisho vilivyoundwa na Katiba hii au kwa Rais kuwakilisha madaraka hayo kwa watu wengine wenye madaraka katika utumishi wa Serikali ya Shirikisho. (5) Ifahamike kwamba masharti yaliyomo katika ibara hii hayatahesabiwa kwamba- (a) yanahamishia kwa Rais madaraka yoyote yakisheria yaliyowekwa na sheria mikononi mwa mtu au mamlaka yoyote ambayo si Rais, au (b) yanalizuia Bunge kukabidhi madaraka yoyote ya kisheria mikononi mwa mtu au watu au mamlaka yoyote ambayo si Rais. Utekelezaji wa shughuli za Serikali 35. Shughuli zote za utendaji za Serikali ya Shirikisho zitatekelezwa na watumishi wa Serikali kwa niaba ya Umma. (2) Amri na maagizo mengine yanayotolewa kwa madhumuni ya ibara hii yatathibitishwa kwa namna itakavyoelezwa katika kanuni zilizowekwa na Rais, au vyombo vya Shirikisho kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii. Mamlaka ya kuanzisha na kuwateua watu wa kushika nafasi za madaraka 36. (1) Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii, Rais kwa kushauriana na Tume zinazohusika atakuwa na mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Shirikisho. (2) Bila ya kuathiri masharti mengine yaliyomo katika Katiba hii, mamlaka ya kuwateua watu kushika nafasi za madaraka katika utumishi wa Serikali ya Shirikisho , na pia mamlaka ya kuwapandisha vyeo watu hao, kuwaondoa katika madaraka, kuwafukuza kazi na mamlaka ya kudhibiti nidhamu ya watu waliokabidhiwa madaraka , yatakuwa mikononi mwa Rais, Tume zinazohusika na mamlaka mengineyo yaliyotajwa na kupewa madaraka kuhusu nafasi yoyote au aina ya nafasi za madaraka kwa mujibu wa Katiba hii. Utekelezaji wa kazi na shughuli za Rais , n.k. 37. (1) Mbali ya kuzingatia masharti yaliyomo katika Katiba hii, utendaji wa kazi na shughuli zake, Rais atalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote au chombo chochote anapotakiwa kupata ushauri au idhini. (2) Endapo Baraza la Mawaziri litaona kuwa Rais hawezi kumudu kazi zake kwa sababu ya maradhi ya mwili au ya akili, laweza kuwasilisha kwa Rais wa Mahakama azimio la kumwomba Rais wa Mahakama athibitishe kwamba Rais, kwa sababu ya maradhi ya mwili au ya akili hawezi kumudu kazi zake. Baada ya kupokea azimio kama hilo, Rais wa Mahakama ndani ya siku saba atateua bodi ya utabibu kutoka miongoni mwa mabingwa wanaotambuliwa na sheria ya matabibu ya Tanzania, na bodi hiyo itachunguza suala hilo na kumshauri Rais wa Mahakama ipasavyo, naye aweza , baada ya kutafakari ushahidi wa kitabibu kuwasilisha kwa Spika hati ya kuthibitisha kwamba Rais kutokana na maradhi ya mwili au ya akili, hamudu kazi zake; na iwapo Rais wa Mahakama hatabatilisha tamko hilo ndani ya siku saba baada ya kuliwasilisha kutokana na Rais kupata nafuu na kurejea kazini, basi itahesabiwa kwamba kiti cha Rais, kiwazi, na masharti yaliyomo katika ibara ndogo ya (3) yatatumika. (3) Ikitokea kwamba Kiti cha Rais ki wazi kutokana na masharti yaliyomo katika ibara ndogo ya (2) endapo kiti cha Rais kiwazi kutokana na sababu nyingine yoyote, na endapo Rais atakuwa hayupo katika Shirikisho, kazi na shughuli za Rais zitatekelezwa na mmoja-wapo wa wafuatao, kwa kufuata orodha kama ilivyopangwa, yaani- (a) Makamu wa Rais au kama nafasi yake i wazi au kama naye hayupo au ni mgonjwa; basi. (b) Spika wa Bunge au, kama nafasi yake i wazi au kama naye hayupo au ni mgonjwa; basi (c) Rais wa Mahakama ya Rufani ya Shirikisho. (4) Endapo yeyote kati ya watu waliotajwa katika aya ya (b) (c) za ibara ndogo ya (3) atatekeleza kazi na shughuli za Rais kutokana na sababu kwamba mtu mwingine anayemtangulia katika orodha hiyo hayupo, basi mtu huyo ataacha kutekeleza kazi na shughuli hizo mara tu mtu huyo mwingine anayemtangulia atakaporejea na akashika na kuanza kutekeleza kazi na shughuli za Rais. (5) Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au akili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais na uchaguzi wa Rais utafanyika ndani ya miezi mitatu isipokuwa tu pale ambapo muda wa Bunge uliobaki hauzidi miezi sita uchaguzi wa Rais utasubiri uchaguzi wa Bunge. (6) Ifahamike kwamba kiti cha Rais hakitakuwa ki wazi na Rais hatahesabiwa kwamba hayuko katika Shirikisho endapo- (a) atakuwa hayupo katika mji ambao ndio makao makuu ya Serikali ya Shirikisho; (b) atakuwa hauyupo katika Shirikisho kwa kipindi cha muda wa saa ishirini na nne; au (c) atakuwa si mgonjwa mahututi. (7) Iwapo kutatokea lolote kati ya mambo yaliyotajwa katika ibara ndogo ya (6) na Rais akiona kuwa inafaa kuwakilisha madaraka yake kwa muda wa jambo hilo, basi aweza kutoa maagizo kwa maandishi ya kumteua yeyote kati ya watu waliotajwa katika aya ya (a) au ya (b) za ibara ndogo ya (3) ya ibara hii kwa ajili ya kutekeleza madaraka ya Rais wakati yeye hayupo au ni mgonjwa, na mtu huyo atakayeteuliwa atatekeleza madaraka hayo ya Rais kwa kufuata masharti yoyote yatakayowekwa na Rais. (8) Rais aweza akiona inafaa kufanya hivyo, na baada
ya kushauriana na Makamu wa Rais kumwagiza kwa maandishi Waziri yeyote
kutekeleza kazi na shughuli zozote za Rais ambazo Rais atazitaja katika
maagizo yake na Waziri aliyeagizwa hivyo kwa mujibu wa masharti ya ibara
hii ndogo, atakuwa na mamlaka ya kutekeleza kazi na shughuli hizo kwa kufuata
masharti ya sheria nyingine yoyote; isipokuwa kwamba-
|
Milipuko ya mabomu Dar, Nairobi: Waislamu
walaani vyombo vya habari
Wanawake Waislamu Tanga waazimia kupigania
haki
Marekani yashambulia Sudan, Afghanistan Maoni: Kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani:
Nguruwe kuzua tafrani Kibamba
Sheikh Mbukuzi ataka vijana
wajihadhari na utamaduni wa Magharibi
TAMPRO kuzindua Tawi Iringa
Tamasha la kusaidia wagonjwa
laanza Moro
Kambi ya matibabu ya Macho Tanga
yaanza
MAONI: Kanisa mshiriki wa ukandamizaji Porojo za Ngatara
Ubatizo kupitia TVZ?
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA
Hoja binafsi: Uhusiano na Marekani
usituletee maafa
Wanamume toeni haki za
wanawake kuepusha ufisadi
MAKALA: Hoja za kutofautisha Yesu
na Issa ni udhaifu, ni uzushi mtupu! - 2
Mwanaadamu alipofikia
|
Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua kwa: webmaster@islamtanzania.org